Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete (aliyeshika mkasi) akikata
utepe kuzindua rasmi ujenzi wa barabara ya Bwanga – Biharamulo. Kushoto
kwa Rais ni Waziri wa Ujenzi Mhe. Dkt. John P. Magufuli na kulia kwa
Rais ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi Alhaj Eng. Mussa Iyombe. Wengine
katika picha ni baadhi ya Mawaziri, Wabunge na Viongozi wa Mikoa ya
Geita na Kagera walioshiriki katika sherehe hizo.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete akimwagilia mti alioupanda
katika eneo la Buziku mkoani Geita wakati wa sherehe za uzinduzi wa
ujenzi wa barabara ya Bwanga – Biharamulo.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete akiteta jambo na Waziri wa
Ujenzi Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli wakati wa sherehe za uzinduzi wa
ujenzi wa barabara ya Bwanga – Biharamulo.
Lori aina ya Scania la Kampuni ya MAP
CO Ltd. likiwa na usajili namba T 895 AFH/T 226 AGB kama lilivyokutwa
eneo la Manyoni mkoani Singida likiwa limekatika katikati kutokana na
kuelemewa na uzito wa mzigo lililoubeba
Umati wa wananchi waliojitokeza
kumlaki Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho
Kikwete alipowasili eneo la Buziku mkoani Geita tayari kwa uzinduzi wa
ujenzi wa barabara ya Bwanga – Biharamulo.(P.T)
JK ampa rungu Magufuli
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete amemtaka Waziri wa Ujenzi
Mheshimiwa Dkt. John Magufuli kuhakikisha kuwa Sheria ya Usalama
Barabarani inasimamiwa vizuri ili kuhakikisha kuwa barabara zinazojengwa
nchini zinadumu kwa muda uliokusudiwa.
Akizungumza katika eneo la Buziku
mkoani Geita wakati akizindua ujenzi wa barabara ya Bwanga hadi
Biharamulo yenye urefu wa kilometa 67, Rais Kikwete alisema kuwa wizara
ya Ujenzi ni lazima ihakikishe inasimamia sheria zilizopo na hasa hii ya
kutoruhusu magari yenye uzito uliozidi viwango vilivyoainishwa katika
Sheria Namba 30 ya Mwaka 1973.
Akisistiza umuhimu wa kutunza barabara
Rais Kikwete alibainisha kuwa "adui wakuu watatu wanao sababisha
barabara kuharibika mapema ni; magari yanayobeba mizigo zaidi ya uzito
uliowekwa kisheria, ujenzi duni usiozingatia viwango na kuachwa kwa maji
kuzagaa barabarani".
Wakati huo huo Rais Kikwete alielezea
kufurahishwa kwa kuanza ujenzi wa mradi huo kwani wapo baadhi ya watu
waliokuwa waliokuwa wakieneza taarifa kuwa sehemu hiyo ya barabara
haiwezi kujengwa lakini sasa wameumbuka.
Awali akitoa maelezo ya mradi huo
Mtendaji Mkuu wa Tanroads Injinia Patrick Mfugale alielezea kuwa mradi
mradi wa ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami umegharimu
Shilingi bilioni 55 fedha zote zikiwa zimetolewa na Serikali ya
Tanzania. "Mradi huu utajengwa kwa muda wa miezi 27 na hivyo kukamilika
mwezi Februari mwaka 2015" alisema Injinia Mfugale.
Naye Waziri wa Ujenzi Mheshimiwa
Magufuli alimhakikishia Rais Kikwete kuwa wizara yake itahakikisha kuwa
inamsimamia mjenzi wa mradi huo ambaye ni Kampuni ya Sinohydro Ltd. ya
kutoka Jamhuri ya Watu wa China ili aukamilishe kwa muda na viwango
vilivyokusudiwa na bila ya visingizio vya nyongeza ya gharama.
Akimpongeza Rais kwa kutekeleza ahadi
yake, Waziri Magufuli alibainisha kuwa wananchi wa mikoa ya Geita na
Kagera wamefurahishwa sana kuona kuwa hatimaye barabara hiyo muhimu
inajengwa kwani hiyo ndiyo sehemu pekee iliyokuwa imebaki ikiwa haina
lami kwa barabara inayounganisha mikoa hiyo ya ziwa.
source: mjengwa blog
No comments:
Post a Comment