*Apanga kuanika aliyobaini Ulaya, ashtushwa na fedha zilizofichwa visiwa vya Uingereza
*Asema ni zaidi ya zile za Uswisi, ayageukia makampuni asema nayo yamo, aonya yakiachwa
*Asema ni zaidi ya zile za Uswisi, ayageukia makampuni asema nayo yamo, aonya yakiachwa
MIEZI 12 tangu serikali iazimie
kuunda timu maalumu kuchunguza sakata la vigogo wanaodaiwa kuficha fedha
haramu nje ya nchi, hususani katika mabenki ya Uswisi, upepo wa suala
hilo sasa unaweza kubadilika wakati wowote, baada ya muasisi wa hoja
hiyo, Zitto Kabwe, kupanga kuibua mazito aliyodai kubaini katika
uchunguzi wake Ulaya. (HM)
Mbunge huyo wa Kigoma Kaskazini
(Chadema), alirejea nchini jana akitokea katika nchi za Ulaya, baada ya
kumaliza kazi ya kuongoza jopo la wataalamu kutoka Shirika la Kimataifa
la Mtandao wa Ulaya wa Madeni na Maendeleo (Eurodad), kufanya uchunguzi
kuhusu masuala ya uwazi katika kodi.
Akizungumza na gazeti hili kwa njia ya
mtandao akiwa nchini Ufaransa siku tatu zilizopita, Zitto alisema;
"Huu
uchunguzi ni mkubwa. Ni jambo kubwa sana. Nikimaliza kazi nitafanya
press conference (mkutano na waandishi wa habari) ili kila Mtanzania
aweze kujua, uchunguzi wa suala hilo ni mkubwa, hivyo kila Mtanzania
anatakiwa kujua kinachoendelea," alisema Zitto kwa kifupi.
Gazeti hili lilipotaka kujua ni mambo
gani hasa ameyabaini ambayo yanaigusa Tanzania moja kwa moja, likiwemo
suala la idadi ya vigogo wanaotajwa kuficha fedha chafu nje ya nchi,
Zitto bado alisisitiza azma yake ya kukutana na waandishi wa habari,
huku akitoa angalizo kuwa inatupasa kuwa makini.
Nikimaliza kazi nitafanya 'press
conference' siku ambayo nitatangaza ili kila Mtanzania aweze kujua,
ninarudi Novemba 2. Uchunguzi ni mkubwa sana na lazima tuwe makini
sana," alisema.
Alisema akiwa huko alikutana na watu
waliokuwa wanafanya kazi kwenye mabenki ya Uswisi na Mauritius, ambao
alisema kuwa wana taarifa nyeti sana.
Zitto, ambaye wakati anawasiliana na
gazeti hili alikuwa mjini London, nchini Uingereza, alisema akiwa hapo
alikutana na mchunguzi mwingine kwa ajili ya akaunti za visiwa vya
Jersey, Isle of man, Guarnsey, Cayman na kisiwa cha British Virgin,
ambako imebainika kuna fedha nyingi zaidi kuliko zile za Uswisi.
Alibainisha kuwa fedha za watu binafsi ni chache kuliko makampuni makubwa yanavyokwepa kodi nchini.
Watu binafsi ni rahisi kuwashughulikia
na kurejesha fedha zilizopatikana kwa wizi, rushwa na biashara ya
madawa ya kulevya. Kazi kubwa ipo kwa makampuni ya kimataifa ambayo
yanakwepa kodi zaidi ya dola 546 milioni kila mwaka," alisema Zitto.
Katika kushughulikia suala hilo la
utoroshwaji wa mabilioni ya fedha nchini, Zitto alisema kuwa ni vyema
makampuni nayo yasisahauliwe.
Akili za watu wengi sasa ni kwa watu
binafsi, lakini tusipokuwa makini tutayaacha makampuni yakiendelea
kunyonya rasilimali zetu na kutolipa kodi," alisisitiza Zitto, ambaye
pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC).
Kwa upande wa kampuni za madini,
alisema tangu mwaka 2001 mpaka 2011 zimeuza nje ya nchi madini ya dola
11.3 bilioni, lakini wamelipa kodi dola 440 milioni, ambayo ni chini ya
asilimia nne ya mauzo yao yote.
Kwa mujibu wa maelezo yake, idadi hiyo
ni mbali na makampuni ya simu na sekta nyingine ambapo ametilia shaka
serikali kupoteza fedha nyingi kwa mtindo huo.
Inaelezwa kuwa takwimu za mtiririko wa
fedha haramu zinazofichwa nje zikitokea Afrika ni mara mbili ya kiasi
cha fedha za msaada zinazotolewa kwa bara hili.
Shirika la Kimataifa la Fedha la
Global Financial Integrity, linakadiria kuwa kiasi cha dola trilioni 1.4
zilihamishwa kutoka Afrika katika kipindi cha miongo mitatu (1970 mpaka
2009).
Katika kipindi hicho, mikopo ya Afrika ilikuwa chini kuliko fedha haramu zinazohamishwa.
Inakadiriwa kuwa kila mwaka, Afrika inaingia hasara ya dola bilioni 50 katika ukwepaji wa kodi.
Hatua hiyo ilisababisha Nicholous
Shaxson kuandika katika kitabu chake "Treasure Islands" kwamba; huwezi
kuelewa umaskini barani Afrika pasipo kujua jukumu la Kodi ya Bandari.
Utafiti huo pia unaonyesha kuwa katika
utawala wa Rais Jakaya Kikwete, fedha zilizofichwa nje ya nchi ni Dola
za Marekani 7,967.4 milioni (sawa na Sh 12.7 trilioni).
Zitto, ambaye pia ni Mwenyekiti wa
Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), kwa muda mrefu amekuwa
akipigia kelele suala hilo ambapo Novemba 9 mwaka jana, katika mkutano
wa Bunge aliwasilisha hoja binafsi ya kulitaka Bunge kuchunguza na
kuielekeza serikali hatua dhidi ya raia wa Tanzania walioficha fedha na
mali haramu nje ya nchi.
Hata hivyo, Bunge liliazimia serikali
ifanye uchunguzi kuhusiana na tuhuma hizo na kuwasilisha ripoti yake
katika mkutano wa Bunge wa Aprili mwaka huu, jambo ambalo haijaweza
kulitekeleza mpaka sasa.
Gazeti hili lilimtafuta Mkurugenzi wa
Shughuli za Bunge, John Joel, kujua ilikoishia ripoti hiyo ya uchunguzi
unaofanywa na serikali. Alisema Spika wa Bunge, Anne Makinda, katika
kikao cha Kamati ya Uongozi ya Bunge kilichofanyika kabla ya kuanza kwa
shughuli za Bunge linaloendelea sasa mjini Dodoma, aliikumbusha serikali
kuhusu kuleta ripoti hiyo.
"Spika katika kikao cha Kamati
aliagiza serikali ilete taarifa, hivyo siwezi kujua, lakini kama ni
taarifa tu ya serikali muda huo utapatikana," alisema Joel.
Alipoulizwa iwapo pia Zitto anaweza
kuwasilisha taarifa yake ya Eurodad katika Bunge hili, alisema
haitawezekana, kutokana na utaratibu wa Bunge kuwa mwisho wa kuwasiliswa
hoja ni siku moja kabla ya kuanza kwa Bunge.
"Sidhani, kwa utaratibu wetu hoja
zinatakiwa ziwasilishwe siku moja kabla ya kuanza, labda kama ataleta na
atakabidhi kwa Katibu wa Bunge kwa ajili ya Bunge lijalo," alisema
Joel.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji
Fredrick Werema, ambaye mara kadhaa amekaririwa akisema kuwa ripoti
kuhusu mabilioni ya fedha ipo tayari, alipotafutwa mara kadhaa na gazeti
hili kujua lini itafikishwa bungeni, ameonekana kutopenda kuweka wazi
suala hilo.
Zitto aliteuliwa mwezi uliopita
kuongoza jopo la wataalamu kutoka Eurodad, ambao ni Mtandao wa Mashirika
yasiyo ya kiserikali yapatayo 48 kutoka nchi 19 za Ulaya, ambayo
yanajihusisha na masuala ya kufutia madeni nchi zilizoendelea, misaada
yenye maana na kodi za haki, kufanya uchunguzi kuhusu masuala ya uwazi
katika kodi.
Mashirika hayo yamekuwa kwenye kampeni
ya kupinga utoroshwaji wa fedha kupitia ukwepaji kodi unaofanywa na
mashirika ya kimataifa kwa nchi zinazoendelea.
Uchunguzi huo uliofanywa katika nchi
za Ulaya, ulianza Oktoba 20 na ulitarajiwa kukamilika Novemba 5, mwaka
huu kwa kuandika ripoti yake.
Chanzo: Rai
No comments:
Post a Comment