Mahakama ya Rufaa nchini Tanzania
imetupilia mbali ombi la warufani wawili Nguza Viking na mwanaye, ambao
waliomba mahakama hiyo kufanya marejeo ya uamuzi wake wa awali wa
kuwapata na hatia kama ambavyo hukumu dhidi yao ilivyotolewa na mahakama
ya Hakimu Mkazi Kisutu mwaka 2004.
Nguza Viking, maarufu kama Babu Seya
na watoto wake watatu walihukumiwa kifungo cha maisha jela kwa makosa ya
kubaka na kulawiti watoto.
Mwaka 2010, rufaa yao ilisikilizwa
katika Mahakama ya Rufaa, na kuwaachia huru Nguza Mashine na Francis
Nguza baada ya kuwaona hawana hatia katika makosa yote waliyoshitakiwa.
Baada ya rufaa hiyo, Babu Seya na
mwanaye Papii Kocha walipatikana na hatia na hivyo kuendelea kutumikia
adhabu ya kifungo cha maisha jela.(P.T)
Tarehe 30 Oktoba mwaka huu, Mahakama
ya Rufaa iliyoketi chini ya jopo la majaji watu, likiongozwa na Nathalia
Kimaro, akisaidiana na Mbarouk Mbarouk na Salum Masati walisikiliza
hoja za pande zote kuhusu ombi la kufanyika mapitio ya uamuzi wa awali
wa mahakama hiyo.
Alhamisi, Mahakama ya Rufaa baada ya
kufanya mapitio ikiwa imeketi chini ya majaji watatu, imeendelea kuwaona
warufani hao wawili kuwa na hatia na hivyo kuendelea kutumikia adhabu
yao.
Upande wa utetezi ukiongozwa na wakili
wao Mabere Marando uliomba kupitiwa upya kwa uamuzi huo, ukidai kuwepo
kasoro katika ushahidi uliowatia hatiani, ikiwemo kukosekana kwa
mashahidi muhimu katika kesi hiyo.
Majaji walisema kuwa kuna uthibitisho kuwa warufani hao wawili waliwabaka watoto wa shule ya msingi mwaka 2003.
Kesi hiyo imewashtua mashabiki wa mwanamuziki Viking nchini Tanzania na kanda nzima ya Afrika Mashariki.
Mwanamuziki huyo mwenye kuimba nyimbo
za Rhumba, ambaye ni mzaliwa wa DRC, ameishi Tanzania kwa miaka mingi na
kuwa na mashabiki wengi.
Mwandishi wa BBC Ben Mwang'onda mjini
Dar es Salaam anasema kuwa Nguza Viking na mtoto wake Johnson Nguza
maarufu kama Papii Kocha ambaye pia ni mwanamuziki, walifika mahakamani
hapo kusikiliza hatma yao.
Walionekana kuwa watulivu wakati majaji walipotupilia mbali ombi lao kutaka hukumu yao kubatilishwa.
Walihukumiwa kwa kuwabaka wasichana 10
wa shule ya msingi waliokuwa kati ya umri wa miaka sita na nane wote
waliokuwa katika shule ya msingi ya Mashujaa wilayani Kinondoni mjini
Dar es Salaam.
Wakili wa muimbaji huyo alisema kuwa mwanamuziki huyo hana matumaini tena ya kupewa rufaa kwani hili ndilo ombi lake la mwisho.
chanzo: mjengwa blog
No comments:
Post a Comment