Dar es Salaam. Mgogoro ndani ya
Chadema umezidi kupamba moto baada ya Kamati Kuu kuwavua uongozi Zitto
Kabwe na Dk Kitila Mkumbo, huku Makamu Mwenyekiti Taifa, Said Arfi
akiandika barua ya kujiuzulu.
Zitto alivuliwa uongozi wa Naibu Katibu
Mkuu Taifa na Naibu Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, wakati
Dk Mkumbo amevuliwa ujumbe wa Kamati Kuu. Wawili hao wanatuhumiwa
kukisaliti chama.
Taarifa zilisema hoja ya kukisaliti chama pia
ilimkumba Arfi akidaiwa kumwezesha Waziri Mkuu Mizengo Pinda kupita
ubunge bila kupingwa, katika uchaguzi mkuu uliopita na ndiyo sababu ya
kuamua kuachia ngazi nafasi ya Makamu Mwenyekiti wa chama hicho Taifa.
Mbali ya kuwavua uongozi Zitto na Dk Mkumbo, pia
Kamati Kuu imewapa siku 14 wajieleze kwa nini wasifukuzwe uanachama. Kwa
uamuzi huo Zitto amebaki na wadhifa wa ubunge wake wa Kigoma Kaskazini
na wadhifa mwingine kwenye Kamati ya Bunge.
Zitto azungumza
Mara baada ya kumalizika kwa kikao hicho, Zitto
aliliambia gazeti hili, “Sina cha kueleza, kikao kilikwenda vizuri na
taarifa rasmi ya chama kuhusu uamuzi wa kikao itatolewa baadaye mchana
(jana saa nane mchana), tusubiri Kamanda.”
Arfi ajiuzulu
Makamu Mwenyekiti wa Taifa, Said Arfi ambaye pia
ni Mbunge wa Jimbo la Mpanda Mjini, jana aliwasilisha barua ya kujiuzulu
nafasi ya uongozi wa chama, akisema; “…kuchoshwa na unafiki unaoendelea
ndani ya chama. Napenda ifahamike pia kwangu masilahi ya wapigakura,
wakazi na wananchi wa Mpanda Mjini na Wilaya ya Mpanda ni muhimu katika
kuwatumikia, hivyo basi sipo tayari kuchaguliwa marafiki.
Katika barua hiyo anasema amechochwa na tuhuma
ambazo zimekuwa zikielekezwa kwake kuwa alimsadia Waziri Mkuu Mizengo
Pinda kupita bila ya kupingwa katika uchaguzi wa ubunge katika uchaguzi
mkuu uliopita.
“Kwa kipindi kirefu zimekuwepo shutuma dhidi yangu
na kutiliwa shaka uhusiano wangu na Mhe Pinda Waziri Mkuu. Pamoja na
kulijadili katika vikao kadhaa Mpanda na Dar es Salaam bado yapo mashaka
kwa nini alipita bila kupingwa. Huo ulikuwa uamuzi wa Wanampanda kwenu
imekuwa ni tatizo, lakini hamsemi kwa nini. Majimbo mengine 16 nchini
yalipita bila kupingwa mlikuwa wapi na nani alaumiwe? Huu ni unafiki wa
kupindukia.
Vilevile, katika barua hiyo, Arfi anasema
amechukizwa na kauli ya mwasisi wa chama hicho, aliyemtaja kwa jina moja
la Mtei kuwachagulia marafiki.
“Aidha mmechukizwa sana kwa nini nilihoji kauli ya
Mwasisi wa chama, Mhe Mtei kutuchagulia viongozi. Naomba ifahamike
wazi kwamba huu ni mtazamo wangu na utabakia hivyo siku zote kwa chama
cha demokrasia kutoruhusu uongozi wa kiimla kwa kukidhi matakwa ya
waasisi ambao huvigeuza vyama kuwa mali binafsi.
Kwa kusema ukweli na kusimamia ukweli daima itabakia kuwa lengo
langu katika maisha yangu siku zote hata kama itanigharimu maisha
yangu.”
Hata hivyo, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willbroad
Slaa alipoulizwa kwa njia ya simu kuhusu barua ya Arfi ya kujiuzulu
uongozi, alisema; “Mimi nimekwishaondoka ofisini.”
Taarifa ya chama
Akitangaza uamuzi wa Kamati Kuu jana Mwanasheria
wa Chadema, Tundu Lissu alisema, Zitto, Dk Mkumbo na Mwenyekiti wa
Chadema mkoani Arusha, Samson Mwigamba walikuwa na mtandao wa kukiua
chama hicho, huku wakitengeneza tuhuma za kuwachafua Mwenyekiti wa
chama hicho, Freeman Mbowe na Katibu wake, Dk Willbroad Slaa.
Alisema kuwa kamati kuu ilibaini kuwapo kwa
mkakati mkubwa wa watu hao kutimiza malengo hayo ambao umeandikwa katika
waraka unaoitwa ‘Mkakati wa Mabadiliko 2013’, ambao umeandaliwa na
kikundi kinachojiita ‘Mtandao wa Ushindi’.
“Kikundi hicho vinara wake wapo wanne, Zitto
anajulikana kama Mhusika Mkuu (MM), Mkumbo (M1), Mwigamba (M3) na mtu
mwingine wa nne hatujamtambua kwa sasa yeye anatumia jina la M2” alisema
Lissu.
Alisema wakati wa kuhojiwa na Kamati Kuu Dk Mkumbo
alikiri kuwa mhusika mkuu wa mtandao huo ni Zitto, lakini Zitto alikana
kuutambua waraka huo licha ya kueleza unamhusu kwa kuwa umetaja jina
lake, kauli ambayo alidai Kamati Kuu haikutaka kuiamini.
Huku akieleza jinsi watu hao walivyokuwa
wakiwasiliana na kupanga mikakati ya kuimaliza Chadema kwa siri chini ya
ufadhili wa fedha kutoka kwa Zitto, Lissu alisema Naibu Katibu Mkuu
huyo wa zamani alikuwa akitumiwa na Chama Tawala (CCM) kuimaliza
Chadema.
“Mkakati wa Mabadiliko 2013 ni mpango haramu na
ambao unaichanachana katiba ya chama chetu. Ni mkakati wa vita dhidi ya
chama chetu na utaratibu wetu wa kikatiba. Hatuwezi kunyamazia mkakati
huu wa kutumaliza, uvumilivu umefika kikomo,” alisema.
Uamuzi
Alisema kutokana na hali hiyo kamati kuu iliamuru
wahusika wote wavuliwe nyadhifa zao zote za uongozi wa chama,
kukubaliana kuunda timu ndogo ya pamoja ya watendaji wa sekretarieti ya
makao makuu ya chama hicho ili kumtambua mtu wa nne (M2).
“Kamati ya Bunge imetakiwa kuchukua hatua za
haraka kuhakikisha Zitto anavuliwa nafasi zote za Naibu Kiongozi wa
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, pia wote wanatakiwa kujieleza ndani ya
siku 14 kwa nini wasivuliwe uanachama na watapewa fursa ya kujitetea,”
alisema.
Alisema Kamati Kuu itakutana kwa dharura kwa ajili ya kufanya uamuzi juu ya hatima ya watuhumiwa hao.
Kauli ya Mbowe
Awali Mbowe alipinga madai kuwa Zitto ameondolewa
kwa kuwa alikuwa akitaka kugombea nafasi ya uenyekiti wa chama hicho,
akasisitiza kuwa uamuzi huo umefanyika kwa kuwa Chadema ni chama cha
watu, siyo mali ya mtu binafsi.
Mvutano Zitto, Lema
Kwa zaidi ya wiki mbili Zitto amekuwa akilumbana na Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema kuhusiana na masuala ya posho.
Vita hiyo ilianzishwa na Lema katika kikao cha wabunge wiki iliyopita aliposema kuwa Zitto anafanya unafiki kukataa posho.
Alimtuhumu mbunge huyo wa Kigoma Kaskazini kwamba
anakataa posho za vikao bungeni, lakini anapokea posho nyingi kutoka
mashirika mbalimbali ya kijamii nchini.
Lema aliweka tuhuma hizo kwenye Mtandao wa Jamii
Forum huku akisema suala hilo halihitaji vikao vya chama kulijadili
isipokuwa vyombo vya habari na hususan, mitandao ya kijamii kwani hata
Zitto hutumia mitandao hiyo.
Zitto alijibu kuwa tangu siku nyingi alikwishapiga
marufuku kwenye Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) kupokea
posho kutoka taasisi au mashirika yanayosimamiwa na kamati hiyo.
Alisema tangu alipokuwa Mwenyekiti wa Kamati ya
Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC), alipiga marufuku posho na
pia aliwahi kuwashtaki Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru)
wabunge wanaochukua posho kutoka taasisi za Serikali.
Zitto pia alipata msukosuko mwingine baada ya
kusambazwa ripoti inayoitwa ‘Taarifa ya Siri ya Chadema’ iliyomtuhumu
kuwa alikuwa anashirikiana na CCM na viongozi wa Idara ya Usalama wa
Taifa kuihujumu Chadema.
Pia, Zitto aliingia katika malumbano na chama
chake baada ya kutuhumu vyama vya siasa kuwa hesabu zake hazikaguliwi na
Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali (CAG), huku akitaka ruzuku
kwenye vyama hivyo isimamishwe.
Chadema ilipinga vikali madai hayo na kueleza kuwa imekuwa
inatumia taasisi binafsi kufanya kazi hiyo. Vyama vinavyopata ruzuku ya
Serikali ni vile vyenye wabunge Chadema, CCM, UDP, TLP, CUF na
NCCR-Mageuzi.
Mvutano kikaoni
Wakati wajumbe wa kikao hicho wakivutana, Zitto
alikuwa njiani akirejea kutoka Sudan Kusini, ambapo alienda na Kamati ya
Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC).
Taarifa kutoka ndani ya kikao hicho zinaeleza
kuwa, baada ya kuibuka sintofahamu hiyo, Mbowe aliwapoza wajumbe wa
kikao hicho, akiwaeleza kuwa haitakuwa busara kumjadili mtu ambaye
hayupo.
“Mbowe alipendekeza kuwa ajenda hiyo iwekwe kando
na itajadiliwa baadaye kutokana na Zitto kutokuwepo katika kikao hicho,”
zilieleza habari hizo.
Baadaye Zitto alituma ujumbe ambao ulitangazwa kwa
wajumbe wote, kwamba alikuwa njiani kurejea Tanzania, kwamba akifika
moja kwa moja atakwenda katika kikao hicho.
Zitto awasili, mzozo waibuka
Kama vile alikuwa akisubiriwa yeye, mara baada ya
kufika katika ukumbi huo saa 2:23 usiku huku akisindikizwa na walinzi
wanne, mvutano mkali uliibuka katika ukumbi huo na mara kadhaa walinzi
wa chama hicho, Red Brigade walionekana kukaa tayari mlangoni kuzuia
vurugu kama ingetokea.
Gazeti hili lilikuwa nje ya ukumbi huo na mara
kadhaa lilisikia sauti za malumbano za baadhi ya viongozi wa chama
hicho, akiwamo Zitto, Mbowe na Lema.
Wakati wakitoa maelezo kwa nyakati tofauti Lema na
Zitto walishutumiana huku kila mmoja akimtaja mwenzake kuwa anatumia
vibaya nafasi yake na mitandao ya kijamii.
“Tatizo lake ni kutumia mitandao ya kijamii
kueleza mambo ya chama wakati akijua siyo utaratibu, ugomvi wangu naye
kwa kiasi kikubwa uko hapo,” alisikika akisema Lema.
Kuna wakati yaliibuka malumbano makali huku sauti za juu zikisikika kutoka ndani ya ukumbi huo, kati ya Zitto, Lema na Mbowe.
Taarifa kutoka ndani ya kikao hicho zinaeleza kuwa Dk Mkumbo
alikumbwa na rungu hilo baada ya kubainika kuwa alikuwa ameanda taarifa
za siri ambazo zilikutwa katika kompyuta mpakato (laptop) ya Mwigamba
ambayo alinyang’anywa baada ya kudaiwa alikuwa anasambaza taarifa za
kuhujumu chama hicho.
Kikao hicho kilimalizika saa 10:00 alfajiri huku
maamuzi hayo yakifanywa siri na Mbowe alipoulizwa kuhusu kuwepo kwa
taarifa za Zitto na Dk Mkumbo kuvuliwa uongozi,” alisema , “Taarifa
zitatolewa baadaye mchana.”
Wasomi wazungumza
Akizungumza na gazeti hili jana, Profesa Gaudence
Mpangala alisema Chadema ni chama kikubwa kinachoweza kushinda uchaguzi
mkuu ujao hivyo kinapaswa kuwa na viongozi walioshikamana na kuwa na nia
moja.
Aliongeza kuwa endapo wapo viongozi wanaoonekana
kwenda kinyume na viongozi wenzao na kwenda kinyume na misimamo ya
Chama, kinayo haki ya kufanya maamuzi ya namna yoyote yenye lengo la
kukinusuru.
“Chadema ni chama kikubwa kinachoweza kushika
dola…kinahitaji mshikamano mkubwa kwa viongozi wake na kuhakikisha
hawatokei wasaliti….kama ni kweli waliosimamishwa ni wasaliti ni halali
kabisa” anasema Profesa Mpangala.
Naye aliyekuwa Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha SAUT,
Dk Charles Kitima alisema wakati umefika kwa vyama vya siasa kutambua
kuwa uwepo wa demokrasia ndani ya vyama vingi vya siasa nchini ni
kusahihishana na kujisahihisha.
Dk Kitima alisema kuwa na mitazamo tofauti siyo
usaliti ni demokrasia na kusema endapo mtu au kiongozi anafanya kitendo
cha kuvunja katika ya nchi huyo moja kwa moja anakuwa mkosaji.
Mbunge wa Jimbo la Wawi (CUF), Hamad Rashid
anasema matukio ya kufukuzana na kutuhumiana baina ya viongozi
yanayofanywa na watendaji mkuu wa vyama vya upinzani yatasababisha
upinzani uzidi kudidimia na kudumaa.
Alisema vyama vya siasa vimekuwa na usultani wa
kuonekana kuwa vinapaswa kuongozwa na baadhi ya watu, na wengine wenye
uwezo na mawazo mapya na yasiyopendwa na wakubwa anatafutiwa mbinu ya
kuondoka.
Rashid alisema hali hiyo inasababishwa na
kukosekana kwa mfumo mzuri wa uongozi ndani ya vyama vya siasa, ambapo
anasema vyama haviongozwi kama taasisi na badala yake vinaongozwa kama
mali za watu.
“Hili linalotokea Chadema sasa ni matokeo ya mfumo
mbovu wa uongozi ndani ya vyama vya siasa nchini….vingi haviongozwi
kama taasisi.” alisema.
source: mwananchi
source: mwananchi
No comments:
Post a Comment