Dar es Salaam. Mwili wa
aliyekuwa Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Dk Sengondo Mvungi
utawasili nchini leo 12.50 jioni kwa ndege ya Shirika la Ndege Afrika
Kusini (Saa) ukitokea Afrika Kusini.
Msemaji wa Tume hiyo, Omega Ngole alisema baada ya
mwili huo kutua kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere,
Dar es Salaam utapelekwa kuhifadhiwa Hospitali ya Lugalo.
Ratiba inaonyesha kuwa kesho saa 4.00 asubuhi
kutakuwa na ibada ya kumwombea itakayofanyika kwenye Kanisa Katoliki la
St Joseph, Dar es Salaam.
Baada ya kumalizika kwa ibada hiyo, mwili
utapelekwa kwenye Viwanja vya Karimjee kwa ajili ya kuagwa kitaifa
kuanzia saa 6.30 mchana na kisha utapelekwa nyumbani kwake
Kibamba-Msakuzi.
Keshokutwa Jumapili kutakuwa na ibada fupi
nyumbani kwake na baada ya hapo, safari ya kuelekea kijijini kwake,
Kisangara Juu, Wilaya ya Mwanga, Kilimanjaro tayari kwa mazishi
yaliyopangwa kufanyika keshokutwa.
Dk Mvungi alifariki dunia, Jumanne iliyopita
kwenye Hospitali ya Millpark Johannesburg, Afrika Kusini baada ya
kuumizwa na watu wasiojulikana waliomvamia nyumbani kwake, Novemba 3
mwaka huu.
Aacha kitabu
Katika hatua nyingine, Dk Mvungi aliwahi kuandika
kitabu kiitwacho ‘Constitutional Reforms For Democratisation in
Tanzania’ mwaka 1992 ambacho asilimia kubwa ya mapendekezo yake ndiyo
yanayotumika katika mchakato wa sasa wa Katiba Mpya.
Akizungumza nyumbani kwa marehemu, Kibamba-Msakuzi
jana, Mkuu wa Shule ya Sheria katika Chuo Kikuu Dar es Salaam (UDSM),
Profesa Bonaventure Rutinwa alisema kitabu hicho ambacho kilitokana na
mijadala mbalimbali kuhusiana na katiba, kinatumiwa pia na wanafunzi wa
sheria.
“Yote ambayo unayaona sasa yakiwamo masuala ya
mabaraza ya katiba, madaraka ya rais, tume huru ya kukusanya maoni,
Bunge la Katiba na mambo mengine yapo katika kitabu hicho,” alisema
Profesa Rutinwa na kuongeza kuwa hata kuchaguliwa kwake katika tume hiyo
hakukuwa jambo la bahati mbaya.
Alisema Dk Mvungi hakwenda katika tume kwa kuvutiwa na malipo au posho bali, uzalendo wake.
“Rais Jakaya Kikwete alijua anamteua mtu wa namna
gani na kikubwa zaidi mapendekezo yaliyomo katika kitabu hicho hata yeye
Rais Kikwete anayajua,” alisema na kuongeza: “Kwa kuandika kitabu cha
namna hiyo wakati wa mfumo wa chama kimoja ulikuwa ujasiri usio wa
kawaida”.
chanzo: mwananchi
chanzo: mwananchi
No comments:
Post a Comment