MWALIMU Nyerere alikuwa Baba wa Taifa
la Tanzania, Baba wa Afrika na Baba wa watetea haki za binadamu duniani kote.
Jambo hili linajidhihirisha kila mwaka watu wanapokusanyika kumkumbuka na
kumwombea.
Sala kubwa ni ile ya kumtaka Mwenyezi
Mungu, kumweka kwenye kundi la watakatifu Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
Hapa Tanzania, kila mwaka Oktoba 14 ni
Siku ya Nyerere (Nyerere Day) na ni siku ya mapumziko. Afrika Kusini nao siku
hii ni ya kumkumbuka Mwalimu kwa majadiliano na tafakuri, juu ya
mawazo yake na mawazo mengine yanayofanana na ya Mwalimu ya haki za binadamu na
masuala ya uchumi wa dunia hii ya Utandawazi.
Kule Amerika, wapenda amani na watetezi
wa haki za binadamu wanakusanyika kusali na kuomba siku ya kukumbuka kifo cha
Mwalimu Nyerere. Serikali ya Rwanda, imetangaza rasmi Oktoba 14 ni Nyerere Day,
ni siku ya kitaifa na watu wanapumzika siku hiyo. Wanyarwanda wanasema
kumbukumbu ya Mwalimu ni sherehe, maana Mwalimu aliacha mambo mengi mazuri
nyuma yake.
Sherehe hizi za kumkumbuka Mwalimu
nchini Rwanda zinaratibiwa na Jumuiya ya Urafiki baina ya Wanyarwanda na
Watanzania – RWATAFA (Rwanda Tanzania Friendship Association).
Kwa faida ya msomaji wa makala hii ni
bora kutambua kwamba RWATAFA ina ndugu yake Tanzania, Jumuiya ya Urafiki
baina ya Watanzania na Wanyarwanda –TARAFA (Tanzania Rwanda Friendship
Association). Kwa pande zote mbili Jumuiya hizi za urafiki zimesajiliwa na
kutambuliwa kisheria.
Mwaka huu sherehe za kumkumbuka Mwalimu
Nyerere zimefanyika Novemba 3, 2013 kwenye Ukumbi wa Hoteli ya Nobleza
mjini Kigali kwa ibada nzuri ya misa iliyoongozwa na mapadri wawili na baadaye
nyimbo, mashairi na hotuba za kumkumbuka Mwalimu Nyerere.
RWATAFA, chini ya Mwenyekiti wake Mzee
Isidore Gahamanyi katika jitihada zake za kutaka kudumisha undugu na urafiki na
TARAFA, iliamua mwaka huu kuwaalika familia ya Mwalimu Nyerere, iliyowakilishwa
na Madaraka Nyerere pamoja na Makongoro Nyerere, pia waliwaalika Makamu
Mwenyekiti wa TARAFA, Mzee Patrick Qoor na mwandishi wa makala hii.
Sherehe za kumkumbuka Mwalimu,
zinatanguliwa na matembezi ya maeneo ya kihistoria na hasa sehemu za Kumbukumbu
ya mauaji ya kimbali. Mwaka huu RWATAFA iliwatembeza wageni wake kwenye
kumbukumbu ya Murambi ambako hadi sasa miili elfu moja inatunzwa.
Miili hii imetunzwa kwa utaalamu wa
hali ya juu, kiasi cha miili hiyo kutoa picha ya aina ya kifo; kukatwa kwa
panga, kupigwa nyundo kichwani, kufungwa mikono na miguu, kubakwa na kuingiziwa
mti kwenye sehemu za siri hadi mti huo ukatokea mdomoni hasa kwa wanawake,
watoto wadogo kupasuliwa vichwa na mateso mengine mengi ya kinyama.
Hapa ndipo mtu anaposhuhudia unyama
uliofanywa wakati wa mauaji ya Kimbali. Wanyarwanda wameendelea kuitunza miili
hii na kuionesha kwa watu ili watambue ubaya wa ubaguzi na ubaya wa siasa zenye
propaganda chafu.
Kila mtu akifika hapa na kujionea
mwenyewe, anakuwa na maswali mengi rohoni mwake. Binafsi, kila nikitembelea
makumbusho haya ambayo ni mengi nchini Rwanda, swali langu ambalo hadi leo hii
halina majibu ni kwa nini mauaji haya yalitokea?
Chuki hii kubwa hivyo kiasi cha kuwaua
watu kinyama na mbaya zaidi hata kuwaua watoto wadogo ambao umri wao haukufika
mwaka mmoja, ilitoka wapi? Nini chanzo cha chuki hii? Ni propaganda za
Wafaransa? Ni siasa mbaya? Ni nini? Ni imani yangu kwamba jibu litapatikana
siku moja.
Wanyarwanda wanamkumbuka na kumuenzi
Mwalimu kwa heshima kubwa. Binafsi nimeshuhudia jambo hili. Wanyarwanda wanasema
wana sababu nyingi za kumkumbuka Mwalimu.
Wanasema, baada ya vita ya 1959,
Umoja wa Mataifa uliamua wakimbizi wa Rwanda wapelekwe Canada, lakini mwalimu
alikataa na kuwapatia hifadhi Tanzania na kwamba wakimbizi wa Rwanda
waliokwenda Burundi, DRC na Uganda, hawakupata uraia wa nchi hizo, lakini wale
waliokimbilia Tanzania walipatiwa uraia, walisoma kwenye shule za serikali,
walitibiwa kwenye hospitali za serikali na walipata huduma zote kama Watanzania
wengine, na kwamba mauaji ya kimbali yalipotokea, Mwalimu Nyerere, alikuwa
kiongozi wa kwanza duniani kukemea na kuyalaani mauaji hayo.
Seneta Kamanzi, akitoa wasifu wa
Mwalimu Nyerere, bila kutafuna maneno alisema; “Mwalimu, alihoji watu kuitwa
wakimbizi. Hakulipenda neno hili, alipendekeza wakimbizi waitwe ‘wageni
wakazi’. Nina imani kama Mwalimu angekuwa bado hai angepinga kwa nguvu zake
zote msamiati huu wa kibaguzi wa wahamiaji haramu.”
Uwepo wa watoto wa Mwalimu kwenye
sherehe hizi ulileta mvuto wa aina yake. Madaraka na Makongoro, walielezea
wanavyomfahamu baba yao; mtu ambaye hakuwa na ubaguzi; aliipenda nchi yake na
kulipenda Bara zima la Afrika.
Wote wawili kila mmoja kwa namna yake;
Makongoro mwanasiasa na Madaraka mtafiti na mtunzaji wa kumbukumbu za Mwalimu
kule Butiama, waliziimba na kuzielezea kwa ufasaha sifa za Mwalimu na kuelezea
wazi kwamba hata Mwalimu alitambua upungufu wake.
“Mwalimu, alikuwa akitwambia kuwa
yeye si malaika, naye ana makosa yake, lakini alisisitiza tuige mazuri yake na
kuachana na makosa yake,” alieleza Madaraka Nyerere.
Rwanda kuna utulivu na amani. Pamoja na
misuguano ya kisiasa iliyojitokeza hivi karibu kati ya Tanzania na Rwanda, bado
Wanyarwanda wana imani kubwa na Watanzania.
Wanaamini siasa ni siasa, zitakuja na
kupita lakini udugu wa Watanzania na Wanyarwanda utadumu milele. Nchi hii ya
jirani ni fursa nzuri kwa Watanzania kwenda na kuwekeza. Kuna Watanzania ambao
wameanza kuwekeza Rwanda na wataalamu wengi wanaofundisha kwenye vyuo vya
Rwanda wanatoka Tanzania.
Hata hivyo bado kuna nafasi kubwa ya
kuwekeza nchini Rwanda. Nchi hii sasa hivi inapiga hatua kubwa ya maendeleo.
Mji wa Kigali ni msafi kuzidi miji mingi, ikiwamo baadhi katika nchi za Ulaya.
Hata kama si kuwekeza, kuna mambo mengi ya kujifunza kutoka Rwanda.
Hakika, kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere
Kigali, ni tukio la kujenga undugu kati ya Tanzania na Rwanda. Na jambo la
kufurahisha ni kwamba undugu huu unajengwa katika ngazi ya wananchi kwa
wananchi. Ni imani ya RWATAFA na TARAFA kwamba undugu ukijengeka baina ya
wananchi wa nchi hizi mbili, serikali zitatekeleza zinataka zisitake.
No comments:
Post a Comment