WAZIRI
Mkuu wa Awamu ya Tatu, Frederick Sumaye, amemtaja mwenzake aliyemfuata baada ya
kuondoka katika wadhifa huo, Waziri Mkuu aliyejiuzulu Edward Lowassa kuhusika
kutoa taarifa za uongo, alizodai kuwa zinalenga kumsaidia kujisafisha.
Akizungumza
na waandishi wa habari Dar es Salaam Jumanne wiki hii, Sumaye alidai Lowassa
alisema uongo kwamba ni yeye pekee aliyefanikisha mradi wa maji wa Ziwa
Victoria, Kanda ya Ziwa na kwamba mawaziri wengine wote walimpinga.
Akinukuu
gazeti moja la kila siku, Sumaye alisema; “Liliandika kuwa siri ya mradi wa
kuvuta maji Ziwa Victoria yafichuliwa na katika maelezo yake, mtoa habari
alisema ni mawaziri wawili tu waliouunga mkono mradi huo na wengine wote
waliupinga.
“Najua
mhusika (Lowassa) ameutumia sana mradi huu kisiasa na sisi wengine tumenyamaza
japo ukweli tunaujua sana. Lakini hili la mradi ametukanyaga vidole wengine na
kutupia miiba na magogo kwenye njia yetu wengine, amenilazimisha niseme ukweli
kuhusu mradi huu kwa sababu mimi ndiye niliyekuwa waziri mkuu na mradi
umetekelezwa chini ya uangalizi wangu kama kiongozi na msimamizi mkuu wa
utekelezaji wa shughuli zote za serikali.
“Pamoja
na kwamba hilo lililoelezwa ni uongo mkavu, mhusika kama waziri
mwandamizi wakati huo na sasa kama anayewinda nafasi kubwa katika nchi
hakutegemewa kutoa siri za baraza la mawaziri; labda amediriki kufanya hivyo
kwa sababu anajua anayoyasema siyo ya kweli vinginevyo ni kosa la jinai na
akishitakiwa anafungwa jela.”
Sumaye
ambaye katika mazungumzo yake hayo na waandishi wa habari alianza kwa kumuunga
mkono Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete kuhusu vitendo vya rushwa katika
siasa za ndani ya CCM, alisema kuna mbinu mbalimbali zinazotumika na wahusika
wanaotafuta nafasi mbalimbali za uongozi kufanikisha malengo yao.
Alisema
ziko mbinu nzuri za kistaarabu na ziko mbinu chafu kama za kupakazana matope (character
assassinations).
“Mbinu
ambazo ni chafu ni pale mhusika anatengeneza mbinu ama za kuwamaliza wengine
wanaodhaniwa kuwa washindani wake baadaye au kuwawekea vikwazo katika mbinu zao
za kujisafishia njia.… huyo ama anachimba mitaro kwenye barabara wanazofyeka
wenzake au anatupia miiba na magogo yanayotoka kwake na kuyatupia kwa wenzake
ili mradi wenzake wakwame wakati ukiwadia,” alisema.
Akizungumzia kwa kina kuhusu mradi wa maji wa Ziwa Victoria,
Sumaye alisema mradi huo ni mradi wa serikali na haukuwa wa mtu.
“Ni
kweli kwa mkataba uliokuwepo wa miaka ya 1952 au 1953 nchi za huku juu mito ya
Nile inapoanzia na inakopitia hazikutakiwa zitumie maji ya Mto Nile ili nchi za
Misri na Sudan zisiathirike. Nchi hizi Tanzania ikiwamo, ziliona makubaliano
hayo siyo sahihi na tulianza kudai mabadiliko ya sheria hiyo.
“Jambo
hili lilishughulikiwa mwanzo na Waziri Dk. Pius Ng’wandu na baadaye
likakamilishwa na ‘Agreed Minutes’ zilizoweka msingi wa makubaliano
baina ya nchi hizo kusainiwa na nchi kumi na kwa Tanzania aliyesaini ambaye kwa
bahati nzuri alikuwa ndiye mwenyekiti wa baraza hilo la nchi kumi alikuwa Musa
Nkhangaa aliyekuwa Waziri wa maji wakati huo,” alisema.
Alisema
katika kusukuma jambo hilo yeye binafsi akiwa Waziri Mkuu aliwahi kukutana
Addis Ababa na marehemu Meles Zenawi, aliyekuwa waziri mkuu wa Ethiopia kabla
ya serikali ya Uholanzi kusaidia kuandika mradi.
Alisema
baada ya Waziri Nkhangaa kutembelea chanzo cha kuchukulia maji cha Smith Sound
na kuona mradi unawezekana, Rais Benjamin Mkapa alishauriwa kuwa mradi huo
unawezekana na kutekeleza ahadi ya kufikisha maji kutoka Ziwa Victoria mkoani
Shinyanga.
“Matatizo
ya maji Shinyanga yalivyotutesa isingewezekana baraza la mawaziri kuupinga
mradi huo na mimi nisingeupinga kabisa maana wakati mji wa Shinyanga ukikosa
maji nilikuwa silali usingizi. Jambo ambalo ni kweli ni kuwa mradi huo uliiva
wakati Lowassa akiwa waziri wa maji na ameusimamia hadi ukakamilika kama
ambavyo angeusimamia waziri mwingine wa maji,” alisema.
Alisema
hakuna waziri mwenye uwezo wa kutekeleza mradi kama baraza la mawaziri
likiukataa na kuhoji: “Fedha atapata wapi za kuendesha mradi huo? Pili mradi
wowote ni wa serikali na unatengenezwa na wizara husika. Katika wizara
wanaofanya kazi sana ni wataalamu chini ya katibu mkuu. Pamoja na kuwa sisi
wanasiasa tunapenda kubeba sifa zote mambo yakienda vizuri na kuwatupia lawama
wataalamu yakienda vibaya, ni vema tujue tunafanya kama timu moja na mwenye
serikali ni moja tu yaani Rais.”
Alisisitiza
kwamba uamuzi wake wa kuzungumzia kauli ya Lowassa si kuingilia mambo ya watu
wengine bali anapoguswa hatoweza kunyamaza.
“Lakini
pia ni wajibu wangu kueleza ukweli pale ukweli unapopotoshwa kwa makusudi.
Nataka niwaase hasa wanasiasa wenzangu kuwa tuwatendee Watanzania haki kwa
kuwapa ukweli mtupu na tusiwape uwongo uliopakwa utamu wa ukweli juu kumbe
ndani ni machungu ya uwongo,” alisema.
Akizungumzia
rushwa na ufisadi, alisema ukiona mtu anatoa rushwa ujue kuna anayedhulumika na
kuumia na hiyo rushwa yako.
“Unapofanya
ufisadi kwa mradi wa serikali unaliumiza taifa katika siku zijazo kwa kuipiga
kiharusi cha uchumi na huduma kwa jamii. Na unapouza dawa za kulevya wewe ni
muuaji wa taifa kwa sababu unaangamiza vijana wa taifa hili ambao ndiyo nguvu
kazi yetu tunayoitegemea,” alisema.
Akimpongeza
Rais Kikwete kuhusiana na rushwa ndani ya CCM, alisema ni imani yake kwamba
waliokabidhiwa dhamana hiyo hawatalionea haya na hawataangalia sura ya mhusika
wakati wa kuchukua hatua.
“Wanachama
wa CCM na wananchi wote tumepata matumaini mapya kwamba kauli ya mwenyekiti wa
chama tawala haitapotelea hewani bali itatekezwa na italeta mabadiliko makubwa
katika vita dhidi ya rushwa nchini. Ndugu mwenyekiti wangu mimi nakupongeza
sana sana kwa kukemea rushwa na ninakuunga mkono katika vita hii na ninaamini
unajua kuwa mimi ni askari wako mojawapo wa mstari wa mbele,” alisema.
Kauli
hiyo ya Sumaye inajitokeza katika wakati ambao vuguvugu la kulenga kuwania
uteuzi wa mgombea urais kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ukipamba moto,
huku rafu zikiwamo za matumizi ya rushwa zikiripotiwa mara kwa mara kufanya na
baadhi ya makundi ya wasaka urais.
No comments:
Post a Comment