ZIMEKUWEPO na zitaendelea kuwapo
tafsiri nyingi juu ya vurugu zilizotokea bungeni Alhamisi ya juma lililopita.
Tafsiri hizi zinahusu mitazamo ya kisheria, kijamii, kisiasa, kiuchumi,
kihistoria na mingine. Ilimradi kila aliyesikia ama kushuhudia atakuwa na
tafsiri ya aina yake.
Pamoja na ukweli kuwa Bunge la Tanzania
sio la kwanza duniani ‘kuruhusu’ vurugu au ngumi ndani ya ukumbi wa mikutano ya
Bunge, ni dhahiri hili lililotokea hapa kwetu wengi wamelichukulia kwa mzito
mkubwa. Hivyo mitazamo inayoendelea kujadiliwa juu ya hili yamkini ni mahsusi
kwa ustawi wa taifa; na inalenga kutusaidia kutafakari wapi tulipopotoka ili
tuweze kujinasua.
Kwa kuwa tafsiri na mitazamo ipo ya
aina nyingi, nachagua kutafakari na kujadili mustakabali wa utaifa na uzalendo
wetu, mintarafu ukada au upenzi wetu kwa vyama vyetu vya siasa.
Kwa kipindi kirefu sasa tumeshuhudia
jinsi mchakato wa uandaaji wa Katiba mpya ulivyogeuzwa kuwa mtaji au chambo cha
baadhi ya vyama vya siasa kukubalika zaidi kwa umma. Hii imeanzia kwenye wazo
lenyewe la umuhimu wa kuwepo kwa mchakato huu wa kuandika Katiba mpya.
Inajulikana wazi kuwa nyakati,
mabadiliko na mahitaji ya Watanzania yalikuwa yanalazimu tu kuwepo kwa mchakato
wa Katiba mpya. Hata hivyo, wakati mchakato ukiwa umeshaanza, ilikuwa nusura
hoja ya nani ndio aliyesukuma uanzishwaji wa mchakato huu (badala ya mchakato
wenyewe)kuwa ndio hoja kuu.
Kwa watu walio wastaarabu na wenye
busara, hapakuwa na haja ya malumbano juu ya hili. Badala yake kama ukweli
unajulikana kuwa mahitaji ya nyakati ndio yalikuwa mwasisi wa jambo hili,
ikijumlishwa na wale waliokuwa mstari wa mbele kulisemea (waasisi namba mbili),
ukweli huu ilipaswa watu kuukiri, na baada ya hapo kusonga mbele. Lakini sasa,
mzimu huu wa ‘nani ndiye mwasisi’ wa Katiba (chini ya miamvuli ya vyama vya
siasa) inaonekana unaendelea kututafuna kwa mtindo mwingine.
Mtindo huu ulioanzia katika ubishani wa
nani ‘Mwasisi wa Katiba’, umegeukia kwenye nani anataka maslahi yake na chama
chake yazingatiwe zaidi (yote) katika rasimu hii tuliyonayo hivi sasa. Mtindo
huu ambao ndio unavuruga mchakato wa uandaaji wa Katiba mpya wanayoihitaji sana
Watanzania, umewafanya baadhi ya watu kulewa kabisa na mapenzi ya U-chama.
Wamesahahu kuwa Katiba hii ni ya nchi na wananchi wa Tanzania; vyama ni matokeo
tu ya Katiba imara inayozaa taifa imara.
Ni ulevi huu wa mapenzi ya vyama vyao
umepelekea baadhi ya vyama na watu wao kufanya vurugu katika mabaraza ya
katiba. Ni ulevi huu huu umepelekea vurugu za bungeni juma lililopita. Kwa
ulevi huu, baadhi yetu (ikiwemo wabunge) wameacha kuzingatia (kwa makusudi)
kanuni za demokrasia kuwa pande mbili zenye mitazamo tofauti lazima zifikie
mahali pa kukubaliana, penye kukidhi lengo lililo kuu zaidi.
Kidemokrasia, kukubaliana kati ya pande
mbili kunategemea uzito au nguvu ya hoja, huku kanuni mbili yaani ya ‘wengi
wape’, na ile ya ‘hekima au busara ya wachache pia itumike (isibezwe)’
zikitiliwa maanani sana.
Kwa mantiki hii, maslahi ya vyama
hayapaswi kuwa juu ya lengo kuu ambalo Watanzania wote wenye mapenzi mema na
nchi yao wanataka litimizwe. Nalo ni kupata Katiba iliyoandaliwa na wananchi
wenyewe na inayokidhi mahitaji yao kwa kadri wanavyotaka.
Tukirejea kilichotokea bungeni juma
lililopita, ni dhahiri kuwa ni wengi waliohusika kwa namna ya moja kwa moja au
nyingine kusababisha kadhia ile. Kwa mfuatano wa jinsi matukio yalivyokuwa,
masuala kadhaa yamewashawishi walio wengi kuamini kuwa ulevi wa mapenzi ya
vyama vya siasa ilikuwa ni sababu mojawapo kubwa iliyolifikisha bunge katika
hali ile.
Kwa kuanzia, kitendo cha Naibu Spika
Job Ndugai kuwa mbogo na kumkatalia katakata fursa ya kuongea Kiongozi wa
Upinzani bungeni, Freeman Mbowe, ambaye ni Waziri Mkuu kivuli hakikuwa cha
busara wala mantiki. Kwa nafasi yake, Mbowe alipaswa kusikilizwa. Laiti kama
Ndugai angetumia busara kidogo tu, kadhia yote ile isingetokea.
Lakini pia manung’uniko kwamba
Wazanzibar hawajashirikishwa inavyopaswa katika kutoa maoni kwa kamati ya bunge
juu ya muswada huo wa marekebisho ya sheria ya mabadiliko ya katiba
hayakuwa ya kubeza kiasi kile. Pamoja na taarifa kutoka kwa Makamu wa pili wa
Rais wa Zanzibar kuonesha kuwa Wazanzibari walishirikishwa, kitendo cha wabunge
wa CUF (ambao ni sehemu ya serikali ya Zanzibar) kuendelea kupinga taarifa hiyo
ya Makamu wa pili wa Rais kilipaswa kuchukuliwa kwa uzito unaostahili.
Kitendo cha Bunge kuendelea na
upitishaji wa muswaada huo bila wabunge karibia asilimia 90 wa kambi ya
upinzani nacho kimetia doa mchakato mzima. Hii pia si ishara njema kwa hatua
nyingine zitakazoendelea katika mchakato mzima wa upatikanaji wa Katiba mpya ya
Watanzania. Ikumbukwe kuwa wabunge hao wa kambi ya upinzani wanawakilisha
maelfu ya Watanzania. Na hivyo wananchi wanaowakilishwa wangependa pia maoni
yao yasikike kupitia kwa wawakilishi wao hao.
Kingine ambacho kiliendelea
kulipunguzia bunge heshima na staha yake ni kitendo cha baadhi ya wabunge wa
CCM waliobaki ukumbini, badala ya kujadili muswada, walitumia muda mwingi
kuwarushia vijembe na kejeli wenzao wa upinzani waliokuwa wametoka. Hili nalo
halikuwa na tija yoyote kwa wananchi waliowatuma kuwawakilisha, na kusimamia
kwa ubora kabisa maslahi ya wananchi hawa.
Kwa kuzingatia hayo yaliyotokea
bungeni, na mengine mengi ambayo yameshuhudiwa katika mchakato huu wa kuandaa
katiba mpya, inabidi hatua madhubuti zichukuliwe ili kuweka mambo sawa huko
tunakoelekea kwa manufaa ya taifa na vizazi vijavyo. Kwa kuanzia kabisa, Rais
Jakaya Kikwete, kwa mamlaka aliyo nayo hana budi kuokoa jahazi ama kwa
kuurejesha muswada huo ujadiliwe tena bungeni au kwa njia nyingine yoyote
itakayofaa.
Pamoja na hayo, wabunge, viongozi
wengine na wananchi kwa ujumla sharti tutambue kwamba lengo mahsusi na lililo
kuu ni kutengeneza Katiba iliyo bora ambayo itadumisha taifa lililo bora.
Mapenzi kwa vyama yasiwe chanzo cha kuwa na Katiba ya hovyo. Tukumbuke kuwa
vyama hivi vitapita lakini taifa litaendelea kuwepo.
Source:
www.raiamwema.co.tz : Paul Dotto
No comments:
Post a Comment