Matukio ya kumwagiwa tindikali yameendelea
kukithiri huku Serikali ikiendelea kutoa ahadi za kudhibiti bila
mafanikio. Hivi karibuni baada ya raia wawili wa Uingereza kumwagiwa
tindikali Zanzibar, Serikali iliweka mikakati mikali ya kudhibiti
matumizi ya kemikali hiyo, lakini bado matukio hayo yameendelea kuwepo.
Tukio la kumwagiwa tindikali kwa Padri wa Kanisa
Katoliki Parokia ya Cheju, Mkoa wa Kusini Unguja, Joseph Mwang’amba ni
mwendelezo wa uhalifu huo ambao Serikali imeshindwa kabisa kuudhibiti.
Akieleza jinsi tukio hilo lilivyotokea, Padri Mwang’amba anasema alikuwa nje ya duka linalotoa huduma za mawasiliano ya mtandao (Sun Shine Internet Caffee) liliopo eneo la Mlandege Wilaya ya Mjini Unguja, ndipo alipotokea kijana mmoja na kumwagia tindikali.
Wakati Padri huyo akieleza hayo, Rais wa Zanzibar Dk Ali Mohamed Shein, ameijia juu polisi kwa kushindwa kudhibiti matukio ya viongozi wa dini na Serikali visiwani humo, kushambuliwa kwa kumwagiwa tindikali huku akilitaka kuwakamata waliohusika na tukio hilo.
Kiongozi huyo wa dini, aliyejeruhiwa maeneo ya usoni, mikononi na kifuani baada ya kumwagiwa tindikali hiyo alisafirishwa jana na ndege ya kukodi ya Shirika la Coastal kutoka visiwani humo hadi Dar es Salaam na baadaye kupelekwa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kwa matibabu zaidi.
Kwa upande wake, Padri wa Parokia ya Mtakatifu Joseph, Zanzibar, Thomas Assenga aliyefuatana na kiongozi huyo mpaka MNH, alisema siku za nyuma Padri Mwang’amba alitolewa vitisho na mtu ambaye hamfahamu wakati akienda kutoa huduma katika kituo cha wazee cha Welezo.
Alisema kabla ya kufika kituoni hapo, kuna eneo ambalo nyakati za asubuhi watu hufanya mazoezi barabarani ambapo kuna mtu mmoja alimtolea maneno ya vitisho.
Tukio hilo linafuatia tukio la Agosti 7, mwaka huu ambapo raia wawili wa Uingereza, Kate Gee (18) na Kirstie Trup (18) walimwagiwa tindikali katika maeneo ya Mji Mkongwe, Zanzibar na vijana wawili waliokuwa wakiendesha pikipiki aina ya Vespa.Waingereza hao walisafirishwa siku tatu baadaye kurudi kwao Uingereza kwa ajili ya matibabu.
Utetezi wa Serikali
Siku tano baada ya tukio la Waingereza hao
kumwagiwa tindikali, Serikali kupitia vyombo vyake vya uchunguzi
iliwataka wananchi kuisaidia kuwafichua na kutoa ushahidi wa uhalifu huo
kwani ni vigumu kuwabaini wahusika.
Kauli hiyo ilitolewa kwa pamoja jana na Mkuu wa
Jeshi la Polisi nchini, IGP Said Mwema, Mkemia Mkuu wa Serikali, Profesa
Samwel Manyele na Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Serikali (DPP) Eliezer
Feleshi, katika mkutano wao na waandishi wa habari, uliolenga kueleza
mikakati ya kupambana na matumizi yasiyo sahihi ya tindikali nchini.
“Mkemia Mkuu, Polisi hawawezi kubaini matukio haya bila ushirikiano wa wananchi kwani Tanzania ni nchi kubwa na ina watu zaidi ya milioni 45. Watu wanaingiza tindikali lakini wapo ambao wanatumia tindikali hiyo kwa matumizi haramu,” alisema IGP Mwema.
Amesema tindikali inaweza kutolewa kwa ajili ya shughuli za viwandani, maabara na usafirishaji na kwamba watu wanapotaka kuitumia kwa ajili ya kufanya uovu wanaweza kugundulika kupitia kwa taarifa zitakazotolewa na wananchi, kwa sababu wanakuwa wamezungukwa na jamii ya watu mbalimbali.
Matukio mengine
Tukio lingine lililoshtua ni lile la bilionea Said
Mohamed Saad ambaye ni mmiliki wa maduka ya Home Shopping Centre,
kumwagiwa tindikali mwanzoni mwa mwezi Agosti.
Said anaendelea na matibabu nchini Afrika Kusini na inaelezwa kuathirika vibaya usoni, mikononi na kifuani.
Alimwagiwa tindikali Julai 19, mwaka huu akiwa kwenye moja ya maduka yake katika Jengo la Msasani Mall, Dar es Salaam.
Taarifa za siku ya tukio zilibainisha kuwa Said alikuwa akizungumza na mfanyakazi wake muda wa saa moja jioni ndipo akatokea kijana mrefu, mwembamba ambaye alimmwagia kimiminika kinachosadikiwa kuwa ni tindikali.
Ilibainishwa kwamba mfanyakazi huyo wa Said, Hassan Ahmad naye alijeruhiwa kidogo katika purukushani hiyo lakini alipopelekwa Hospitali ya Ami Wellness Centre, alitibiwa na kuruhusiwa huku bosi wake akipelekwa Afrika Kusini usiku huohuo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Camilius Wambura anasema matukio ya kutumia pikipiki yanaonyesha kupangwa hivyo inakuwa vigumu kuwabaini wahalifu mapema.
Tukio hilo linafanana na lile lililotokea Septemba 8, mwaka huu ambapo mfanyabiashara wa vifaa vya ujenzi, Christian Msema wa Mburahati jijini Dar es Salaam, alimwagiwa kemikali hiyo na watu waliokuwa kwenye pikipiki ya matairi matatu.
Msema maarufu kama Mnyalu amelihusisha tukio hilo lilitokea jioni ya Jumamosi Septemba 8 na mgogoro wa eneo la wazi ambapo yeye alikuwa akipinga mfanyabiashara mmoja (jina linahifadhiwa) kulitumia kuegesha magari yake.
Akizungumza kwa shida katika hospitali ya Taifa ya
Muhimbili alikolazwa anakiri kuwa mstari wa mbele kupinga eneo hilo
kutumiwa kinyume na sheria.
“Awali vijana wasio na ajira waliomba eneo hilo ili walitumie
kwa mradi wa kuegesha magari, wakaandika barua, lakini Serikali ya mtaa
ikakataa ikisema hilo ni eneo la kazi. Hiyo ilikuwa mwezi Oktoba mwaka
jana, ilipofika Novemva, tukaona malori yanaegeshwa pale. Tulipofuatilia
tukaambiwa ni mwenyekiti wa mtaa ameruhusu,” anasema na kuongeza:
“Tukajiorodhesha wana mtaa tukafika kama watu 60 na mimi nikawa mwenyekiti wao, tukapeleka barua yetu kwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni ambaye aliipeleka kwa ofisa wa mipango miji.”
Ameongeza kuwa ofisi ya mipango miji ya Kinondoni
ilisema hilo ni eneo lililotengwa kwa ajili ya ujenzi wa shule ya
sekondari hivyo ikaagizwa kuwa magari hayo yaondolewe.
“Kampuni iliyopewa tenda ya kuondoa yale magari ilifanya kazi bila kutoa notisi, ndipo yule mwenye magari akaenda kulalamika kwa mkuu wa mkoa. Malalamiko yakafika kwa Mkurugenzi ambaye aliagiza kampuni hiyo irejeshe hayo magari ili utaratibu ufuatwe,” alisema. Aliendelea kusema kuwa yule mfanyabiashara aliendelea kukaidi kwa kuongeza magari mengine kwenye uwanja huo hadi yalipokuja kuondolewa kwa nguvu.
Msema alisema wakati mvutano huo ukiendelea, aliwahi kukutana na mlinzi wa mfanyabiashara huyo ambaye alimtahadharisha kuwa harakati zake hizo zitamponza kwani anafuatiliwa.
“Mimi sikukata tamaa kwani lile ni eneo la umma kwa nini mtu ang’ang’anie? Lakini watu wengi walinitahadharisha kuwa yule jamaa ananifuatilia, ndiyo maana siku ile ya tukio kuna bajaji kumbe ilikuwa inanifuatilia kwa muda mrefu,” anasema.
Mwenyekiti wa mtaa wa Mburahati, Tungaraza amekanusha kuwepo kwa mgogoro huo huku akimtaka mwandishi afike ofisini kwake kwanza. Matukio hayo yameanza muda mrefu na wakati mwingine yamehusishwa na chuki za kisiasa.
Baadhi ya wananchi wanashauri Serikali kuwa imara na tindikali hasa katika chaguzi zijazo, kwani tindikali ni rahisi kuibeba.
source: mwananchi
No comments:
Post a Comment