Wakati Rais Jakaya Kikwete akisema
Serikali yake haitawatetea Watanzania wanaokamatwa wakijishughulisha na
biashara ya dawa za kulevya, Watanzania wawili Agnes Masongange na
mwenzake, Melisa Edward jana walinyimwa dhamana na Mahakama Kuu ya North
Gauteng katika kesi ya dawa ya kukamatwa na dawa hizo
Rais Kikwete alisema Serikali yake
itakabiliana na biashara hiyo kwa nguvu zote kwa kuwa ni haramu na ni
kinyume na sheria za nchi.
Alisema hayo juzi usiku alipokutana na
Watanzania wanaoishi katika Jimbo la California, Marekani..."Serikali
yangu haitawatetea watu wanaojishughulisha na ubebaji wa dawa za kulevya
na kusafirisha nje ya nchi. Hii ni biashara haramu na inavunja sheria
za nchi yetu."
Masogange na Melisa walikamatwa Julai
2, mwaka huu kwenye Uwanja wa Oliver Tambo, Afrika Kusini wakituhumiwa
kusafirisha kilo 150 za dawa za kulevya zenye thamani ya Sh6 bilioni.
Aidha, amesema hayo siku chache baada
ya meli ya mizigo ya Gold Star iliyosajiliwa nchini kukamatwa na maofisa
forodha na askari wa doria wa Italia katika Pwani ya Sicily, Bahari ya
Mediterranean ikiwa na tani 30 ya dawa ya kulevya aina ya bangi zenye
thamani ya Paundi za Uingereza 50 milioni (Sh125 bilioni).
Pia, Agosti 31, mwaka huu,
mshambuliaji nyota wa zamani wa timu ya soka ya Simba na Taifa, Joseph
Kaniki 'Golota' na bondia Mkwanda Matumla walikamatwa kwenye Uwanja wa
Ndege wa Bole, Addis Ababa walipokuwa wakijiandaa kwenda Paris, Ufaransa
wakituhumiwa kubeba dawa za kulevya.
Juzi, Rais Kikwete alisema ni wajibu
wa Watanzania wanaoishi ughaibuni kuwa raia wema, kufuata na kuheshimu
sheria katika nchi wanazoishi kwa sababu wakizivunja, Serikali yake
haitawatetea.
"Ukikamatwa na dawa za kulevya
hatukutetei kwa sababu hata sheria za nchi yetu zinazuia biashara hiyo.
Sisi hatuwezi kuendelea kuwa na sifa ya kufanya biashara za ovyoovyo
kiasi hicho. Serikali itawatetea Watanzania wanaoishi nchi za nje ikiwa
wataonewa. Lakini ukifanya biashara ya dawa ya kulevya au kubaka watu
hatukutetei kamwe," alisema.
Masogange, Melisa wakwama dhamana
Masogange na mwenzake Melisa jana
walikosa dhamana baada ya kupandishwa kizimbani katika Mahakama Kuu ya
North Gauteng, Afrika Kusini kujibu mashtaka ya kusafirisha dawa
zinazodaiwa kutumika kutengenezea dawa aina ya amphetamine (maarufu kama
tik).
Taarifa kutoka Mahakama hiyo zinaeleza
kuwa, Masogange na Melissa walirudishwa rumande na kesi yao
itasikilizwa tena Novemba mwaka huu.
Mkuu wa Kitengo cha Kudhibiti Dawa za
Kulevya cha Polisi nchini, Kamanda Godfrey Nzowa alithibitisha kuwa
watuhumiwa hao walipanda kizimbani jana kujibu mashtaka yanayowakabili
ya kusafirisha dawa za kulevya na kwamba wamerudishwa rumande hadi
Novemba.
Awahoji akina Masogange Nzowa alisema alikwenda Afrika Kusini
kuwahoji Melisa na Masogange kabla ya kupandishwa kizimbani lakini
alisema hawakumpa ushirikiano.
Kamanda huyo alisema imebainika kuwa
mzigo walioubeba wasichana hao haukuwa dawa halisi za kulevya, bali
kemikali zinazotumika kutengeneza dawa zinazoitwa amphetamine. Kutokana
na madai hayo, Nzowa alisema wanaweza kupewa dhamana na kesi yao
kuendelea kusikilizwa nchini baada ya yeye (Nzowa) kushauriana na
Kitengo cha Dawa za Kulevya cha Afrika Kusini.
Alisema, inawezekana watuhumiwa wakapewa hukumu nyepesi kidogo kutokana na kosa hilo.
Chanzo:Mwananchi
No comments:
Post a Comment