Ndugu zangu,
Hivi Watanzania ni watu wenye kupenda ' Vurugu Mechi'? Maana, magazetini leo habari kubwa na picha ni ' vurugu mechi' bungeni.
Ni picha ya aibu. Shabaan Robert
alipata kuandika, tena miaka 50 iliyopita, kuwa isifike mahali wazungu
wakarudi wakatukuta bado hatujamulikiwa na nuru, kwamba Waafrika bado
tunapigana hadharani!(P.T)
Shaabani Robert alikuwa na maana ya kuwa hayo ni mambo ya kishenzi na hayapaswi kufanywa na watu wastaarabu.
Na afadhali wasomaji wa magazeti kwa
lugha ya Kizungu leo hawakuonyeshwa picha za sisi Waafrika tulivyo hata
baada ya miaka 50 ya uhuru. The Citizen na Daily News wao walipamba sura
za mbele za magazeti yao kwa habari kubwa ya JK na PK ( Kikwete na
Kagame) walivyokutana Kampala jana.
Habari za aibu ya bungeni zilipewa
nafasi ya pili tena bila picha. Pongezi kwa wahariri wa magazeti hayo
kwa kutufichia aibu yetu.
Na Daily News wao wametoka na kichwa kizuri cha habari; " MPs, police in a shameful flurry of fists"
Kwa kweli ni aibu. Kwa nini tumefika
mahali hapa? Kwamba watu wazima Bungeni wasitumie mazungumzo katika
kumaliza tofauti zinazojitokeza badala ya kushikana mashati, kuburuzana
na hata kupigana makonde.
Na mitaani leo kona nyingi nimewasikia
watu wakizungumzia ' Senema ya jana Bungeni'. Na kilichowavutia sana ni
hiyo ' Vurugu mechi' na hususan masumbwi na kupigana ngwala!
Na wengi hawakujikita kwenye nini hasa
msingi wa vurugu mechi hiyo. Wamefurahishwa tu na ' Vurugu mechi',
basi! Na hakika, magazeti yaliyopambwa na picha za vurugu mechi ile leo
yameuzwa ' kama njugu'.
Na bwana mmoja mtaani nimemsikia akitamka; " Sasa tunataka kuona masumbwi ya wabunge wa upinzani dhidi ya wa CCM!"
Tumefika pabaya, kwamba habari za aibu
za watu wazima kupigana na kushikana mashati hadharani ndizo
zinazowavutia wasomaji watu wazima!
Hivi watoto wetu tunawafundisha nini?
Kwamba katika nchi hii unaweza kuwa
maarufu na hata ukafika mbali kwa kurusha ngumi badala ya kuwa na uwezo
wa kujenga hoja kwa kutumia kichwa, mdomo au kalamu.
Si tunajua, tuna hata mwanasiasa
katika nchi hii aliyerumshia ngumi mwanahabari hadharani, na tangu siku
hiyo akajipatia umaarufu na hata kupewa jina la ' Tyson'!
Ndio, ni katika nchi zetu hizi za hovyo hovyo ambapo ngumi zinaweza kukupeleka hata IKULU!
Usiku Mwema.
Maggid.
Dar es Salaam.
Dar es Salaam.
No comments:
Post a Comment