Simba imekata mzizi wa fitina kwa kuichapa
Mtibwa Sugar kwa mabao 2-0, huku mabingwa watetezi Yanga, Azam
wakilazimisha sare ugenini dhidi Mbeya City na Kagera Sugar.
Kiungo Henry Joseph na mshambuliaji Betram Mwombeki waliingia wakitokea benchi na kuifungia Simba mabao hayo mawili muhimu katika kipindi cha pili. Mabingwa watetezi Yanga, waliokolewa na bao la Didier Kavumbagu wakilazimisha sare 1-1 na Mbeya City waliopanda daraja msimu huu.
JKT Ruvu imeendelea kung’ang’ania kileleni baada ya kuichapa Ashanti United kwa bao 1-0 na kuweka rekodi ya kushinda mechi tatu mfululizo.
MBEYA
Mechi hiyo ilitawaliwa na vurugu na vituko vingi
kabla ya kuanza kwake baada ya basi lililobeba wachezaji wa Yanga
kushambuliwa kwa mawe, chupa za maji, bia na mashabiki wa Mbeya City
wakati likiingia uwanjani na kusababisha kuvunja kioo cha dirisha la
dereva.
Dakika chache kabla ya mechi kuanza meneja wa Uwanja wa Sokoine, Modest Mwaluka aliokota mayai matatu katikati ya uwanja.
Mwigane Yahya ndiye aliamsha shangwe za mashabiki wa Mbeya baada ya kuifungia Mbeya City bao la kuongoza katika dakika 49 akiunganisha krosi ya Mazanda.
Baada ya bao hilo Yanga, iliwapumzisha Nizar na Bahanuzi na kuwaingiza Oscar na Jerry Tegete mabadiliko yaliyozaa matunda kwani dakika ya 71 walisawazisha bao hilo kupitia Kavumbagu akimalizia krosi ya Tegete.
Dar es Salaam
Kocha wa Simba, Abdallah Kibaden aliwapumzisha
Said Khamis, Twaha Ibrahimu na kuwaingiza Henry Joseph na Betram
Mwombeki ili kuimarisha safu ya kiungo iliyoonekana kuzidiwa nguvu na
vijana wa Mtibwa.
Mabadiliko hayo yalizaa faida katika dakika ya 67, pale Joseph Shindika alipoipatia Simba bao la kuongoza akiunganisha kwa kichwa krosi ya Amri Kiemba.
Dakika ya 90, Mwombeki aliwainua mashabiki wa
Simba kwa kufunga bao la pili akimalizia vizuri pasi ya Ramadhani
Singano ambaye kabla aligongeana vyema na Joseph.
Safari ya Ashanti United kurudi ilipotoka
imezidi kushika kasi baada ya jana kukubali kipigo cha bao 1-0 kutoka
kwa JKT Ruvu, goli pekee la Amos Mgisa.
Azam wameendelea na mwendo wa kusuasua baada ya kulazimisha sare ya 1-1 na Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Kaitaba.
Mshambuliaji Temi Felix aliwainua mashabiki wa Kagera Sugar,ambapo kiungo Hamisi Mcha aliisawazishia Azam. Katika michezo mingine Tanga, Coastal Union ilitoka sare 0-0 na Prisonsi.
Arusha wenyeji Oljoro JKT walilazimishwa sare 1 -1 na Rhino Rangers, wageni Rhino walipata bao la kuongoza kupitia Saad Kipanga kabla ya Amiry Omary kuisawazishia Oljoro katika dakika 27.
Vilevile Ruvu Shooting ilichapa Mgambo JKT kwa bao 1-0 shukrani k wa bao Elias Maguli.
Imeandaliwa na Vicky Kimaro, Jessica Nangawe (Dar), Msafiri Sanjito (Kibaha), William Paul (Kagera), Mosses Mashalla (Arusha), Doris Maliyaga (Mbeya) Salim
Mohamed (Tanga).
source: Mwananchi
source: Mwananchi
No comments:
Post a Comment