NIMESEMA kwamba kila tendo tunalofanya
huzaa tendo-rejea, na kwamba kuku tuliowaachia asubuhi ni wale wale wanaorejea
nyumbani mwisho wa siku. Kwa hiyo tusishangae.
Tumezembea sana kuwekeza katika elimu
ya taifa letu, tukaichukulia elimu kama kitu cha mzaha kinachoweza kuongozwa na
yeyote miongoni mwetu. Tumeifanya wizara inayosimamia elimu isiwe na jina
linalotambulika, tukiibadilisha majina kila tunapounda serikali, ikiunganishwa
na hiki leo na kile kesho.
Walimu wanalalamikia mishahara yao
midogo na isiyolipwa kwa wakati, mazingira mabovu na ukosefu wa vitendea kazi,
tunawaona ni wakorofi, wenye uroho wa fedha, wasiokuwa wazalendo. Tunawatolea
vitisho mpaka wanalazimika kuacha mgomo wao, wanarudi kufundisha shingo-upande.
Wala hakuna asiyejua kwamba walimu
waliolazimishwa kurudi madarasani kwa nguvu za dola hawatafundisha kama
wanavyotakiwa kufundisha. Tunajua kwamba walimu wamerudi darasani
shingo-upande, tunajua kwamba hawaridhiki kuifanya kazi yao katika mazingira
yale, tunajua kwamba wataifanya “bora liende,’ lakini bado tunawaachia
waendelee kuwalea watoto wetu na wala hatuonyeshi kuwa na wasiwasi. La msingi
kwetu ni kwamba hakuna mgomo tena, walimu wamo darasani na watoto (eti)
wanasoma.
Wakati haya yanaendelea tunawasikia na
kuwaona wanasiasa wetu wakiendelea kujiongezea malipo haramu kila wanapohisi
haja ya kufidia matumizi yao yasiyo na kikomo. Mwenye akili timamu angeweza
kujiuliza, hasa hawa wanasiasa tunawalipa kwa kazi gani wanayotufanyia? Je,
kati ya mwalimu na mwanasiasa nani hasa ni muhimu kwa taifa hili?
Lakini tunaendelea kama tulivyo: Walimu
wanadharauliwa, hawalipwi stahili yao, wakigoma tunawatisha, “wanasiasa”
wababaishaji walio bungeni na kwingineko wanalipwa wasivyostahili, watoto
wanapita shuleni kama wanaotembea usingizini, tunaendelea kujenga taifa la
wajinga.
Kuku wetu wanaanza kurudi nyumbani
magharibi pale tunapopata matokeo ya kutia hofu ya mitihani ya kidato cha nne.
Karibu wanafunzi wote wameshindwa, kisha tunatahayuri, tunatapatapa,
tunataharuki kutafuta kisa na mkasa. Hivi hatukujua kwamba tuliwekeza katika
ujinga tangu mwanzo?
Halafu tunaongeza vichekesho vingine
visivyochekesha, mzaha na upuuzi wa hali ya chini kabisa. Eti kuna watu
wanaodhani kwamba watoto wakichapwa viboko watapata akili hata kama hawana
walimu wenye sifa, na hata kama wazazi wao ni wapuuzi wa aina niliyoieleza.
Tunaiua elimu hivi hivi tukiona.
Tunajua, ama tunatakiwa tujue, kwamba matendo yetu wenyewe ndiyo
yaliyotufikisha katika matokeo haya ya kutisha, tunatakiwa tujue kwamba
tumelinyang’anya taifa letu mustakabali wake kwa kuwanyima watoto wetu elimu
iliyo bora, lakini suluhisho letu ni viboko.
Kama si viboko ni kurejea matokeo na
kuyapaka wanja ili yapendeze, tunapunguza alama za ufaulu, kisha tunatangaza
kwamba kile tulichokitangaza awali kama kushindwa kubaya kwa watoto wetu,
kihalisia ni ufaulu mkubwa uliozidi hata miaka iliyotangulia.
Sasa huu ndio ule ujuha ambao aliueleza
rafiki yangu marehemu Seithy Chachage, aliyeuita “collective imbecilisation,”
ama kufanywa majuha kihalaiki. Jambo la kushangaza ni kwamba, kwa sababu hakuna
mgomo tena, hakuna tatizo, na maisha yetu yanaendelea “kama kawaida.”
Lakini tatizo bado lipo, tena kubwa,
ila linakuja katika sura nyingine. Tumo ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki,
tena kwa hiari yetu, si kwa kulazimishwa na mtu yeyote. Katika mikataba
tunayosaini imo mikataba inayotutaka tufungue milango katika maeneo kadhaa ili
kuruhusu majirani zetu waingie nchini mwetu, na bidhaa zao, na huduma zao pia,
sawa sawa na vile ambavyo na wao wanatakiwa wafungue mipaka yao ili nasi tuweze
kuingia kwao.
Tukifika hapo tunagota, kwa sababu
tunagundua (kama vile ndiyo tunashituka usingizini) kwamba wale kuku wetu
wanarejea nyumbani. Vijana wetu wanagundulika kwamba hawana elimu ya ubora wa
kuweza kushindana na wenzao kutoka nchi jirani. Suluhisho linakuwa ni kuzuia au
kupiga breki dhidi ya muendelezo wa ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa sababu
tunayo hofu kwamba majirani zetu watatuzidi kete.
Suluhisho letu hatulioni katika kuketi
chini na kujiuliza kwa dhati ni nini tunatakiwa kufanya kuhusu elimu yetu
iliyokufa, hapana; suluhisho tunaliona katika kuzuia maendeleo ya Jumuiya kwa
kukataa wanachopendekeza bila sisi kusema tunataka nini, kimsingi kwa sababu
hatujui tunachotaka.
Tunajikuta katika kona ya ajabu. Kutoka
katika Jumuiya ya Afrika Mashariki hatutoki; kushiriki katika muendelezo wa
Jumuiya kama tulivyokubaliana hatushiriki; hatusemi nini hatutaki na kusema
nini tunataka; tunaonekana kama kikwazo kwa wenzetu.
Kuku wetu wanazidi kurudi nyumbani.
Wenzetu wanaona kama kikwazo hawako tayari kutusubiri hadi tuamue kama tunataka
kwenda kushoto, kulia ama nyuma; wanaamua kwenda zao huku wakituambia kwamba
tunaweza kujiunga nao tutakapokuwa tayari. Sisi tunashangaa, tunataka watuambie
wanapokutana wanajadili nini, na kwa nini hawatushirikishi. Ni kuku wetu wote
hawa.
Tunapozungumza masuala ya Afrika
Mashariki tungetakiwa turejeee nyuma kidogo tu, wala si sana. Tungerejea katika
malalamiko ya walimu wetu, na migomo yao inayozimwa kwa vitisho na matumizi ya
mabavu, tungetambua kwamba matatizo tunayoyashuhudia leo hii kati yetu na ndugu
zetu wa Afrika Mashariki yanatokana, kwa kiasi fulani, na jinsi tunavyowatendea
walimu wetu.
Hivyo ndivyo kuku wetu wanavyorudi
nyumbani, halafu tunawatazama kama vile hatuwajui.
Source:www.raiamwema.co.tz:
Jenerali Ulimwengu
No comments:
Post a Comment