KATIKA toleo lililopita nilijadili,
miongoni mwa mambo mengine, hatari ya kuvunjika kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki
endapo Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi zitaendelea na tabia ya sasa ya
kuitenga Tanzania – tabia ambayo niliihusisha na kuharibika, kwa hivi karibuni,
kwa mahusiano kati ya Rais Kagame na Rais Kikwete.
Tafakauri yangu hiyo ilikaribisha sms
na emails nyingi kutoka kwa wasomaji wangu, lakini iliyonifikirisha
zaidi ni ile ya msomaji wangu mwenye simu Na. 0713 228000 ambaye
alihalalisha Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi kukutana zenyewe bila Tanzania
kuharakisha mipango yao ya maendeleo.
“Ndugu yangu Mbwambo, wa kulaumu ni
Kikwete mwenyewe. Nadhani wenzake walishamuona hana maono ya mbali. Wakati
wenzake wanakutana pamoja kuweka mikakati ya kikanda, yeye yuko nje ya nchi
(Austria) akitembea.”
Nasema ujumbe huo ulinifikirisha upya
kwa kuwa huko nyuma nilipata kujadili katika safu hii tabia hii ya Rais Kikwete
kuzifurahia sana safari za nje; badala ya kukita juhudi zake katika kuisaidia
nchi kujenga misingi ya kujitegemea.
Sina hakika mpaka sasa safari zake za nje zimefikia ngapi na zimegharimu kiasi gani cha mapesa ya walipakodi (hata jamiiforums naona sasa imechoka kuendelea kuorodhesha idadi yake), lakini nikumbushe tu kwamba kabla ya kwenda Austria alikuwa Malawi kwenye mkutano wa SADC na baada ya kurejea Austria alikwenda Kampala.
Kwa ufupi, mwezi haushi bila Rais
Kikwete kusafiri nje. Ikizingatiwa kuwa safari hizi zinachosha (jet-lag), na
hasa zile za masafa marefu za kukatisha bahari, huwa najiuliuza kama arudipo
anakuwa na nguvu za kutosha kupitia kwa makini mafaili nyeti ofisini kwake, na
hata kufuatilia masuala nyeti kadha wa kadha.
Nayasema haya yote nikitambua wazi
umuhimu wa kiongozi wa nchi kusafiri nje – kuvutia wawekezaji, kuhudhuria
mikutano muhimu ya nje nk. Nayasema haya nikitambua pia kwamba Kikwete si
kiongozi wa kwanza duniani kufanya safari nyingi za nje.
Kwa hakika, kumbukumbu zinatuonyesha
kwamba tabia hii ya wakuu wa nchi duniani na viongozi wengine kusafiri nje kwa
safari za kiserikali ilianza katika karne ya 20. Kinara wa kwanza alikuwa Rais
Woodrow wa Marekani ambaye alisafiri kwa meli na kukaa Ulaya kwa miezi saba
mara baada ya vita vya kwanza vya dunia kumalizika.
Rekodi zinaonyesha kwamba kiongozi
barani Ulaya anayeshikilia nafasi ya kwanza kwa kusafiri sana duniani ni Malkia
Elizabeth wa Pili wa Uingereza ambaye katika miaka yake 61 ya umalia amefanya
ziara za nje za kiserikali 261.
Viongozi wengine katika miaka ya
karibuni walioingia katika orodha ya waliosafiri sana safari za kiserikali ni
pamoja na Hillary Clinton ambaye katika miaka yake minne ya kuwa Waziri wa
Mambo ya Nje wa Marekani alisafiri katika nchi 100, na hivyo kuvunja rekodi ya
aliyemtangulia, Madelaine Albright, aliyesafiri katika nchi 96.
Tusisahau kuwa mifano yote hiyo ni ya
mataifa tajiri ambayo angalau yana fedha za kutosha kuhalalisha safari hizo za
nje; lakini vipi kwa bara masikini la Afrika? Hakika, kope hupepesa anapotokea
kiongozi wa Kiafrika kushabikia sana safari hizo za nje zinazogharimiwa kwa
pesa za walipakodi!
Kama nilivyosema mwanzo, sina hakika
kuwa Rais wetu Kikwete amefikisha idadi ya safari ngapi za nje, na pia sina
takwimu za wenzake wa Afrika Mashariki - kina Kagame, Museveni, Nkurunzinza
(achana na Uhuru ambaye kaupata urais majuzi tu) ili kulinganisha; maana
takwimu katika Afrika ni tatizo jingine kubwa linalotusumbua.
Hata hivyo, angalau hakuna ubishi
kwamba katika Afrika rekodi inashikiliwa na mtawala wa zamani wa Nigeria,
Olusegun Obasanjo. Ni maoni yangu kwamba kama Kikwete hatapunguza kasi yake ya
sasa ya kusafiri nje, anaweza kuingia kwenye ‘ligi aliyocheza’ Obasanjo na anayoendelea
kuicheza hata sasa ingawa ameshaachia urais!
Rekodi zinaonyesha kuwa hadi Mei 29,
2007 wakati anakabidhi urais kwa rais mpya wa Nigeria, Obasanjo alikuwa
amefanya safari za nje ya nchi hiyo zinazofikia 400! Hebu fikiria; safari 400
zinazolipiwa kwa fedha za walipakodi kwa kipindi kifupi tu cha utawala wake wa
miaka minane (1999 -2007)!
Lakini huyo ndiye Obasanjo. Unaweza
kusema kuwa ana ‘ugonjwa’ wa kupenda kusafiri nje ya nchi; maana tabia hiyo
anaiendeleza hata sasa ingawa sio tena mkuu wa nchi.
Kuna utani, hivi sasa, barani Afrika,
kwamba kama una ka-semina au ka-mkutano kako sehemu yoyote ile Afrika na
unataka Obasanjo akafungue au akafunge kama mgeni rasmi, unachotakiwa kufanya
ni kumtumia tu tiketi ya ndege na kumpangia hoteli nzuri ya kukaa – atakubali
kuja!
Vyovyote vile; Obasanjo huwajibu
wanaomshutumu kuwa alipenda mno kusafiri nje ya nchi alipokuwa rais kwamba,
kama si safari zake hizo Nigeria isingekuwa ilivyo leo. Yaani, anahusisha kukua
kwa uchumi wa Nigeria na safari zake hizo!
Sidhani kama msomaji wangu atapata
taabu kukumbuka kuwa hoja hiyo hiyo ya Obasanjo ndiyo inayotumiwa na Rais wetu
Kikwete kuwajibu kina sisi tunaolalamika kuwa anapenda sana kusafiri nje kuomba
misaada badala ya kutumia muda wake mwingi hapa nchini kutujengea uwezo na
utamaduni wa kujitegemea.
Na hiyo inanikumbusha moja ya kauli za
Kikwete zenye utata (ukakasi) aliyoitoa kwenye mkutano wa kampeni ya urais,
Oktoba 2010, mjini Mbeya. Kauli hiyo ni ile aliyoitoa kuwajibu wanaomshutumu
kwamba anatumia mapesa mengi ya walipa kodi kufanya ziara nyingi za nje zisizo
na ulazima.
Alisema maneno mengi kwenye mkutano huo
kuhalalisha ziara hizo, lakini yaliyoniacha hoi ni haya: “Mimi nakwenda kule
(Ulaya na Marekani) kuhemea. Nikirudi, narudi na vibaba.”
Kama nilivyoandika kwenye safu hii
wakati huo (2010), ningemwelewa Kikwete kama angeueleza umati ule kwa hali ya
kusikitisha kwamba sisi Watanzania tunamwangusha kwa sababu hatuchapi kazi vya
kutosha; kiasi cha kufikia hatua ya kujitegemea, na hivyo tunamfanya
ajidhalilishe kwa kwenda Ulaya na Marekani kuombaomba hata mambo ambayo
tungeyamudu wenyewe kujitafutia.
Ningemwelewa Kikwete kama angeielezea
hali ile kwa uchungu na kwa masikitiko, na hata kutisha kwamba hatakubali tena
kwenda Ulaya na Marekani kuombaomba mambo ambayo sisi wenyewe tuna uwezo nayo.
Lakini sivyo alivyofanya kwenye hotuba
hiyo ya Mbeya, au hata sasa anapokosolewa kuhusu ziara hizo za nje. Hoja zake
za utetezi anazitoa katika namna inayoonyesha kuwa anazifurahia ziara hizo za
nje za kuomba misaada.
Na hiyo ndiyo inayonitia shaka kwamba
labda naye ana kale ‘ka-gonjwa’ ka kupenda kusafiri nje kanakomsumbua
Obasanjo hata sasa miaka sita baada ya kuuacha urais! Kama naye ana ‘ka-gonjwa’
hako, basi, tutaendelea kumwona akisafiri sana Ulaya na Marekani hata baada ya
kuuacha urais mwaka 2015!
Nikumbushe tena kwamba safari hizo za
kuomba misaada na mikopo nje ya nchi zina faida, lakini sio faida kubwa
kulinganisha na ile ya kuijengea nchi uwezo na utamaduni wa kujitegemea
yenyewe. Tujiulize, je; kuna nchi dunia iliyopata kuendelea na kuondokana na
umasikini kwa kutegemea misaada ya nje ya nchi?
Ndugu zangu, kwa sasa, tunaweza
kuikejeli siasa ya Ujamaa ya Mwalimu Nyerere, lakini ni upofu na ujinga
kuitelekeza dhana yake ya Kujitegemea. Tutalia na kusaga meno siku Wazungu
watakapotuchoka kabisa Waafrika.
Na siku hizo za Wazungu kutuchoka
kabisa hazipo mbali. Juzi nilikuwa naangalia televisheni ya BBC wakati
mtangazaji akiwahoji Wajerumani, mjini Berlin, kuhusu kupanda kwa gharama za
maisha. Wengi walizungumza kwa jazba wakiilaumu serikali yao kwa kutoa mapesa
mengi ya walipakodi kusaidia kuinua uchumi wa Ugiriki badala ya kuyabakisha
nyumbani yatatue matatizo yao mengi.
Sasa, kama Wajerumani wanachukizwa na
hatua ya serikali yao kuzisaidia Ugiriki au Hispania ambazo ni majirani na ni
Wazungu wenzao, vipi litakapokuja suala la kusaidia nchi za Kiafrika? Na hisia
hizo za Wajerumani ndizo pia hisia za nchi nyingine za Ulaya.
Kwa mtazamo wangu, hisia hizo za sasa
za Wazungu ni maandiko ukutani kwa watawala wetu…. ni kengele ya uamsho kwa
watawala wetu. Na uamsho wenyewe ni kwamba zama za Waafrika kutegemea misaada
ya Wazungu zimepita.
Tena siku hizi mtawala hahitaji
kusafiri na ndege kuvuka bahari ya Atlantic kuhudhuria mkutano wa kuomba
msaada; maana siku hizi kuna utaalamu wa teknolojia ya kisasa ya kuendesha
mkutano na mtu bila kuonana ana kwa ana - wenyewe wanaiita teleconference.
Sasa, kama kuna utaalamu huo, na
ikizingatiwa kuwa ziara hizo za kuomba misaada zimepitwa na wakati; utitiri huu
wa safari za nje kwa watawala wetu wa nini?
Tafakari.
Source:
www.raiamwema.co.tz: Johnson Mbwambo
No comments:
Post a Comment