WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Thursday, September 19, 2013

Tunapokaribia 2015, JK akumbuke zigo la ahadi


“Wakati wa kampeni nilibezwa sana, lakini sasa ninawaomba walionibeza kufika vijijini na kuangalia ukamilishaji wa ahadi zangu. Nataka waje waone, kwa sasa ninakamilisha usambazaji wa umeme katika vijiji vyote ili kufikia lengo la Watanzania asilimi 30 kufikiwa na nishati hiyo. Hadi 2015 umeme utakuwa umesambaa nchi nzima. Rais Kikwete 

Ahadi ni deni, kumbe isipotimizwa inabaki kuwa deni kwa mhusika
Akiwa ziarani mkoani Mwanza hivi karibuni, Rais Jakaya Kikwete amesema wale wote wanaombeza kuhusu utendaji wake, wataona aibu atakapomaliza muhula wake mwaka 2015.

Kikwete amewananga pia baadhi ya wanaCCM wenzake kwa kushindwa kuyaelezea mafanikio ya Serikali yao.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mradi wa kusambaza umeme katika mikoa ya Mwanza na Geita unaofadhiliwa na Mfuko wa Changamoto za Milenia (MCC), Rais Kikwete alisema:

“Wakati wa kampeni nilibezwa sana, lakini sasa ninawaomba walionibeza kufika vijijini na kuangalia ukamilishaji wa ahadi zangu.

“Nataka waje waone, kwa sasa ninakamilisha usambazaji wa umeme katika vijiji vyote ili kufikia lengo la Watanzania asilimi 30 kufikiwa na nishati hiyo. Hadi 2015 umeme utakuwa umesambaa nchi nzima.
 “La umeme, leo nazindua nataka kuwaeleza walionibeza waje waone sasa ahadi zangu...hayo yote niliyasema kwenye ahadi zangu 2010.”

Mradi huo umegharimu Dola za Marekani 15.54 milioni sawa na Sh24.87 bilioni kwa Mwanza na Geita pekee, fedha ambazo ni asilimia 25 ya Dola za Marekani 62.6 milioni sawa na Sh103.24 bilioni zilizotengwa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi 225 ya upanuzi wa njia za kusambazia umeme katika mikoa kumi nchini.

Rais Kikwete alisema Serikali inajipanga kusambaza umeme na kufikiwa vijiji vyote na kubainisha kuwa mpango huo unakwenda sambamba na uanzishaji wa vyanzo vipya vya umeme ili viweze kuzalisha megawati 3,000 ifikapo mwaka 2015 na kwamba ziada itauzwa nje ya nchi.

Kikwete akawageukia baadhi ya viongozi wa chama chake na kusema kuwa ni dhaifu katika uongozi kwani wameshindwa kueleza mafanikio ya serikali yao ya CCM.

Ahadi za Kikwete 2010-2015
Wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu, Kikwete alitoa zaidi ya ahadi 70 na hadi sasa nyingi hazijatekelezwa. Zifuatazo ni baadhi ya ahadi hizo.

Viwanda
Akiwa jijini Tanga, alitoa ahadi ya kulifanya jiji hilo kuwa la viwanda, hadi sasa hakuna hata dalili kwani baadhi ya viwanda vimeendelea kufa.

Aliahidi pia kuifanya Mtwara kuwa mji wa viwanda. Ndoto hizo ziko mbioni kutimia hasa kutokana na uvumbuzi wa gesi. Tayari, kuna kiwanda cha saruji kimeanza kujengwa.

Vilevile, aliahidi ujenzi wa kwanda cha dawa ya kuua viluilui vya mbu na kuifanya wilaya ya Kibaha kuwa eneo maalumu la viwanda.

Maji
Ahadi nyingine ni ile aliyoitoa wilayani Igunga ya kuufanya mkoa wa Tabora kutumia maji ya Ziwa Victoria. Mradi huo bado unaendelea kutekelezwa.
Aliahidi pia kuvipatia maji vijiji vyote vilivyoko kilomita 15 kutoka kwenye bomba kuu la mradi mkuu wa maji wa Ziwa Victoria - Shinyanga-Kahama.

Kilimo
Kuhusu kilimo, aliahidi kulipa madeni ya Chama Kikuu cha Ushirika Mkoa wa Shinyanga (SHIRECU).

Aliahidi pia kumaliza migogoro ya ardhi nchini na kwamba wakulima wataacha kutumia jembe la mkono na kuwapatia matrekta alipokuwa mkoani Dodoma.
Hadi sasa zaidi ya asilimia 75 ya Watanzania wamejiajiri kwenye kilimo huku asilimia 90 wakitegemea jembe la mkono.

Katika suala la nishati aliahidi kupatikana kwa umeme eneo la Mutukula mkoani Kagera. Umeme huo ni kutoka Uganda.

Aliahidi pia kuiunganisha mikoa ya Kagera, Kigoma, Lindi, Rukwa na Ruvuma katika gridi ya taifa ya umeme ahadi ambayo inaendelea kutekelezwa.
Aliahidi kununua meli kubwa kuliko Mv Bukoba alipokuwa mkoani Kagera. Meli hiyo haijanunuliwa hadi leo, japo mwenyewe ameendelea kusisitiza kuwa atanunua meli mbili.

“Serikali yangu itavunja rekodi ya kusambaza umeme katika vijiji vingi nchini…Tumejenga mtandao wa barabara kwa sasa, hali yetu ya barabara ni bora Afrika Mashariki, tuliahidi meli Bukoba, naomba niwaeleze kuwa zinakuja, tena siyo moja ni meli mbili,” amesema wiki iliyopita alipokuwa jijini Mwanza.
Alipokuwa jijini Mwanza aliahidi kuanzisha benki ndogondogo kwa ajili ya wajasiriamali na Serikali kuvisaidia vyama vya ushirika.

Aliahidi pia kuimarisha usalama Ziwa Victoria na Ziwa Tanganyika kwa kupeleka kikosi maalumu chenye vifaa kupambana na wahalifu.

Akiwa mkoani Mbeya mjini aliahidi kununua meli mpya kubwa Ziwa Nyasa, lakini hadi sasa haijatimizwa.
Aliahidi pia kujenga bandari ya Kasanga alipokuwa mkoani Rukwa.

Elimu
Akiwa Songea, Ruvuma, Kikwete aliahidi kumaliza tatizo la walimu. Hata hivyo, ahadi hii inaonekana kushindikana kutokana na mvutano wa kimasilahi kati ya walimu chini ya chama chao (CWT) kiasi cha kufikishana mahakamani.

Hivi karibuni, Mwenyekiti wa CWT, Gratian Mukoba alisema walimu wanaidai Serikali kiasi cha Sh33 bilioni.

Mbali na madai ya elimu, kumekuwa na anguko kubwa la ufaulu wa wanafunzi. Matokeo ya kidato cha nne ya mwaka 2012 yameonyesha angoko hilo ambapo waliopata daraja sifuri wamefikia zaidi ya asilimia 60.

Afya  
Akiwa Iringa, aliahidi kununua pikipiki za matairi matatu (bajaj)  400 kwa ajili ya kubeba wajawazito hasa vijijini

Aliahidi pia kununua vyandarua viwili kwa kila kaya akiwa mjini Mbeya.

Aliahidi pia kuzipandisha hadhi hospitali maalumu saba nchini kuwa za rufaa ili kuipunguzia mzigo Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MHN). Hiyo ni ahadi ya Hydom mkoani Manyara.

Licha ya kuanza kutekelezwa kwa baadhi ya ahadi katika sekta ya afya, mwaka 2012 umekuwa na matukio ya migomo ya madaktari wakidai nyongeza ya mishahara na posho.

Mgomo huo uliishia kwa aliyekuwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari, Dk Steven Ulimboka kutekwa na kuteswa katika msitu wa Pande nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam.

Huku Kikwete akisisitiza Serikali yake kutohusika na utekaji huo, hakufikia mwafaka na madaktari hao licha ya kutekeleza baadhi ya madai yao.

Miundombinu
Kuhusu miundombinu aliahidi kujenga Uwanja wa Ndege wa Misenyi Mkoani Kagera na kupanua Uwanja wa ndege Bukoba  alipokuwa Bukoba Mjini na alipokuwa Kigoma mjini aliahidi kujenga uwanja mkubwa wa ndege.

Hadi sasa ahadi hiyo inaendelea kutekelezwa. 
Akiwa Same, Kilimanjaro, aliahidi pia kujenga Barabara yenye kiwango cha lami kutoka Same - Kisiwani, Kihurio na kuiunganisha na barabara kuu ya Moshi - Dar es Salaam.

Pia, aliahidi kujenga barabara ya Njombe - Makete kwa kiwango cha lami, urefu wa kilomita 109 akiwa Iringa mjini na kujenga barabara Musoma hadi Mto wa Mbu akiwa Arusha.

Aliahidi pia kujenga barabara ya lami  ya Manyoni, Kigoma Kaliua na Tabora na kuboresha barabara ya Handeni, Kondoa- Singida.  Ahadi hii inaendelea kutekelezwa.

Aliahidi pia kujenga reli mpya kutoka Dar es Salaam mpaka mikoa ya Kanda ya Ziwa. Aliitia akiwa wilayani Nzega mkoani Tabora na bado haijatekelezwa hadi sasa.

Uhasama wa kidini
Akiwa wilayani Musoma, Mkoa wa Mara, Rais Kikwete aliahidi kulinda amani nchini kwa kuzuia chokochoko za kidini, kikabila na kisiasa.

Hata hivyo, katika kipindi hiki, uhasama huo umeongezeka kiasi cha kuwepo kwa vurugu za uchomaji makanisa, misikiti, viongozi wa dini kumwagiwa tindikali na wengine kuuawa kwa risasi.

source: mjengwa blog

No comments:

Post a Comment