Ndugu Zangu,
TUMEKUWA tukitamka; Ukistaajabia ya Mussa , utayaona ya Firauni! Si wengi wenye kuyajua ya Mussa ni yepi na ya Firauni pia.
Jana niliandika, kuwa kusamehe ni jambo lililo bora kabisa kwa mwanadamu kulifanya kwa mwanadamu mwenzake.
Na hakika, wanadamu sisi ni viumbe wa
ajabu, maana, huwa tuna kawaida ya kutaka kutatua matatizo yetu kwa
namna tunavyotaka sisi yatatuliwe. Tunapoomba ushauri huwa tumeshakuwa
na majibu tayari. Unapokuja ushauri tofauti na matarajio yetu huwa
wepesi sana wa kuung'aka.
Na hapa kuna simulizi niliyopata
kuipokea. Kuwa alipata kutokea bwana mmoja. Yeye na mkewe walisubiri kwa
miaka mingi kupata mtoto. Ikafika siku mkewe akatunga mimba. Na
katikati ya kuilea mimba hiyo, bwana yule akapata safari. Naam.
Akasafiri kwenda mbali. Nyumbani kamwacha mkewe mjamzito.
Huku nyuma, mke akapata maumivu.
Mganga akamwambia; ili mimba isalimike, basi, ni sharti ale maini ya
mbuzi, na afanye hivyo kila anapopata mimba.
Nyumbani hakukuwa na mbuzi wa kuchinja. Mama yule akaenda kwa ndugu wa mumewe mwenye zizi la mbuzi. Akamweleza shida yake.
Bwana yule mfuga mbuzi akakataa
katakata. Kuwa hawezi kuchinja mbuzi wake kwa ajili ya kupata maini ya
tiba tu. Mama mjamzito akarudi nyumbani akiwa mnyonge. Na mimba ile
ikaharibika.
Mume aliporudi akasimuliwa na mkewe.
Hakuamini masikio yake. Iweje nduguye amfanyie hivyo? Alijiuliza.
Akafunga safari mpaka kwa Mussa kuomba ushauri.
Alipofika kwa Mussa akasimulia kisa
chake. Mussa alimsikiliza kwa makini. Na kwa vile aliombwa kutoa
ushauri, basi, Mussa akamwambia; " Hayo yameshatokea, msamehe nduguyo!"
Bwana yule akaushangaa sana ushauri wa
Mussa. Kwamba amsamehe tu mtu aliyesababisha mimba ya mkewe iharibike!
Basi, akafunga safari hadi kwa Firauni kupata ushauri wake. Firauni naye
akasikiliza kwa makini kisa chote.
Na kwa vile aliombwa kutoa ushauri, basi, akatamka; " E bwana ee, mimi naona umsamehe tu nduguyo!"
Bwana yule akaupinga ushauri ule.
Akamtaka Firauni aje na ushauri ulio na busara zaidi. Basi, kwa vile
Firauni aliombwa aje na ushauri tofauti na wa mwanzo, naye akatamka;
" Basi, mimi naona ni vema ukamkabidhi
mkeo kwa nduguyo aliyekataa kumchinja mbuzi ili maini ya tiba
yapatikane. Na akae na mkeo hadi atakapompa mimba. Na kwa vile mimba
itakuwa ya kwake, basi, nduguyo atalazimika kumchinja mbuzi ili
ipatikane tiba. Na mtoto akizaliwa, we nenda kamchukue mkeo na mtoto!"
Naam, ndio hayo ya kustaajabia ya
Mussa na kuyaona ya Firauni! Na siye tuliokulia pwani mtu akikwambia; "
Acha Ufirauni!" Basi, ujue amekasirika.
Ndio, na hata katika jamii yetu, na
hususan kwenye fikra zetu, kuna mahali ambapo akina Mussa Na Firauni
wamechangia katika kutufikisha tulipo sasa. Na hili nitalijadili zaidi
huko twendako.
Maana, mara nyingi, kama wanadamu, makosa tuyafanyao hutokana na makosa ya wengine. Tunachofanya ni kuyarudia makosa.
Je, unafanyaje pale kipofu
anapokuvamia na kukusababishia maumivu makali? Jibu; Utakasirika kwa
sababu ya maumivu uliyoyapata. Hiyo ni hali ya kibinadamu.
Lakini, ukiamua kulipiza kisasi, kwa wewe kujitoboa macho na kumvamia kipofu, basi, hapo utakuwa umetenda lisilo na busara.
Ni Neno la Leo.Tafakari!
Maggid
Iringa,
Iringa,
No comments:
Post a Comment