Hivi karibuni
tumeshuhudia mikanganyiko, udhalilishaji na lugha chafu bungeni kutokana na mswada
wa sheria ya marekebisho ya uundwaji wa katiba mpya. Hatimaye mswada huo umepitishwa kama
ulivyoletwa maana hakuna mbunge aliyeujadili. Wabunge wa upinzani waliususia
baada ya kupuuzwa, wakatoka nje. Wabunge wa CCM, baada ya wabunge wa upinzani
kutoka nje na kuususia, nao wakaamua kutokuujadili na badala yake wakatumia
muda wa kuujadili mswada kuwatukana wabunge wa vyama va upinzani. Naibu Spika,
akaruhusu wabunge watumie muda wao kutukana badala ya kujadili mswada.
Kwa
watanzania tulio nje, tumeweza kuona kwa uwazi mkubwa kuwa bunge letu la sasa
halina uwezo wa kutunga sheria ya kutuelekeza namna iliyo bora ya kupata katiba
mpya. Wakati wabunge wa vyama vya upinzani vinapigania ushiriki zaidi wa
wananchi katika kutengeneza katiba yao, wabunge wa CCM wanapigania zaidi
uundwaji wa katiba ambao utahodhiwa na Chama Cha Mapinduzi, Bunge na Rais.
Wakati wa mijadala
ya sheria zinazohusu uundwaji wa Katiba Mpya bungeni, tangu mwanzo, tumeshuhudia
kwa kiwango kikubwa kumekuwa na mashindano kati ya wabunge wa vyama vya
upinzani na wabunge wa CCM. Wabunge wa CCM wanaonekana kutokukubali hoja yoyote
ya mbunge wa upinzani hata kama ni nzuri, na inaonekana, ka upande wao kufanya
hivyo ni kama itaonekana kukubali kuwa wapinzani wameshinda na CM imeshindwa.
Fikra za namna hii haziwezi kutusaidia kupata katiba iliyo nzuri. Tungeweza
kupata katiba nzuri endapo tu wabunge wetu wanapoliongelea suala lolote la
katiba, wangekuwa wanaongozwa na utaifa na siyo ushindani wa siasa za vyama.
Kuna mambo ya
msingi ya kuzingatiwa katika sheria zinazotuelekeza kuipata katiba mpya, ambapo
kama sheria yoyote au muundo wowote hautupeleki kwenye kuutambua na kukuukubali
ukweli huu, basi sheria au muundo huo ni batili:
1.
Katiba
ni ya watanzania wote, hakuna mwenye haki zaidi kuliko mwingine
2.
Katiba
nzuri itatokana na ushiriki mkubwa wa wananchi wote kupitia uwakilishi wa moja
kwa moja au uwakilishi wa asasi na taasisi mbalimbali
3.
Mwungano
wetu ulikuwa wa matafa mawili, Tanganyika na Zanzibar, na kwa kuwa katiba ni ya
mwungano lazima uwakilishi wake uzingatie ukweli huu
4.
Rais,
bunge, serikali, mahakama ni mazao ya katiba si wao wanaotakiwa kuitengeneza
katiba bali katiba ndiyo inayotakiwa kuwatengeneza wao
5.
Bunge,
serikali, mahakama, Rais, ni wadau wa kutengeneza katiba na wala hawana mamlaka
ya kuunda katiba pekee yao au kuhodhi mchakato wa kupata katiba mpya
6.
Wabunge
wengi waliopo bungeni sasa, upatikanaji wao umehusisha michakato iliyoendana na
hila, udanganyifu, upendeleo, wizi wa kura na rushwa. Tunatengeneza katiba ya
kuzuia hayo, hivyo wawakilishi na viongozi waliopatikana kwa njia hizo, kamwe
hawawezi kututengenezea katiba nzuri itakayozuia njia ambazo huwa wanapitia
kuupata uwakilishi
Kwa
kuzingatia hoja hizo 6 hapo juu, si busara na haki hata kidogo kumpa mamlaka
makubwa kupindukia Rais katika kupata katiba mpya wakati yeye ni tunda la
katiba na siyo kinyume chake. Kwenye hilo, wabunge wa upinzani walikuwa sahihi
kabisa kutaka mamlaka ya uteuzi ya Rais katika kupata wajumbe wa bunge la
katiba, yapunguzwe sana au kuondolewa ili katiba itakayopatikana iwe ya
wananchi na siyo ya Rais. Na hilo ni lazima lionekane wazi kwa kila mtu siyo
kwa kufanya kuambiwa. Na ninamtahadharisha Rais Kikwete kuwa akikubaliana na
mambo yanayofanyika bungeni sasa na ofisi ya mwanansheria mkuu na waziri wa
sheria, atapata aibu kubwa huku mbeleni. Naamini
Rais anataka historia imkumbuke kuwa alianzisha na kusimamia mchakato wa kupata
Katiba ya kwanza ya wananchi iliyozingatia matakwa ya Watanzania. Lakini kwenye
kulifikia hili ana maadui wengi wakubwa ndani ya chama na serikali yake. Na
wengine wametamka wazi kabisa kuwa haikuwa ajenda ya CCM. Mwanasheria Mkuu na
Waziri wa sheria wa wakati mchakato unaanza waliwahi kutamka wazi kabisa kuwa
hakuna haja ya kuwa na katiba mpya. Nilitegmea kuwa baada ya Rais kuamua kuwa
ni lazima tuwe na katiba mpya, kwanza angemwondoa Mwanasheria Mkuu ambaye ni
wazi anasimamia uandaji wa miswada ya kupata katiba mpya huku yeye mwenyewe akiwa
haamini kama kuna haja hiyo. Rais alistahili kuwa na watu wanaofanana na yeye
katika kuona umuhimu wa kuwa na katiba mpya. Ikumbukwe kuwa wabunge wengi wa
CCM hawataki katiba mpya ingawa wananchi tunaihitaji sana. Rais ni lazima
asimame kidete na Watanzania kupata katiba mpya, na yeyote anayelizuia hilo
ajulikane wazi kuwa ni adui wa Watanzania na ni adui wa Rais pia.
Kwa
kuzingatia ukweli kuwa wabunge tulio nao sasa, wengi wao waliupata huo ubunge
kwa ghiliba, wizi wa kura, rushwa na udanganyifu, ndiyo maana kuna kila sababu
ya kuzuia bunge hili kuwa sehemu ya bunge la katiba. Tunataka bunge letu hili
lichukuliwe kama taasisi mojawapo ambayo itatengewa uwakilishi katika bunge la
katiba kama zilivyo taasisi nyinginezo.
Bunge la sasa
lifanye kazi moja tu ya kuainisha asasi zinazotakiwa kutoa wajumbe wa baraza la
katiba kwa kuzingatia ukubwa wa uwakilishi. Baada ya kupatikana wajumbe wa
baraza la katiba, wakutane na kupitisha shaeia zote zitakazotumika katika
kusimamia mchakato wa upatikanaji katiba mpya. Kwangu mimi taasisi ambazo
zingechukuliwa kuwa ni muhimu katika kutoa wajumbe wa kuunda bunge la katiba zingekuwa
kama zifuatazo:
§
Wawakilishi
wa Bunge la Jamhuri ya Tanzania kwa kuzingatia mikoa wanayotoka na vyama
wanavyowakilisha (mbunge mmoja toka kila mkoa)
§
Wawakilishi
kutoka Bunge la wawakilishi Zanzibar
§
Wawakilishi
wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar
§
Wawakilishi
wa serikali kuu ya Jamhuri ya Mwungano (bara tu kwa niaba ya Tanganyika)
§
Wawakilishi
wa serikali za mitaa
§
Madhehebu
ya dini mbalimbali yanayotambulika kisheria
§
Taasisi
za Elimu ya juu
§
Taasisi
za kitaaluma
§
Mahakama
Kuu
§
Taasisi
za kibiashara, n.k.
Wajumbe hao
ndiyo wamchague Spika wao, Naibu Spika na Katibu wa bunge. Spika awe na mamlaka
ya kupendekeza wajumbe wengine ambao kutokana au na utaalam wao au uzoefu wao, mchango
wao unaweza kuongeza ubora wa katiba itakayotengenezwa au sheria ziatakazoongoza
mchakato wa kutengeneza katiba mpya.
Jambo la
kusisitiza ni kuwa ni lazima na ni muhimu, kama tunataka katiba ya watanzania
wote, katiba iliyo nzuri, tupunguze sana au kuondoa kabisa ushiriki wa bunge
tulilo nalo sasa au kututengenezea sheria za kutuongoza katika mchakato wa
kupata katiba mpya au kutuandalia sheria za kutengeneza katiba mpya. Bunge hili
na Rais, majukumu yao ya mwisho yaishie kwenye kuidhinisha wajumbe watakaounda
bunge la katiba, na sheria itamke wazi kuwa Rais jukumu lake kuu litakuwa
kutangaza majina ya wajumbe walioteuliwa na asasi zao kuziwakilisha kwenye
bunge la Katiba. Na baada ya hapo, sheria nyingine zote zitakazoongoza mchakato
mzima ziundwe na kupitishwa na Bunge la Katiba na siyo hili bunge letu la sasa.
Bunge letu la sasa limegeuza uundwaji wa katiba mpya ni ushindani wa Kichama,
ni ukweli huo ndiyo unaolifanya lisiwe chombo sahihi cha kutupeleka tunakotaka.
source: Bartholomew Mkinga (bmkinga@yahoo.com)
No comments:
Post a Comment