NIANZE kwa kumpongeza Waziri wa Mambo
ya Nje
na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, kwa jitihada zake kubwa kupigania
kupitishwa kwa sheria ya uraia pacha.
Pamoja na upinzani mkubwa katika suala
hilo, Waziri Membe ameendelea kusimama kidete na majuzi tu aliendeleza jitihada
hizo katika mkutano wa rasimu ya Katiba Mpya uliofanyika katika wizara yake.
Binafsi, ninaelewa mantiki ya hoja za
wanaopinga uraia pacha. Hata hivyo, mantiki hizo zimepitwa na wakati. Kimsingi,
moja ya sababu za kuharamisha uraia pacha ni siasa yetu ya nje
katika zama za Ujamaa. Wakati huo, nchi yetu ilielemea upande wa Wakomunisti,
na kwa hakika enzi hizo za kinachofahamika kama Vita Baridi zilitawaliwa sana
na matishio ya kiusalama. Kwa wakati huo, raia mwenye uraia wa nchi mbili
angeweza kuonekana kama kibaraka wa nchi za Magharibi na hivyo kuwapo kwa
uwezekano wa raia huyo kutumiwa kuihujumu nchi.
Kwa sasa hakuna hoja nzito dhidi ya
uraia pacha. Kama ni suala la utiifu kwa nchi (hoja ambayo imekuwa ikipigiwa
mstari kwa nguvu na wapinzani wa uraia pacha), sote tunafahamu jinsi nchi yetu
inavyohujumiwa na kutafunwa na Watanzania wenzetu ambao naamini baadhi yao
hawajawahi kutoka nje
ya mipaka ya nchi yetu.
Kadhalika, baada ya kuua na kuzika
itikadi ya Ujamaa, tumeshuhudia sio tu wageni kutoka nchi mbalimbali wakija
huko nyumbani kwa minajili ya uwekezaji au ajira bali pia watawala wetu
wamekuwa wakizunguka kila kona ya dunia kuhamasisha wageni kuja huko nyumbani,
si kutalii bali kuifanya Tanzania kuwa nyumbani kwao kwingine (second home).
Sasa kama ni ruksa kwa wageni ambao
hawana ‘udugu’ na nchi yetu kuwa na haki ya kuifanya Tanzania kuwa nyumbani
kwao, kwa nini isiwe hivyo kwa Watanzania ambao kwa sababu moja au nyingine
walilazimika kuchukua uraia wa nchi nyingine?
Na kwa vile kwa mujibu wa sheria
zilizopo, Mtanzania akichukua uraia wa nchi nyingine anapoteza uraia wa
Tanzania, basi pengine kuwahukumu waliolazimika kuukana uraia wa Tanzania ili
wapate uraia wa nchi nyingine sio kuwatendea haki.
Ninatambua kunaweza kuwa na hoja “kwa
nini utake uraia wa nchi nyingine ilhali tayari una uraia wako wa kuzaliwa (wa
Tanzania)?” Jibu jepesi ni kwamba sio kila aliyeamua kuchukua uraia wa nchi
nyingine (na hivyo kulazimika kuukana uraia wa Tanzania) alifanya hivyo kwa
kupenda. Kuna baadhi ya wenzetu waliolazimika kutafuta hifadhi ya ukimbizi nje
ya nchi yetu na hatimaye kupatiwa uraia wa nchi zilizowapa hifadhi (mfano ni
kundi la Wazanzibari waliopewa hifadhi Uingereza kutokana na vurugu za Uchaguzi
Mkuu wa mwaka 2000)
Lakini kubwa zaidi katika suala hili la
uraia pacha ni ukweli kwamba kumlazimisha Mtanzania anayetaka uraia wa nchi
nyingine akane uraia wa nchi yetu ni kinyume cha haki za binadamu za raia huyo
kwa sababu kimsingi ni Mtanzania kwa kuzaliwa. Huwezi kumnyima mtu haki kwa
sababu za kufikirika kama hizo za kukosa utiifu kwa nchi. Kama ni hivyo basi
hata wanasiasa wanapogombea kutuongoza katika chaguzi tungelazimika kuwanyima
haki ya kuongoza kwa hisia tu ya “kuna wanasiasa wasio na utiifu kwa nchi
yetu.”
Majuzi nimemsikia Mzee Kingunge
Ngombale Mwiru akizungumzia suala la uraia pacha. Binafsi nadhani japo tunaaswa
kusikiliza ushauri wa wazee wetu lakini sababu za kibaiolojia zinaweza
kutufundisha kuwa uwezo wa kiakili huathiriwa na umri. Tumeshasikia habari za
wazee “wanaozeeka vibaya,” na japo ninamheshimu Mzee Kingunge lakini nadhani
anazeeka vibaya.
Nisingependa kumjadili Kingunge kwa
undani katika makala hii bali binafsi nimekuwa nikimwona mzee huyo kama mmoja
wa watu waliomsaliti Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere, walishirikiana katika
jitihada za kujenga jamii ya usawa na haki lakini akamsaliti kwa kuungana na
makundi ya kifisadi yaliyoifikisha Tanzania ilipo sasa. Ushauri wangu mwepesi
ni kumpuuza Mzee Kingunge kwani mitizamo yake iliyopitwa na wakati haina nafasi
katika Tanzania tunayoihitaji sasa.
Kimsingi, suala la Mtanzania kuishi nje
ya nchi yake linaambatana na hisia za kibaguzi kwa namna fulani. Majuzi tu
niliingia katika malumbano na ndugu yangu mmoja kuhusu mustakabali wa taifa
nililolizungumzia. Alidai kuwa kwa vile nipo mbali na huko nyumbani (Tanzania)
basi nitakuwa “mtu wa kuambiwa tu” (kana kwamba kila tunachoambiwa si sahihi).
Kuna kasumba ya kibaguzi iliyoshamiri
kwa muda mrefu kwa baadhi ya wenzetu huko nyumbani kutoangalia Watanzania tulio
nje ya nchi yetu kama “Watanzania vipande” (yaani si Watanzania kamili). Japo
ni ruhusa kwao kubobea kwenye uchambuzi wa Ligi Kuu ya England kana kwamba
wanaishi hapa, ni “kosa la jinai” kwa sie tulio mbali na nyumbani kuzungumzia
masuala yanayoigusa Tanzania yetu. Hawa ni wabaguzi tu wasiotaka kuelewa kuwa
kwa sie wengine uwepo wetu huku unapelekea “kukabwa koo” na swali “Kwa nini iwe
hivi kwa wenzetu lakini kwetu sivyo?”
Sina maana kila linalofanyika hapa
Uingereza, kwa mfano, ni jema na ningetamani liwe hivyo huko nyumbani. Lakini
kuna maswali kadhaa, hususan katika mfumo wa utawala unaotanguliza maslahi ya
taifa badala ya watu binafsi au itikadi za kisiasa, au kufanikiwa kutenganisha
taasisi na mtu binafsi. Kadhalika, wenzetu hawa licha ya wengi wao kutokuwa
wacha Mungu wamefanikiwa sana kutilia mkazo maadili katika uongozi, huduma kwa
umma na utawala bora kwa ujumla.
Ninaamini kuna wazalendo wengi tu
Watanzania waliolazimika kuchukua uraia wa nchi nyingine lakini nafsi na akili
zao zipo huko nyumbani. Na hiyo ni kuweka kando ukweli kwamba wengi wetu bado
tuna ndugu, jamaa na marafiki huko nyumbani. Kuwanyima Watanzania hawa haki ya
kushiriki katika ujenzi wa Taifa letu ‘changa’ (na sasa kushiriki katika
jitihada za kupigania uhuru wa pili dhidi ya maadui wa nchi yetu kama vile
ufisadi) ni kutowatendea haki.
Ninatambua kuwa baadhi ya wasomaji
watahusisha mtizamo wangu katika suala la uraia pacha na ukweli kuwa nami ni
miongoni mwa Watanzania walio nje, lakini ukweli ni kwamba hakuna sababu japo
moja ya msingi ya kuwabagua Watanzania wenzetu, iwe ni kwa waliochukua uraia wa
nje au kwa sababu nyingine yoyote ile. Ubaguzi ni suala lisilokubalika.
Nihitimishe makala hii kwa kutoa wito
kwa Watanzania wenzangu kuunga mkono jitihada za Waziri Membe katika suala la
uraia pacha, huku nikitegemea kuwa Katiba Mpya itatambua umuhimu wa suala hilo
na hatimaye kuliruhusu. Umoja na nguvu.
www.
raiamwema.co.tz: Evarist Chahali
No comments:
Post a Comment