Mshambuliaji
aliye katika kiwango cha kucheka na nyavu kama ananawa Amisi Tambwe,
alifikisha jumla ya mabao sita katika mechi mbili za ligi kuu ya Bara
jana, lakini akaangushwa na matokeo baada ya Simba kulazimishwa sare ya
2-2 na Mbeya City katika mechi ya kusisimua, kwenye Uwanja wa Taifa.
Kwa matokeo hayo Simba imefikisha pointi
11 kutokana na michezo mitano, pointi tano mbele ya Yanga ambao wana
mchezo mmoja mkononi hata hivyo huku City iliyopanda daraja ikiwa pointi
moja juu ya mabingwa watetezi hao.
Richard Peter aliyeingia kutoka benchi
aliifungia City iliyotawala mchezo huo kwa muda mwingi bao la
kusawazisha dakika 10 tangu aingie uwanjani kuchukua nafasi ya Mwagane
Yeya katika dakika ya 60, alipounganisha mpira wa adhabu ndogo wa
Anthony Matogolo.
City ambayo ilitoka sare ya 1-1 na Yanga
katika raundi ya tatu, ingeweza kuibuka na ushindi dhidi ya kigogo
kingine cha ligi kuu jana kama si uhodari wa Abel Dhaira aliyepangua
mpira hatari wa Peter na kuwa kona katika dakika ya 72.
Tambwe ambaye alifumania nyavu mara nne
katika mchezo dhidi ya Mgambo JKT katikati ya wiki, aliifungia Simba bao
la kuongoza na lake la tano katika michezo miwili nusu saa tangu kuanza
kwa mchezo huo.
Mkali huyo aliyesajiliwa kutoka Vital'O ya
Burundi katika dirisha lililopita la usajili, alifunga bao hilo baada
ya kupokea pasi ya Harun Chanongo na kupiga shuti lililomshinda David
Baruani katika lango la City.
Kuchukuliwa kwa Tambwe kulikuwa ni
jitihada za dakika za majeruhi za Simba kumaliza tatizo la ufungaji
linaloikabili tangu Januari ilipomuuza Mganda Emmanuel Okwi ambaye jana
alikuwa mmoja wa watazamaji uwanjani hapo kwa Etoile du Sahil ya
Tunisia.
Ilimchukua mfungaji bora wa Kombe la
Kagame la klabu bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Tambwe dakika tatu
zaidi kuipatia Simba bao la pili, akitumbukiza wavuni mpira kutokana na
pasi ya Betram Mwombeki.
Shangwe za Simba zilitulizwa japo kwa muda
katika dakika ya 37 baada ya City, ambayo ilitawala dakika 20 za kwanza
na 10 za mwisho za kipindi cha kwanza, kupata bao kupitia kwa Paul
Nonga kutokana na shuti kali.
Timu zilikuwa:
SIMBA: Abel Dhaira, Wiiliam Lucian, Issa
Rashid, Gilbert Kaze (Hassan Khatib dk.65), Joseph Owino, Jonas Mkude,
Twaha Ibrahim (Ramadhani Chombo dk.50), Amri Kiemba (Ramadhani Singano
dk.79), Betram Mwombeki, Amisi Tambwe, Harun Chanongo.
CITY: David Baruani, John Kabanda, Hassan
Mwasapili, Deo Julius, Yohana Morris, Anthony Matogolo, Mwagane Yeya
(Richard Peter (dk.60), Steven Mazanda, Paul Nonga, Deus Kaseke, Yusuph
Wilson.
CHANZO:
NIPASHE JUMAPILI
No comments:
Post a Comment