INAWEZEKANA kwamba sasa watu wengi
zaidi wanatambua yale yaliyokuwa yakisemwa huku yakibezwa, na wanaona yale
waliyokuwa wakiambiwa waone huku wakikataa kuona, japo wanayo macho.
Tumekuwa na tabia, kwa muda mrefu hadi
sasa ni utamaduni, kwamba tunaposikia jambo lisilotupendeza tunaziba masikio na
tunapoonyeshwa kitu kisichotufurahisha tunafumba macho. Tunasahau kwamba kuziba
masikio au kufumba macho hakulifanyi jambo hilo na wala hakusababishi kitu
hicho kutoweka.
Baadhi yetu tumekuwa tukionya kwamba
mambo tunayoyafanya leo yanazo athari zake kesho na keshokutwa, na kwamba kila
tendo lina tendo-rejea (For every action there is a reaction), lakini
bado tunao watu miongoni mwetu wanaoelekea kuamini kwamba wanaweza kutenda
watakavyo na zisitokee athari zozote.
Mifano ni mingi, lakini inatosha
kuchukua miwili au mitatu. Hivi sasa Tanzania imejijengea sifa ya hovyo, sifa
ya aibu, ya kuwa njia ya mpito (transit) ya dawa za kulevya ziendazo
huko ziendako. Inaumiza roho kila mara unapopata habari kwamba Mtanzania
mwingine amekamatwa akivuka mpaka wa nchi nyingine akiwa amebeba mihadarati.
Kama lilivyosema gazeti moja nchini,
Watanzania wamegeuka ‘punda’ wa kubeba mizigo ya mihadarati ya watu wengine
(siku hizi wabebaji hao wanaitwa makontena kwa sababu ya kubeba dawa hizo
tumboni). Maana yake ni kwamba mizigo wanayobeba si ya kwao, bali wao ni
wapagazi wa kuwabebea hao wenye mizigo yao.
Kwa kuangalia tatizo hili juu-juu, bila
uchambuzi kidogo tunawaona vijana hawa waliogeuka kuwa punda kama wana wapotevu
waliokosa maadili na waliowaasi wazazi wao na wanaolisaliti taifa lao.
Aidha, tumekuwa na janga la baadhi yetu
kuwaua na kuwakata viungo wenzetu wenye ulemavu wa ngozi (albino) kiasi
kwamba dunia nzima sifa moja ya nchi yetu ni kwamba albino hawana usalama hapa.
Watu wengi wanaotupenda wamesumbuliwa na jambo hili, wakijiuliza ni jinsi gani
nchi iliyowahi kuwa na sifa ya utu, uungwana na ukarimu inaweza kugeuka na kuwa
na jamii ya nyang’au kama hawa.
Najaribu kuzichukua sifa hizi mbili za
aibu kwa pamoja, huku nikijaribu kudadisi chimbuko lake na jinsi
zilivyojitokeza kuwa ni sifa za taifa letu. Sifa hizi mbili ni matokeo ya kile
nilichokiita tendo-rejea, ‘reaction.’ Jamii inayoachana na maadili ya
uongofu, ikashindwa kuwafundisha watoto wake jinsi ya kuishi katika uadilifu;
jamii inayoonyesha dhahiri kwamba utajiri kwa njia yoyote ile ni jambo jema na
kwamba ukiiba si tatizo bali tatizo ni kukamatwa; jamii inayotukuza wezi na
matapeli, badala ya kuwasweka jela inawachagua na kuwatuma bungeni, jamii hiyo
inalea punda wa mizigo ya mihadarati.
Hali kadhalika, tunapopuuza elimu
yakinifu ya watu wetu na watoto wetu wakafundishwa kushinda mitihani bila
kupata maarifa; tunapokubali kwamba ‘multiple choice’ ndio wa kupima
uwezo wa mwanafunzi, na tunapowaachia watu wachache wafanye wanachotaka na
elimu ya watoto wetu bila kuwasaili, tunakuza u-mbumbumbu ambao baadaye
unajitokeza katika medani zote za maisha ya jamii yetu, kutoka ngazi za chini
hadi za juu.
U-mbumbumbu huu ndio huo unaotufanya
tukubali kwamba kuna mzee mmoja Loliondo anayetibu maradhi halaiki kwa kikombe
kimoja na taifa zima likaonekana liko mbugani kwenda ‘kunywa kikombe.’ Watu
wanakufa kwa kuacha dawa zao, hospitali zinaachia wagonjwa waende kupata
‘kikombe,’ sote tunaonekana wajinga, lakini mwisho wa siku hakuna mtu wa kutoa
maelezo ya kuridhisha kuhusu hicho ‘kikombe’ na tunajifanya hamnazo, kama vile
hakuna kilichotokea. Tunajibaraguza, hatuoni haya!
Ujuha huu ni ujuha unaoambukiza,
haubakii kwa mtu mmoja mmoja, kwa sababu unayo misingi yake katika elimu ya
ujuha, na hii maana yake ni kwamba mbegu zake zimesambazwa shamba zima.
Sasa, ujuha unaotokana na elimu ya
uzuzu inapokutana na mmomonyoko wa maadili unaotokana na kufundishana wizi,
tunakuwa tumefanikisha kupata muungano baina ya punda wa kubeba mihadarati na
dalali wa kuchinja albino. Hawa wawili, baba yao ni ujinga na mama yao ni
mmomonyoko wa maadili. Mkunga aliyewazalisha ni uongozi mbovu.
Nataka nieleweke kwamba nasema uongozi
mbovu ni wetu sote: Tunajiongoza vibaya, tunaongozana vibaya na tunawaongoza
vibaya hao tunaotakiwa kuwaongoza. Binafsi hupenda kusema kwamba kiongozi si
yule aliyakabidhiwa ofisi kwani huyo ni ofisa tu; kiongozi ni yule anayeonyesha
njia. Katika mambo haya ninayoyajadili sote ni viongozi, na sote tumewasaliti
watu wetu.
Maofisa waliokabidhiwa ofisi hizi
tumewachagua wenyewe, na kwa sababu ofisi hizo wanazozishikilia ni sisi
tuliowakabidhi, kwa kawaida ni juu yetu kuwaandama ili waziendeshe vyema kwa
maslahi yetu. Kwa kweli, ni sisi tunaotakiwa kubeba lawama iwapo tumewakabidhi
ofisi zetu watu wasio na uwezo wa kutufanyia kazi.
Iwapo sisi ni wakweli katika nafsi
zetu, iwapo tutajichunguza kwa undani na kujisaili kwa dhati, tutagundua kwamba
masuala mazito na yenye umuhimu mkubwa tunayachukulia kipuuzi, tunayachezea na
kuyatomasatomasa na kuyatania, kama vile hatujui hatari zinazotokana na upuuzi
huo. Halafu yanapotulipukia, ni kama tunashangaa.
Tunaposhangaa tunataharuki na kuchukua
hatua za kuchekesha – kama tunaweza kucheka -- ambazo hazina chembe ya
kuonyesha kwamba tumetambua chanzo cha tatizo. Hatua tunazochukua ni za
kujishikiza tu, kama vile tunasubiri kitu fulani kitokee ndipo tuokoke, na kwa
jinsi hii tunasogea kwa mtindo wa siku hadi siku, mpaka hapo itakapotokea
gharika.
Nakumbushia tena, kila tendo lina
tendo-rejea, na Waingereza wana msemo kuhusu “chickens coming home to roost,”
ambao maana yake ni kwamba kuku unaowafungulia asubuhi usiwashangae ukiwaona
wanarudi nyumbani jioni; ni wako hao, na wanakuja kulala.
Naangalia kila upande, kila idara, kila
medani, kila eneo la maisha (siasa, uchumi, elimu, afya, kilimo, michezo,
utamaduni, maadili) na ninaona kuku wengi wanarudi, mmoja baada ya mwingine, na
nikiwaangalia vizuri na kuchunguza rangi za manyoya yao, naona ni wale wale
kuku wetu tuliowafungulia asubuhi. Sasa tunashangaa nini?
Source:
www.raiamwema.co.tz: Jenerali Ulimwengu
No comments:
Post a Comment