WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Monday, September 30, 2013

Kufungiwa magazeti: Wahafidhina sasa wanaongoza @ZittoKabwe

Imeandikwa na Zitto Kabwe, Mb — Kwa mshtuko na masikitiko makubwa kuanzia jana jioni tumepokea taarifa za kufungiwa kwa magazeti mawili ya kila siku hapa nchini ya Mwananchi na Mtanzania. Serikali imechukua uamuzi huo kwa kutumia sheria ya kidikteta ya magazeti ya mwaka 1976 ambayo Tume ya Jaji Francis Nyalali iliiorodhesha kama sheria kandamizi. Sababu zilizotolewa kuhalalisha uamuzi huu ni sababu zisizo na maana na ambazo Serikali ingeweza kufungua mashtaka ya kawaida kabisa mahakamani kushtaki magazeti hayo iwapo haikupendezwa na habari walizochapisha.

Moja ya sababu ya kufungiwa kwa gazeti la Mwananchi ni kuchapisha taarifa kuhusu mishahara ya Serikali. Serikali inasema habari hii ni siri. Serikali hii hii ambayo imesaini makubaliano ya kuendesha serikali kwa uwazi (Open Government Initiative) na kumwagiwa sifa na Rais Barack Obama wa Marekani inalifungia gazeti kwa kuandika habari za mishahara ya watumishi wa Serikali. Mishahara kuanzia mshahara wa Rais mpaka wa mtendaji wa Kijiji haipaswi kuwa jambo la siri. Kuonyesha kuwa
jambo hili linapaswa kuwa wazi mkutano ujao wa Bunge tutatafuta kila namna kutaja mshahara wa Rais, Makamu wa Rais, Waziri Mkuu na baadhi ya Watendaji wa Mashirika makubwa ya Umma kama njia ya kuwaunga mkono gazeti la Mwananchi kwa habari yao hiyo. Mapato ya Mbunge yanajulikana sasa kuwa ni shilingi milioni 11.2 kwa mwezi kabla ya kuongeza posho za vikao za shilingi laki 200,000 kwa siku na posho ya kujikimu ya shilingi 130,000 kwa siku. Watanzania wana haki ya kujua wanawalipa kiasi gani watumishi wao. Tutaanza na mshahara wa Rais!

Gazeti la Mtanzania limefungiwa pamoja na mambo mengine kwa kuandika 'mapinduzi ni lazima'. Inashangaza Serikali ya Chama cha Mapinduzi inaogopa neno mapinduzi. Marehemu Mzee Steven Salum Nandonde, aliyekuwa mbunge wa Jimbo la Tandahimba alipata kusema bungeni kuwa 'lazima nchi ipinduliwe'. Ni matumizi ya lugha tu. Mzee Nandonde yeye alikuwa analalamikia maendeleo duni ya mikoa ya kusini na kutaka Kaskazini iwe Kusini na Kusini iwe Kaskazini. Serikali inafungia gazeti kwa sababu ya kuandika Mapinduzi ni lazima ilhali kila siku Zanzibar wanasema Mapinduzi daima!

Gazeti la Mtanzania linahaririwa na Absalom Kibanda, mwandishi wa habari ambaye bado anaponya majeraha ya mwili na kisaikolojia ya kuteswa na watu ambao mpaka leo hawajakamatwa. Badala ya Serikali kuwakamata watesaji wa Kibanda, inamnyima kazi Kibanda ili ateseke kwa njaa kwa kukaa miezi mitatu bila kazi. Pia wanatutesa Watanzania kwa njaa ya kupata habari ambayo ni haki ya msingi ya kikatiba. Hii ndio zawadi Serikali inampa Kibanda baada ya kung'olewa kucha, kunyofolewa jicho, kukatwa vidole na kuteswa kwa namna isiyoelezeka.

Matukio ya hivi karibuni na namna Serikali inavyoyachukulia yanaonyesha dhahiri kwamba Rais Kikwete kazidiwa nguvu na kundi la wahafidhina ndani ya chama na Serikali yake. Rais ambaye alianza kwa kuhubiri uvumilivu wa hali ya juu na hata yeye mwenyewe kupata kusema uvumilivu huu wengine wanauona kama udhaifu lakini ameamua kujenga Taifa la kuvumiliana. Rais alipata kulalamika hadharani kwamba kuna wenzake wanataka aongeze ukali. Ni dhahiri kundi hili la wahafidhina sasa ndio linalomwongoza Rais Jakaya Kikwete. Kitu kimoja tu Rais azingatie, kundi hili linaongozwa na maslahi binafsi ya kubakia kwenye utawala wakati yeye anapaswa kuacha 'legacy'. Rais Kikwete asipokuwa makini atakuwa Rais karatasi (lame duck) tu tunapoelekea mwisho wa utawala wake. Maamuzi ya hovyo na ya kidikteta ya kufungia magazeti yanamchora vibaya mbele ya wananchi na jamii ya kimataifa. Wahafidhina kuwa nguvu zaidi ya kiutawala ni makosa ambayo watanzania hawapaswi kuyakubali kamwe.

Wananchi sasa waifanye Serikali kujutia uamuzi wake wa kufungia magazeti. Nimeamua mimi binafsi kama mbunge kesho Jumatatu tarehe 30 Septemba, 2013 kupeleka taarifa rasmi kwa Katibu wa Bunge ya kupeleka muswada Bungeni wa kuifuta kabisa Sheria kandamizi ya magazeti ya mwaka 1976. Sasa tupambane na kundi dogo la wahafidhina ndani ya Serikali na CCM wasiopenda mabadiliko na iwe fundisho kwa wahafidhina wengine wowote waliopo ndani ya Serikali au nje ya Serikali kwamba Uhuru wa habari sio jambo la kuchezea kama gololi.

Neno La Leo: Mussa Na Firauni Walivyotufikisha Hapa...!

musa_1fb7d.jpg
Ndugu Zangu,
TUMEKUWA tukitamka; Ukistaajabia ya Mussa , utayaona ya Firauni! Si wengi wenye kuyajua ya Mussa ni yepi na ya Firauni pia.
Jana niliandika, kuwa kusamehe ni jambo lililo bora kabisa kwa mwanadamu kulifanya kwa mwanadamu mwenzake.
Na hakika, wanadamu sisi ni viumbe wa ajabu, maana, huwa tuna kawaida ya kutaka kutatua matatizo yetu kwa namna tunavyotaka sisi yatatuliwe. Tunapoomba ushauri huwa tumeshakuwa na majibu tayari. Unapokuja ushauri tofauti na matarajio yetu huwa wepesi sana wa kuung'aka.

Na hapa kuna simulizi niliyopata kuipokea. Kuwa alipata kutokea bwana mmoja. Yeye na mkewe walisubiri kwa miaka mingi kupata mtoto. Ikafika siku mkewe akatunga mimba. Na katikati ya kuilea mimba hiyo, bwana yule akapata safari. Naam. Akasafiri kwenda mbali. Nyumbani kamwacha mkewe mjamzito.
Huku nyuma, mke akapata maumivu. Mganga akamwambia; ili mimba isalimike, basi, ni sharti ale maini ya mbuzi, na afanye hivyo kila anapopata mimba.

Nyumbani hakukuwa na mbuzi wa kuchinja. Mama yule akaenda kwa ndugu wa mumewe mwenye zizi la mbuzi. Akamweleza shida yake.

Bwana yule mfuga mbuzi akakataa katakata. Kuwa hawezi kuchinja mbuzi wake kwa ajili ya kupata maini ya tiba tu. Mama mjamzito akarudi nyumbani akiwa mnyonge. Na mimba ile ikaharibika.
Mume aliporudi akasimuliwa na mkewe. Hakuamini masikio yake. Iweje nduguye amfanyie hivyo? Alijiuliza. Akafunga safari mpaka kwa Mussa kuomba ushauri.

Alipofika kwa Mussa akasimulia kisa chake. Mussa alimsikiliza kwa makini. Na kwa vile aliombwa kutoa ushauri, basi, Mussa akamwambia; " Hayo yameshatokea, msamehe nduguyo!"

Bwana yule akaushangaa sana ushauri wa Mussa. Kwamba amsamehe tu mtu aliyesababisha mimba ya mkewe iharibike! Basi, akafunga safari hadi kwa Firauni kupata ushauri wake. Firauni naye akasikiliza kwa makini kisa chote.

Na kwa vile aliombwa kutoa ushauri, basi, akatamka; " E bwana ee, mimi naona umsamehe tu nduguyo!"
Bwana yule akaupinga ushauri ule. Akamtaka Firauni aje na ushauri ulio na busara zaidi. Basi, kwa vile Firauni aliombwa aje na ushauri tofauti na wa mwanzo, naye akatamka;

" Basi, mimi naona ni vema ukamkabidhi mkeo kwa nduguyo aliyekataa kumchinja mbuzi ili maini ya tiba yapatikane. Na akae na mkeo hadi atakapompa mimba. Na kwa vile mimba itakuwa ya kwake, basi, nduguyo atalazimika kumchinja mbuzi ili ipatikane tiba. Na mtoto akizaliwa, we nenda kamchukue mkeo na mtoto!"

Naam, ndio hayo ya kustaajabia ya Mussa na kuyaona ya Firauni! Na siye tuliokulia pwani mtu akikwambia; " Acha Ufirauni!" Basi, ujue amekasirika.

Ndio, na hata katika jamii yetu, na hususan kwenye fikra zetu, kuna mahali ambapo akina Mussa Na Firauni wamechangia katika kutufikisha tulipo sasa. Na hili nitalijadili zaidi huko twendako.
Maana, mara nyingi, kama wanadamu, makosa tuyafanyao hutokana na makosa ya wengine. Tunachofanya ni kuyarudia makosa.

Je, unafanyaje pale kipofu anapokuvamia na kukusababishia maumivu makali? Jibu; Utakasirika kwa sababu ya maumivu uliyoyapata. Hiyo ni hali ya kibinadamu.

Lakini, ukiamua kulipiza kisasi, kwa wewe kujitoboa macho na kumvamia kipofu, basi, hapo utakuwa umetenda lisilo na busara.
 
Ni Neno la Leo.Tafakari!
Maggid
Iringa,

Saturday, September 28, 2013

Tamko la Serikali la kuyafungia kuchapishwa magazeti ya Mwananchi na Mtanzania

Serikali imeyafungia kutochapishwa Magazeti ya MWANANCHI na MTANZANIA kuanzia 27 Septemba, 2013 kutokana na mwenendo wa magazeti hayo kuandika habari na makala za uchochezi na uhasama kwa nia ya kusababisha wananchi wakose imani kwa vyombo vya dola hivyo kuhatarisha amani na mshikamano ulipo nchini.

Gazeti la MWANANCHI limefungiwa kutochapishwa kwa siku kumi na nne (14) kuanzia 27 Septemba, 2013. Adhabu hii imetangazwa kwa Tangazo la Serikali (Government Notice) Namba 333 la tarehe 27 Septemba, 2013.
Gazeti la MWANANCHI limepewa adhabu hiyo kutokana na hivi karibuni kuchapisha habari zenye mwelekeo wa 
uchochezi na uvunjifu wa amani, mfano tarehe 17 Julai, 2013 katika toleo Namba 4774 ilichapisha habari isemayo “MISHAHARA MIPYA SERIKALINI 2013” kwa kuchapisha waraka uliozuiliwa kwa matumizi ya vyombo vya habari waraka huo ulikuwa wa Siri haukupaswa kuchapishwa Magazetini.

Aidha, katika toleo la Jumamosi, tarehe 17 Agosti, 2013 lilichapisha habari yenye kichwa kisemacho “WAISLAM WASALI CHINI YA ULINZI MKALI” habari hiyo ilikolezwe na picha ya mbwa mkali mwenye hasira.

Habari na picha hiyo ilitoa tafsiri ya kuwa Jeshi la Polisi lilipeleka mbwa katika maeneo ya ibada ya waumini wa dini ya Kiislam. Jambo ambalo halikuwa la ukweli.

Jeshi la Polisi katika doria siku hiyo halikupeleka mbwa katika maeneo ya Misikiti. Serikali na jeshi la Polisi linaheshimu na kuzingatia maadili ya dini ya Kiislamu na kwa hiyo Jeshi lake hakiwezi kupitisaha au kuingiza mbwa katika maeneo ya ibada.

Hivyo basi, kwa gazeti hili kuchapisha habari iliyokolezwa na picha ya mbwa ni uchochezi wa kulichonganisha Jeshi la Polisi na waumini wa dini ya kiislam mbwa ni najisi hapaswi kuingia katika maeneo ya ibada.

Gazeti la MTANZANIA limefungiwa kutochapishwa kwa siku tisini (90) kuanzia tarehe 27 Septemba, 2013 kwa kuchapisha habari zenye uchochezi.

Gazeti hili limeonywa mara nyingi lirekebishe mtindo wake wa uandishi wa kichochezi na lizingatie maadili na Sheria na Kanuni za fani ya Habari.

Pamoja na kuonywa gazeti hili halikuonyesha kuzingatia maelekezo ya Msajili wa Magazeti, mfano ;katika toleo na 7262 la 20 Machi, 2013 liliandika habari yenye kichwa kisemacho “URAIS WA DAMU”, tarehe 12 Juni, 2013, toleo Namba 7344 lilichapisha makala isemayo “MAPINDUZI HAYAEPUKIKI”.

Aidha, siku ya Jumatano, tarehe 18 Septemba, 2013 katika toleo Namba 73414 ukurasa wa mbele lilichapisha Kichwa cha habari kisemacho “SERIKALI YANUKA DAMU” taarifa hiyo ilikolezwa na picha zilizo unganishwa kwa ustadi mkubwa kwa kutumia kompyuta kutapakaza rangi nyekundu mithili ya damu nyingi kumwagika.

Katika habari hiyo gazeti hilo limedai bila uthibitisho kuwa Jeshi la Polisi linahusika na wahanga waliomizwa na watu wasiojulikana kwa kumwagiwa tindikali na waliyovamiwa na kujeruhiwa vibaya.

Vile vile gazeti hilo limeishtumu serikali kuwa goigoi katika kushughulikia matukio yenye sura ya kigaidi.

Kwa ujumla wake habari hiyo ni ya kichochezi ina lengo la kuwafanya wananchi wavichukie vyombo vya ulinzi na usalama wavione kuwa haviwasaidii.

Kutokana na makosa yalitajwa hapo juu serikali imelifungia gazeti la Mtanzania kutochapishwa kwa muda wa siku tisini(90) kwa Tangazo la Serikali Namba 332 (Government Notice No.332) la tarehe 27 Septemba, 2013,.
Serikali inawataka wamiliki,wahariri na wanahabari kwa ujumla kuwa makini, kuzingatia weledi, miiko na madili yataaluma uandishi wa habari.

Serikali inawataka wamiliki na hasa wahariri kuhakisha kuwa habari wanazoziandika na vipindi wanavyoviandaa vinazingatia taaluma, kuweka mbele maslahi ya taifa letu kwa kuwa na uzalendo wa hali ya juu.

Serikali inavionya vyombo vya habari vinavyoutumia uhuru wa habari bila wajibu kuwa haitasita kuvichukulia hatua kali ikiwemo ya kuvifungia. Serikali haitakubali kuona vyombo vya habari kuwa chanzo cha uvunjifu wa amani nchini.

Imetolewa na

MKURUGENZI IDARA YA HABARI
WIZARA YA HABARI, VIJANA, UTAMADUNI NA MICHEZO
28 SEPTEMBA, 2013

Warioba: Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ina upungufu


Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Mstaafu, Joseph Warioba akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana. Kushoto ni Makamu wake, Jaji Mkuu Mstaafu, Augustino Ramadhani.
Dar es Salaam. Wakati wananchi wa kada mbalimbali wakishinikiza Rais Jakaya Kikwete kutokusaini Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba 2013, kwa maelezo kuwa una kasoro, Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba naye amesema sheria ina upungufu.

Warioba alisema jana kwamba ni jambo la kushangaza sheria hiyo kueleza kuwa tume hiyo itavunjwa baada ya kukabidhi Rasimu ya Katiba kwenye Bunge Maalumu la Katiba, wakati huohuo ikieleza kuwa itahusika tena kusimamia utoaji wa elimu ya kura ya maoni.

Kauli hiyo ya Warioba imekuja wakati vyama vya NCCR Mageuzi, Chadema na CUF, vikifanya mikutano nchi nzima kuwashawishi wananchi kupinga kile wanachokiita hujuma dhidi ya upatikanaji wa Katiba Mpya.
Sheria hiyo ambayo Warioba amesema ina upungufu, muswada wa marekebisho yake ulijadiliwa na kupitishwa wa wabunge Septemba 6, mwaka huu katika Mkutano wa 12 wa Bunge Mjini Dodoma, ikiwa ni baada ya kubadilishwa kwa baadhi ya vifungu na hivi sasa Rais Kikwete anasubiriwa kuusaini ili iwe sheria kamili. Akizungumza na waandishi wa habari jana, Jaji Warioba alisema: “Mwisho wa kazi ya tume ni baada ya kukabidhi rasimu, hilo ni tatizo. Maana tume itakuwa imeshavunjwa, sasa itafanyaje kazi ya kutoa elimu kwenye kura ya maoni?”

Jaji Warioba pamoja na kukiri upungufu huo, alisema kurekebisha au kutokurekebisha kasoro hizo si jukumu la tume hiyo.

“Tunawaomba watafakari, waone jinsi gani tume ambayo imekwishavunjwa itakuja kutoa elimu wakati wa kura ya maoni, sheria ina ‘contradiction’ (ina mkanganyiko),” alisema.

Muswada huo ulipitishwa na wabunge wa CCM baada ya wale wa upinzani kutoka nje baada ya Kiongozi wa Kambi ya Upinzani, Freeman Mbowe kuamuriwa na Naibu Spika, Job Ndugai kutoka nje kutokana na kukaidi kwake amri ya kukaa chini alipokuwa akitaka kutoa hoja kabla ya mjadala wake kuanza.

Muswada huo unapingwa kwa kuwa Rais amepewa mamlaka ya kuteua wajumbe 166, ambao si wabunge wala wawakilishi na Zanzibar kutokushirikishwa kikamilifu kwenye maandalizi ya muswada huo.

Hata hivyo, Warioba alisema pamoja na kasoro hizo Tume hiyo inafanya kazi yake kwa kufuata sheria hiyo huku akisisitiza, “Wanaotunga sheria ni wengine siyo sisi, tulipoteuliwa tulikuta sheria na kuanza kazi kwa kuifuata. Imefanyiwa marekebisho sisi tunafuata.”

Alisema waliofanya mabadiliko ya sheria hiyo wana haki ya kufanya hivyo na kwamba Tume ya Mabadiliko ya Katiba haiwezi kuzuia kutokufanyika kwa mabadiliko hayo, kwani yapo baadhi yanaihusu.

Alisema baada ya kuipata sheria hiyo: “Tulijiuliza maswali kwa sababu miswada huwa inapelekwa bungeni na Serikali ikiwemo ya Katiba. Anayeipeleka kama ni waziri ndiye anayetoa ufafanuzi pale inapohitajika.”

Alisema kulingana na sheria, tume yake ndiyo inayotakiwa kutoa ufafanuzi katika Bunge la Katiba, kama ambavyo Waziri hutoa maelezo anapowasilisha muswada bungeni.


“Tulipouliza tulielezwa kwamba sisi ambao tumepewa jukumu la kupata maoni ya wananchi na kuandaa rasimu ndiyo tutaitwa pale tu patakapohitajika ufafanuzi wa jambo fulani,” alisema.

Alisema kazi ya kuandaa Rasimu ya Katiba itafanyika na kukamilika katika muda uliopangwa na Sheria ya Mabadiliko ya Katiba.

“Tulianza kazi Mei mwaka jana na tunatakiwa kumaliza Novemba mwaka huu, sheria inaruhusu kuongeza miezi miwili kama tutakuwa hatujakamilisha kazi. Katiba Mpya inatakiwa iwe imekamilika Aprili 26, 2014,” alisema.

source: mwananchi

Monday, September 23, 2013

Seif: Viongozi watawala wanasababisha vurugu

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), Maalim Seif Sharif Hamad
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), Maalim Seif Sharif Hamad amesema matatizo mengi ya uvunjifu wa amani na yanayoashiria kuzuka kwa  vurugu yanasababishwa na viongozi watawala katika baadhi ya nchi duniani.
Kauli hiyo ilitolewa jana mjini Kibaha  kwa niaba yake na Mwenyeki wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Mkoa wa Dar es Salaam, Alhaji Ramadhan Madabida kwenye kongamano la amani lililoandaliwa na Jumuiya ya akina mama waislamu (Juwakita) Mkoa wa Pwani.

Maalim Seif ambaye alikuwa mgeni  katika kongamano hilo,  alisema ikifuatiliwa kwa undani itabainika kuwa  chanzo cha mifarakano hiyo ni dhuluma wanayofanyiwa watawaliwa.

Alisema kwa sasa kuna  viongozi wengi duniani ambao wamekuwa wakiongoza umma kwa utashi wao na kusahau kuwa jukumu hilowalipewa na jamii kwa sababu tu ya kuwaamini.

Madabida ambaye alimlimwakilisha Maalim Seif baada ya kupatwa na msiba wa mtoto wa ndugu yake, alisema katika maeneo mengi ulimwenguni mambo mengi yanayozungumzwa ni uongozi katika nyanja mbalimbali.

Alkisema  watawala wake wanalalamikiwa kuwadhulumu watawaliwa kwa njia tofauti na hivyo kuzusha mifarakano kwa jamii.

"Dhambi kubwa ambayo haisameheki mbinguni hadi uliowakosea wanakusamehi ni hii ya dhuluma, jamani wapo baadhi ya viongozi duniani wamekuwa chanzo cha mifarakano aina mbalimbali kwa sababu tu ya dhuluma zao, si lazima dhuluma hizo ziwe za fedha,mali ama chakula lakini hata ya utoaji taarifa sahihi kwa watawaliwa ama utoaji ufafanuzi wa majambo yanayotokea"alisema madabida

"Jamani ndugu zangu JUWAVITA, kuna mambo yanatokea ya uvunjifu wa amani, yanatokea si kwa sababu watu hawataki bali wamechoka na mtawala wao, hili nalo lazima liangaliwe kiundani katika maeneo mengi duniani, inaweza ikawa ni taarifa tu ya uweli hujawapa unaoowaongoza, na unasahau nyuma yako wapo wenye akili na uadilifu zaidi yako wanajua kila kitu undani wake,,lazima itatokea vurugu, "aliongeza.

Aliwataka viongozi nchini kudumisha amani, wasichezee watekeleze majukumu yao wakijua wazi hivi sasa wanaoongozwa ni wasoni,wenye akili, waadilifu  na pia wenye sifa za uongozi na hivyo wanafatilia kila jambo.

Awali Mkurugenzi wa Taasisi ya Kiislamu ya World Islamic Call Society ya nchini Libya Sheik,Mohamed Qusuri ambaye pamoja na mabo mengine aliwasisitiza wanawake kuhubiri amani na upendo kwani amani haiwezi kuchezewa , ni tunu ambayo haiwezi kufanyiwa utani popote ulimwengu maana ikipotea inaleta madhara hata kwa familia na siyo adui tu.

Kadhi Mkuu wa Mkoa wa Pwani,  Sheikh Ramadhan Mtupa alitaja mada zilizojadiliwa  katika kongamano hilo kuwa ni kudumisha amani nchini,  kuishi kwa kuvumiliana, nafasi ya mwanamke wa kiislamu katika kuleta na kudumisha amani, machango wa vyama vya siasa ,vyombo vya dola na jamii kudumiosha amani.

Akifunga  kongamano hilo, Katibu wa JUWAKITA wa Mkoa huo,  Azama Masasa aliwataka   wanawake kudumisha amani kuanzia watoto na wawaletee kwa maadili ya kumuoga Mungu ili kuondokana na taifa lenye vijana wadogo wanaojihusisha na dawa za kulevya na mambo mengine ya uvunjifu wa amani
CHANZO: NIPASHE

Amisi Tambwe ang'ara Simba ikishikwa

Mshambuliaji aliye katika kiwango cha kucheka na nyavu kama ananawa Amisi Tambwe, alifikisha jumla ya mabao sita katika mechi mbili za ligi kuu ya Bara jana, lakini akaangushwa na matokeo baada ya Simba kulazimishwa sare ya 2-2 na Mbeya City katika mechi ya kusisimua, kwenye Uwanja wa Taifa.
Kwa matokeo hayo Simba imefikisha pointi 11 kutokana na michezo mitano, pointi tano mbele ya Yanga ambao wana mchezo mmoja mkononi hata hivyo huku City iliyopanda daraja ikiwa pointi moja juu ya mabingwa watetezi hao.
Richard Peter aliyeingia kutoka benchi aliifungia City iliyotawala mchezo huo kwa muda mwingi bao la kusawazisha dakika 10 tangu aingie uwanjani kuchukua nafasi ya Mwagane Yeya katika dakika ya 60, alipounganisha mpira wa adhabu ndogo wa Anthony Matogolo.
City ambayo ilitoka sare ya 1-1 na Yanga katika raundi ya tatu, ingeweza kuibuka na ushindi dhidi ya kigogo kingine cha ligi kuu jana kama si uhodari wa Abel Dhaira aliyepangua mpira hatari wa Peter na kuwa kona katika dakika ya 72.
Tambwe ambaye alifumania nyavu mara nne katika mchezo dhidi ya Mgambo JKT katikati ya wiki, aliifungia Simba bao la kuongoza na lake la tano katika michezo miwili nusu saa tangu kuanza kwa mchezo huo.
Mkali huyo aliyesajiliwa kutoka Vital'O ya Burundi katika dirisha lililopita la usajili, alifunga bao hilo baada ya kupokea pasi ya Harun Chanongo na kupiga shuti lililomshinda David Baruani katika lango la City.
Kuchukuliwa kwa Tambwe kulikuwa ni jitihada za dakika za majeruhi za Simba kumaliza tatizo la ufungaji linaloikabili tangu Januari ilipomuuza Mganda Emmanuel Okwi ambaye jana alikuwa mmoja wa watazamaji uwanjani hapo kwa Etoile du Sahil ya Tunisia.
Ilimchukua mfungaji bora wa Kombe la Kagame la klabu bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Tambwe dakika tatu zaidi kuipatia Simba bao la pili, akitumbukiza wavuni mpira kutokana na pasi ya Betram Mwombeki.
Shangwe za Simba zilitulizwa japo kwa muda katika dakika ya 37 baada ya City, ambayo ilitawala dakika 20 za kwanza na 10 za mwisho za kipindi cha kwanza, kupata bao kupitia kwa Paul Nonga kutokana na shuti kali.
Timu zilikuwa:
SIMBA: Abel Dhaira, Wiiliam Lucian, Issa Rashid, Gilbert Kaze (Hassan Khatib dk.65), Joseph Owino, Jonas Mkude, Twaha Ibrahim (Ramadhani Chombo dk.50), Amri Kiemba (Ramadhani Singano dk.79), Betram Mwombeki, Amisi Tambwe, Harun Chanongo.
CITY: David Baruani, John Kabanda, Hassan Mwasapili, Deo Julius, Yohana Morris, Anthony Matogolo, Mwagane Yeya (Richard Peter (dk.60), Steven Mazanda, Paul Nonga, Deus Kaseke, Yusuph Wilson.    
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

Azam yaichakaza Yanga


Wachezaji wa Yanga wakiwa hawaamini kilichotokea baada ya kufungwa bao la tatu katika dakika ya 90 na Azam. Picha na Michael Matemanga. 

Azam ilifunga bao dakika ya kwanza na dakika ya 90.
Dar es Salaam / Tanga. Mshambuliaji chipukizi, Joseph Kimwaga aliingia akitokea benchi na kuifungia Azam bao la ushindi hivyo kuichapa Yanga kwa mabao 3-2 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Kimwaga aliyeingia katika dakika ya 73 kuchukua nafasi ya Farid Musa, aliwakata maini mashabiki wa Yanga waliojitokeza kwa wingi uwanjani hapo baada ya kufunga bao lake la kwanza katika Ligi Kuu Tanzania Bara.

Azam waliuanza vizuri mchezo huo na kupata bao la kuongoza katika dakika ya kwanza kupitia kwa mshambuliaji John Bocco, lakini Yanga walisawazisha kupitia Didier Kavumbagu kabla ya Hamisi Kiiza kupachika bao la pili katika dakika ya 65, lakini dakika nne baadaye Azam walisawazisha kwa penalti ya Kipre Tchetche baada ya Haruna Niyonzima kushika mpira eneo la hatari.

Wakati mashabiki wakiamini mechi hiyo itamalizika kwa sare 2-2, Azam walifanya shambulizi la kushtukiza na Kimwaga alimalizia vizuri kwa shuti kali lililojaa wavuni katika dakika ya 90 na kufanya mchezo huo kumalizika kwa 3-2.
Kocha wa Azam, Stewart Hall amewasifu wachezaji wake kwa kutumia nafasi chache walizopata kupata ushindi huo.

“Yanga walicheza vizuri na kutengeneza nafasi nyingi za kufunga, lakini vijana wangu walitumia nafasi chache walizozipata kupata ushindi huu,” alisema Hall.
Yanga watajilaumu wenyewe kwa kipigo hicho baada ya washambuliaji wake Jerryson Tegete na Haruna Niyonzima kupoteza nafasi nyingi za kufunga wakiwa wao na kipa Aishi Manula. 

Katika michezo mingine JKT Ruvu na Ruvu Shooting wamepokea vipigo vya kwanza msimu huu baada ya kufungwa bao 1-0  na Oljoro JKT na Coastal Union.
Tanga. Coastal Union wakiwa kwenye uwanja wao wa Mkwakwani walipata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Ruvu Shooting. Kiungo Haruna Moshi ‘Boban’ aliwainua mashabiki wa Coastal dakika ya 80 akiunganisha vizuri krosi ya  Keneth Masumbuko.

Chamazi, JKT Ruvu walikubali kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa Oljoro JKT shukrani kwa goli la Paul Malipesa.

source: mwananchi

Friday, September 20, 2013

Uchambuzi wa Habari; Waziri Chikawe, Katiba Na Kelele Za Wapinzani....!


islammboye_be136.jpg
Ndugu zangu,
Imeripotiwa kwenye gazeti la Mwananchi, leo Ijumaa Septemba 20,kuwa Waziri wa Sheria na Katiba, Mheshimiwa Chikawe, amemwomba Rais Kikwete asaini Muswaada wa Marekebisho ya sheria ya Mabadiliko ya Katiba uliopitishwa na Bunge Septemba 6, mwaka huu. Kwamba Rais afanye hivyo ili kuepuka vurugu.

Hakika, huu ni wakati wa kuongozwa zaidi na hekima na busara kuliko hisia na ushabiki na hususan wenye sura za vyama na kuangalia maslahi ya muda mfupi na ya kibinafsi zaidi.

Rais wa Nchi anaongoza watu, na si mawe. Msingi wa kukubalika kisiasa ni lazima utokane na kukubalika na watu. Na wapinzani hao pia nyuma yao si mawe yaliyojipanga. Ni watu. Hivyo basi, inahusu watu. Inahusu Wananchi. Katiba ni mkataba baina ya watu katika jamii. Si miti na mawe.

Hivyo, ni muhimu sana watu kwa maana ya wananchi wakasikilizwa. Kama kuna manung'uniko yatafutiwe majawabu ili tufike salama kwenye kulifikia lengo kuu; Katiba ya Wananchi. Si ya chama tawala wala vyama vya upinzani. Ni jambo litakalotupeleka hata miaka 100 ijayo.

Maisha yetu hapa duniani ni mafupi sana. Wengi wetu hatutakuwepo, hata pale nchi yetu itakapotimiza miaka 100 ya Uhuru. Desemba 9, 2061.

Na Waziri Chikawe asiwe na hofu. Watanzania kwa desturi si wapenda vurugu. Hata katika hili la Katiba hawatafanya vurugu. Ila wakipewa nafasi ya kuonyesha masikitiko yao, basi, watayaonyesha, bila kufanya vurugu.

Maggid.
Iringa.
0754 678 252

Comments!

Nelson Msita Mie huwa najiuliza hivi hawa mawaziri wa chama tawala..huwa wanajiongoza kwa akili zao au kwa akili za chama.!?na kama ni kwa akilo za chama je chama kimetoa wapi akili hizo..:?
22 minutes ago via mobile · Like

Mtanzania Kihange Ni vyema Busara ikitumika na sio mitazamo ya watu binafsi

20 minutes ago via mobile · Like

Muhidin Thabeet Kiss Bado Naendelea Kuamini Matatizo Mengi Yanayoikumba Nchi Yetu Yanatokana na Kukosa Busara na Hekma Kwa Viongozi Wetu.

19 minutes ago · Like

Rashid Katakwa ni vizuri tukakumbuka ya kwamba ktk serikali ya rais jk,hakuna hata kiongozi mmoja aliyekuwa na wazo la katiba hata chama chake hakikuwa na ajenda ya katiba,ni busara za rais jk za kuazisha mchakato wa katiba,kwa busara hizo hizo naamini atatuvusha salama hao kina chikawe na wenzake hawajui watendalo!

10 minutes ago · Edited · Like

Mtumishi Stanley Mngoni Rashid unasema ni busara za JK kuanzisha mchakato wa katiba una uhakika na kauli yako?

8 minutes ago · Like

Rashid Katakwa ndio!kwani ilikuwa ktk ilani ya chama chake?

7 minutes ago · Like

Rashid Katakwa katiba haikuwa ktk ilani ya ccm!karibia vyama vyote vya upinzani walitaka katiba mpya!shinikizo toka kwa vyama pamoja na asasi za kiraia kupiga kelele ndio maana jk akatumia busara kusikiliza kelele za wengi!ni busara tu ndugu yangu au ww busara unaitafsiri vp?@mngoni

Thursday, September 19, 2013

Katiba mpya majaliwa


Waziri wa Katiba na Sheria,Mathias Chikawe
Mchakato wa kupata Katiba mpya umeendelea kupingwa, baada ya wanaharakati kuungana na kutoa tamko la kutaka usiharakishwe huku na Rais Jakaya Kikwete, kutousaini Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Mabadiliko ya Katiba kutokana na kutokuwapo kwa uelewa mpana hususani maeneo ya ukinzani likiwamo suala la Muungano.
Kadhalika, wanaharakati hao wamesema uchaguzi wa viongozi wa serikali za mitaa utakaofanyika mwakani pamoja na uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, kisiwe kichocheo cha kuharakisha upatikanaji wa Katiba mpya.

Mbali na kutoa tamko hilo, wanaharakati hao walisema wanajiandaa kwenda Ikulu kumshinikiza Rais Kikwete kutosaini muswada huo sambamba na kumpatia tamko hilo litakalokuwa katika maandishi atakaporejea kutoka nje ya nchi kwa shughuli za kikazi.

Akisoma tamko hilo jana jijini Dar es Salaam kwa niaba ya taasisi nyingine kwenye mjadala wa wazi uliojadili mada kuhusu “Tunajifunza nini kutokana na mchakato wa Katiba nchini Tanzania”, Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), Usu Mallya, alisema asasi zote nchini zisizo za serikali, zijipange upya kwa kuungana kwa lengo la kuurudisha upya mchakato wa kupata Katiba mpya.

Alisema mchakato wa kupata  Katiba mpya usitishwe kwa sasa kwa lengo la kujenga uelewa zaidi wa wananchi juu ya masuala ya Katiba.

Asasi zilizozoungana na kutoa tamko hilo ni pamoja na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (Tamwa), Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), TGNP, Hakielimu, Mfuko wa Wanawake Tanzania (WFT), Jukwaa la Katiba Tanzania na Policy Forum.

Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba Tanzania, Deus Kibamba, alisema mchakato wa kupata Katiba mpya umeanza kushindikana kutokana na kuwapo kwa migongano kwa baadhi ya wadau.

Alisema hamasa kwa wananchi juu ya utoaji na uelewa wa masula ya Katiba bado uko chini tangu mchakato huo ulipoanza.

Kibamba alidai kuwa misingi mikuu mitano ya kutengeneza Katiba imekiukwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba.

Aliyataja mambo hayo ambayo kuwa ni uelewa mdogo wa wananchi juu ya masuala ya Katiba, ushiriki mdogo wa wananchi, umilikishwaji wa Katiba kwa wananchi, uhamasishwaji wa wananchi katika kushiriki mchakato wa kutoa maoni katika Katiba na utekelezaji wa wananchi katika Katiba mpya ulikuwa duni.

“Rais asisaini wala usifike kabisa muswada huo Ikulu, ningependa Rais akirudi kutoka safari zake, asiukute muswada huo Ikulu,” alisema Kibamba.

Aliongeza kuwa endapo Katiba mpya haitapatikana kwa muda uliopangwa, kuna wasiwasi wa watawala waliopo madarakani kuendelea kutawala hadi pale Katiba mpya itakapopatikana.
Alisema pia kuna wasiwasi mkubwa Katiba mpya isipopatikana, uwezekano wa kuendelea kutumika Katiba ya mwaka 1977 utakuwa mkubwa.

Mkuu wa Dawati la Katiba la LHRC, Anna Henga, alisema uelewa wa wananchi wa masuala ya Katiba ni mdogo kutokana na kuchanganya na kushindwa kutofautisha Katiba na siasa.

Alisema mpaka sasa wananchi wengi wanajua siasa ni Katiba na Katiba ndiyo siasa, jambo ambalo siyo kweli na kueleza kuwa siasa ipo ndani ya Katiba, lakini Katiba haipo ndani ya siasa.

Alisema katika rasimu yote ya Katiba, wananchi walikuwa wanajadili mambo ya serikali tatu, Rais, Bunge la Katiba litakuwaje, mambo ambayo ni siasa pasipo kuzungumzia makundi ya kijamii.

Alisema Bunge la Katiba litakuwa na wanasiasa wengi ambao ni wabunge kuliko wananchi, na kueleza kuwa wanasiasa watakuwa asilimia 72.5 na wananchi asilimia 27.

Alifafanua kuwa kutokana na hali hiyo, mchakato wa kupata Katiba mpya umeingia dosari, hivyo Rais asiusaini muswada huo.

“Tutakwenda kwa Rais kushinikiza mchakato huu usisainiwe, sheria ipo inayoruhusu hayo, tuna uwezo wa kuusimamisha kwa kipindi cha miezi sita,” alisema Henge.

Naye Dk. Azaveri Lwaitama, kutoka Kigoda cha Mwalimu Nyerere, alisema shinikizo kutoka nje ya Bunge linaweza kuleta Katiba ambayo siyo makini, na kueleza kuwa rasimu imekuja na mapendekezo ambayo siyo rafiki kwa wananchi.

Alisema Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba, aendelee na mchakato huu hadi mwisho pasipo watu wengine kuuendeleza kwa kuwa itasababisha uchakuaji wa Katiba hiyo.

Aidha, alitaka kujengwa kwa uelewano baina ya Wabunge na wawakilishi wa Bunge Maalum la Katiba ili kuondoa mgangano utakaoweza kutokea.

Aliongeza kuwa  asasi za serikali zilizowahi kuwasilisha maombi ya kupatikana kwa Katiba mpya miaka 10 iliyopita, zimshinikize Rais angalie uteuzi wa wajumbe watakaoingia katika Bunge la Katiba.

“Mchakato usiharakishwe, twende taratibu kwanza, Rais asisaini muswada huo, gharama tuliyoingia katika kuandaa mchakato wa kupata Katiba mpya ni kubwa, hivyo isipotee bure,” alisema Dk. Lwaitama.

Mbunge wa Ubungo (Chadema), John Mnyika, alisema ni vigumu kupunguza idadi ya Wabunge katika Bunge la Katiba badala yake waongezwe wawakilishi na kuwa inawezekana.

Alisema sheria ya kura ya maoni inayokwenda kujadiliwa katika Mkutano ujao wa Bunge itakuwa na umuhimu mkubwa kuliko ile ya Muswada wa Mabadiliko ya Katiba mpya.

Wanaharakati wameungana kupinga mchakato wa Katiba siku chache baada ya vyama vya NCCR-Mageuzi, CUF na Chadema kuungana kuupinga mchakato huo na kushinikiza Rais Kikwete asiusaini Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2013.

Wenyeviti wa vyama hivyo James Mbatia (NCCR-Mageuzi), Profesa Ibrahim Lipumba (CUF) na Freeman Mbowe (Chadema), Jumapili iliyopita walikutana na kukubaliana kuungana kuupinga mchakato huo kwa maelezo kuwa umehodhiwa na  Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Waliazimia kwenda kwa wananchi nchi nzima kuwaelimisha kuupinga mchakato huo na kwa kuanzia, keshokutwa watafanya mkutano wa pamoja katika Viwanja vya Jangwani.
Juzi, viongozi hao walianza kukutana na wadau kadhaa kwa lengo la kufanya mashauriano kuhusu mchakato wa Katiba.

Akizungumza kwa niaba ya wenzake, Profesa Lipumba alisema kuwa uamuzi wao wa kuungana ni kuhakikisha Katiba haitekwi nyara na chama tawala ili Watanzania wapate Katiba mpya na nzuri ambayo imewashirikisha wadau wote.

Wabunge wa vyama hivyo walilazimika kutoka nje ya ukumbi wa Bunge  Septemba 4, 5, na 6 wakipinga kuendeshwa kibabe na Sheria na Kanuni za Bunge kwa kuunyima upande wa Zanzibar haki ya kushiriki katika mchakato wa Katiba mpya.

BARAZA LA VYAMA VYA SIASA KUKUTANA
Wakati huo huo, Baraza la Vyama vya Siasa nchini, linatarajia kukutana Zanzibar kujadili mvutano uliopo wa Katiba mpya na kutoa tamko kuhusu nini kifanyike ili kuinusuru nchi isitumbukie katika machafuko.

Mwenyekiti wa baraza hilo, Peter Kuga Mziray, aliliambia NIPASHE jana kuwa mkutano huo utafanyika Septemba 24, mwaka huu, ambao pamoja na mambo mengine, wajumbe watajadili Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Mabadiliko ya Katiba uliozua vurugu Bungeni.

”Kwenye vikao na Kamati ya Katiba na Sheria, tumeeleza yote haya lakini serikali haikutusikia na sasa imefika mahali mchakato wote wa Katiba umekuwa nuksi,” alisema.

Mziray alisema Rais kama atakubali kusaini muswada, ni wazi kuwa ataiingiza nchi kwenye mgogoro wa Katiba, jambo ambalo litaitumbukiza nchi katika machafuko.

Alisema ajenda ya Katiba mpya siyo ya CCM na kuwa kinachotakiwa kufanywa na serikali ni kuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba itakapomaliza kazi zake na kukabidhiwa ripoti, makabrasha yawekwe kusubiri Rais mwingine atakayekuja aendelee na mchakato wa Katiba mpya.

Aliongeza kuwa kama itaonekana kwamba kuna ulazima sana wa kupata Katiba mpya muda wa serikali ya awamu nne ukipita, iundwe serikali ya umoja wa kitaifa ambayo itaandaa Katiba mpya na uchaguzi mkuu.
 
CHANZO: NIPASHE

Tambwe apiga 4 Simba ikiua 6, Yanga hoi

 
Mshambuliaji wa Simba, Amisi Tambwe akishangilia goli alilofunga dhidi ya Mgambo JKT kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam jana. Tambwe alifunga magoli manne katika mechi hiyo ambayo Simba ilishinda 6-0.
Mshambuliaji mpya wa Simba, Mrundi Tambwe Amisi, jana alifanya ambacho hakijafanyika kwa miaka mingi nchini baada ya kufunga magoli manne peke yake na kuisaidia timu yake kutoa kipigo kikubwa zaidi msimu huu cha magoli 6-0 dhidi ya ya Mgambo JKT, wakati mabingwa Yanga walidondosha pointi nne katika mechi mbili za mjini Mbeya baada ya jana pia kushikiliwa kwa sare ya 1-1 dhidi ya Prisons.
Washindi wa pili mwaka jana, Azam nao walilazimishwa sare ya 1-1 dhidi ya timu iliyopanda daraja ya Ashanti, ambayo ilianza ligi hiyo vibaya kwa kipigo cha 5-0 kutoka kwa Yanga, ambacho ni kipigo cha pili kwa ukubwa katika rekodi mwaka huu Bara.
 
Ushindi kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam uliwaweka Simba kileleni mwa msimamo baada ya kufikisha pointi 10, wakiwashusha waliokuwa vinara wasiotarajiwa JKT Ruvu (9), ambao jana walikumbana na kipigo cha 1-0 kutoka kwa ndugu zao wa Ruvu Shooting.

Shujaa wa siku ya jana, Tambwe alisema baada ya mechi hiyo kwamba kazi sasa imeanza baada ya kuuzoea mfumo wa timu huyo lakini akasisitiza kuwa bado ligi ya Tanzania Bara ni ngumu kuliko ya kwao Burundi.

Tambwe alisema licha ya kuwafunga Mgambo idadi hiyo kubwa ya magoli, timu hiyo ya tanga ni ngumu na kamwe hataidharau timu yoyote.

Mrundi huyo, mfungaji bora wa ligi kuu ya Burundi ambako alifunga magoli 21 katika mechi 18, na kisha kuwa mfungaji bora wa Kombe la Kagame ambako alifunga magoli sita katika mechi sita za michuano hiyo ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati iliyofanyika mjini Darfur, Sudan na kuisaidia timu yake ya zamani ya Vital'O, sasa ndiye kinara wa mabao wa ligi kuu ya Bara akiwa na magoli manne baada ya mechi nne.Anafuatiwa na Jerry Tegete wa Yanga mwenye magoli matatu. 

Hata hivyo, Tambwe si mchezaji pekee kuwahi kufunga idadi kubwa ya magoli peke yake katika mechi moja.

Licha ya magoli yake manne ya jana kuvunja rekodi iliyowekwa misimu miwili iliyopita na mshambuliaji wa Polisi Dodoma, Juma Semsue ambaye alikuwa mchezaji wa mwisho kufunga 'hat-trick' katika Ligi Kuu ya Bara 2011-12, rekodi ya juu kabisa bado inashikiliwa na Edibily Lunyamila aliyefunga magoli sita peke yake wakati Yanga ilipoisambaratisha RTC Kagera kwa magoli 8-0 kwenye ligi hiyo ya juu zaidi nchini mwaka 1998.  

Tambwe aliiandikia Simba goli la kwanza akimalizia kwa kichwa krosi murua ya Issa Rashid 'Baba Ubaya'. Hilo lilikuwa goli la kwanza Mrundi huyo kuifungia Simba ligi kuu msimu huu. Hakufunga katika mechi mbili mfululizo dhidi ya Oljoro JKT na Mtibwa ambazo alicheza dakika zote 180.

Haruna Chanongo alifungia Simba goli la pili katika dakika ya 33 kwa juhudi binafsi akimlamba chenga kipa Kulwa Manzi wa Mgambo lakini mpira ukambabatiza beki Lufunga akapiga tena 'kishuti mtoto' kikatinga wavuni.

Tambwe, ambaye ni mfungaji bora wa ligi kuu ya Burundi, alithibitisha makali yake baada ya kumalizia mpira wa shuti kali la Chanongo lililotemwa na kipa Manzi na kuiandikia Simba goli la tatu katika dakika ya 42.

Dakika moja kabla ya mapumziko, Tambwe alikamilisha 'hat-trick' yake ya kwanza kwenye ligi hiyo mpya kwake na kuwa 'hat-trick' ya kwanza katika Ligi Kuu ya Tanzania Bara tangu msimu wa 2011-12, wakati alipofanya hivyo, Juma Semsue wa Polisi Dodoma, ambayo hata hivyo ilishuka daraja mwaka huo huo. Alifunga goli lake la nne kwa njia ya penalti katika dakika ya 77.

Kikosi cha kocha Abdallah Kibadeni 'King' kilichoanza jana kilikuwa na beki wa kulia Miraji Adam aliyekosa mechi ya Jumamosi walioshinda 2-0 dhidi ya Mtibwa.

Pia kiungo Henry Joseph na mshambuliaji Betram Mwombeki ambao waliingia kipindi cha pili katika mechi ya Jumamosi, walianza katika mechi ya jana huku beki wa kulia Nassoro Masoud 'Chollo', viungo Twaha Ibraham na Said Hamis walioanza Jumamosi, walikuwa benchini jana.

Beki Novat Lufunga wa Mgambo alikuwa na bahati kwa kutoonyeshwa kadi nyekundu baada ya kumpiga kiwiko Tambwe ambaye hakuwa na mpira katikati ya uwanja. Refa Jacob Adonyo kutoka Mara hakumuonyesha kadi yoyote licha ya mfungaji bora wa Kombe la Kagame Tambwe kulazimika kugangwa kwa dakika moja ndani ya uwanja.

Dakika 4 baadaye mshambuliaji Betram Mwombeki, aliyesajiliwa msimu huu akitoka Pamba ya Mwanza, alifanya kosa kama hilo dhidi ya beki Bakari Mtama aliyelazimika pia kugangwa uwanjani lakini hakuonyeshwa kadi yoyote.

Jerry Tegete aliifungia Yanga goli la kuongoza katika dakika ya 41 akimalizia krosi iliyochongwa na Simon Msuva.

Hata hivyo, Prisons walisawazisha goli hilo katika dakika ya 77 kupitia kwa Ibrahim Isaka aliyeunganisha kwa kichwa mpira wa kona iliyochongwa na nyota wa zamani wa Yanga, Omega Seme.

Kabla ya sare ya jana, Yanga pia ilishikiliwa katika sare ya 1-1 dhidi ya Mbeya City Jumamosi kwenye uwanja huo huo wa Sokoine mjini Mbeya. Yanga sasa ina pointi sita baada ya ushindi mmoja na sare tatu. 

Katika mechi nyingine za jana, Kagera Sugar ilishinda 2-0 nyumbani dhidi ya JKT Oljoro, Coastal ilitoka 1-1 dhidi ya Rhino Rangers, Mtibwa ilitoka 0-0 dhidi ya Mbeya City.
Vikosi vilikuwa;

Simba: Abel Dhaira, Miraji Adam, Issa Rashid 'Baba Ubaya', Gilbert Kaze, Joseph Owino, Jonas Mkude, Amri Kiemba, Henry Joseph, Betram Mombeki, Amisi Tambwe, Haruna Chanongo.

Mgambo: Kulwa Manzi, Francis Anyosisye, Salum Mlima, Bakari Mtama, Novat Lufunga, Salum Kipaga, Nassoro Gumbo, Peter Mwalianzi, Mohamed Neto, Fully Maganga, Salum Gila.

Yanga: Ali Mustapha 'Barthez', Mbuyu Twite, David Luhende, Nadir Haroub 'Cannavaro', Kelvin Yondani, Athuman Idd 'Chuji', Simon Msuva, Salum Telela/ Frank Domayo (dk.68), Didier Kavumbagu, Jerry Tegete/ Said Bahanunzi (dk. 72) na Haruna Niyonzima.

Prisons: Beno David, Beno David, Salum Kimenya, Laurian Shabani, Jumanne Elfadhili, Nurdin Issa, Jimmy Shoji, Fredy Chudu, Ibrahim Isaka, Six Ali, Jeremia Juma, Lugano Mwagomba.
 
CHANZO: NIPASHE

Tanzania yashitukia Afrika Mashariki;

sitta21_13c02.jpg

SERIKALI ya Tanzania imeshitukia mikakati ya baadhi ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), ya kutaka kuharakisha Shirikisho. Akizungumza na waandishi wa habari jana, Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta, alisema Kenya, Uganda na Rwanda zimeitenga Tanania katika masuala ya Jumuiya.

Katika hili, alisema nchi hizo zilikubaliana ifikapo Oktoba 15, Rasimu ya Kwanza ya Uundwaji Shirikisho itolewe na ifikapo mwakani nchi hizo zianze kutumia viza moja.
 
Alifafanua, kwamba kwa mujibu wa Ibara ya 7(E) ya Mkataba wa EAC, baadhi ya nchi wanachama wana haki kukutana na kuharakisha zaidi katika mambo ya ushirikiano, lakini mikutano na makubaliano vinatakiwa kupita kwenye sekretarieti, ili nchi wanachama zielewe kinachoendelea, jambo ambalo halifanyiki.
"Nchi mbili au tatu zinaruhusiwa kwenda kwa kasi zaidi katika mambo yanayohusu ushirikiano na hilo si jambo la ajabu. Kushirikiana katika miradi ya nchi tatu au nne si jambo la ajabu, lakini kufanya hivyo kwa kuitenga nchi iliyo kwenye Jumuia moja kwa moja, ni tatizo," alisema Sitta.
 
Kutengwa Alisema Kenya, Rwanda na Uganda tayari zina makubaliano yao, mbali na kuanza kutumia viza moja, bali Oktoba 15 waanze kutumia vitambulisho vya Taifa, kuvuka mipakani. Alikiri kuwa katika mikutano iliyofanywa na nchi hizo wanachama wa EAC iliyofikia uamuzi huo, Tanzania haikushirikishwa.
"Suala la viza moja hatuko tayari, kama wenzetu wanaona linawasaidia basi waendelee, suala la kutumia vitambulisho vya Taifa katika kuvuka mipaka hatuko tayari, wao wanaweza kuendelea na uharakishwaji wa kuunda Shirikisho hatuko tayari," alisema.
 
Msimamo "Kama msimamo wa wenzetu ni kuundwa kwanza kwa Shirikisho na matatizo mengi yatatuliwe ndani, wao kama nchi wana uhuru wa kufanya hivyo na tunachoomba ni kushirikishwa, ili kuona tunaingia vipi tukiwa tayari.
 
"Sisi tuna uzoefu wa kuungana na kama hawataki kusikiliza, basi waendelee ... hatutaki kuwa mbali na tutakapoona mambo mazuri ndani ya Shirikisho hilo tutajiunga baadaye," alisema.
Alifafanua, kwamba katika kuhakikisha Shirikisho linakuwa endelevu, walikubaliana kukamilisha hatua tatu za utengamano; kwanza kabla ya Shirikisho, ambazo ni ushuru wa pamoja, soko la pamoja na mfumo wa sarafu moja.
Kwa mujibu wa Sitta, ukamilishaji wa hatua hizo, ndio utawapa wananchi kujiamini katika kuanzisha Shirikisho. Katika utekelezaji wa hatua za kwenda katika Shirikisho, Sitta alisema Tume ya Wataalamu iliundwa, kutafuta maoni ya wananchi kuhusu Shirikisho na muundo wake.
Pia katika kura ya maoni ya wananchi mwaka 2006 /2007, asilimia 84 ya Watanzania walisema hawapendi Shirikisho liharakishwe.
 
"Hiyo Tume ya Wataalamu inayoundwa na wajumbe kutoka nchi zote za Jumuiya, wanatakiwa kutoa taarifa kwa wakuu wa nchi Novemba, na tumetumia fedha kufanywa utafiti huo," alisema.
Miradi hatarini Sitta alisema kutoshirikishwa kikamalifu kwa nchi moja au mbili katika mikutano na uamuzi, kunachangia utekelezaji wa miradi iliyokubaliwa kwenye Jumuiya kutofanikiwa.
 
"Mfano, mwaka jana chini ya Rais Mwai Kibaki wa Kenya, kila nchi ilipeleka miradi na tulikubaliana kusaidiana kutafuta fedha za kuikamilisha, mfano ujenzi wa reli, na wa nguzo za umeme kwenda Kenya.
"Sasa wakifanya mikutano bila kushirikishana, tunaweza kuendelea na miradi ambayo sisi si kipaumbele chetu, ukiamini kuwa inachangia kwenye jumuiya kumbe wengine hawataki.
 
"Huwezi ukaweka kipaumbele katika kujenga reli mpaka nchi jirani, wakati nchi husika haitapitisha mizigo kwako, hapo kuna faida gani na hata kama sehemu kubwa ya reli itasaidia usafiri nchini kwako?" Alihoji.
Baadhi ya miradi ya ushirikiano ambayo Tanzania ilitakiwa kuitekeleza ni ujenzi wa reli kutoka Isaka kwenda Rusumo mpakani na Rwanda na Uvinza hadi mpakani mwa Burundi na ujenzi wa nguzo za umeme wa kilowati 400 kupitia Namanga kwenda Kenya. Tanzania na Burundi ndizo nchi pekee ambazo hazijaalikwa kwenye mikutano ya uundwaji wa Shirikisho unaofanywa na Kenya, Rwanda na Uganda.
 
Hivi karibuni, Tanzania na Rwanda ziliingia katika sintofahamu, baada ya Rais Jakaya Kikwete, kwa nia njema, kumshauri Rais Paul Kagame akae meza moja na waasi kuzungumzia amani akakataa na kumshutumu mshauri huyo.

source: mjengwa blog

Tunapokaribia 2015, JK akumbuke zigo la ahadi


“Wakati wa kampeni nilibezwa sana, lakini sasa ninawaomba walionibeza kufika vijijini na kuangalia ukamilishaji wa ahadi zangu. Nataka waje waone, kwa sasa ninakamilisha usambazaji wa umeme katika vijiji vyote ili kufikia lengo la Watanzania asilimi 30 kufikiwa na nishati hiyo. Hadi 2015 umeme utakuwa umesambaa nchi nzima. Rais Kikwete 

Ahadi ni deni, kumbe isipotimizwa inabaki kuwa deni kwa mhusika
Akiwa ziarani mkoani Mwanza hivi karibuni, Rais Jakaya Kikwete amesema wale wote wanaombeza kuhusu utendaji wake, wataona aibu atakapomaliza muhula wake mwaka 2015.

Kikwete amewananga pia baadhi ya wanaCCM wenzake kwa kushindwa kuyaelezea mafanikio ya Serikali yao.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mradi wa kusambaza umeme katika mikoa ya Mwanza na Geita unaofadhiliwa na Mfuko wa Changamoto za Milenia (MCC), Rais Kikwete alisema:

“Wakati wa kampeni nilibezwa sana, lakini sasa ninawaomba walionibeza kufika vijijini na kuangalia ukamilishaji wa ahadi zangu.

“Nataka waje waone, kwa sasa ninakamilisha usambazaji wa umeme katika vijiji vyote ili kufikia lengo la Watanzania asilimi 30 kufikiwa na nishati hiyo. Hadi 2015 umeme utakuwa umesambaa nchi nzima.
 “La umeme, leo nazindua nataka kuwaeleza walionibeza waje waone sasa ahadi zangu...hayo yote niliyasema kwenye ahadi zangu 2010.”

Mradi huo umegharimu Dola za Marekani 15.54 milioni sawa na Sh24.87 bilioni kwa Mwanza na Geita pekee, fedha ambazo ni asilimia 25 ya Dola za Marekani 62.6 milioni sawa na Sh103.24 bilioni zilizotengwa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi 225 ya upanuzi wa njia za kusambazia umeme katika mikoa kumi nchini.

Rais Kikwete alisema Serikali inajipanga kusambaza umeme na kufikiwa vijiji vyote na kubainisha kuwa mpango huo unakwenda sambamba na uanzishaji wa vyanzo vipya vya umeme ili viweze kuzalisha megawati 3,000 ifikapo mwaka 2015 na kwamba ziada itauzwa nje ya nchi.

Kikwete akawageukia baadhi ya viongozi wa chama chake na kusema kuwa ni dhaifu katika uongozi kwani wameshindwa kueleza mafanikio ya serikali yao ya CCM.

Ahadi za Kikwete 2010-2015
Wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu, Kikwete alitoa zaidi ya ahadi 70 na hadi sasa nyingi hazijatekelezwa. Zifuatazo ni baadhi ya ahadi hizo.

Viwanda
Akiwa jijini Tanga, alitoa ahadi ya kulifanya jiji hilo kuwa la viwanda, hadi sasa hakuna hata dalili kwani baadhi ya viwanda vimeendelea kufa.

Aliahidi pia kuifanya Mtwara kuwa mji wa viwanda. Ndoto hizo ziko mbioni kutimia hasa kutokana na uvumbuzi wa gesi. Tayari, kuna kiwanda cha saruji kimeanza kujengwa.

Vilevile, aliahidi ujenzi wa kwanda cha dawa ya kuua viluilui vya mbu na kuifanya wilaya ya Kibaha kuwa eneo maalumu la viwanda.

Maji
Ahadi nyingine ni ile aliyoitoa wilayani Igunga ya kuufanya mkoa wa Tabora kutumia maji ya Ziwa Victoria. Mradi huo bado unaendelea kutekelezwa.
Aliahidi pia kuvipatia maji vijiji vyote vilivyoko kilomita 15 kutoka kwenye bomba kuu la mradi mkuu wa maji wa Ziwa Victoria - Shinyanga-Kahama.

Kilimo
Kuhusu kilimo, aliahidi kulipa madeni ya Chama Kikuu cha Ushirika Mkoa wa Shinyanga (SHIRECU).

Aliahidi pia kumaliza migogoro ya ardhi nchini na kwamba wakulima wataacha kutumia jembe la mkono na kuwapatia matrekta alipokuwa mkoani Dodoma.
Hadi sasa zaidi ya asilimia 75 ya Watanzania wamejiajiri kwenye kilimo huku asilimia 90 wakitegemea jembe la mkono.

Katika suala la nishati aliahidi kupatikana kwa umeme eneo la Mutukula mkoani Kagera. Umeme huo ni kutoka Uganda.

Aliahidi pia kuiunganisha mikoa ya Kagera, Kigoma, Lindi, Rukwa na Ruvuma katika gridi ya taifa ya umeme ahadi ambayo inaendelea kutekelezwa.
Aliahidi kununua meli kubwa kuliko Mv Bukoba alipokuwa mkoani Kagera. Meli hiyo haijanunuliwa hadi leo, japo mwenyewe ameendelea kusisitiza kuwa atanunua meli mbili.

“Serikali yangu itavunja rekodi ya kusambaza umeme katika vijiji vingi nchini…Tumejenga mtandao wa barabara kwa sasa, hali yetu ya barabara ni bora Afrika Mashariki, tuliahidi meli Bukoba, naomba niwaeleze kuwa zinakuja, tena siyo moja ni meli mbili,” amesema wiki iliyopita alipokuwa jijini Mwanza.
Alipokuwa jijini Mwanza aliahidi kuanzisha benki ndogondogo kwa ajili ya wajasiriamali na Serikali kuvisaidia vyama vya ushirika.

Aliahidi pia kuimarisha usalama Ziwa Victoria na Ziwa Tanganyika kwa kupeleka kikosi maalumu chenye vifaa kupambana na wahalifu.

Akiwa mkoani Mbeya mjini aliahidi kununua meli mpya kubwa Ziwa Nyasa, lakini hadi sasa haijatimizwa.
Aliahidi pia kujenga bandari ya Kasanga alipokuwa mkoani Rukwa.

Elimu
Akiwa Songea, Ruvuma, Kikwete aliahidi kumaliza tatizo la walimu. Hata hivyo, ahadi hii inaonekana kushindikana kutokana na mvutano wa kimasilahi kati ya walimu chini ya chama chao (CWT) kiasi cha kufikishana mahakamani.

Hivi karibuni, Mwenyekiti wa CWT, Gratian Mukoba alisema walimu wanaidai Serikali kiasi cha Sh33 bilioni.

Mbali na madai ya elimu, kumekuwa na anguko kubwa la ufaulu wa wanafunzi. Matokeo ya kidato cha nne ya mwaka 2012 yameonyesha angoko hilo ambapo waliopata daraja sifuri wamefikia zaidi ya asilimia 60.

Afya  
Akiwa Iringa, aliahidi kununua pikipiki za matairi matatu (bajaj)  400 kwa ajili ya kubeba wajawazito hasa vijijini

Aliahidi pia kununua vyandarua viwili kwa kila kaya akiwa mjini Mbeya.

Aliahidi pia kuzipandisha hadhi hospitali maalumu saba nchini kuwa za rufaa ili kuipunguzia mzigo Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MHN). Hiyo ni ahadi ya Hydom mkoani Manyara.

Licha ya kuanza kutekelezwa kwa baadhi ya ahadi katika sekta ya afya, mwaka 2012 umekuwa na matukio ya migomo ya madaktari wakidai nyongeza ya mishahara na posho.

Mgomo huo uliishia kwa aliyekuwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari, Dk Steven Ulimboka kutekwa na kuteswa katika msitu wa Pande nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam.

Huku Kikwete akisisitiza Serikali yake kutohusika na utekaji huo, hakufikia mwafaka na madaktari hao licha ya kutekeleza baadhi ya madai yao.

Miundombinu
Kuhusu miundombinu aliahidi kujenga Uwanja wa Ndege wa Misenyi Mkoani Kagera na kupanua Uwanja wa ndege Bukoba  alipokuwa Bukoba Mjini na alipokuwa Kigoma mjini aliahidi kujenga uwanja mkubwa wa ndege.

Hadi sasa ahadi hiyo inaendelea kutekelezwa. 
Akiwa Same, Kilimanjaro, aliahidi pia kujenga Barabara yenye kiwango cha lami kutoka Same - Kisiwani, Kihurio na kuiunganisha na barabara kuu ya Moshi - Dar es Salaam.

Pia, aliahidi kujenga barabara ya Njombe - Makete kwa kiwango cha lami, urefu wa kilomita 109 akiwa Iringa mjini na kujenga barabara Musoma hadi Mto wa Mbu akiwa Arusha.

Aliahidi pia kujenga barabara ya lami  ya Manyoni, Kigoma Kaliua na Tabora na kuboresha barabara ya Handeni, Kondoa- Singida.  Ahadi hii inaendelea kutekelezwa.

Aliahidi pia kujenga reli mpya kutoka Dar es Salaam mpaka mikoa ya Kanda ya Ziwa. Aliitia akiwa wilayani Nzega mkoani Tabora na bado haijatekelezwa hadi sasa.

Uhasama wa kidini
Akiwa wilayani Musoma, Mkoa wa Mara, Rais Kikwete aliahidi kulinda amani nchini kwa kuzuia chokochoko za kidini, kikabila na kisiasa.

Hata hivyo, katika kipindi hiki, uhasama huo umeongezeka kiasi cha kuwepo kwa vurugu za uchomaji makanisa, misikiti, viongozi wa dini kumwagiwa tindikali na wengine kuuawa kwa risasi.

source: mjengwa blog