Ndugu zangu,
Ndugu Kingunge Ngombale Mwiru ni mmoja wa wanasiasa ninaowaheshimu sana. Nimemsikia Kingunge tangu nikiwa na miaka saba.
Lakini, kama ilivyokuwa kwa Mwalimu Nyerere, hakuwa malaika, Kingunge naye ni mwanadamu kama wengine. Si malaika.
Nimeyasikia mawazo ya Kingunge juu ya
Serikali Tatu na hata Uraia wa Nchi Mbili. Ni mawazo yake, nayaheshimu,
ingawa, kwa mtazamo wangu, Kingunge hayuko sahihi kwenye yote mawili.
Na hapa nitalizungumzia hili moja tu la mapendekezo ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba juu ya muundo wa Muungano wa Serikali Tatu.
Kimsingi haya ni mapendekezo yenye
kutokana na maoni Wananchi. Hivyo, Tume imewasilisha tu. Si mapendekezo
ya Jaji Warioba au wajumbe wake.
Hii ni tofauti kubwa na mazoea ya '
Ukale' ya Mzee Kingunge ambayo hata sasa anataka yafuatwe; kuwa jambo
kubwa la muundo wa Muungano liachiwe Chama Cha Mapinduzi na vikao vyake.
Ni jambo jema kwa mwanadamu kujifunza
kutokana na historia, lakini, si jambo jema kwa mwanadamu kuwa mtumwa wa
historia. Ni bahati mbaya, kuwa Mzee wetu mpendwa, Kingunge Ngombare
Mwiru, anataka tubaki kwenye utumwa wa historia. Hatutaki.
Na hakika Mzee Kingunge anapaswa
kuelewa, kuwa nchi hii ni zaidi ya Chama cha Siasa. Na chama cha siasa
kilicho madarakani hakiongozi mawe. Na hata kama kingekuwa kinaongoza
tumbiri, bado kingekumbwa na changamoto ya uwepo wa tumbiri wenye kutaka
mabadiliko, kulingana na mahitaji ya wakati.
Tukubali, kuwa yalifanyika makosa
makubwa ya kiuongozi huko nyuma. Ni pale masuala makubwa ya kitaifa
kuachwa maamuzi yake kufanywa na kundi dogo la watu kwa kutumia nyadhifa
za uongozi wa chama. Kwenye masuala makubwa ya nchi Chama kiliamua juu
ya vichwa vya watu bila kushirikisha mawazo ya wananchi wenyewe, iwe kwa
kupitia kura za maoni au kukusanya tu maoni ya makundi wakilishi. Huo
ni msingi wa manung'uniko mengi ya sasa.
Kwangu mimi, Jakaya Kikwete ni
mwanamageuzi wa kweli ambaye, kama kiongozi, ameonyesha ujasiri mkubwa
wa kuzipa mgongo fikra za ukale na kuiangalia zaidi nchi na mustakabali
wake kwa miaka mingi ijayo. Anafanya hivyo bila kujali nani au chama
gani kitakuwa madarakani.
Wakati Mzee Kingunge na wahafidhina (
wasiotaka mabadiliko) wengine ndani ya mfumo uliopo wanatoka mahandakini
huku wakihaha kujaribu kuurudisha nyuma mshale wa mabadiliko chanya kwa
jamii , Jakaya Kikwete anaonekana, kuwa sio tu amesimama imara katika
kuhakikisha mshale wa saa ya mabadiliko chanya kwa nchi unakwenda mbele,
bali, unakwenda mbele kwa kasi.
Ni imani yetu, Wananchi walio wengi,
kuwa Jakaya Kikwete hatakatishwa tamaa wala kuyumbishwa katika
kukamilisha ajenda yake njema ya mabadiliko chanya kwa jamii ya
Watanzania kuelekea miaka 50 ijayo.
Mzee Kingunge aelewe pia, kuwa wakati umebadilika. Kuwa ya mwaka 1974 alipojiunga na TANU ni tofauti na ya sasa, mwaka 2013. Huu ni wakati wa kiongozi kuonyesha uwezo wa kusoma alama za nyakati. Hivyo, kujitahidi kuendana na mabadiliko ya nyakati.
Hiyo pia ndio tafsiri ya kuwa ' Kiongozi wa Kisasa na Kimaendeleo'- A modern and progressive leader. Jakaya Kikwete kwa sasa yumo kwenye kundi hilo.
Na wenzake ndani ya CCM wakimsaidia
katika kazi yake, basi, ni fursa pia kwa Chama chao kuiteka tena mioyo
ya Wananchi wengi, mijini na vijijini. Maana, kati ya ambayo
yanawachosha wananchi ni kukosekana kwa mawazo ya usasa na ya
kimaendeleo kutoka kwa miongoni mwa viongozi wa CCM. Ni moja ya sababu
ya chama hicho kupungukiwa na mvuto hususan kwenye kundi kubwa la
vijana.
Na hakika, hata kama hatuoni leo,
historia itakuja kumkumbuka Jakaya Kikwete kama mmoja wa viongozi
Wana-Mageuzi ndani ya Chama chake CCM, na nchi kwa ujumla.
Maggid.
Iringa.
0754 678 252
Iringa.
0754 678 252
Comments!
Thabit Molly Ni kweli japo na mimi napingana na wewe katika suala la uraia wA NCHI MBILI
41 minutes ago · Like · 1
Goddy Semwaiko
sijakuelewa Maggid. hujaeleza Kingunge kaongea nini na kwa point zipi
wewe unapishana nae. hebu nifafanulie tuweze kuchangia na kujadiliana.
naona umetumia muda mwingi kumlaumu, nadhani na yeye ana uhuru wa mawazo
na mchango wake. Haya mimi sijamsikia huyu babu kaongea nini,
nihadithie
36 minutes ago · Like · 2
Thabit Molly Kama uko Tz fatilia magazeti yote yameongelea alichoongea mzee Kingunge jana@Goddy Semwaiko
29 minutes ago · Edited · Like · 1
Maggid Mjengwa Baada
ya kukaa kimya muda mrefu, mwanasiasa mkongwe nchini, Kingune
Ngombale-Mwiru, ameibuka na kuwatupia lawama viongozi wa CCM, kwa kutaka
kupenyeza suala la uraia wa nchi mbili ndani ya Katiba Mpya.Akizungumza
na waandishi wa habari nyumbani kwake, ...See More
32 minutes ago · Like · 2
Goddy Semwaiko OK.
Mimi sioni tatizo na naungana mkono moja kwa moja na huyu mzee.
Nakubaliana nae kabisa, kama hoja ya muhimu inajadiliwa na kundi dogo la
watu na kutumia fursa yao kutengeneza Kitabu wanachokiita Ufafanuzi wa
Rasimu ya Katiba, sidhani kama watu hao wana haki ndani ya kundi kubwa
la wanachama. Sasa Maggid wewe unalalamika nini hapo? Kiasi cha
kumshambulia huyu mzee???
27 minutes ago · Like
Maggid Mjengwa Goddy,
nimejikita kwenye Serikali Tatu. Kingunge hataki Serikali Tatu, anataka
tubaki tulikokuwa. Hayuko sahihi. Kwa mtazamo wangu. Hata la Uraia wa
nchi mbili napingana nae. Nitalifafanua.
14 minutes ago · Like
Goddy Semwaiko Mimi
Naona serikali tatu ni tatizo Kubwa mno, na gharama zisizo na sababu.
Kama serikali moja haiwezekani, basi serikali mbili ziangaliwe upya.
Ingawa najua upande wa pili hawataki kusikia swala la serikali mbili.
Mimi binafsi kwakweli serikali tatu ni kudanganya wenyewe, kwani haiwezi
kudumu wala hakutakuwa na la msingi kwa hii serikali ya muungano.
Kuhusiana
na swala la Uraia wa nchi mbili pia, sioni umuhimu, na swala la fursa
na uwekezaji, bado wanaotaka kuwekeza nchini mwao wanaweza tu, mbona
kuna wawekezaji ambao si raia wa nchi hii na wanafanya vizuri
kibiashara? Iweje raia anaepata fursa huko nje ashindwe kuwekeza hapa,
hata kama akiukana uraia wa nchi hii, anaweza kuwekeza kama mgeni, tena
atakuwa mgeni mwenye kujua in and out. Swala la uwekezaji kutetea uraia
wa nchi mbili nalo naliona halina mashiko....
Leta hoja Maggid...
source: mjengwa blog