WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Friday, February 28, 2014

Neno Fupi La Leo: Bunge La Katiba Na Kisa Cha Risasi Ya Mwisho...!

Ndugu zangu,
Jana katika nyakati tofauti nimefuatilia mjadala wa rasimu ya kanuni za Bunge hilo.
Kuna wakati nimejiuliza; hivi wote mle ndani wanajua maana ya dhamana kubwa waliyobeba kwa ajili ya nchi hii, leo na kesho?
Kwamba hawapaswi kuonyesha aibu ile ya kujikita kwenye kujadili mustakabali wa taifa kwa kuvaa miwani ya makundi na vyama vyao vya siasa. Kuingia kwenye ushabiki kama wa Simba na Yanga. Maana, inahusua masuala ya msingi yaliyo mbele ya uhai wa vyama vya siasa.
Katiba ni dira ya nchi. Ni ramani ya kutuongoza Watanzania wa leo na wajao, bila kujali makundi na vyama vya siasa.
Kwa WaTanzania, madai ya kupata Katiba mpya ni madai halali yanayotokana pia na kukosekana kwa Haki, Uwazi na Uwajibikaji, hususan kutoka kwa baadhi ya wenye kupewa dhamana za uongozi.
Watanzania ni kama kisa cha wanakijiji waliokuwa kwenye shida ya njaa ya miaka hamsini. Na katika kuhangaika kwao,na kwa risasi yao ya mwisho waliyobaki nayo kwenye gobore moja na la pekee kijiji kizima, wamekaa kikao na kujadili wafanyeje ili wampate mwenzao atakayekwenda mbugani kuwinda mnyama ili aokoe njaa yao.
Na Jemedari wao, baada ya kutafakari, amewateulia mwenzao anayedhaniwa kuwa makini na mahiri kwa uwindaji. Mwenye uwezo wa kulenga shabaha, na hivyo, kuitumia vema risasi hiyo moja iliyobaki kwenye kumlenga nyati na kumwangusha. Kwamba abebe gobore lenye risasi moja, na aingie nalo msituni kuifanya kazi hiyo.
Aliyekwenda mbugani nyuma amewaacha wengi wenye matumaini ya kuusikia mlio wa gobore utakaoshiria mnyama mkubwa ameangushwa mbugani.
Na hakuna habari mbaya, kama wanakijiji wale watakapousikia mlio huo na kukimbilia mbugani kujionea. Na huko wamkute mwenzao ameitumia risasi ile ya mwisho kwa kumlenga na kumwangusha nyani badala ya nyati waliyemtarajia!
Na kwa mila za wanakijiji wale, nyani haliwi,na ni mwiko.
Na Bunge la Katiba lijione kuwa lina fursa adhimu ya kutimiza ndoto ya Watanzania ya kupata Katiba Bora yenye kukidhi mahitaji ya sasa na hata miaka mia moja ijayo.
Kwa Wabunge wa Bunge la Katiba kwenda Dodoma na kurudi na nyani badala ya nyati, sio tu kutawakatisha tamaa Watanzania, bali, kutawafanya Watanzania wawadharau Wabunge hao na hata kuhoji uzalendo wao kwa nchi yao waliyozaliwa.
Ni Neno Fupi La Leo.
Maggid Mjengwa,
Dar es Salaam.
0754 678 252(P.T)

Tuesday, February 25, 2014

Marekani kupitia upya uhusiano wake na Uganda

Uganda_Gays_Leff_16b7f.jpg
 
Na Fadhy Mtanga SERIKALI ya Marekani imeanza mchakato wa kuupitia upya uhusiano wake na Uganda, taifa la Afrika Mashariki baada ya rais wa nchi hiyo kutia saini mswada unaoharamisha vitendo vyote vya kishoga nchini humo.  Hapo jana, jijini Entebbe, rais wa Uganda aliweka saini katika msaada huo ili kuwa sheria rasmi ya Uganda.  Kitendo hicho kimelalamikiwa sana na mataifa ya Marekani na Uingereza kwa madai kinakiuka haki za kibinadamu.
 Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani imetoa taarifa kupitia kwa waziri wake, John Kerry ikieleza kuwa serikali ya rais Barack Obama itahakikisha uhusiano wake na Uganda unazingatia sera yake ya kuzuia unyanyasaji wa aina yoyote.
 Katika taarifa hiyo iliyotumwa kwa barua-pepe kwenda kwenye gazeti la Daily Nation la Kenya, Kerry amesema, "Kwa kuwa sasa hii sheria imekwishapitishwa, tunaanza mchakato wa ndani kuhusiana na uhusiano wetu na Serikali ya Uganda ili kuhakikisha namna zote za mahusiano yetu, ikijumuisha misaada ya kimaendeleo zinaakisi dhima yetu ya kuondoa unyanyasaji na ubaguzi."
 Waziri huyo wa mashauri ya kigeni wa Marekani amepigia chapuo kufutwa kwa sheria hiyo.  "Hii ni siku ya msiba mkubwa kwa Uganda na wote wanaojali kuhusu haki za kibindamu.  Kimsingi, suluhisho pekee ni kufutwa kwa sheria hii."
 Kuwekwa sahihi kwa sheria hiyo kumewagutua Marekani, Uingereza na jumuiya zingine zinazopigia debe mashoga kupewa haki.  Tayari rais Barack Obama ametoa taarifa kupitia kwa katibu wake kuwa, "rais wa Uganda amefanya kitendo kichachostahili kujutiwa kwa kuwa ameirudisha nchi yake nyuma badala ya kusimamia uhuru na haki sawa kwa watu wake."
 Kerry, katika taarifa yake ameeleza wazi kuwa Marekani imekuwa ikiupinga mswada huo toka ulipofahamika miaka minne iliyopita.  Ameeleza zaidi kuwa sheria hiyo inakinzana na uwepo wa Tume ya Haki za Binadamu ambayo ipo kwa mujibu wa katiba ya Uganda.
 "Kutoka Nigeria hadi Russia na Uganda, tunafanya kazi ulimwengu mzima kuhamasisha na kulinda haki za kibidamu kwa watu wote.  Marekani itaendelea kusimama imara dhidi ya jitihada zozote kuwatenga, kuwaharamisha na kuwaadhibu wahanga wowote wake katika jamii yoyote ile."  Alisema Kerry.
 Kitendo hicho cha Museveni kimeibua hisia kali kutoka kwa baadhi ya taasisi za kimataifa ikiwemo makao makuu Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani.  Tayari Katibu Mkuu Ban Ki-moon ameeleza azma yake ya kulijadili jambo hilo la kupinga ushoga pindi atakapokutana na balozi wa Uganda katika Umoja wa Mataifa
source: mjengwa blog

Anayeona posho haimtoshi afungashe virago’

bunge_4f64b.jpg
Dodoma. Wizara ya Fedha imepigilia msumari maombi ya wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba ya kutaka waongezewe posho na kusema anayeona ameacha kazi inayomlipa zaidi kwenda bungeni afungashe virago na kuondoka.
Msimamo huo umekuja siku moja tu baada ya gazeti hili kudokeza kuwa madai ya wajumbe wa bunge hilo kutaka waongezewe posho kutoka Sh300,000 za sasa kwa siku, yamegonga mwamba baada ya kamati iliyoteuliwa kuchunguza uhalali wake kusema kiwango hicho kinatosha.
Mwenyekiti wa muda wa bunge hilo, Pandu Kificho alisema jana bila kutaja viwango, kuwa ripoti ya kamati hiyo imewasilishwa kwa Rais Jakaya Kikwete kwa uamuzi.
Madai ya wajumbe kutaka waongezewe posho, yamechafua hali ya hewa ndani na nje ya Bunge, huku baadhi ya wananchi wakipaza sauti zao na kumsihi Rais Kikwete alivunje bunge hilo iwapo wajumbe watashikilia msimamo wa kutaka nyongeza ya posho.
Jana, Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba alisema wanaoshiriki kutunga Katiba ni Watanzania na siyo wataalamu washauri waliokodiwa kutoka nje.
Alisema kwa msingi huo, Serikali ilitarajia kuwaona watu hao wakitanguliza uzalendo zaidi badala ya kudai malipo manono.
"Katika kutengeneza Katiba hii, hatujakodi consultants (wataalamu washauri) kutoka Uingereza, Marekani, Kenya, Uganda wala nchi nyingine yoyote... Hawa ni Watanzania na kazi wanayoifanya ni yao," alisema.
"Wangekuwa wataalamu wa kukodi wangeweza kudai malipo hayo, lakini hapa ni tofauti... wanafanya kazi yao na kila mtu anafanya kazi yake na anapaswa kujivunia kushiriki katika tendo hili la kihistoria kwa kutanguliza uzalendo," alisema.
Nchemba alisema anazielewa hoja za baadhi ya wajumbe walioibua suala la posho, lakini kwa mtazamo wake, hoja hiyo hata kama ingekuwa na mashiko kiasi gani, imewasilishwa wakati usiokuwa mwafaka. Alisema wapo makandarasi na wazabuni waliotoa huduma kwenye taasisi mbalimbali za umma lakini hawajalipwa.
Alisema kwa kawaida, Februari ni mwezi mbaya kwa kuwa baadhi ya wilaya zina historia ya kukumbwa na uhaba wa chakula hivyo kuhitaji fedha nyingi za Serikali ili kuokoa maisha ya watu katika maeneo hayo.
Pia alisema si wakati mwafaka wa kudai nyongeza hiyo hasa ikizingatiwa kuwa kuna walimu wapya 30,000 nchini kote ambao hawajapangiwa vituo kutokana na kukosekana kwa fedha za kulipa stahiki zao.
Nchemba alisema mbali na walimu hao wapya kutokupangiwa vituo, walimu wengine wanadai malimbikizo ya fedha zao na kwamba hawajalipwa kutokana na ufinyu wa bajeti serikalini.
"Siku zote ukweli unauma. Nasema kama kuna mjumbe ambaye anaona huko alikokuwa kabla ya kuteuliwa alikuwa anapata pesa zaidi kuliko hii, basi kwa heshima afungashe virago na kuondoka," alisema.
Aibu kwa mjumbe
Akizungumzia suala hilo la posho, Mjumbe wa Bunge hilo, David Kafulila (picha ndogo chini) alisema ni aibu kwa wajumbe ambao wameaminiwa na Watanzania na kupewa jukumu zito la kutunga Katiba, kuanza kujadili nyongeza ya posho.
"Ninachokiona ni tatizo la standard (viwango) vya posho... hakuna standard kwamba posho ilipweje, kwa nani na kwa kiasi gani. Mtu akidai leo kwamba Sh300,000 ni ndogo tunajiuliza ni kwa standard ipi?" alihoji.
Kamati ya Posho
Kamati iliyoundwa na Mwenyekiti wa Muda wa bunge hilo, Pandu Ameir Kificho kushughulikia madai ya nyongeza hizo, zinasema imeshauri kuwa kiwango kinacholipwa sasa kinatosha.
Kamati hiyo inaundwa na William Lukuvi, Mohamed Abood Mohamed, Freeman Mbowe, Paul Kimiti, Jenister Mhagama na Asha Bakari na taarifa yake imekwishakabidhiwa kwa Kificho.
Mmoja wa makatibu wa bunge hilo, Yahya Khamis Hamad alikaririwa juzi akisema suala la posho limetoka mikononi mwa Kificho na mapendekezo yake yameshapelekwa serikalini.
Hoja ya kutaka nyongeza ya posho iliibuliwa na wajumbe wawili ambao pia ni wabunge wa CCM, Richard Ndasa (Sumve) na Suleiman Nchambi (Kishapu).

CHANZO: MWANANCHI

Monday, February 24, 2014

museveni atia sahihi muswada wa sheria ya mapenzi ya jinsia moja

yoweri-museveni-007 33b7d
Hatimae Rais wa Uganda YOWER KAGUTA MUSEVEN mapema leo mchana ametia sain muswada wa sheria ya mapenzi na ndoa za jinsia moja, ambapo sasa raia wa uganda atakae patikana na kosa hilo atatahukumiwa kifungo cha maisha jela. Museveni amesisistiza kwamba ametia sain muswada huo kwa kuzingatia kwamba suala ushoga na usagaji   si udhaifu wa kimaumbile wakuzaliwa nao  bali ni tabia ya kujifunza.(Hudugu)

source: mjengwa blog

Kuhusu Milipuko Ya Mabomu Zanzibar...

Mji wa kitalii wa Zanzibar wa Stone Town ambako raia wawili wa Uingereza wamemwagiwa tindi kali
Ndugu zangu,
Nimepokea kwa mshtuko na masikitiko habari juu ya matukio ya milipuko ya mabomu mawili ya kutengenezwa nyumbani; moja jirani na kanisa na lingine kwenye mgahawa ambao pia ni maarufu kwa watalii wa kigeni. Hakuna aliyepoteza maisha.
Naungana na ndugu zetu wa Zanzibar kulaani vitendo hivi vya kishenzi na vyenye kutishia uhai wa raia wema na wasio na hatia.
Na hakika, habari hizi hazitoi taswira njema ya Zanzibar na nchi yetu kimataifa. Tayari habari za tukio la mabomu limesharipotiwa kwenye vyombo vya habari kimataifa, http://www.dn.se/nyheter/varlden/bomber-exploderade-pa-zanzibar/,hivyo basi, ni athari mbaya ya moja kwa moja kwa biashara ya utalii ambayo pia ni moja ya mihimili ya uchumi wa Zanzibar.
Ni matumaini yetu, kuwa wahusika na ulipuaji wa mabomu hayo watasakwa popote walipo na kutiwa nguvuni.
Maggid,
Iringa.(P.T)

Sunday, February 23, 2014

Warioba ampa somo Werema

Jaji Warioba 

Dodoma. Siku moja baada ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema kusema wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, wanaweza kubadili chochote, isipokuwa tunu za Taifa, Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba, ameonya kuwa jambo hilo linapaswa kufanywa kwa uangalifu mkubwa.
Jaji Warioba alipingana na kauli hiyo ya Jaji Werema na kusisitiza kuwa Katiba ni mali ya wananchi, hivyo mawazo na mapendekezo  yaliyokusanywa na tume yake kupitia Mabaraza ya Katiba “yanapaswa kuheshimiwa”.
Jaji Warioba alitoa kauli hiyo alipotakiwa na gazeti hili kufafanua kile kinachoonekana kama mkanganyiko wa kauli za viongozi hao wakuu kuhusu majukumu ya Bunge la Mabadiliko ya Katiba.
“Katika hili mimi ndiyo msemaji wa mwisho. Kwenye mchakato huu, sisi sote ni washauri  tu, someni vizuri sheria mtajua. Tangu mwanzo, wananchi  ndio waliotoa maoni yao, Tume ya Mabadiliko ya Katiba ikayakusanya na kutengeneza rasimu ya kwanza,” alisema Jaji Warioba na kuendelea: “Baadaye tukairudisha rasimu hiyo kwa wananchi wenyewe, baada ya kuiboresha kupitia mabaraza ya katiba ya wilaya. Wakaibadili wenyewe, kuridhia na hatimaye tukapata Rasimu ya Pili ya Katiba. Hivyo hata hii rasimu itakayojadiliwa bungeni, bado ni mali ya wananchi.”
Jaji Warioba alisema tofauti na nchi nyingine ambako Bunge la Katiba linaruhusiwa kufanya mabadiliko kwenye rasimu, utaratibu tuliouchukua hapa nchini, ni Bunge hilo kuliondolea mamlaka hayo.
“Hii ni kutokana na ukweli kwamba wenzetu Bunge lao linakuwa na uwakilishi wa wananchi  waliochaguliwa kwa ajili ya katiba tu. Kwa maana hiyo ni wananchi wenyewe. Lakini sisi  kwenye Bunge letu tumechanganya wajumbe wa Katiba na wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano na wale wa Baraza la Wawakilishi ambao kimsingi, hawakuchaguliwa kwa kazi hiyo,” alisema. Aliongeza: “Kwa utaratibu huu wa kwetu, wananchi wana mamlaka zaidi juu ya Katiba yao kuliko Bunge. Bunge na sisi wengine wote tunashauri tu, ndiyo maana hata Tume ilipotengeneza rasimu ya kwanza, ilibidi iirudishe tena kwa wananchi.
Jaji Warioba alienda mbali zaidi na kufafanua kazi ya Bunge hilo kuwa ni kuboresha Katiba.
“Ukiangalia kwa undani, huwezi kuboresha bila kubadili, ila unaboresha kwa kiwango gani na mamlaka yako ya kuboresha yainaishia wapi. Ndiyo maana sisi kwenye Tume tulipoboresha maoni ya wananchi na kutengeneza Rasimu ya Kwanza ya Katiba, tukairudisha kwa wananchi,” alisema.
Alisema kazi ya Bunge Maalumu la Katiba ni kuiboresha rasimu hiyo kwa kutoa ushauri na maoni yake ambayo hata hivyo si lazima yakubalike na wananachi ambao ndio wenye Katiba yao.
Alichosema Werema
Akijibu maswali ya wajumbe wa Bunge Maalumu juzi, Jaji Werema alisema Bunge Maalumu linaweza kubadili vifungu mbalimbali vilivyomo katika Rasimu ya Katiba, isipokuwa vilivyotajwa katika kifungu cha 9 (2) cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba.
Alisema kama kazi ya Bunge hilo ingekuwa kufanyiwa maboresho kwa vifungu vya rasimu hiyo tu, kusingekuwa na maana ya kuwepo kwake.
“Kwanza idadi ya watu waliotoa maoni ya Katiba Mpya ni Ndogo ikilinganishwa na idadi ya wananchi wote wa nchi hii. Bunge hili halipitishi Katiba na ndiyo maana kuna hatua nyingine ya wananchi kupiga kura. Kama itaonekana kuna kitu kinafaa na kinaweza kuingizwa na kukubalika ni sawa,” alisema na kuongeza:
“Nyinyi kama mngekuwa mnafanya maboresho tu au ukarabati sidhani kama kungekuwa na umuhimu wa kuwa na Bunge hili.” Alisema hata mawazo mazuri ambayo yapo katika nyaraka za makundi mbalimbali, vikiwamo vyama vya siasa yanaweza kujadiliwa katika Bunge hilo.
“Kisichotakiwa ni nyaraka hizo kutoingizwa humu bungeni. Rasimu inayojulikana na kukubalika ni hii iliyotolewa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba tu,” alisema.
Mambo yaliyomo katika kifungu hicho ambayo hayatakiwi kubadilishwa ni uwepo wa Jamhuri ya Muungano, uwepo wa Serikali, Bunge na Mahakama, mfumo wa kiutawala na kijamhuri na uwepo wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Mengine ni umoja wa kitaifa, amani na utulivu, uchaguzi wa kidemokrasia wa mara kwa mara katika vipindi maalumu, ukuzaji na uhifadhi wa haki za binadamu, utu usawa mbele ya sheria na mwenendo wa sheria na uwepo wa Jamhuri ya Muungano isiyofungamana na dini yoyote na inayoheshimu uhuru wa kuabudu.
“Fanyeni vyote lakini katika kifungu cha tisa hamtaruhusiwa kubadili chochote labda muongeze tu baadhi ya mambo lakini siyo kupunguza,” alisema Werema.

source:mwananchi

Vita ya uenyekiti Bunge la Katiba

Andrew Chenge na aliyekuwa Spika wa Bunge, Samuel Sitta, ambao wametajwa kutaka kuwania nafasi ya uenyekiti wa Bunge la Katiba wakipeana mikono siku za hivi karibuni. 


Dodoma. Kadiri siku zinavyosogelea uchaguzi wa Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, ndivyo mpasuko ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) unavyozidi, kutokana na kuwapo kwa makundi mawili yanayojipanga kusimamisha wagombea na ambayo yameanza kuendesha kampeni kuchafuana.
Uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa makundi hayo ni yale yanayomsaidia aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Andrew Chenge na aliyekuwa Spika wa Bunge, Samuel Sitta, ambao wametajwa kutaka kuwania nafasi hiyo.
Hata hivyo, wakati Chenge akiwa hayuko tayari kuthibitisha nia yake hiyo, Sitta hakupatikana jana kuzungumzia suala hilo. Lakini habari zinasema vigogo hao wameshajipanga kwa ajili ya mbio hizo za uchaguzi na sasa wanatafuta watu wa kuwasaidia.
Makundi hayo yalianza wakati wa kikao cha ndani cha CCM kilichofanyika mjini Dodoma chini ya Mwenyekiti wake, Rais Jakaya Kikwete, ambako habari zilisema, baada ya chama kumteua Pandu Ameir Kificho kuwania nafasi ya mwenyekiti wa muda wa Bunge la Katiba, mmoja wa wajumbe wa kikao hicho walimpendekeza Chenge kuwa mwenyekiti wa kudumu wa bunge hilo.
“Hapo ndipo mgogoro ulipoanza. Kwanza tulimkubali Kificho ili kupunguza wingu la ushindani kwenye uchaguzi wa mwenyekiti wa kudumu. Lakini wajumbe tulimkataa Chenge kwa hoja nzito na mwenyekiti alikubali na kuamua kuwa watu wakagombee bungeni.”
Tuhuma dhidi ya Chenge
Baadhi ya wabunge wa CCM wamesema ni ukweli ulio wazi kwamba Sitta na Chenge ndio wanaofaa kuwania nafasi hiyo, lakini mchuano utakuwa mkali kutokana na kila mmoja kuwa na ushawishi wa aina yake kwa wajumbe ambao ndio watakaopiga kura kumchagua mwenyekiti.
 “Wakati wa kuapa, wajumbe watatakiwa kushika Biblia au Qur’an. Ila tusema ukweli, unawezaje kufanya kiapo cha utii mbele ya mwenyekiti ambaye uadilifu wake unatia shaka? Alihoji mmoja wa wajumbe wanaomuungano mkono Sitta.
Mjumbe mwingine alisema Chenge hazuiwi kugombea, lakini ajiandae kujibu maswali makuu matatu, moja likihoji uadilifu wake wakati kuna mikataba mingi ya wawekezaji kwenye kampuni za madini iliyoshuhudiwa na yeye akiwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, ni mibovu.
“Pia tutamtaka aeleze kwa nini alikubali Uenyekiti wa Kamati ya Bajeti ya Bunge la Jamhuri kwa uteuzi wa Spika, wakati kanuni zinasema wenyeviti wachaguliwe na wabunge wenyewe,” alisema mjumbe huyo ambaye hakupenda kutajwa jina lake.
Kauli ya Chenge
Chenge mwenyewe amepuuza tuhuma hizo akisema kuwa ni za watu wasiopenda kuelewa.
“Hayo yote na mengi zaidi nimeyasikia ndiyo maana nimeamua kuondoka Dodoma. Siko Dodoma nitarudi Jumatatu,” alisema Chenge na kuendelea;
“Lakini ndugu yangu, mi naona hakuna haja ya kulumbana na watu ambao hawataki kuelewa. Kama watu wanatuhumu, lakini hawana kielelezo cha kwenda nacho mahakamani, wanaambiwa kwa ushahidi kuwa tuhuma zao hazina msingi na hawataki kusikia, unadhani tutawafanyaje zaidi ya kuwaacha tu?”
Alipotakiwa kuthibitisha kuwa kweli ana mpango wa kugombea nafasi hiyo ya Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba alijibu;
“Chama kina utaratibu wake na mipango yake. Ni taasisi inayopaswa kuheshimiwa, kwa nini tulumbane leo wakati chenyewe kina msimamo wake juu ya hilo?”
Alipoulizwa tena kueleza namna anavyojiandaa kujibu maswali matatu magumu yanayoandaliwa na wapinzani wake, endapo atasimama kunadi sera zake akitakiwa kugombea nafasi hiyo alijibu;
“…Bwana! Chenge ni huyo huyo, chaguzi ni hizo hizo ambazo ameshinda mara kadhaa na nchi hii ni yetu sote.”
Sitta
Sitta hakupatikana jana kuzungumzia suala hilo, lakini mmoja wa wanaomuunga mkono ambaye hakutaka jina lake litajwe, amesema hawana shaka kwamba akisimama na Chenge kwa kura za haki, atapita.
Tayari kumeripotiwa taarifa za rushwa kwenye mbio hizo za kuwania nafasi ya Mwenyekiti wa Bunge la Katiba. Hata hivyo, Waziri Mkuu Mizengo Pinda ameonya vitendo hivyo na kuzitaka jumuiya za CCM kuwa macho dhidi ya suala hilo.
Pinda alitoa karipio hilo jana alipokuwa akizungumza na Jumuiya ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi mjini Dodoma.
Alisema viongozi wanaopatikana kwa njia ya rushwa siyo viongozi bora na kuhoji, “Hivi mtu anayetumia fedha kuingia madarakani akipata madaraka fedha hizo atazirudishaje?”
Pinda ametaka jumuiya hiyo kuwa mstari wa mbele kusimamia uendeshaji wa chaguzi ndani ya chama kwa misingi ya maadili, kwani wanaomwaga fedha ili kupata uongozi ndani ya chama wanawavuruga na hiyo siyo njia ya kukijenga chama.
Pinda aliwaasa wanachama wa CCM waache kupanga nani agombee na nani asigombee na kufafanua kuwa hali hiyo hujenga makundi ndani ya chama hicho.
“Tunahitaji kupata viongozi kwa kuzingatia umoja wetu na mshikamano miongoni mwa wanachama. CCM ikiwa imara itaunda Serikali imara. Chama kikiwa dhaifu ni wazi kuwa hata Serikali yake nayo itakuwa dhaifu,” alisema.

source: mwananchi

Saturday, February 22, 2014

Yanga ‘yaibipu’ Al Ahly, Mbeya City hoi

Mshambuliaji wa Yanga, Emmanuel Okwi (katikati) akiwatoka mabeki  wa Ruvu Shooting, Stephano Mwasika (kulia) na Shabaan Suzan wakati wa mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, jana kwenye Uwanja wa Taifa. Yanga ilishinda 7-0. Picha na Michael Matemanga 

Mabingwa watetezi Yanga wametuma salama kwa Al Ahly baada ya kuisambaratisha Ruvu Shooting kwa mabao 7-0, huku Mbeya City wakinyukwa 2-0 na Coastal Union.
Yanga inayojiandaa na mechi ya Ligi ya Mabingwa dhidi ya Al Ahly wiki ijayo ilipata mabao yake kupitia washambuliaji wake Didier Kavumbagu, Simon Msuva waliofunga mabao mawili kila moja, huku Emmanuel Okwi, Mrisho Ngassa na Khamisi Kiiza kila moja alifunga bao moja.
Kwa matokeo hayo Yanga imefikisha pointi 39, wakati Mbeya City waliopokea kipigo wamebaki nafasi ya tatu na pointi zao 35, Azam wameshuka nafasi ya pili na pointi 36 na Simba ya nne (32).
Kipigo cha Ruvu Shooting cha mabao 7-0 kimekuja ikiwa ni siku nne tu zimepita tangu ndugu zao wa JKT Ruvu kunyukwa 6-0 na Tanzania Prisons.
Yanga ilianza mechi hiyo kwa kishindo kwa kupata bao katika dakika ya kwanza lililofunga na Kavumbagu kwa shuti la mguu wa kushoto akipokea pasi ya Okwi, wakati Shooting wakishangaa Msuva aliifungia Yanga bao la pili dakika ya pili akimalizia pasi ndefu ya Ngassa.
Shooting waliamka na kufanya shambulizi dakika ya 12, lakini mpira wa kichwa wa Michael Aidan ulidakwa na Deogratus Munishi.
Kocha msaidizi wa Yanga, Boniface Mkwasa aliyekuwa Misri kuishuhudia Al Ahly aliingia uwanjani hapo dakika 15 na kwenda moja kwa moja kwenye benchi.
Mshambuliaji Okwi aliwainua mashabiki dakika ya 28 kwa kupachika bao la tatu baada ya kumlamba chenga kipa wa Shooting, Abdallah Ramadhani.
Ngassa aliendeleza kulizamisha jahazi la Shooting dakika ya 34 baada ya kumzidi ujanja beki Mangasi Mbonosi na kipa wake Ramadhani na kufunga bao la nne.
Kasi ya washambuliaji wa Yanga, Kavumbagu, Okwi, Ngassa na Msuva iliwashinda kabisa mabeki wa Shooting.
Kocha wa Shooting, Tom Olaba aliwapumzisha Juma Nade, Hamis Ali, Shabaan Suzan na kuwaingiza Said Madega, Ayoub Kitala na Gedion Sepo.
Wakati Hans Pluijm aliwapumzisha Mbuyu Twite, Ngassa, Kavumbagu na kuingia Juma Abdul, Kiiza na Said Bahanuzi.
Mabadiliko hayo yalikuwa na faida kubwa kwa Yanga, katika dakika ya 53, Kavumbagu alitumia vyema krosi ya Msuva kufunga bao la tano.
Kiiza alipachika bao la sita kwa kuunganisha krosi ya Msuva bao lililomfanya kocha wa Shooting, Olaba kuondoka uwanjani hapo na kuingia vyumbani, lakini baadaye alirejea.
Msuva alihitimisha karamu hiyo kwa kufunga bao la saba kwa shuti kali akimalizia mpira uliorushwa na Juma Abdul katika dakika ya 77.
Tanga, Wenyeji mabingwa wa 1988, Coastal Union walithibitisha utu uzima dawa baada ya kuinyuka Mbeya City mabao 2-0 kwenye Uwanja wa Mkwakwani.
Mabao ya Coastal Union yalifungwa na Mohamed Mtindi katika dakika ya 79 na 89 na kuzima kasi ya Mbeya City ambayo ilitawala sehemu kubwa ya mchezo huo, lakini washambuliaji wake walikosa umakini kwenye umaliziaji.
Katika mchezo mwingine Mtibwa Sugar iliichapa Ashanti United 2-1, mabao ya Mohamed Mkopi na Abdalla Juma huku Musa Mgosi akipewa kadi nyekundu.
Arusha JKT Oljoro ililoa 2-1 kutoka kwa Mgambo Shooting, huku Kagera Sugar wakiiadhibu Rhino Ranger 1-0 bao la Suleiman Kibuta.
Azam, Simba vitani leo
Azam FC ina shughuli pevu leo itakapokabiliana na Prisons kwenye uwanja wake wa Azam Complex, wakati  Simba itateremka kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kupepetana na JKT Ruvu.
Ni wazi, Azam itaingia uwanjani ikiwa na mawazo ya kusaka ushindi ili kujipoza na machungu ya kutupwa nje ya Michuano ya Kombe la Shirikisho baada ya kuchapwa jumla ya mabao 2-1 na Ferroviario ya Msumbiji.
Hata hivyo, kazi haitakuwa nyepesi kwa Azam, kwani Prisons nayo imeingia mzunguko wa pili ikiwa na staili mpya ya kutoa vichapo vikali bila kujali inacheza na nani. Prisons inayokamata nafasi ya tisa ikiwa na pointi 19, haijapoteza mchezo wowote katika mechi zake tatu za mzunguko wa pili ilizokwishacheza ambapo ililazimishwa sare ya 0-0 na Coastal Union, ikaichapa Mtibwa mabao 3-1 kisha ikainyuka JKT Ruvu mabao 6-0.
Nayo Simba baada ya ziara ngumu mikoani iliyoshuhudiwa ikikosa ushindi hata mmoja katika mechi zake tatu, itakuwa na fikra za kusaka ushindi ili kurejesha furaha ya mashabiki wake mbele ya JKT Ruvu.
Kocha wa Simba, Zdravko Logarusic amewaambia wachezaji wake kwamba hataki mzaha tena anahitaji ushindi tu kuanzia mchezo wa leo.

Imeandaliwa na Sosthenes Nyoni (Dar), Burhan Yakubu (Tanga), Musa Juma (Arusha), Juma Mtanda (Moro) na Phinias Bashaya (Kagera)

source: mwananchi

Friday, February 21, 2014

Membe apongeza kufungiwa CCM

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa,Bernard Membe.
Siku mbili baada ya makada sita wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kupewa adhabu ya onyo na kuzuiwa kugombea nafasi za uongozi kwa mwaka mmoja, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, amefunguka na kupongeza uamuzi huo uliofanywa na Kamati Kuu (CC) ya chama hicho.
Membe ambaye ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu yaTaifa (Nec) ya CCM, ni miongoni mwa makada hao walioadhibiwa kwa tuhuma za kuanza kampeni za kutaka wateuliwe na chama chao kugombea urais wa mwaka 2015 pamoja na kukiuka taratibu na kanuni za chama hicho.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Membe aliupongeza uamuzi huo na kueleza kuwa ni wa lazima kwa kuwa unajenga nidhamu ndani ya Chama.

Makada wengine waliothibikika kukiuka kanuni na taratibu hizo ni Mawaziri Wakuu wastaafu, Edward Lowassa na Frederick Sumaye na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Mahusiano na Uratibu), Stephen Wassira.

Wengine ni Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba na Waziri wa zamani wa Nishati na Madini, William Ngeleja.

Membe alisema adhabu iliyotolewa na CCM ni taratibu za kawaida na za lazima ambazo zinapaswa kuigwa na vyama vingine.

Alisema dunia imekuwa ikiiga matendo na kanuni za maisha ya waumini wa Kanisa Katoliki, lakini wameshindwa kuiga namna wanavyofanya uchaguzi wa kumteua mkuu wa kanisa hilo Baba Mtakatifu, kwa utulivu na amani, hivyo kubaki kufanya chaguzi za fujo na vurugu.

“Hakuna yeyote duniani aliyeiga kanuni na taratibu za Waroma wanavyompata Papa wa kuliongoza kanisa, hivyo kila chama kina wajibu wa kuweka taratibu na kanuni kwa wagombea wake ili nidhamu iwepo ndani ya Chama, ili taratibu na kanuni zisipofuatwa hatua zichukuliwe,” alisema Membe.

Alisema kuwa msimamo wa CCM wa kuwadhibiti kutokana na kuona kuwa taratibu na kanuni zilizowekwa na chama hicho zinakiukwa ni mzuri, na kwamba kama kuna chama hakifanyi hivyo, hakuna faida ya kuendelea kuwapo.

“Utaratibu huu ni mzuri na wa kawaida na ni wa lazima, hauwezi kukwepwa kwa waliooteshwa na wasiyooteshwa kuwa viongozi,” alisema Membe.

CCM kupitia Katibu wake wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye,  Jumanne wiki hii, alitangamza msimamo wa CC wa kuwapa onyo kali makada hao kwa kosa la kubainika kufanya kampeni kabla ya wakati na kuvunja kanuni na taratibu za chama hicho.

Nape alisema msimamo huo ulifuatia vikao vyake kuanzia Februari 13 hadi 18, mwaka huu mjini Dodoma, kujadili masuala mbalimbali likiwamo la makada hao ambao wote walihojiwa na Kamati ya Maadili kabla ya kupatiwa adhabu hiyo.

“Makada hawa watakuwa na wakati mgumu kwani hawataruhusiwa kujihusisha na aina yeyote ya siasa, hivyo kama watajihusisha kanuni na taratibu hazitamruhusu kugombea nafasi yeyote ya uongozi ndani ya Chama, kwa hiyo tunaweza kusema wako kwenye ‘Danger Zone,’ alisema Nape.

Alisema pia chama hicho kimetangaza kuwaita na kuwahoji wapambe na mawakala wote wanaoshirikiana na makada waliopewa onyo na wengine ambao hawajabainika kufanya kampeni za chini chini ili kuwachukulia hatua stahiki.

Nape alisema Kamati ya Maadili inaendelea kuwachunguza na kuwafuatilia kwa makini na baadaye watawaita ili kuwapatia adhabu kutokana na utovu huo wa nidhamu unaokichafua Chama na jamii kwa ujumla.

Katika hatua nyingine, Membe alisema Tanzania inatarajia kupeleka majeshi yake Sudani Kusini ili kulinda usalama wa nchi hiyo iliyotumbukia katika vita.

Alisema hatua hiyo imefuatiwa ombi la Umoja wa Mataifa kutokana na jeshi hilo kuaminika na uzoefu wake katika kulinda amani katika nchi mbalimbali duniani.

Kuhusu usuluhishi wa mpaka wa Tanzania na Malawi, Membe alisema pande zote zinatarajiwa kwenda Msumbiji mwishoni mwa mwezi huu na kuwasilisha utetezi wao wakiwa na vielelezo.

Akizungumzia kuzorota kwa uhusiano kati ya Tanzania na Rwanda, alisema Rais Jakaya Kikwete na Rais Paul Kagame, wamekubaliana kukutana mara kwa mara ili kujadili masuala ya usalama wa nchi zao na kwamba Tanzania haifikirii kugombana na nchi yoyote ya jirani.
 
CHANZO: NIPASHE

Posho zapingwa kila kona


Slaa_1_2b62b.png

Dar es Salaam. Wakati maombi ya baadhi ya wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba ya kuongezewa posho yakipingwa kila kona, uongozi wa muda wa Bunge hilo umeunda kamati kuchunguza uhalali wa maombi hayo.
Juzi, ndani ya kikao cha Bunge hilo, baadhi ya wajumbe walieleza mahitaji yao ya posho kuongezwa wakisema kiwango cha Sh300,000 (Sh80,000 za kujikimu na Sh220,000 kwa kikao), hakitoshi
.
Baada ya maombi hayo, Mwenyekiti wa Muda wa Bunge, Pandu Ameir Kificho aliahidi kuliwasilisha suala hilo serikalini ili lifanyiwe kazi, lakini jana aliamua kuunda timu ya wajumbe sita kuchunguza uhalali wa posho hizo.
Posho kupingwa
Baadhi ya vyama vya siasa, wanaharakati na wananchi wa kawaida wameshangazwa na maombi hayo ya posho, wakisema wajumbe wamesahau kilichowapeleka bungeni na kukimbilia kutetea masilahi yao.
Vyama vya Chadema na CUF kwa nyakati tofauti, vilisema kuwa vitaanzisha juhudi za kuwataka wabunge wao ambao ni wajumbe wasusie agenda yoyote inayotaka kuongezwa kwa posho hizo.
Tamko la vyama hivyo limetolewa huku Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambacho wajumbe wake ndio wanaodaiwa kupigia debe mpango huo, kikisema kitatoa ufafanuzi juu ya hoja hizo baada ya kupata 'taarifa rasmi'.
Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa alisema jana kuwa wajumbe hao hawakupaswa kudai nyongeza ya posho kwa vile hawakutumwa kwenda Dodoma kudai marupurupu ya fedha.
Alisema kuanza kujadili suala la nyongeza ya posho badala ya kuzungumzia hoja za msingi zilizopo kwenye Rasimu ya Katiba, ni sawa na kuwapuuza wananchi ambao wanasubiri kupata Katiba Mpya.
"Wametoka kwenye hoja na kutupeleka kwenye mambo mengine ambayo hayana msingi wowote. Sisi kama Chadema tunapinga na tunataka wabunge wetu watambue hilo," alisema.
Alisema wale wanaolalamika kwamba Sh300, 000 hazitoshi wanajaribu kupindisha ukweli, kwani kuna baadhi ya watumishi wa Serikali wanalipwa kiasi hicho ikiwa ni mshahara wao wa kila mwezi.
Alisema Chadema kimewataka wabunge wake kutojiingiza kwenye malalamiko hayo badala yake wazingatie kile walichotumwa na wananchi kwenda Dodoma

Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Julius Mtatiro alisema amesikitishwa na maombi hayo ya posho na kuahidi kuanzisha kampeni ya kuyakwamisha kwa sababu hayana tija kwa wananchi.

"Tunafahamu kuwa kuna njama zinapangwa ili wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba waongezewe fedha zaidi, binafsi na wenzangu wengi tumepanga kutumia kila uwezo kuzuia nia hiyo ovu. Ifikie wakati tuambiane ukweli, vinginevyo nchi hii watu watakufa maskini," alisema Mtatiro ambaye pia ni mjumbe wa Bunge hilo.

"Sh300,000 tunazopewa kwa siku zinatosha kabisa, ambaye hazimtoshi aongeze za kwake na ambaye anaona hawezi kuongeza fedha zake aondoke Dodoma ili kupisha wanaoweza kutunga Katiba waendelee." Alipotakiwa kutoa msimamo wa CCM kuhusiana na hatua hiyo, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho, Nape Nnauye alisema: "Sina chochote cha kuzungumza sasa hadi pale nitakapoletewa taarifa rasmi kwani siwezi kufanya kazi kupitia magazeti."

Akizungumzia posho hizo, Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba alipinga madai kwamba viwango vilivyotangazwa vya wajumbe wa Bunge la Katiba (Sh300, 000) kwa siku ni pungufu kwa vilivyotolewa kwa wajumbe wa Tume.

Bila ya kutaja kiwango alisema: "Ninachofahamu, posho ya wajumbe wetu ilikuwa chini ya hiyo."
Hata hivyo, taarifa kutoka ndani ya tume hiyo, zinaeleza kuwa wajumbe hao walikuwa wakipokea Sh200,000 kwa siku.

Kuhusu madai kwamba kazi inayofanywa na Bunge Maalumu la Katiba ni nzito kuliko iliyofanywa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Warioba alisema hawezi kupima uzito wa kazi ya Tume kwa kuilinganisha na inayofanywa na Bunge la Katiba na hafahamu waliotoa madai hayo wametumia utaalamu gani
Kamati yaundwa

Kutokana na kupanda kwa joto la posho hiyo, jana asubuhi, Kificho alitoa maelezo kwa wajumbe kuwa uongozi unatafakari namna bora ya kuwafanya wajumbe waishi kwa amani mjini Dodoma.
"Kwanza tulikubaliana kuwa kikao kianze leo (jana) saa nne asubuhi, lakini tumechelewa kwa sababu muhimu, kwani lazima mtambue kuwa kila jambo mnalozungumza hapa halitupwi kama jiwe," alisema Kificho na kuongeza:

"Mlinituma tuzingatie namna gani tutakaa Dodoma kwa amani, ili tuweze kumudu na kuishi vizuri katika kazi hii nzito iliyoko mbele yetu."
Alisema kuwa walikuwa wameshauriana na wataalamu wake ambao ni makatibu na kukubaliana kuunda timu ya kufuatilia na kuishauri Serikali jinsi ya kuongeza posho hizo

Aliwataja walioteuliwa kuunda timu hiyo kuwa ni, William Lukuvi, Mohamed Aboud Mohamed, Freeman Mbowe, Paul Kimiti, Asha Bakari na Jenister Mhagama.
Wakati akiitangaza timu hiyo iliyopaswa kuanza kazi yake jana, jina la Lukuvi ambaye pia ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge) lilizua kelele kutoka miongoni mwa wajumbe wakipinga uteuzi wake.

"Hatufai huyo, hatufai huyo, hilo jina liondoeni na kulitupa kapuni kwani mbona wapo wengine, kwa nini mkaingiza jina la Lukuvi?" zilisikika sauti za juu kutoka ndani ya ukumbi, lakini lilipotajwa jina la Mhagama wajumbe wengi walishangilia.

Imeandikwa na George Njogopa, Editha Majura na Habel Chidawali

source:  Mwananchi

Matokeo ya Mtihani wa Kitaifa 2013 Kidato cha Nne na QT


Links za kutizamia matokeo:

  1. Bofya hapa kwa matokeo ya CSEE 2013 
  2. Bofya hapa kwa  matokeo ya QT 2013

source: wavuti.com

Friday, February 14, 2014

OKWI RUKSA YANGA


emosting_37d10.jpg
Mshambuliaji wa kimataifa wa timu ya Taifa Uganda na klabu ya Young Africans Emmanuel Arnold Okwi leo ameruhiswa ramsi kuanza kuitumikia timu yake katika michezo ya Ligi Kuu na Mashindano ya klabu Bingwa Barani Afrika kufuatia shirikisho la soka nchini TFF kuiandikia barua klabu ya Young Africans.
Okwi ambaye alisajiliw aa Young Africans mwishoni mwa mwaka jana na kucheza michezo ya kirafiki ya kujiandaa na msimu mpya, alisimamishwa na Shirikisho la Soka la Nchini TFF wakati wakisubiria kupata udhibitisho wa usajili wake kutoka FIFA.

Mara baada ya barua hiyo, Okwi anatarajiwa kuungana na wenzake mwishoni mwa wiki mara timu itakaporejea kutoka Visiwa vya Comoro na ataanza kuonekana katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom dhidi ya Ruvu Shooting siku ya jumamosi Februari 22 mwaka huu.

Uongozi wa Young Africans unawashukuru wanachama, wapenzi na wadau kwa ujumla kwa kuwa wavumilivu wakati wa suala na hili na hatimaye limepatiwa ufumbuzi.

chanzo: mjengwa blog

Thursday, February 13, 2014

Warioba: Kazi ya Bunge la Katiba siyo kubadili Rasimu




Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba amesema litakuwa jambo lisilo la kawaida kwa Bunge Maalumu la Katiba kubadili hoja ya msingi iliyopo kwenye Rasimu ya Katiba, akisisitiza kuwa jukumu lake ni kuifanyia marekebisho.

Akihutubia mkutano ulioandaliwa na Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD), wa tafakuri na maridhiano kuelekea Katiba Mpya jana, Jaji Warioba alisema:

“Madaraka ya Bunge Maalumu yamekuwa yanabadilika kwa kutegemea aina ya mchakato unaotumika. Afrika Kusini, Namibia na Cambodia, Bunge Maalumu lenyewe ndilo lilipewa jukumu la kuandika Rasimu ya Katiba. Katika mazingira haya, Bunge Maalumu lilikuwa na madaraka ya kubadilisha mambo mengi katika Rasimu ya Katiba… lilikuwa na madaraka ya kuachana na Rasimu ya Katiba na kuandika Rasimu Mbadala.
“Madaraka ya Bunge Maalumu yanakuwa na mipaka endapo Rasimu ya Katiba imeandaliwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba au chombo cha aina hiyo.

Bunge Maalumu linaweza kuwa huru kurekebisha baadhi ya masharti yaliyomo kwenye Rasimu ya Katiba lakini si suala la kawaida Bunge Maalumu kubadili hoja ya msingi. Jinsi ushirikishaji wa wananchi unavyokuwa wa wazi na mpana ndivyo madaraka ya Bunge Maalumu yanavyopungua.”
“Mantiki ni kuzuia Bunge Maalumu kunyang’anya madaraka ya wananchi, yaani “act of popular sovereignty”. Wataalamu wa masuala ya Katiba wanaeleza kuwa madaraka ya Bunge Maalumu katika mazingira haya ni kuboresha Rasimu ya Katiba.

“Kwa mujibu wa Kifungu cha 25(1) cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Sura ya 83, Bunge Maalumu limepewa madaraka ya kujadili na kupitisha masharti ya Katiba, kutunga Sheria ya Masharti ya Mpito na Masharti yatokanayo na kabla ya kuanza kazi hiyo, Bunge Maalumu litapitisha Kanuni za Bunge Maalumu ambazo zitaongoza utekelezaji wa mamlaka ya Bunge Maalumu.”

Bunge Maalumu la Katiba litaanza kukutana Jumanne ijayo kujadili Rasimu ya Katiba iliyotolewa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba Desemba 30, mwaka jana.

Moja ya masuala yanayotazamiwa kusababisha mvutano mkubwa kwenye vikao vyake ni lile la muundo Muungano na hasa suala la Serikali Tatu uliopendekezwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinataka kusukuma ajenda ya kuendelea kwa muundo wa Serikali Mbili Bunge la Katiba wakati vyama vya upinzani vinataka mapendekezo ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba ya Serikali tatu yaheshimiwe.

Jaji Warioba alisema Bunge Maalumu linapaswa lifanye kazi ya kuboresha masharti ya kikatiba yaliyomo ndani ya Rasimu ya Katiba pasipo kuweka masharti mapya ambayo kwa taathira yake yanabadilisha au kufifisha yaliyomo kwenye rasimu hiyo.

Kuhusu mchakato wa kupata Katiba Mpya Tanzania, Jaji Warioba alisema kila mtu anafahamu kuwa ulifuata utaratibu wa kuandaliwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba ndiyo maana hata Bunge Maalumu la Katiba litakapokutana Dodoma litatakiwa kufuata utaratibu huo.

Jaji Warioba alisema utungaji wa Katiba unatakiwa kuwa shirikishi kwa maana ya kuwahusisha wananchi katika hatua zote za mchakato kwa maelezo kuwa kwa kadri mchakato wa kuandika Katiba unavyowashirikisha kwa mapana, ndivyo utakavyoongeza uwezekano wa kukubalika, kuheshimika na utekelezaji wa Katiba utakavyokuwa rahisi.

“Wananchi wanaposhiriki katika utungaji wa Katiba na pale matakwa yao yanapozingatiwa ndani ya Katiba, wananchi hao huimiliki Katiba hiyo na kuiona kuwa ni yao. Wananchi huona hivyo kwa sababu licha ya kushiriki lakini pia Katiba hiyo huakisi utashi wao na ndoto zao na hivyo kukubali kuongozwa na masharti yaliyomo ndani ya Katiba,” alisema.

Apinga kura kupitisha maoni
Akizungumzia upigaji wa kura katika kufanikisha mchakato wa kupatikana kwa Katiba Mpya, Jaji Warioba alionya akisema hatua hiyo itasababisha kuzaa Katiba itakayopingwa na wananchi wengi.
“Bunge la Katiba lina jukumu la kusimamia mchakato mzima wa upatikanaji wa Katiba ya wananchi wote. Kama tunataka kuunganisha Taifa, tukubaliane kwa maridhiano, mkikubaliana kwa kupiga kura siku hiyohiyo Katiba itaanza kupingwa,” alisema Jaji Warioba.

Dk Bilal asema kura itaamua
Akifungua mkutano huo, Makamu wa Rais, Dk Mohamed Gharib Bilal alisema suala la mchakato wa Katiba ni zito na hutokea mara chache katika maisha hivyo kumtaka kila aliyepata wasaa wa kushiriki katika Bunge Maalumu la Katiba, kutumia fursa kwa busara.

Dk Bilal alisema ni vizuri wanasiasa na wadau wote kujiandaa kupokea matokeo ya kura kama itakavyopigwa na wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba.
Aliwataka viongozi wa vyama vya siasa kuonyesha mfano kwa kuhubiri amani ili mchakato wa Katiba umalizike kwa amani huku kila mmoja akiweka masilahi ya taifa kwanza na yale ya kisiasa baadaye.
“Katiba ni yetu wote, hatuna haja ya kutoana ngeu… tukiweka Tanzania kwanza tutafanikiwa, lakini tukiweka masilahi yetu ya siasa mbele hatuwezi kufanikiwa… kila mmoja wetu atumie fursa hii kwa busara,” alisema.

Mbatia atoa angalizo
Mwenyekiti wa TCD, James Mbatia alisema Katiba siyo mali ya viongozi na wanasiasa, bali ni ya wananchi wote na kuwakumbusha wote waliopewa jukumu la kuiandaa kuelewa kuwa wananchi wanataka Katiba inayoakisi ndoto na matarajio yao na itakayopunguza na au kuondoa hofu waliyonayo ya kuzidi kuwa maskini na fukara.
“Katiba haipatikani kwa wingi wa kura, bali kwa kugusa mioyo ya kila anayeshiriki kuona kwamba amekuwa sehemu ya maridhiano yaliyopatikana. Ni vizuri tukubaliane leo na kesho kuweka misingi ya pamoja ya kuhakikisha tunapata Katiba Mpya kwa njia ya kujadiliana na kuridhiana,” alisema Mbatia, ambaye pia ni Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi.

source: mwananchi

Kingunge:Ushabiki uachwe suala la Katiba mpya

Mwanasiasa mkongwe nchini, Kingunge Ngombale-Mwiru
Jumatano iliyopita mwanasiasa mkongwe nchini, Kingunge Ngombale-Mwiru ktika mahojiano maalum na NIPASHE kupitia safu ya makala alizungumzia umuhimu wa mwanachama yoyote wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), anayetaka kugombea urais  kujitokeza mapema ili watu wamjue na kwamba kwa kufanya hivyo sio kosa.
Kauli hiyo inaweza isieleweke sana kwa viongozi wa juu wa CCM, ambao mara kadhaa wamekuwa wakisisitiza kwamba hakuna mwanachama yoyote anayeruhusiwa kujitokeza kwa sasa kutangaza kugombea urais ifikapo mwakani.

Leo Kingunge anazungumzia umuhimu wa Tanzania kupata Katiba mpya iliyo bora ambayo itasaidia kutatua kero ambazo zimekuwa zikilikumba taifa kwa miaka zaidi ya 50 tangu upatikane Uhuru.

Mkongwe huyo wa sisasa hapa nchini anasema yapo mambo ya msingi ambayo yanapaswa kuwamo kwenye katiba mpya ijayo.

Mchakato wa kupata Katiba mpya unaendelea na wiki ijayo rasimu ya pili itaanza kujadiliwa na Bunge maalum la Katiba mjini Dodoma.

Kingunge anasema kunahitajika busara, weredi na uvumilivu katika kuijadili rasimu ili wabunge waweze  kuipatia Tanzania Katiba iliyo bora itakayosaidia kizazi cha sasa na kijacho.

Anasema anasema mjadala juu ya Katiba mpya haupaswi kufanywa kwa jazba, ushabiki wa kisiasa, kidini au ukabila badala yake ufanywe kwa umakini mkubwa ili kusaidia kupatikana kwa majawabu ya yale ambayo yamekuwa au yanaonekana ni mapungufu ndani ya Katiba iliyopo sasa.

"Kubwa ipatikane Katiba  mpaya iliyo bora  itakayoimarisha na itakayosaidia kuujenga umoja, amani, utulivu, mshikamano na udugu wetu ambao kwa takribani miaka  50 tangu Tanzania kuwa Jamhuri ya Muungano umekuwa ukizingatiwa," anasema.

Anasema hakuna ubishi kwamba kuna mapungufu makubwa katika  Muungano uliopo na ndani ya Katiba ya sasa, hivyo ni vyema mapungufu hayo yakarekebishwa pamoja na kuyapa uhai mapendekezo mapya kwa manufaa ya taifa.

Kingunge anasema mawazo mapya yaliyosahaulika katika Katiba ya sasa ni muhimu yazingatiwe ili mradi yana manufaa kwa taifa.

"Matatizo ya msingi yapo na kama Katiba itakuwa kimya katika mambo hayo haiwezi kuwa bora, mfano makundi yasiyo na uhakika kuwamo kwenye mkondo wa maendeleo kama Wafugaj na Wahamaji, inayowahusisha Wamasai, Wabarbaig, Wasukuma na hata Wanyamwezi wanaohama kutoka sehemu moja kwenda nyingine kutafuta chakula cha mifugo yao.

Anasema kundi hili limekuwa wahanga na kutengwa badala ya kusaidiwa kuwawekea miundo mbinu itakayowafanya wafanye shughuli zao kwa ufanisi na kupata maendeleo na kuwaepusha kuingia kwenye mizozo ya mara kwa mara dhidi ya wakulima.

"Rasimu ya Katiba ya sasa haielezi namna ya kutatua migogoro na mauaji ya wafugaji na wakulima badala yake imejikita kwenye masuala ya vyeo na mgawanyo wa madaraka tu, yaani ulaji wakati mambo kama haya yanapaswa kuainishwa mapema, suala la wavuvi wadogo au wakulima wadogo. Tunakimbilia wakulima wakubwa kupitia Kilimo Kwanza, wakati watu wanaolisha taifa kwa kutumia jembe la mkono wamesahauliwa," anasema Kingunge

Anasema tangu uhuru vita vya wakulima na wafugaji imekuwa ikitokea, lakini utatuzi wake umekuwa wa kisiasa na kushindwa kumalizika, kitu anachotaka katiba mpya ijayo iweke bayana hilo ili kufanya makundi hayo kufanya shughuli zao na kujiletea maendeleo huku watoto wa jamii ya wafugaji wahamaji wanapata nafasi ya kusoma na kinamama kupata haki zao za ndoa.

"Katiba ikiwa wazi katika suala la makundi kama hayo hata suala la uharibifu wa mazingira utapatiwa ufumbuzi kwa sababu mfugaji anapohama na mifugo yake anasababisha uharibifu mkubwa wa ardhi, je wafanyeje na wakati ni lazima wawapatie mifugo yao vitu hivyo ili wasife....ni Katiba pekee yenye majiu hayo," anasema.

Kingunge anasema ni lazima mjadala wa Katiba mpya upewe nafasi pana na kuwaachia wananchi kujiamulia mambo yao na hasa kwenye suala la mfumo wa serikali tatu, badala ya Tume na wanasiasa kuanza kuwajibia wananchi.

"Tume imefanya kazi kubwa katika kukusanya maoni na mapendekezo yaliyozalisha rasimu mbili tofauti za katiba, lakini bado haiwezi kuwa kama kipaza sauti cha kuwasemea wananchi juu ya mfumo gani wa Muungano wanaoutaka katika Katiba hiyo," anasema.

Anaongeza kuwa hakubaliani na mfumo uliopendekezwa ndani ya rasimu ya Katiba serikali tatu kwa maana ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Zanzibar.

Anasema watanzania wanapaswa kujifunza kwa mataifa kama Marekani, India, China na kwingine yenye kuundwa na mfumo wa muungano jinsi yanavyokuwa wazalendo katika utaifa wao kuliko umajimbo au nchi zilizochangia kuunda mataifa hayo.

Anasema matatizo ya Muungano yaliyopo sasa yanachangiwa na uzembe wa viongozi wenyewe kwa kunyamazia izkiwamo baadhi ya kero zinazopigiwa kelele huku akihoji kwa mfano serikali ya Jamhuri ilikuwa wapi wakati Zanzibar wakipitisha katiba yao inayokinzana na ile yao na kuja kuibuka sasa baadhi ya wanasiasa kuliona hilo.

Kingunge anasema anaamini watanzania wakikaa chini na kujadili kwa kina mambo yao wanaweza kupata Katiba mpya itakayowapa nafasi kuendelea kufurahia amani, utulivu na undugu wao vinginevyo watu wakiendesha mambo kwa ushabiki na tamaa ya maslahi yao taifa la Tanzania litaangamia na kuja kujuta baadaye.
CHANZO: NIPASHE