Ndugu zangu,
Jana nikiwa mahali fulani hapa Dar
nilikutana na kaka na mwalimu wangu kwenye tasnia ya habari, ni ndugu
yangu Mobhare Matinyi. Huyu alianza kuhariri kazi zangu tangu nikiwa
Sweden miaka ya 90. Wakati huo Matinyi alikuwa Mhariri gazeti la Majira.
Nilimkuta kaka Matinyi kwenye
mazingira ya kulalamika, tena kwa sauti. Kaka Matinyi alikuwa
akilalamikia taratibu za mahali hapo. Zilikuwa ni taratibu za hovyo.
Nilimwacha Matinyi alalamike kwanza kabla sijamsalimia, maana,
wakati akilalamika hakujua, kuwa nami pia nipo mahali hapo.
Kaka Matinyi akatulia. Nikamfuata
kumsalimu na kumpongeza pia kwa kutoa sauti yake juu ya kile
kilichokuwepo hapo. Nikamwambia; kuwa hiyo ndio demokrasia, kama ya
Marekani vile! Maana, Matinyi wala hakugombana na mtu, alikuwa akiyasema
ya moyoni mwake, kwa sauti, basi!
Baada ya hapo Matinyi na mimi tukajikita kuzungumzia fikra zetu kama Watanzania. Matinyi anasema;
“ Unajua Maggid, zamani Watanzania
tulikuwa wazalendo sana, na sasa kama vile tunalipizia, kuwa tunafanya
yale yasio ya uzalendo. Ona, kila mahali utasikia watu wanatumia nafasi
zao kupiga! ( Kuiba)
Hapo Matinyi akanikumbusha kauli ya Waziri Emmanuel Nchimbi alipokuwa bungeni. Nilimwona na kumsikia Nchimbi akitamka;
“ Jamani Watanzania tuache mambo ya
wizi wa mali za umma, yaani, kuna mtu hata kama ni mradi wa ujenzi
unaotumia mifuko sita ya sementi bado anataka kupiga, tubadilike!”
Anasema Emmanuel Nchimbi na kuasa.
Hakika wizi ni tatizo. Na hatari ni
pale wizi unapopewa majina mengine wakati wenye kuiba ni wezi kama wezi
wengine. Ni wahalifu. Leo utasikia mwenye hali nzuri anasifiwa mitaani
kwa kusemwa “ Jamaa kapiga hela ndefu!”
Naam, mhalifu anasifiwa badala ya
kulaaniwa. Na tabia hii ya wizi inaongezeka, hasa kwa kutumia vibaya
ofisi na mamlaka tulizokabidhiwa. Inakuwaje basi ofisini wakubwa
wanaposhiriki ‘ kupiga!’ mali ya umma. Bila shaka walio chini wataiga
hivyo hivyo.
Na majaribu yako mengi, lakini,
Watanzania hatuna hulka ya wizi. Na kama tutasimamia kwenye kanuni na
kuongozwa na maadili, hatuwezi kuiba mali za wananchi. Ni dhambi, ni
kukosa uzalendo. Watu wamekalia kufoji risiti za manunuzi, mafuta ya
magari mpaka risiti za teksi.
Kuna wakati nilikuwa kituo cha mafuta
pale Morogoro. Niliendesha gari la ofisini, Dada mhudumu nikamwambia
anijazie mafuta ya laki na nusu. Hayo yalikuwa kwa gharama ya ofisi.
Nikamwambia anipe risiti pia. Kisha nikamwambia anijazie mengine ya
shilingi hamsini elfu. Hayo ni kwa gharama yangu na ya safari zangu
binafsi. Anipe risiti pia.
Alipomaliza kunijazia mafuta dada yule mhudumu akaniuliza; “ Sasa kaka na mimi nitakula wapi?”
Nikampa shilingi elfu mbili, kisha nikamwambia; “ Hiyo inatoka mfukono mwangu, ikusaidie kwa chakula!”
Hakika, katika kazi zetu hizi, na
maisha ya kila siku, tunakumbana na changamoto nyingi. Hulka ya wizi
imekuwa tatizo. Wengi wanatamani ‘kupiga’ kwa vile tu mwingine ‘
anapiga’ na kwamba mambo yake yanakwenda vizuri.
Tunatafuta njia za mkato katika kupata
mafanikio. Hatutaki kuumiza vichwa na kuongeza juhudi za kazi ili
tupate zaidi. Ni tatizo. Sasa kama kila anayekabidhiwa ofisi atafanya
kazi ya ‘ kupiga’ nchi itabaki na nini? Na wananchi watakuwa katika hali
gani?
Na shida ni pale wanaojitahidi kuishi
maisha adilifu wanaposhushwa majukwaani na kufanywa kuwa wahalifu!
Maana, katika sehemu nyingine wenye kujitahidi kuishi maisha adilifu
hata kwenye kazi wanaambiwa; “ Wanajifanya wazalendo sana”
Na sehemu nyingine huwa ni mwanzo wa kuundiwa zengwe na hata kutengenezewa kashfa za kutungwa.
Na nahofia, kuwa kauli ya Mizengo
Pinda ya kusema; ‘ Pigeni Tu!’ inaweza kutafsiriwa vibaya kwa wenye
hulka ya ‘ kupiga’ kwa maana ya kuiba. Kwamba Pinda amewaambia ‘ kupiga
ni ruksa!’ – Kwa maana ya kuiba!
Hapana, ni kweli maisha ni magumu,
lakini, tuifikirie pia nchi yetu na watu wake. Ni wakati sasa wa
kuwaundia zengwe wale wenye hulka ya ‘ kupiga’ kwa maana ya kuiba.
Kwamba jamii iwaite kwa majina yao halisi- WEZI WA MALI YA UMMA. Full
Stop!
Maggid,
Dar es Salaam.
0754 678 252
No comments:
Post a Comment