Rais wa Marekani, Barack Obama anatua nchini kwa ziara ya siku mbili ikiwa ni hatua yake ya mwisho ya ziara yake barani Afrika.
Dar es Salaam. Yametimia! Baada
ya siku kadhaa za kusubiri kwa hamu, vitabu vya historia ya Tanzania
vinaongezewa kumbukumbu wakati Rais wa Marekani, Barack Obama
atakapowasili nchini leo mchana kwa ziara ya siku mbili. Ndege ya Air
Force One itakayombeba Obama na msafara wake itakanyaga ardhi ya
Tanzania saa 8.40 mchana kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius
Nyerere ambako atapokelewa na mwenyeji wake, Rais Jakaya Kikwete.
Obama ambaye anafuatana na mkewe Michelle na
binti zake, Malia na Sasha, anatua Tanzania ikiwa ni sehemu yake ya
mwisho ya ziara yake barani Afrika.
Anawasili Tanzania akitokea Afrika Kusini ambako alikwenda Ijumaa baada ya ziara yake ya Senegal.
Historia imetimia
Imepita miaka 50, tangu Baba wa Taifa, Mwalimu
Julius Nyerere alipotembelea Marekani, Julai 13, 1963 na kukutana rais
wa nchi hiyo wakati huo, John F Kennedy na ziara hiyo inaaminika
kuanzisha urafiki wa viongozi hao ambao umedumu hadi sasa.
Ujio wa Rais Obama una maana na faida kubwa kwa
Tanzania katika maeneo ukiangalia kihistoria, kisiasa, kidiplomasia na
kiuchumi pia.
Ziara ya Obama ni heshima kubwa kwa Tanzania na
itaingia katika vitabu vya kihistoria kwani ana rekodi ya kuwa mtu
mweusi wa kwanza kuchaguliwa kuongoza taifa la Marekani. Kuchaguliwa
kwake (Obama), ambaye baba yake mzazi alikuwa na asili ya Kenya
kuliashiria nuru mpya kwa siasa za Marekani kwani watu weusi wa taifa
hilo kwa miaka mingi walikuwa wakipigania haki za kufaidika na fursa za
kiuchumi na kisiasa katika taifa la Marekani.
Tanzania, kwa miaka mingi ilikuwa inaunga mkono
harakati za watu weusi na ndiyo maana iliikuwa karibu na viongozi wa
harakati za kupigania haki za watu weusi.
Mwalimu Julius Nyerere alikuwa karibu na Martin
Luther King na mkewe Correta , ambao waliongoza harakati za mtu mweusi
kujikomboa.Pia, viongozi wengine wa harakati hizo za mtu mweusi
kutambuliwa kule Marekani, Jesse Jackson, Andrew Young na Malcolm X
waliitembelea Tanzania mara nyingi. Obama alipochaguliwa kushika
nafasi hiyo mwaka 2008 alifurahiwa na wapenda amani kote duniani na hasa
Waafrika kwani walimhesabu kuwa ni sehemu yao.
Kuja kwake leo ni heshima kubwa kwani Tanzania
inakuwa nchi ya nne Afrika kutembelewa na Obama baada ya Ghana mwaka
2009 na ziara yake ya hivi karibuni ya nchi za Senegal na Afrika Kusini.
Ukizingatia kuwa Obama ana miaka mitatu na nusu
kabla ya kumaliza kipindi chake cha pili cha uongozi wake huenda ziara
hii ndiyo ikawa ya mwisho kwake barani Afrika akiwa na wadhifa wa rais.
Hata hivyo, Tanzania itabakia katika vitabu ya kihistoria kuwa
ni kati ya nchi chache za Afrika zilizotembelewa na rais mweusi wa
kwanza wa Marekani.
Kwa jumla, Tanzania iko juu katika vipaumbele vya
Marekani kwa bara la Afrika kwani katika kipindi cha miaka 13
itatembelewa na marais watatu , Bill Clinton aliyekuja mwaka 2000 na
George W. Bush 2008.
Kwa nini Obama anakuja Tanzania?
Ujio wake umekuwa gumzo kubwa miongoni mwa
Watanzania huku mijadala ikiendelea katika mitandao ya kijamii, vijiweni
na hata kada za wasomi na wachambuzi pia zinachambua ugeni huo.
Ziara hiyo ya Obama imetafsiriwa inatokana na
Tanzania kuwa na rasilimali nyingi na hasa kugunduliwa kwa gesi na
dalili za kuwapo mafuta kwenye sehemu mbalimbali za nchi hii. Pia,
kuwepo kwa rasilimali za madini kama dhahabu, almasi na urani, ambayo
ina manufaa makubwa kwa vinu vya nyuklia vya nchi hiyo, inaweza kuwa
kichocheo cha ziara hiyo.
Ingawa, pia kuna sababu nyingine kama hofu ya
China kutawala uchumi wa dunia, nchi ambayo katika miaka ya karibuni
imeibuka kuwa tishio katika uchumi wa dunia na inawekeza kwa kasi barani
Afrika, pia ni sababu inayotajwa na wengi.
Hofu hiyo inaweza kuoanishwa na ujio wa Rais wa China, Xi Jinping, ambaye aliitembelea Tanzania mwezi Machi mwaka huu.
Kumbuka, Tanzania ilikuwa nchi ya pili kutembelewa
na kiongozi huyo alipochaguliwa kuliongoza taifa hilo lenye idadi
kubwa ya watu duniani.
Rais Jinping aliahidi msaada kwenye miradi yenye
thamani ya Dola 800 milioni baada ya kusaini mikataba 17 katika maeneo
ya miradi na misaada kutoka China.
Akizungumza na waandishi wa habari hivi karibuni,
Balozi wa Marekani, Alfonso Lenhardt alipinga dhana kuwa Obama anakuja
kwa sababu ya rasilimali na kuwaonya Watanzania waondoe hofu kwa wageni
kuiba rasilimali zao.
Pia, alisema Marekani haina hofu na China kutoa
misaada na kuwekeza Tanzania lakini angependa kuona urafiki huo
unawanufaisha Watanzania.
Balozi Lenhardt alitaja sababu za ujio wa kiongozi
huyo Tanzania kuwa ni kutokana na Tanzania kuwa na utawala bora
ukilinganisha na nchi nyingi kusini mwa Jangwa la Sahara.
Alisema kuwa sababu nyingine inayofanya Obama kuzuru Tanzania
ni kutokana na jitihada za Serikali yake katika kutengeneza mazingira
mazuri ya uwekezaji na kasi ya ukuaji wa uchumi.
“Rais Obama anakuja kuunga mkono juhudi za
Watanzania katika kutengeneza mazuri ya uwekezaji lakini bila kusahau
kuwa kasi ya ukuaji wa uchumi wa Tanzania umeivutia Serikali ya
Marekani,” aliongeza Balozi Leinhardt.
Balozi huyo alieleza sababu nyingine inayomleta
Obama kuwa ni kuisaidia Tanzania katika kuendeleza fursa mbalimbali za
kujiletea maendeleo.
Balozi Lenhardt alisema kuwa Marekani ni kati ya
inaongoza kwa kutoa misaada kwa Tanzania na mwaka 2012 pekee ilitoa Dola
750 milioni kupitia Shirika la Millenium Challenge (MCC) ikisaidia
sekta za umeme, maji na miundo mbinu.
Alieleza pia kuwa Tanzania inaunga mkono jitihada
za Serikali kujitosheleza kwa chakula ikifadhili Mkakati wa Kukuza
Kilimo Kusini mwa Tanzania (SAGCOT).
Sababu nyingine ya ujio wa Obama ni kuhimiza haja
ya bara la Afrika kutayarisha viongozi wa kizazi kijacho. Obama
ameanzisha programu ya kuandaa viongozi wa kizazi inayotwa `Young
African Leaders Initiative’ na Watanzania watatu, Modesta Lilian Mahiga,
Masoud Salim Mohamed na Malula Hassan Nkanyemka walishiriki katika
mpango huo na kukutana na kiongozi huyo mwaka 2010.
Balozi Maajar anena
Naye Balozi wa zamani wa Tanzania nchini Marekani,
Mwanaidi Maajar alikaririwa na gazeti dada la The Citizen akisema
uhusiano kati ya Marekani na Tanzania ni kwa misingi ya heshima.
Balozi Maajar alisema kuwa Serikali ya Marekani
inaichukulia Tanzania kuwa nchi ya mfano kwa utawala bora barani Afrika
na ndiyo maana inataka kuisaidia.
Alisema katika kipindi alichokuwa Marekani, hata
Rais Obama alisema anataka kuona Tanzania ikipiga hatua kiuchumi
kutokana na utawala bora. “Marekani inataka kuona Tanzania ikiwa mfano
wa nchi ambazo zimeinuka kiuchumi kutokana na misaada yake,” aliongeza
Balozi Maajar.
Rais Obama awekewa ulinzi mkali
Makachero wapatao 300 wanatazamiwa kuwa nchini katika kipindi chote cha ziara yake nchini Tanzania
Pamoja na makachero pia manowari ya kivita imesogezwa karibu na
pwani ya Tanzania, pia helikopta na ndege ziko tayari nchini kusaidia
safari hiyo ya kihistoria.Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Dar es Salaam
atakapotua leo nao uko chini ya walinzi wa maofisa wa usalama wa nchi
yake na wenzao wa Tanzania.
Wamepanga kufanya hata upekuzi wa mizigo kwa
abiria watakaokuwa wanaingia kwenye uwanja huo. Pia, magari yapatayo 150
nayo yameingizwa nchini kwa ajili ya kusaidia safari hiyo katika
kipindi chote Obama atakapokuwa nchini.
Barabara kufungwa Dar
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadiq
amesema kuwa baadhi ya barabara za Jiji la Dar es Salaam zitafungwa leo
na kesho wakati wa ugeni wa Rais Obama.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Sadiq alisema barabara ya Nyerere itafungwa kuanzia saa 6.30 mchana hadi saa 9.30.
Sadiq alisema barabara hiyo itafungwa katika muda huo ili kupisha msafara wa Rais Obama, ambaye atatua nchini saa 8.40 mchana.
Alisema msafara huo utapita Barabara ya Nyerere
katika maeneo ya Kipawa, Jet Club, Vingunguti, Tazara, Kamata, Gerezani
na maeneo ya posta ya zamani, Magogoni hadi Ikulu.
Pia aliagiza maofisa wa Serikali, sekta binafsi na
watu wengine wasiokuwa na mahala maalumu pa kuegesha magari kwenye
Barabara ya Samora kutokuyaingiza magari yao.
“Tukikuta gari liko sehemu isiyokuwa na maegesho basi litavutwa na kupelekwa Kituo cha Polisi,” alionya Sadiq.
Alisema kesho Obama atatembelea mitambo ya kufufua
umeme ya Symbion iliyopo Ubungo kuanzia saa 4:00 asubuhi na barabara za
Ali Hassan Mwinyi, Sam Nujoma na Morogoro zitafungwa kuanzia 3:00 hadi
saa 5:00.
Alisema baada ya hapo msafara huo utatoka katika
mitambo ya Symbio kwenda Uwanja wa Ndege kupitia katika Barabara za
Mandela hadi Tazara kuingia Barabara ya Nyerere hadi Uwanja wa Ndegesource: mwananchi
No comments:
Post a Comment