WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Saturday, July 6, 2013

Rasimu ya Warioba yamkuna Brigedia mstaafu




Baada ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba (CRC) kutangaza rasimu ya mapendekezo yake Juni 3, mwaka huu wadau malimbali wanaendelea kuipongeza na kuikosoa tume hiyo na Brigedia Ramadhan Haji Faki, Waziri Kiongozi mstaafu wa Zanzibar pia anaeleza alivyoyapokea mapendekezo hayo kaa alivyohojiwa na Mwandishi Juma Mohammed.
Swali: Tanzania inaelekea kwenye kuandika Katiba mpya, umeyapokeaje mapendekezo ya Jaji Warioba juu ya muundo wa Muungano?

Jibu: Mwaka 1984 kwenye mkutano wa Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi (NEC) pale Dodoma nilisema na leo nasema tena naunga mkono muundo wa serikali tatu katika Muungano wetu - Zanzibar na Tanganyika.

Swali: Nini kilitokea hadi ukasema unaunga mkono serikali tatu?

Jibu: Umenikumbusha jambo ambalo siwezi kulisahau, nakumbuka kwenye kikao cha NEC liliibuka suala la Muungano baadhi ya Wazanzibari tukiwa na mashaka na mfumo wa serikali mbili, tukataka mabadiliko kuleta sura ya serikal tatu, Mwalimu (Julius Kambarage Nyerere) aliniuliza; hivi hata na wewe Brigedia Faki unasema moja na moja ni tatu? Sikusita kujibu kwa sababu naamini katika mfumo wa muundo wa Muungano wa Serikali tatu, ndiyo mfumo bora ambao utaondoa kasoro nyingi zilizopo mpaka sasa kwenye Muungano wetu wa Serikali mbili.

Swali: Unasemaje juu ya hofu kwamba muundo wa serikali tatu utavunja Muungano?

Jibu: Serikali tatu sio kuvunja Muungano, wala sio kudhoofisha Muungano, Muungano wetu ni ahadi ndani ya manifesto yetu ya Afro Shiraz Party, hatukuficha msimamo huo, tulisema wazi tangu wakati wa kupigania uhuru neno hilo likifahamika kwamba ASP tunaunga mkono Muungano hata wa Bara la Afrika.

Swali: Je, rasimu imekidhi matakwa ya Zanzibar?

Jibu: Wamekidhi–Tume ya Mabadiliko ya Katiba – kwa kurudia kile tulichokuwa tumekitaka sisi, mimi na Jumbe. Serikali tatu si jambo geni, mie naliunga mkono pendekezo la Tume, halina matatizo. Unaijuwa ile nyumba inayoitwa White Villa? Pale ndimo nilimokuwa nikikaa nilipokuwa Waziri Kiongozi, baada ya mashaka yale ya Dodoma nilikuja mule nikaandika barua ya kujiuzulu nikasema mie basi masuala ya siasa.

Swali: Kujiuzulu kwa Mzee Aboud Jumbe na wewe kuliondoa shinikizo la kudai mfumo wa serikali tatu katika muundo wa Muungano?

Jibu: Kujiuzulu kwetu haikuwa dawa wala tiba, hoja ya kuwemo mabadiliko katika mfumo wa muundo wa Muungano ilikuja kuibuka tena mwaka 1993, Wabunge wapatao 55 wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutoka majimbo ya Tanzania Bara walitaka kuundwa kwa Serikali ya Tanganyika.
Swali: Kwanini kasi ya kudai mabadiliko ya muundo wa Muungano iliibuka mwaka 1984?

Jibu: Mzee Jumbe - wakati huo Rais wa Zanzibar - alitaka kuimarisha Muungano kwa vitendo Muungano kwa kuwa karibu na Rais wa Jamhuri ya Muungano, kiutendaji. Hii ni kwa kuwa Jumbe alikuwa karibu na nyumba kubwa (Ikulu) wakati wa Mzee Karume, bila shaka alijifunza mengi kwa mzee yule na ndio maana aliweza kuamini kuwa muundo wa Muungano uliokusudiwa ni wa ‘Shirikisho’ sio Serikali mbili.

Swali: unategemea nini baada ya Tume ya Jaji Warioba kutoa mapendekezo hayo?

Jibu: Ulimwengu huu ni wa maafikiano, hivyo haitegemewi kusikia kuna mtu au watu wanawabeza wengine kwa tofauti ya maoni. Hoja ya Serikali tatu ni hai,yenye mashiko na ambayo itaijenga nyumba yetu kwa nguzo imara zaidi. Sioni mantiki ya kuendelea na mfumo wa Serikali mbili katika mazingira yaliyopo, mfumo uliopo umezalisha kero nyingi. Hatuwezi kuwafunga midomo wananchi wanaotaka mfumo wa shirikisho, maana Katiba tunayotaka kuandika inawahusu watu wote sio jamii fulani.


Mwandishi wa Makala haya ni mwanafunzi wa Shahada ya Uzamivu(PhD) katika siasa za kimataifa,Chuo Kikuu cha Central China Normal University

 
CHANZO: NIPASHE     

No comments:

Post a Comment