Tunachokishuhudia hivi sasa ni hangaiko
kuu lililotukumba kutokana na kushindwa kwetu kujiletea maendeleo tuliyojiahidi
sisi wenyewe yapata miongo mitano iliyopita.
Nafsi zetu zinatusuta, na zinapotusuta
tunakataa kukubali kwamba tunastahili kusutwa, na badala yake tunatafuta kila
aina ya visingizio ili tuepuke uwajibikaji. Hebu turejee historia yetu kwa
ufupi.
Tulipopata Uhuru tuliiahidi dunia, huku
tukijiahidi sisi wenywe (hapa nazungumzia Watanganyika) kwamba tutafanya kazi
kwa bidii na maarifa kuijenga nchi yetu na kuweza kuonyesha matunda mazuri
zaidi kuliko yote waliyofanya Waingereza katika kipindi cha miaka arobaini
waliyotutawala.
Mwaka 1958, muasisi
wa Taifa la Tanganyika, Mwalimu Julius Nyerere alitamka, kwa niaba yetu, kwamba
tungependa kuwasha mwenge na kuuweka juu ta Mlima Kilimanjaro, umulike nje ya mipaka yetu na ulete
tumaini kila kusiko kuwa na tumaini, upendo kulikojaa chuki, na heshima
kulikojaa dharau.
Haya ni maneno yaliyofanana sana na
yale ya Mtakatifu Francisco wa Asissi, ambaye
aliyafunga maisha yake katika utumishi na huduma kwa masikini ingawaje
alitokana na familia tajiri ya mjini Assisi na katika ujana wake alishiriki
katika biashara na kukuza ukwasi wa baba yake.
Baada ya “kuona mwanga,”
Francisco aliukana ukwasi wa familia yake na akajikita katika utumishi wa watu
na viumbe hai wengine. Ni kwa heshima yake ulianzishwa utawala wa Wafransiska
(Franciscans) ambao itikadi yao inakumbatia umasikini na unyenyekevu katika
utumishi wa Mungu na watu wake.
Mwaka 1961, Mwalimu aliwaambia
Waingereza (kupitia Richard Turnbull, gavana wa mwisho) kwamba angewaalika
baada ya miaka kumi waje wajionee
maendeleo ya Tanganyika waliyokuwa wameiacha masikini, hio, hahehahe,
baada ya utawala wao wa miaka arobaini.
Na kweli, miaka kumi baadaye,
aliwaalika na wakaja kulikuta Taifa lililojiamini na lililokuwa linaonyesha
kila dalili ya kupiga hatua za kusonga
mbele. Desemba 1971 nilikuwa mwanafunzi wa Chuo Kikuu na nilikuwa mwongozaji
(guide) wa wageni mashuhuri (VIP) wa kitaifa. Nilishuhudia binafsi ari na
fahari iliyokuwepo wakati wa maadhimisho hayo, pamoja na hali tete ya usalama iliyosababishwa
na kile kilichoelezwa kuwa njama za Wareno na vibaraka wao wa
ndani.
Wakati huo Tanganyika ilikwisha
kuungana na Zanzibar kuunda taifa jipya la Tanzania, na hatima ya nchi yetu
ilikuwa inaandikwa kwa ustadi mkubwa. Tulikuwa na viwanda vyetu vya nguo, vifaa
vya kilimo na kadhalika, tulikuwa na asasi zetu za fedha na biashara, tulikuwa
na uhuru wetu wa kuwaambia wakuu wa dunia wakome na wakakoma.
Tulijenga msingi, angalau mwanzo tu, na
matumaini yalikuwa makubwa juu ya mustakabali wa nchi yetu. Tulikuwa ni nguzo
kuu ya mapambano ya kulikomboa bara la Afrika, na vita ya ukombozi ilikuwa inarindima
Msumbiji, Angola, Zimbabwe, Namibia na kwingineko. Ilikuwa fahari kubwa
kuwa Mtanzania.
Miaka hamsini baada ya Uhuru, tumekuwa wanyonge
zaidi. Sababu kubwa ya unyonge huu ni kwamba hatujafanikiwa kufasiri ndoto za
zama zile kwa kuwapa wananchi wetu, hasa masikini kabisa miongoni mwao,
matumaini, angalau matumaini tu, ya maisha bora kwa wao wenyewe au kwa uzao
wao. Badala yake, katika medani kadhaa, tumewapa sababu za kukata tamaa kabisa.
Naomba nieleweke vyema hapa. Hali
ninayoieleza haikuanza leo hii wala jana, wala juzi. Tunaweza kuonyesha ni
jinsi gani tulivyoanza kuteleza taratibu tangu awamu ya kwanza kabisa, chini ya
uongozi wa muasisi tunaye muenzi. Hili nimeliandika mara nyingi mno, na sidhani
kwamba yupo yeyote anayeweza kushuku dhamira yangu.
Tatizo ninaloliona ni kwamba hatutaki
kuyajadili matatizo yetu, na badala yake tunaona faraja katika kuyafunikiza,
kama vile tunaamini kwamba yasipoonyeshwa hadharani, yasipoonekana na
kujadiliwa, yatatoweka. Mawe!
Hayatoweki, na badala yake kila
siku yanakua na kuchukua sura mpya, mbaya zaidi na ya hatari zaidi. Kila
unapotokea mlipuko watawala wetu wanadhani kwamba ni tatizo jipya, kwa hiyo
wanaushughulikia mlipuko huo kwa nguvu zao zote (nguvu zao zote kwa maana
halisi ya nguvu zisizo kiasi, nguvu za “kupiga,” si kwa umahiri wowote wa
tafakuri na utafiti wa utatuzi wa suluhu).
Tofauti na tafakuri, kupiga ni rahisi
kwa watawala, kwa sababu wakati tafakuri inawahitaji wao ndio watafakari,
kupiga hakuwahitaji wao wafanye lolote zaidi ya kutoa amri, “Piga!”
Wapigaji wapo wa kutosha.
Kwa bahati mbaya (nzuri kwa wengine),
historia inatuonyesha (pale tunapotaka kuona) kwamba kila kipigo cha uonevu
huzaa uadui usioisha, uhasama wa kudumu na ghadhabu za masafa marefu. Aidha
historia inatufundisha (pale tunapokuwa tunafundishika) kwamba jamii
haziburuzwi kwa maguvu ili zipate maendeleo; jamii hujenga utashi wa maendeleo
taratibu, kila kizazi kikijenga juu ya msingi ulioachwa na kile
kilichotangulia, kwa kudunduliza (incrementally).
Ule msemo wa zamani, kwamba mchungaji
mmoja anaweza kuwaswaga ng’ombe mia kwenda mtoni, lakini wachungaji mia hawana
uwezo wa kumlazimisha ng’ombe mmoja tu kunywa maji, unahusika hapa.
Naamini kwamba haya yote tunayajua,
hata kama kwa sababu fulani, zilizofichika na zilizo wazi, hatutaki, au
hatuwezi kuyaishi (kwa maana ya kuyatafsiri katika maisha yetu na kazi zetu).
Kwa mfano, tuchukue “ukorofi” wa baadhi
ya wananchi wa Mtwara kuhusu gesi. Wanapigwa. Ikija kutokea “ukorofi” wa
wananchi wa Kigoma kwa gesi hiyo hiyo, watapigwa. Wananchi wa Dodoma
wakiandamana kuhusu madhara ya urani, watapigwa. Halafu wananchi wa Mbeya
wakihoji juu ya makaa ya mawe, wapigwe, na kadhalika.
Ni dhahiri kwangu kwamba nchini humu,
na katika maeneo mengi yaliyotofautiana kwa maumbile, wananchi wanazo sababu
lukuki za kutoridhishwa na jinsi mambo yanavyoendeshwa na watawala. Ikiwa kila
watakapoandamana, kulalama au kukataa kutii amri wanazoziona kama za kuwaumiza
watapigwa, kipigo kitakuwa ni kila mahali nchini.
Tayari, katika maeneo kadhaa, kipigo
kimekuwa ni jambo la kawaida. Tayari tumeona wazi wazi ambavyo watu wameumizwa
kwa vipigo nje ya hukumu ya sheria. Bado tunasema watapigwa zaidi?
Ule mwenge tuliosema tutauweka juu ya
Mlima Kilimanjaro (hadi leo tunaimba wimbo huu) ni wa kueneza vipigo kila
ambako hakuna vipigo, vilio mahali pasipo na vilio na simanzi kwa wote wasio na
simanzi?
No comments:
Post a Comment