UMEWAHI kujiuliza swali hili moja
tu? Kwamba kuna tofauti gani kubwa ya msingi baina ya marais Benjamin Mkapa na
Thabo Mbeki na waliowafuatia madarakani, Jacob Zuma na Jakaya Kikwete?
Au ungerudi nyuma kidogo tu; kwamba
ilikuwapo tofauti gani kubwa baina ya marais Nelson Mandela na Julius Nyerere
na waliowafuata yaani Thabo Mbeki na Ali Hassan Mwinyi?
Unaweza ukaenda mbali zaidi.
Ukajiuliza kuhusu tofauti baina ya Nicholas Sarkozy na Francois Hollande kule
Ufaransa, Mwai Kibaki na Uhuru Kenyatta hapo jirani Kenya na Iddi Amin
Dada na Prof. Yusuf Lule pale Uganda.
Sizungumzii tofauti za kimwonekano,
nguo wanazovaa au matamshi ya lugha mbalimbali. Ninachozungumzia ni tofauti
katika utendaji wao wa kazi. Nimejaribu kuwatafiti kidogo na nimebaini kwamba
kuna tofauti kubwa baina ya viongozi wa bara letu hivi sasa kulinganisha na
enzi za uhuru.
Hebu angalia kuhusu Nyerere na
Mandela. Ingawa wameongoza katika nyakati tofauti, Nyerere na Madiba ni watu wa
rika lililokuwa pamoja wakati wa harakati za kudai uhuru, ingawa kiongozi huyo
wa Afrika Kusini alikuwa mkubwa kidogo.
Nyerere alikuwa mzuri kama msomi
(intellectually) na mzuri pia kwa siasa za watu wa hali ya chini (grassroots
politics). Ndiyo maana aliweza kuja na kitu kama Azimio la Arusha lililoeleza
kinaga ubaga wapi Tanzania inatakiwa kuelekea.
Kisomi pia, Nyerere aliweza kuandika
vitabu na maandishi ya kutosha kuhusu msimamo wake wa masuala mbalimbali. Wengi
pia wanamsifu kwa namna alivyoweza kutafsiri vitabu vya Kiingereza kwa lugha ya
Kiswahili katika namna rahisi kabisa.
Msomi maarufu katika ukanda huu wa
Afrika Mashariki, Profesa Ali Mazrui, anasema katika Bara la Afrika, mwanasiasa
pekee anayeweza kusema alikuwa na kiwango cha usomi wa Mwalimu Nyerere ni
aliyekuwa Rais wa Senegal, Joseph Sedar Senghor.
Katika siasa za watu wa hali ya
chini, Mwalimu pia alikuwa juu. Mara nyingi akionekana anacheza mchezo wa bao
na wananchi ambao wengi wao walikuwa wakulima na wafanyakazi wa kiwango cha
chini kabisa.
Hawa ni watu ambao katika hali ya
kawaida kabisa wasingetaraji kukaa meza moja na rais. Mwalimu alionekana mara
nyingi akiwa amevaa nguo kama mkulima wa kawaida na akilima.
Katika Dar es Salaam ya miaka ile ya
1960 na 1970 ambayo asilimia kubwa ya wakazi wake walikuwa ni Waislamu, Nyerere
alionekana kama mwenzao kwa tabia yake ya kuvaa kofia za aina ya baraghashia.
Nilisoma katika kitabu kimoja cha
Mohamed Said kwamba wakati wa msiba wa Abdul Wahid Sykes,
Nyerere alisimama
msibani muda wote kama watu wa kawaida na hata alipoletewa kiti hakukaa.
Alitembea pia kwa mguu kutoka Gerezani ulipokuwapo msiba hadi Kisutu kwenye
makaburi.
Huyu alikuwa mtu wa watu.
Ukimlinganisha na Mandela, kama msomi, Nyerere alikuwa juu kidogo ingawa
Mandela alikuwa msomi pia wa kiwango cha kuridhisha.
Harakati zake za kisiasa zilimfanya
Mandela kuwa kipenzi cha watu wa chini kama ilivyokuwa enzi za Nyerere. Kwenye
kitabu chake cha The Long Walk to Freedom, Mandela anaeleza namna alivyovutiwa
na Mwalimu Nyerere kwa vile alimkuta akiwa anaendesha gari mwenyewe wakati
tayari alikuwa kiongozi wa juu kabisa wa Taifa la Tanganyika.
Hivyo, Mandela na Nyerere walikuwa
wazuri kwa siasa za watu wa chini. Nyerere alimzidi Mandela kama msomi lakini
Mandela alimzidi Nyerere kwenye eneo la uadilifu (integrity).
Kwa kiasi fulani Mwalimu alikuwa
kipenzi cha wazungu. Mwenyewe pia aliwapenda wazungu na ndiyo maana hata hati
(mwandiko) yake ilikuwa ya kizungu kabisa. Mandela alikuwa chukizo la makaburu.
Kwa mateso ambayo yeye binafsi na familia yake waliyapata kwa makaburu, ni
vigumu kuona aliweza kuwasamehe kabisa.
Hakulipiza kisasi. Kwenye utawala wa
Nyerere, kuna hadithi za watu waliowekwa kizuizini bila makosa. Kuna
walioharibiwa kabisa maisha yao. Na pia, Nyerere hakutaka kuweka kifungu cha
Haki za Binadamu (Bill of Rights) katika Katiba ya Tanzania.
Kwa matendo yake haya, Nyerere
amezidiwa na Mandela kwa kiasi fulani kwenye eneo hili la uadilifu. Mandela ni
kama vile hakumuonea mtu. Kuna wakati, alimwachia kiti chake cha urais mpinzani
wake namba moja wa kisiasa, Chifu Mongosuthu Buthelezi.
Hata hivyo, tunaweza kukubaliana
kitu kimoja; kwamba Mandela na Nyerere wote walikuwa wasomi, wanaojali watu wa
chini na wenye kiwango maridhawa tu cha uadilifu. Ila walikuwa wakizidiana
kidogo kwenye maeneo fulani fulani.
Ukichunguza kwa makini, utabaini
kwamba wengi wa waliokuwa viongozi wa Afrika katika zama za kudai uhuru na
wakati wa uhuru, walikuwa na sifa zinazofanana na zile za Mwalimu na Mandela.
Tizama kwa Kwame Nkrumah na Milton
Obote. Angalia kwa Modibo Keita na Ahmed Sekou Toure. Watazame Gamal Abdel
Nasser na Tom Mboya au Jaramogi Oginga Odinga.
Tangu kwa Patrice Lumumba na
Augustinho Neto. Wote, kwa ujumla wao, walikuwa na mambo makubwa matatu ingawa
kiwango walipishana kidogo; Usomi na Uelewa wa Mambo, Uadilifu na Wafuasi.Tuje
kwa waliowafuatia.
Mzee Mwinyi ni msomi wa kiwango
chake (ila si kama Nyerere). Kwa bahati nzuri, alikuwa na mapenzi ya dhati kwa
masikini. Ndiyo maana sera zake za RUKSA zilisaidia sana kubadilisha maisha ya
watu.
Mzee Mwinyi pia alikuwa na uadilifu.
Ndiyo maana leo anaweza kupita popote hapa nchini na watu wakamshangilia. Hata
hivyo, hakuna anayemkumbuka Mzee Mwinyi kwa usomi wake wala uadilifu wake.
Atakumbukwa zaidi kwa kuondoa shida za wananchi zilizokuwapo wakati akirithi
madaraka.
Mbadala wa Mzee Mandela alikuwa
Mbeki. Mbeki alikulia kwenye mafunzo ya Oliver Tambo.
Nilizungumza na Balozi wa zamani wa
Tanzania nchini Afrika Kusini, Ami Mpungwe, majuzi tu na akaniambia Tambo
alikuwa miongoni mwa viongozi wenye bongo zinazochemka kweli kweli. Alikuwa
akimlinganisha na Mwalimu.
Mbeki hakukumbwa na kashfa yoyote ya
kifisadi. Alikuwa mwadilifu. Alikuja na mipango kabambe ya kulikwamua bara la
Afrika kiuchumi kama vile NEPAD na African Renaissance. Hata hivyo, ni katika
siasa za watu wa chini ndipo Mbeki alipokwama kabisa.
Mbeki alikuwa mtu mshaufu. Mwenye
majidai na asiyeingilika kwa watu wa chini. Na ndiyo maana ilikuwa rahisi kwa
Jacob Zuma kumpindua. Thabo hakuwa kabisa na watu wa kumpigania.
Zuma naye ana yake. Hakuwahi
kumaliza hata sekondari. Hayumo katika kundi la wasomi. Uadilifu wake unatia
shaka kutokana na kashfa mbalimbali zilizomkuta hadi sasa. Ila Zuma ana kitu
kimoja, watu.
Kwenye siasa za wananchi Zuma hana
mfanowe nchini Afrika Kusini. Nilikuwa Johannesburg muda mfupi kabla ya
uchaguzi uliomwingiza madarakani na nakumbuka kumsikia aliyekuwa Mwenyekiti wa
Umoja wa Vijana wa ANC, Julius Malema (sasa ametimuliwa), akisema yu tayari
kufa ali mradi ‘JZ’ aingie madarakani.
Mkapa alikuwa sawa na Mbeki. Mipango
mikubwa mikubwa ya kujikwamua kiuchumi na utetezi wa mfumo wa utandawazi ambao
wananchi wengi walikuwa hawaujui. Uadilifu wake unatia shaka kutokana na
tuhuma mbalimbali zilizomkabili.
Hata hivyo, sehemu ambayo Mkapa
hakufanya vizuri, ukiondoa kwenye uadilifu, ni kwenye suala zima la siasa za
watu wa chini. Nina imani, zikipigwa kura leo kati ya Mkapa na Mwinyi, Mzee
Ruksa ataibuka na ushindi asubuhi na mapema.
Mkapa hakuwa na nguvu kwa watu. Na
ndiyo maana, alishindwa kuwashawishi watu wamchague mtu aliyemtaka yeye amrithi
urais. Akaamua kwenda na ‘muvu’ kwa kuchagua mtu ambaye “wenye chama”
walimtaka.
Kikwete naye ni msomi (ingawa si wa
kiwango cha Nyerere na Mandela) na ana uadilifu kama wa Mzee Ruksa. Alicho
mahiri Jakaya ni kwenye siasa za chini. Kwenye kipindi cha kuelekea mwaka 2005,
kuna watu ninaowafahamu ambao walikuwa tayari kupoteza kazi au kufa ili Jakaya
aukwae urais.
Kwa hiyo, hana usomi wa kiwango cha
Mwalimu. Hana uadilifu wa kiwango cha Mwalimu lakini ana ufuasi unaokaribiana
na aliokuwa nao Mwalimu. Mkapa alisogelea kwenye usomi na uelewa lakini akafeli
kwenye uadilifu na wafuasi.
Kama Mkapa angeendeleza ile taswira
yake ya Mr. Clean aliyokuwa nayo kabla hajapata urais na kwa kiwango chake cha
usomi na uelewa wa mambo, huenda angepata wafuasi wengi sana. Na naamini
angeweza kufikia walau nusu ya mafanikio ya Mwalimu.
Iddi Amin hakuwa msomi lakini katika
miaka yake ya mwanzoni, alikuwa akipendwa sana na wananchi. Profesa Lule
alikuwa msomi mzuri lakini hakuwa na wafuasi.
Sarkozy alikuwa msomi mzuri na mwenye
mipango mikubwa. Huenda alikuwa na uadilifu mzuri tu. Hata hivyo, alishindwa
kwa sababu hakuwa na wafuasi. Kwa upande wake, Hollande anaonekana atapata
wafuasi wengi.
Ana sera nzuri za kuvutia masikini.
Matajiri wanaanza kumchukia. Anaweza asiwe msomi mzuri kama Sarkozy lakini ana
wafuasi.
Katika kinyang’anyiro cha kuwania
kumrithi JK mwaka 2015, naona majina mbalimbali yakitajwa. Kwenye upembuzi
wangu, naona wengi wana hili lakini hawana lile.
Sioni mtu ambaye ana sifa zote tatu.
Mwenye usomi na uelewa wa kutosha wa masuala muhimu, mwenye wafuasi wa kutosha
na mwenye uadilifu usio na shaka.
Mambo ni yaleyale… Hatuwezi kumpata
Nyerere mwingine. Ni ama tumpate kama Mkapa au kama Kikwete.
Ni mara chache miungu wanakupa vyote
kama ilivyokuwa kwa Mwalimu. Hata hivyo, ni mara nyingi wanakupa hiki au
kukunyima kile.
Wanasema Mungu hamnyimi mja wake.
No comments:
Post a Comment