Johannesburg.
Mke wa Nelson
Mandela, Graca Machel kwa mara ya kwanza amejitokeza hadharani
kuzungumzia hali ya kiafya ya mumewe kwamba kuna wakati anazidiwa lakini
hajambo.
Graca alisema hayo jana kwenye sherehe za uzinduzi
wa siku ya Utamaduni na Michezo ya Nelson Mandela iliyofanyika kwenye
Kituo cha Kumbukumbu ya Rais huyo wa zamani wa Afrika Kusini.
Alieleza sababu za kuhudhuria sherehe hizo kwamba
kubwa ni kuwashukuru kwa kuwa pamoja na kumwombea afya njema Mandela
tangu alipolazwa hospitali Juni 8, mwaka huu.
Graca alisema pamoja na kwamba Mandela amelala
akiugua hospitali, lakini ameendelea kutoa zawadi kwa wanajamii wote ya
kuwaunganisha pamoja, ambayo ni michezo na utamaduni.
“Madiba kuna wakati hayuko vizuri. Wakati mwingine
anakuwa na maumivu. Lakini hajambo,” alinukuliwa Graca akizungumza
katika sherehe hizo.
Katika hatua nyingine mjini Pretoria, Rais Jacob
Zuma juzi alisema kuwa hali ya Rais wa zamani wa Afrika Kusini Nelson
Mandela bado ni mbaya na hakuna mabadiliko.
Rais Zuma alisema hayo baada ya juzi (Jumatano) jioni kwenda hospitali kumjulia hali Mandela, ambapo alikuwa na msafara mkubwa.
Kiongozi huyo pia aliwaomba wananchi wa Afrika
Kusini kutenga dakika 67 kwa ajili ya Siku ya Mandela ya Julai 18,
ambayo ni siku yake ya kuzaliwa.
Alisema kauli mbiu ya siku hiyo ni “Chukua hatua;
penda mabadiliko; fanya kila siku iwe siku ya Mandela kwa kujielekeza
katika masuala ya chakula, makazi na elimu.
Wakati huohuo, kumekuwa na hali ya utulivu katika
eneo la Hospitali ya Medi-Clinic aliyolazwa Mandela, tofauti na
ilivyozoeleka kuwa na pilikapilika nyingi.
Kwa mujibu wa taarifa, watu wanaopita eneo hilo la
hospitali wamekuwa wakionekana wakiwa na hali ya utulivu, huku wengine
wakipiga picha kwenye kadi, maua, bendera, vipeperushi na mabango
yaliyowekwa kandokando ya hospitali hiyo, yakiwa na ujumbe wa kumtakia
nafuu ya kuumwa Madiba.
Wakati hali hiyo ikiendelea kutokea mjukuu wa
Mandela, Mandla Mandela ameendelea kuikoroga familia hiyo, baada ya
kuzungumza na waandishi wa habari akidai kushangazwa na mahakama
ilivyoharakisha kesi hiyo kuhusu mvutano wa sehemu ya kuzikwa Mandela na
siyo miaka miwili iliyopita baada ya yeye kufukua makaburi.
Mandla aliendelea kutetea msimamo wake kwamba ana haki zote za
kuamua sehemu ambayo atazikwa babu yake. “Babu yangu amekuwa
akinikumbusha kuwa jukumu langu la kwanza ni kuwaongoza watu wetu,”
alisisitiza.
Alisema alipewa wadhifa huo siku nyingi
“Watu wanahoji mamlaka yangu, wamesubiri kwa miaka
yote,” alisema Mandla na kuongeza kuwa Mvezo ni kijiji chenye watu
maskini na wasio na ajira, hakuna maji salama ya kunywa, ufaulu katika
shule za sekondari ni mdogo na eneo limekumbwa na ugonjwa wa Ukimwi.
source: mwnanchi
No comments:
Post a Comment