Kiungo wa Tanzania, Amri Kiemba akipasua ngome ya Uganda katika mchezo wa leo Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam (HM)
BAO pekee la Dennis Iguma dakika ya 46
jioni hii limeiwezesha Uganda kuibuka na ushindi wa 1-0 dhidi ya
wenyeji, Tanzania kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na kujiweka
katika nafasi nzuri ya kusonga mbele kwenye michuano ya Ubingwa wa
Mataifa wa Mataifa Afrika (CHAN), inayohusisha wachezaji wanaocheza ligi
za nchini mwao pekee.
Iguma aliifungia The Cranes bao hilo,
baada ya kutokea piga nikupige langoni mwa Stars kufuatia krosi maridadi
ya Brian Majwega, ambaye leo alikuwa mwiba mkali kwa Taifa Stars.
Hadi mapumziko hakuna timu
iliyofanikiwa kuona lango la mwenzake na kwa ujumla katika dakika zote
hizo 45 hakukuwa na shambulizi la kutisha kwa pande zote.
Brian Majwega alifanikiwa kumgeuza
uchochoro Erasto Nyoni na kuingia ndani mara kadhaa, lakini pasi na
krosi zake ziliokolewa na mabeki wa Stars inayofundishwa na Mdenmark,
Kim Poulsen.
Mrisho Ngassa alipewa mipira mirefu
kadhaa, lakini mabeki wa Uganda wakiongozwa na mkongwe, Nahodha wao,
Hassan Wasswa walisimama imara kumdhibiti.
Mashambulizi mengine ya Stars
yalipitia kwa John Bocco ‘Adebayor’, ambaye alikuwa anapigiwa mipira
mirefu, lakini alidhibitiwa pia. Timu zote zilicheza sawa kipindi cha
kwanza.
Kipindi cha pili timu zote zilifanya
mabadiliko, Stars ikiwapumzisha beki Erasto Nyoni na kiungo Mwinyi
Kazimoto na kuwaingiza David Luhende na Haroun Chanongo, lakini walikuwa
ni Uganda wanaofundishwa na makocha wa zamani wa klabu ya Yanga,
Mserbia Milutin Sredojevic ‘Micho’ anayesaidiwa na Sam Timbe waliobuka
vinara.
Lakini baada ya kufungwa Stars,
waliongeza kasi na nguvu ya uchezaji na kufanikiwa tu kulitia misukosuko
lango la Uganda na si kupata bao japo la kusawazisha.
Matokeo hayo yanamaanisha Stars
itahitaji kushinda ugenini kuanzia mabao 2-0 wiki mbili zijazo ili
isonge mbele, vinginevyo itakuwa imetupwa nje ya mashindano hayo. Katika
mchezo wa leo kikosi cha Stars kilikuwa;
Taifa Stars; Juma Kaseja, Erasto
Nyoni/David Luhende, Shomary Kapombe, Aggrey Morris, Kevin Yondan, Frank
Domayo, Amri Kiemba, Salum Abubakar, John Bocco ‘Adebayor’, Mwinyi
Kazimoto/Haruna Chanongo na Mrisho Ngassa.
The Cranes; Hamza Muwonge, Hassan
Wasswa, Nico Wadada, Brian Majwega, Savio Kabugo, Richard Kasaga, Dennis
Iguma, Said Kyeyune, Joseph Mpanda, Patrick Edema/Ivan Ntege na Tonny
Odur/Frank Kalanda.
Chanzo: Binzubeiry
No comments:
Post a Comment