Dar es salaam. Kuna mambo mengi ambayo yanaonekana kama ni funzo kwa Watanzania kutoka kwa Rais wa Marekani, Barack Obama.
Mojawapo ya mambo hayo ni umuhimu wa viongozi kujali wananchi na taifa kwa jumla kama njia ya kusaidia kuharakisha maendeleo.
Sifa za kiongozi bora
Kulingana na wasomi, Cleeton na Mason (1934)
uongozi maana yake ni hali ya kuonyesha uwezo wa kushawishi watu, na
matokeo ya kiongozi huonekana kwa namna ambavyo anakubalika au hakuliki
katika jamii. Kiongozi hupata mafanikio kupitia kushawishi watu hatimaye
wafanye kwa hiari yao, siyo kwa kutumia nguvu.
Kitendo cha wingi wa watu waliometanda barabarani
katika maeneo mbalimbali ya Dar es Salaam kumlaki Obama ni ishara nzuri
ya kuwa ni kiongozi wa watu.
Ziara yake Afrika
Obama alianza ziara yake Afrika hivi karibuni kwa
kuanza kutembelea Senegal, ambako aliisifia kwa kuzingatia demokrasia na
kusema kwa hakika inafaa kuigwa na mataifa mengine ya Afrika.
Baadaye akaenda Afrika Kusini, ambako pamoja na
mambo mengine alitembelea Kisiwa cha Robben, mahali ambapo Nelson
Mandela alifungwa kwa miaka 27.
Aidha baada ya kutoka Afrika kusini, Obama aliingia Tanzania. Aliongea mambo mengi, ikiwemo kusifia uwepo wa amani nchini.
Anaipenda Afrika
Obama anaipenda Afrika, ni bara alilozaliwa baba
yake mzazi, Dk Barack Hussein Obama, Sir. Baba yake alikufa katika ajali
ya gari Nairobi, ni baada ya kuandamwa na mfumo wa Serikali ya Mzee
Jommo Kenyatta, kwa vile tu, baba yake Obama alikuwa anafikiri tofauti
na watawala.
Baba yake Obama alikuwa rafiki wa karibu sana wa
Tom Mboya aliyeuawa katika mazingira ya kutatanisha. Inaaminika, aliuawa
kwa vile alifikiri tofauti na watawala, baba yake Obama inadaiwa
alikuwa ana siri juu ya kifo cha Mboya.Obama anazijua vizuri siasa za
Afrika.
Serikali isimamie vizuri miradi
Akiwa nchini, Obama aliitaka Serikali ya Tanzania
kusimamia vizuri miradi ya maendeleo, ikiwemo ile ambayo Serikali yake
imeingia mikataba na Serikali ya Tanzania.
Obama na uwazi
Akizungumza mbele ya mwenyeji wake, Rais Jakaya
Kikwete, Rais Obama alisema utamaduni wa kuchelewesha utekelezaji wa
miradi haufai kufumbiwa macho kwani unakawiza maendeleo kwa wananchi
wenye shida.
“Utakuta mradi unakaa kwa miaka saba au minane
bila ya kutekelezwa, jambo hilo hatutaki litokee. Mara mradi unapopangwa
na mipango kukamilika, basi utekelezwe haraka iwezekanavyo ili wananchi
waone faida zake,” alisisitiza Rais Obama.
Tanzania siyo tu imekuwa ikilaumiwa kwa
kuchelewesha utekelezaji wa mikataba, bali hata fedha zinazotengezwa kwa
ajili ya shughuli fulani zimekuwa hazipelekwi kwa wakati, kama ambavyo
katika bunge lililopita wabunge kadhaa waliwahi kulalamika.
Obama na ndoa yake
Anaonekana ni mwenye kuipenda ndoa na familia yake
kutoka usoni na hata matendo yake, tofauti na hali ilivyo kwa ndoa
nyingi za viongozi na wanasiasa wa Afrika ambazo baadhi yake ni maigizo,
huku kukiwa na kashfa na makahaba kuongezeka Dodoma wakati wa vikao vya
Bunge, madai ambayo wanasiasa wamekuwa wakiyakanusha vikali kuwahusisha
nao.
Wapo wanasiasa nchini wanadaiwa kuwa na utitiri wa
wanawake kila kona, wanaoa kila wanapojisikia, nje wana heshima lakini
ndani wananuka kwa uchafu wa ngono za kila aina.
Maisha ya Obama yanatoa funzo na yanaonyesha
umuhimu wa wanasiasa kuwa wasafi katika suala la ndoa pia.Obama huwa
karibu na familia yake, hucheza na watoto na hata mbwa wake.
Kuna wanasiasa nchini hawana muda na familia zao,
bize na anasa, akitoka kazini anaishia baa kunywa na wenza wa nje, sio
mumewe au mkewe.
Hii kwa mujibu wa msomi wa masuala ya uongozi,
Richard Bass, sio maisha yanayofaa kwa kiongozi.Je, ndio za wanasiasa na
viongozi wa Tanzania zikoje? Jibu sahihi wanalo wenyewe.
source: mwananchi
No comments:
Post a Comment