MARA nyingi hatujiulizi swali hili.
Kwenye kitabu chake cha mwaka 1962; TUJISAHIHISHE, Mwalimu Julius
Nyerere anaandika; “Nataka kutaja makosa machache ambayo mara nyingi
huzuia umoja wowote kuwa imara hata ushindwe kutimiza madhumuni yake. Ukiondoa
matatizo wayapatayo binadamu kwa sababu ya mambo kama mafuriko, nzige,
kiangazi, matatizo yao mengi hutokana na ubinafsi.”
“Swali ambalo twalisikia mara kwa mara;
hali yetu ya baadaye itakuwaje? Mtu anayeuliza anafikiri kuwa TANU iliundwa kwa
faida yake yeye binafsi. Ni kama kwamba TANU ilipoundwa ilimwahidi kwamba ikiwa
atakubali kuwa mwanachama, au kiongozi, basi, TANU itamfanyia yeye jambo fulani
kama tunzo! Anasahu kabisa kuwa TANU inajishughulisha na haja za jumuiya kwa
ujumla.
“Lakini, kwa mtu wa aina hiyo, hata kama
TANU inatimiza madhumuni yake ya Jumuiya, ataona kuwa ni umoja ambao hauna
maana kwa sababu haumtimizii haja zote za nafsi yake! Huu ni ubinafsi.
Kama wanachama wa TANU, na hasa
viongozi, hawatakiuhukumu chama chetu kwa mahitaji ya jamii yao, bali watakihukumu
kwa mahitaji ya nafsi zao wenyewe, chama hakitadumu. Wanachama wa aina hiyo ni
ugonjwa katika chama.”
Mwalimu Nyerere anaendelea; “Dalili
nyingine ya ubinafsi na ambayo ni ugonjwa mbaya sana, ni fitina. Kanuni moja ya
TANU inasema; nitasema kweli daima. Fitina kwangu ni mwiko. Lakini bado tunao
wanachama ambao ni wafitini wakubwa bila kujitambua.”
Miaka 50 baadaye, yaani leo hii,
bado aliyoyaandika Mwalimu yanahitaji kusomwa na kufuatwa na kila aliye makini
ndani na nje ya chama alichoshiriki kukiasisi, CCM. Hakuna ajuaye na aliye
hodari kwa kila jambo.
Hata Mwalimu alikuwa tayari
kujisahihisha, nasi hatujachelewa. Tunayaona makosa yakitendeka. Tusione aibu
ya kujisahihisha.
Maana, chama cha siasa ni mkusanyiko wa
watu wenye itikadi, madhumuni, shabaha na malengo yenye kufanana. Ni chama
kilichojiwekea kanuni za kufuatwa kwa viongozi na wanachama wake. Ni vigumu
kukawa na chama cha siasa kitakachodumu muda mrefu kikiundwa na watu wenye
itikadi tofauti na wasiokubaliana katika madhumuni na malengo ya msingi.
Kikishindwa kuwa na hivyo muhimu,
hakiwezi kuwa na kanuni zitakazofuatwa. Hicho ni chama kwa nadharia, lakini
kimatendo, ni mkusanyiko wa vikundi vya watu wenye malengo, madhumuni na
shabaha tofauti chini ya kivuli cha “chama nadharia”.
Tunahitaji uwepo wa utamaduni wa vyama
vya siasa vyenye kuendesha mambo yake kwa uwazi na ukweli. Katika siasa, ukweli
na uwazi ni vitu muhimu sana, na hivi kamwe visipuuzwe kwa kujali maslahi ya
mtu badala ya jumuiya. Kwani, siasa ni mapambano ya hoja. Siku zote,
kinachopingwa iwe ni hoja na si mtu aliyetoa hoja. Tusizihukumu hoja kabla
hazijawasilishwa.
Tujenge utamaduni wa kujifunza
kusikiliza hoja zinazotolewa, tuzijibu hoja kwa kuzikubali au kuzikataa, bila
kujali uhusiano wetu na mtoa hoja.
Tujifunze kujenga hoja na hata kubomoa
hoja za wengine, kwa nguvu za hoja, si kunyume chake. Hayo ndio mambo ya siasa
na hufanywa na wanasiasa. Tusijifunze kujenga fitna, mizengwe na majungu. Hayo
ni mambo ya umbeya na hufanywa na wambeya, hayaendani na ustaarabu wa kisiasa.
Na tutafakari madhara yanayotokana na
wanasiasa wenye malengo binafsi ya kuwania madaraka bila kuwa na
misingi ya kiitikadi na malengo yaliyo bayana. Wanasiasa wasioweka bayana
kanuni za kuwaongoza. Hawa hujali sana maslahi yao, watakuwa tayari kufanya
lolote, ilimradi waingie au wabaki madarakani. Hawaamini katika siasa kwa maana
tunayoifahamu. Kwao wao, itikadi, malengo, madhumuni na shabaha ya chama
yatabaki kuwa ya chama, na wao wanayo ya kwao wenyewe! “Kila mtu na lwake!”
Na siasa ni nini? Siasa ni hatua za
majadiliano endelevu. Majadiliano yasiyokoma. Hakuna kitu kibaya katika siasa
kama kutafuta njia za mkato katika kufikia malengo, njia hizi zina gharama
kubwa kwa jamii. Njia za mkato uhusisha hoja za nguvu, hila na hata vitisho.
Ni kweli, kuwa demokrasia na
amani katika jamii huenda isiwepo bila wachache kukubali matakwa ya wengi.
Matakwa ya wengi hujulikana kwa njia ya mazungumzo ya wazi wazi, kwa mbinu za
wazi kisiasa. Vivyo hivyo, kinyume chake, yaani matakwa ya wachache. Hata baada
ya majadiliano, baada ya uchaguzi, wachache walioshindwa wanapaswa kukubali
kushindwa. Wanapaswa kufanya hivyo kama kulikuwepo na uhuru na haki katika
majadiliano na hata uchaguzi.
Hata hivyo, kukubali kwao kushindwa
hakuwanyimi haki yao ya kuendelea kuamini katika kile walichokiamini. Hapa
demokrasia inawapa haki watu hawa, na ukweli unawapa wajibu wa kuyaendeleza
mawazo yao, hadi pale walio wengi wayakubali.
No comments:
Post a Comment