WAKATI taifa likiwa katika maombolezo ya vifo vya mashujaa wetu
saba waliouawa huko Darfur, Sudan, wakitumikia kikosi cha Umoja wa Mataifa cha
kulinda amani nchini humo, Jeshi letu la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) lilifanya
tukio linalostahili pongezi nyingi, japo huenda ni wananchi wachache tu wenye
taarifa nalo.
Jumapili iliyopita jeshi hilo lilianza
kutumia rasmi mtandao wa kijamii wa twitter
likitumia ‘handle’ @jw_tz.
Hatua hiyo ni ya kimaendeleo na inaonyesha kuwa jeshi letu limedhamiria kwenda
na kukumbatia teknolojia ya kisasa ya mawasiliano.
Mtandao wa twitter na pengine mitandao ya jamii kwa ujumla, bado
ni suala geni kwa Watanzania wengi. Na licha ya ugeni huo, ukweli kwamba
umiliki na upatikanaji wa huduma ya kompyuta bado ni ‘anasa’ wanayomudu watu
wachache unafanya matumizi ya twitter (na mitandao mingine ya kijamii) kutokuwa
suala muhimu au maarufu kwa jamii yetu.
Hata hivyo, mitandao ya kijamii hivi sasa
imekuwa sehemu muhimu ya mawasiliano; huku ikibadili kwa kiasi kikubwa
upatikanaji na kupashana habari. Wakati kwa muda mrefu mawasiliano kati ya mtu
na mtu yamekuwa yakitegemea aidha neno la mdomo (kwa maana ya watu kukutana au
kwa njia ya barua) au magazeti na redio, na kwa kiasi fulani runinga, mitandao
ya jamii na teknolojia ya mawasiliano kwa ujumla imetokea kuwa njia ya haraka
ya mawasiliano katika jamii.
Ukitaka kupata mfano wa umuhimu wa
teknolojia hiyo ya mawasiliano, ni jinsi
ziara ya kihistoria ya Rais wa Marekani Barack Obama huko nyumbani Tanzania,
hivi karibuni, ilivyoripotiwa in real time (kadri matukio yalivyokuwa
yakitokea) badala ya kusubiri gazeti la kesho au ripoti za redioni au kwenye
runinga.
Kadhalika, kwa kutumia mtandao wa
twitter, wananchi wamekuwa wakiendesha kampeni mbalimbali, na ya hivi karibuni kabisa ni
ile inayohamasisha kupinga kodi ya sim card ambapo inatumia
hashtag #NoSIMcardTax.
Iwapo Serikali itasikiliza kilio cha
wananchi na kusitisha au kufuta kodi hiyo, basi kampeni hiyo ya mtandaoni (hususan huko
twitter) itastahili pongezi kubwa.
Pamoja na pongezi zangu kwa hatua hiyo
ya JWTZ kujiunga na mtandao wa twitter, bado taasisi hiyo inakabiliwa na
changamoto kubwa; hususan kutumia ipasavyo mtandao huo kama nafasi kwa jeshi
hilo kuupasha umma habari stahili.
Kwa mfano, juzi Rais Jakaya Kikwete
aliwaongoza Watanzania kutoa heshima zao za mwisho kwa miili ya wanajeshi wetu
waliouawa Darfur, na katika mazingira mwafaka, tungetegemea akaunti ya twitter
ya JWTZ ingetulea tukio hilo ‘live’ lakini haikuwa hivyo. Siwalaumu kwa vile
pengine ni ugeni tu katika matumizi ya teknolojia hiyo.
Licha ya ujio huo wa JWTZ huko
twitter, mtandao huo wa kijamii unatumiwa pia na baadhi ya viongozi wetu wa
serikali na wanasiasa, japo idadi yao ni ndogo. Rais Kikwete ni miongoni mwa
viongozi hao; huku akiweka historia ya kuwa mmoja wa marais wachache wa Afrika
wanaotumia mitandao ya kijamii.
Miongoni mwa mawaziri wachache
wanaotumia mtandao wa twitter ni Mheshimiwa Lazaro Nyalandu (@LazaroNyalandu),
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii. Uwepo wake katika mtandao huo umenisaidia
kumfahamu katika namna ambayo pengine Watanzania wengi hawaifahamu.
Nyalandu amekuwa mfano bora wa jinsi
inavyostahili na inavyowezekana kuweka maslahi ya nchi mbele ya maslahi ya
kiitikadi. Lilipotokea tukio la milipuko ya mabomu jijini Arusha, Waziri
Nyalandu alishiriki kikamilifu kuufahamisha umma kuhusu hatua mbalimbali
zilizokuwa zikifanyika kuwasaidia majeruhi.
Na japo Nyalandu ni Mbunge
wa CCM, kamwe hajawahi ku-tweet mambo ya kiitikadi, na badala yake tweets zake
zimekuwa zikihusu masuala ya Tanzania na Watanzania, badala ya masuala ya CCM.
Kingine kinachopendeza kuhusu Naibu
Waziri huyo ni usikivu kwa hoja mbalimbali zinazowasilishwa kwake kupitia
mtandao huo. Kama ilivyo kwa Naibu Waziri mwingine, Januari Makamba (@JMakamba), Nyalandu
huwasiliana na wananchi waliopo twitter kwa heshima na unyenyekevu mkubwa,
kiasi yaweza kuwa vigumu kudhani ni mtu mwenye dhamana kubwa serikalini.
Ni kwa sababu hiyo, kupitia mtandao wa
twitter Jumapili iliyopita nilimtumia ombi Waziri Nyalandu kumsihi awasilishe
kilio cha msanii Johnson Nguza (Papii Kocha) ambaye, pamoja na baba yake Nguza Viking
na kaka zake wawili, wanatumikia kifungo kirefu jela kwa kosa la kubaka.
Mwishoni wa wiki, blog mbalimbali
zilichapisha barua iliyoandikwa na msanii huyo (Papii Kocha) kwenda kwa Rais
Kikwete akiomba msamaha kwa yeye na familia yake, na kumwomba Rais awatoe
gerezani.
Nina sababu mbili za msingi za kuguswa
na suala la ‘Babu Seya’ na wanae ambao wamekuwa gerezani kwa takriban miaka 10
sasa. Kwanza, japo kuna msemo maarufu kwenye kila jela kuwa ‘kila mfungwa hana
hatia’ (yaani amefungwa kwa kuonewa), tangu Nguza na wanae walipokamatwa na
hatimaye kufungwa nimebaki na hisia kuwa sheria ilipindishwa dhidi yao.
Mengi yameshasemwa huko mitaani kwamba
kesi hiyo ilisababishwa na visasi binafsi dhidi ya msanii huyo na wanae.
Ikumbukwe kuwa katika nchi zetu masikini kuna ‘haki za aina mbili,’ kwa
wanyonge ambao wanaweza kwenda jela kwa kusingiziwa tu, na kwa vigogo ambao ni
kama wana kinga ya kudumu ya kisheria.
Sababu ya pili ya kumwomba Waziri
Nyalandu amfikishie Rais Kikwete ujumbe wa Papii Kocha ni ya kibinadamu zaidi.
Tuweke kando hisia kuwa kifungo cha Nguza na wanae ni sheria kufuata mkondo au
kupindishwa.
Kama binadamu, na hasa katika Mwezi huu
Mtukufu wa Ramadhan, unajiskiaje ukisoma barua ya kutoa majonzi kutoka kwa
kijana mfungwa anayezeekea jela akiomba msamaha kuhusu hukumu ambayo tangu
mwanzo wafungwa hao wamekuwa wakidai ni ya uonevu tu dhidi yao?
Ndio, huko jela ‘kila mfungwa hana
hatia’ (yaani wafungwa wengi hudai wamefungwa kwa kuonewa hata kama walikamatwa
red-handed wakifanya makosa).Lakini katika mazingira ya kawaida, ni wafungwa
wangapi waliopo jela kwa takriban miaka 10 na wanaendelea kusisitiza kuwa
walifungwa kwa uonevu na wanaomba hukumu dhidi yao ziangaliwe upya au
wasamehewe?
Laiti ukisoma barua hiyo ya Papii Kocha
(na amekuwa akiandika barua kama hiyo mara kadhaa) usipolengwa na machozi basi
utakuwa na ‘moyo mgumu’ kweli.
Lakini hata tukiweka kando huruma
ambayo baadhi yetu tunayo kwa Nguza na wanae, katika ubinadamu tu, msanii huyo
na wanae wameshatumikia adhabu ndefu (bila kujali walitenda kosa au la), na
adhabu waliyokwishapata inatosha kutoa fundisho kwao na kwa jamii kwa ujumla.
Hivi sisi kama jamii tutaathirika vipi iwapo Nguza na wanawe wakisamehewa?
Kama nilivyotarajia, ‘mtu wa watu’
Naibu Waziri Nyalandu alinijibu juzi akisema kwa tweet (namnukuu) “copy that...”
akimaanisha amesikia ombi langu na atalifanyia kazi.
Licha ya imani yangu kwa Nyalandu, nina
imani pia kuwa Rais Kikwete atasikiliza ujumbe huo kutoka kwa mteuliwa wake.
Vilevile ukweli kuwa huu ni Mwezi Mtukufu, na nina hakika Rais amefunga pia,
roho ya huruma itamsukuma kusikiliza kilio cha mara kwa mara kutoka kwa Papii
Kocha, kaka zake na baba yao.
Mwisho, ninaomba kila Mtanzania mwenye
kuamini katika kuwasamehe waliotukosea (ikiwa ni pamoja na wanaotajwa kuwa
wahanga wa makosa yaliyofanywa na ‘Babu Seya na wanawe) atajumuika nami
kuwaombea msamaha wasanii hao.
Maandiko Matakatifu katika Surat Al
I’mran 155 ya Kurani Tukufu na Marko 11:25 ya Biblia Takatifu ni baadhi za aya
lukuki zinazotusisitiza kuhusu msamaha.