Dar es Salaam.
Shirika la Afya Duniani (WHO), limejiunga katika mapambano dhidi ya
ugonjwa wa homa ya dengue kwa kuagiza vipimo 1,000 kwa ajili ya upimaji
nchi nzima.
WHO
imechukua hatua hiyo kusaidia juhudi zinazoendelea za kupambana na homa
hiyo na imeagiza utafiti zaidi ufanyike ili kutambua aina halisi ya
virusi vya dengue vilivyopo nchini kwa kulinganisha na vile
vinavyopatikana katika maeneo mengine duniani.
Akizungumza
na gazeti hili jana, Ofisa wa Taaluma na Udhibiti wa Magonjwa wa WHO,
Dk Grace Saguti alisema tayari chombo hicho kimeagiza vipimo hivyo
vitakavyogharimu Sh17.7 milioni na kila kimoja kinaweza kupima sampuli
25, hivyo kunufaisha watu 25,000.
Hatua
hiyo imechukuliwa huku kukiwa na taarifa kwamba baadhi ya hospitali za
Serikali za wilaya na rufaa zinakabiliwa na uhaba wa vipimo, hali
iliyosababisha kutoza kati ya Sh25,000 hadi Sh30,000 kwa ajili ya kupima
mgonjwa mmoja.
Katika vituo binafsi, wagonjwa wamekuwa wakipimwa kwa gharama inayofikia Sh50,000 hadi 60,000 kwa kila mtu.
Juhudi
hizo za WHO zimetangazwa siku moja baada ya Serikali kupitia Naibu
Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Steven Kebwe kulieleza Bunge kuwa
kwa sasa vipo vipimo 350 na Serikali inatarajia kuagiza vingine 750.
Dk Saguti
alisema WHO imeshatengeneza miongozo, mikakati na mafunzo pamoja na
kutoa vitendea kazi ili kujua namna ya upimaji na udhibiti.
“Sheria
za afya za kimataifa za mwaka 2005 hadi 2007, zinaelekeza nchi kuhusu
tatizo lolote lisilo la kawaida liripotiwe WHO. Serikali ya Tanzania
ilifanya hivyo na miongozo ya homa ya dengue ikatolewa,” alisema.
Alisema
miongozo iliyotolewa na WHO ni pamoja na tatizo la dengue lisiachwe
mikononi mwa Wizara ya Afya pekee, bali sekta zote zihusishwe katika
kuudhibiti.
Miongozo
mingine ni uhamasishaji wa upatikanaji wa vipimo ili kuhakikisha watu
wenye dalili hizo na ambao wamepimwa hawana malaria, wanapimwa na
kutibiwa kama inavyotakiwa.
Alisema miongozo mingine ya WHO ni kuwapo rasilimali fedha ili vituo vya afya viwe na dawa pamoja na vipimo.
Tayari
Rais Jakaya Kikwete ameagiza Wizara ya Fedha na ile ya Afya kushirikiana
na Bohari Kuu ya Dawa (MSD) kupambana na ugonjwa huo kwa dharura.
Takwimu
Jambo
lingine ambalo WHO imeishauri Serikali ni kutafuta takwimu sahihi ili
kujua ukubwa wa tatizo na kulifanyia kazi kulingana na uzito wake.
“Uhakiki
wa takwimu, ushahidi na taarifa sahihi za magonjwa ni suala muhimu
katika kudhibiti. Ndiyo maana tunaitaka wizara kuhakikisha inapata
takwimu sahihi,” alisema.
Alisema
wizara hiyo inatakiwa iwe na mfumo mzuri wa takwimu kuanzia ngazi ya
chini na ihusishe sekta za Serikali na zile binafsi.
Wakati
hadi jana takwimu za Serikali zilionyesha kuwa idadi ya watu waliougua
wamefikia 460, takwimu zilizopatikana katika baadhi ya hospitali jijini
Dar es Salaam zilionyesha kuwa walikuwa wamefikia 677, achilia mbali
waliokuwa wameugua kati ya Oktoba mwaka jana hadi Machi.
Katika
uchunguzi huo wa gazeti hili, ilibainika kuwa Mwananyamala wamefikia
wagonjwa 142, Amana (54), Maabara ya Lancet (53), Hindul Mandal (26),
Aga Khan (11), Kliniki ya IST (245), Regency (63), Temeke (15), Dk
Mvungi (3) Muhimbili (65).
MSD: Tuna vipimo vya kutosha
Wakati
baadhi ya hospitali zikiripoti uhaba wa vipimo, Kaimu Mkurugenzi wa MSD,
Cosmas Mwaifani amesema inavyo vya kutosheleza mahitaji.
“Sisi
wakati wote tupo tayari kupambana na dharura, si tu kwa sababu ya
mlipuko, pia hatuhusiki kabisa na masuala ya kuongezeka kwa bei za
vifaatiba au dawa hospitalini kwa sababu ni taasisi ya Serikali,”
alisema.
Mmoja wa
wasambazaji wa vipimo vya upimaji wa dengue, Ally Hamimu alipiga simu
chumba cha habari jana na kueleza wasiwasi wake kuhusu gharama za vipimo
kuwa akisema ni kubwa kuliko uhalisia.
??Tunaamini
kuna vipimo mbalimbali vya kupima homa ya dengue lakini hata kama
hospitali zinatafuta faida, zinatakiwa kutoza kati ya Sh13,000 na Sh15,
000 kwa kipimo,” alisema Hamimu na kutolea mfano vitendanishi vya Dial
Lab Dengue lgG/lgM ambavyo boksi la vipimo 30 huuzwa kati ya Sh175,000
na Sh190,000.
“Hii
inamaanisha kuwa kipimo kimoja kwa rejareja kinaweza kuuzwa kati ya
Sh6,500 hadi Sh7,500 na huduma za kupima zisizozidi Sh15,000.
“Sasa
kutokana na mahitaji kuwa makubwa ya vipimo hivi baada ya mlipuko wa
dengue, baadhi ya wamiliki wa hospitali wanapandisha bei, wananchi
wasikubali,” aliongeza Hamim.
Dk Buberwa azikwa
Wakati
huohuo, mamia ya wakazi wa Dar es Salaam wakiwamo madaktari na watumishi
wa hospitali mbalimbali, jana walijitokeza katika Makaburi ya Tabata
Kinyerezi, Dar es Salaam kumzika Dk Gilbert Buberwa aliyefariki dunia
Jumapili kutokana na homa ya dengue.
Dk
Buberwa aliyekuwa daktari bingwa na mkuu wa kitengo cha magonjwa ya
akili katika Hospitali ya Temeke, ameacha mke na watoto wawili.
Andrew Msechu, Florence Majani, Nuzulack Dausen na Julius Mathias (FS)source: mjengwa blog
No comments:
Post a Comment