Dk Shein amewataka wajumbe kuwa na
subira kwa kipindi hiki hadi hali itakaporuhusu kiuchumi na suala hilo
linaweza kufikiriwa.PICHA|MAKTABA.
Zanzibar. Rais wa Zanzibar, Dk Ali
Mohamed Shein amekataa maombi ya kuwaongezea posho wajumbe wa Baraza la
Wawakilishi Zanzibar (BLW) kutoka Sh150,000 hadi Sh200,000. (J M)
Uamuzi huo wa Dk Shein umetokana na hali ya uchumi Zanzibar kutoruhusu nyongeza hiyo kwa sasa.
Katibu wa BLW, Yahya Khamisi Hamad
alithibitisha jana kuwa baraza hilo lilipeleka kwa Rais Shein maombi la
kutaka posho ya vikao hivyo iangaliwe upya kutokana na sababu
mbalimbali, lakini kulingana na mazingira ya hali ya uchumi ilivyo kwa
wakati huu imeshindikana kufanya hivyo.
Hamad alisema Dk Shein amewataka
wajumbe kuwa na subira kwa kipindi hiki hadi hali itakaporuhusu kiuchumi
na suala hilo linaweza kufikiriwa.
Alisema Dk Shein alitoa msimamo huo
alipokutana na Spika wa baraza hilo, Pandu Ameir Kificho kwa nia ya
kumweleza uamuzi kuhusu suala hilo. “Rais amekataa maombi ya nyongeza ya
posho za vikao vya wajumbe wa BLW kutokana na hali ya mazingira ya
kiuchumi kutokuwa mazuri kwa wakati huu, amewataka wawe na subira hadi
hali ya mambo itakapotengamaa,” alisema Hamad.
Alisema kamati ya uongozi ya baraza
hilo tayari imekwishataarifiwa kuhusu maombi ya posho kukataliwa na
wajumbe wote kutoka CCM na CUF walitarajiwa kutaarifiwa jana kuhusu
uamuzi huo.
Wajumbe hao wamekuwa wakilipwa posho
ya Sh 150,000 kwa siku mbali na mshahara na posho nyingine zinazokaribia
Sh4,500,000 kwa mwezi.
Akizungumzia kikao cha bajeti
kinachoanza leo mjini Zanzibar, Hamad alisema kikao hicho kitalazimika
kupunguzwa kwa siku ili kuwahi Bunge Maalumu la Katiba ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania linalofanyika Dodoma ambalo lipo likizo na
linatarajiwa kukutana Agosti 5.
Alisema kwa mujibu wa ratiba, kikao
cha bajeti kinatarajia kutumia siku 56, tofauti na miaka mingine ili
kukimbizana na muda na kuwataka wajumbe kujadili bajeti ili kuokoa muda
na kuwahi Bunge la Katiba.
Aidha, katibu huyo wa BLW alisema
kikao hicho kitakuwa na maswali 90, miswada miwili ya sheria ukiwamo wa
Sheria ya Fedha na ule wa Sheria ya Kuidhinisha Matumizi ya Serikali
mwaka 2014/2015.
Tayari, Waziri wa Fedha, Omar Yussuf
Mzee amesema SMZ katika mwaka huu wa fedha inatarajia kutumia Sh 705.1
bilioni, kati ya hizo, makusanyo ya Serikali yatakuwa ni Sh 399 bilioni
na kiasi kingine cha Sh 305.3 bilioni ni misaada ya wahisani na mikopo
mbalimbali.
CHANZO, MWANANCHI
No comments:
Post a Comment