Kamati namba tano ni moja ya kamati 12 za Bunge
Maalumu la Katiba, zilizoundwa na kuanza kuboresha Rasimu ya Pili ya
Katiba, Machi 31 mwaka huu.
Tayari kamati zote zimeboresha Sura ya kwanza na
Sita za Rasimu na kuwasilisha taarifa zake bungeni, ambako zimejadiliwa.
Kamati hiyo namba tano ikiongozwa na mwenyekiti, Hamad Rashid Mohammed,
haikuafikiana katika Ibara ndogo ya (1).
Hiyo imetokana na kura za Wazanzibari katika
kuamua kipengele hicho, kutosha theluthi mbili lakini wakaangushwa na
Watanganyika kwa kura zao kutofikia idadi hiyo.
Kwa upande wa Zanzibar, ibara hiyo ilifanikiwa
kupata theluthi mbili ya kura za wajumbe wote. Hiyo ikimaanisha kuwa
ibara hiyo ilishindikana kubadilishwa kama ilivyokusudiwa na maoni ya
wengi.
Miongoni mwa wajumbe 53 wanaounda kamati hiyo ni
Dk AshaRose Migiro, Aggrey Mwanri, Andrew Chenge, Gerson Hosea Lwenge,
Lazaro Nyalandu, Dk Mary Nagu, Gregory Teu, Godfrey Simbeye, Musa Yusufu
Kundecha, Dk Aley Soud Nasoro, Yasmin Yusufali Haloo, Ezekiah Oluoch na
Jina Hassan Silima.
Wengine ni Joseph Selasini, David Kafulila Hawa
Mchafu, Hamis Dambaya, Khamis Salum, Paulo Makonda, Rehema Said Shamte,
Omar Yussuf Mzee, Asaa Othman Hamad, Mahmoud Thabit Kombo, Fatma
Abdulhabib Fereji, Rashid Seif Suleiman, Ali Abdallah Ali, John Komba,
Omar Nundu, Said Nkumba, Esther Matiko, Leticia Nyerere, Muhammad Amour
Chombo na Thuwayba Idrisa Mohamed.
Pia wako Charles Kitwanga, Shadya Mohamed Suleiman, Luhanga Mpina, Dismas Bwanausi, Devotha Likokola, na Mgeni Juma.
Ibara ndogo (1) inasema, Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania ni Nchi na Shirikisho lenye mamlaka kamili inayotokana na
Muungano wa nchi mbili za Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa
Zanzibar, ambazo kabla ya Hati ya Makubaliano ya Muungano ya mwaka 1964,
zilikuwa nchi huru.
Mapendekezo ya walio wengi ndani ya kamati hii, wakataka ibara ndogo hii ibadilishwe ili isomeke;
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni nchi moja yenye
mamlaka kamili, ambayo imetokana na muungano wa nchi mbili zilizokuwa
Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar, ambazo kabla ya
Hati ya Makubaliano ya Muungano ya mwaka 1964 zilikuwa huru.
Kutokana na kukosekana theruthi mbili ya kura
zilizopigwa na wajumbe wote kwa upande wa Bara, mapendekezo hayo
hayakufanyika, ibara ikabaki kama ilivyo na hivyo Kamati ikalazimika
kuiwasilisha tena bungeni kwa hatua zaidi.
Hata hivyo, ibara ndogo ya (2) na (3) za sura hiyo
ya kwanza katika rasimu, zimepata theluthi mbili ya kura za wajumbe
wote kutoka Zanzibar na Tanganyika.
Kwa nini wengi wanataka mabadiliko?
Waliotaka mabadiliko kwenye ibara ndogo ya kwanza
wanataja sababu ya kwanza kuwa ni Hati ya Makubaliano ya Muungano ya
mwaka 1964, kuwa msingi wa kuwa na Muundo wa Serikali mbili.
Wanasema katika makubaliano hayo, Zanzibar
ilikubali kuhamishia sehemu ya mamlaka yake kwenye Serikali ya Muungano,
huku iliyokuwa Tanganyika ikikubali kuhamishia mambo yake yote kwenye
Serikali ya Muungano.
Wanasema Muundo wa serikali moja haukukubalika kwa
sababu Zanzibar ni ndogo, iliyokuwa na watu 300,000, wakati Tanganyika
ikiwa na watu 12 milioni. Hata kiuchumi, Tanganyika ilikuwa juu zaidi ya
Zanzibar hivyo ingeonekana imemezwa na iliyokuwa Tanganyika.
Ikaonekana Zanzibar ibaki na utambulisho wake kwa maana ya serikali na vyombo vingine vya utendaji.
Kamati hiyo inasema ukweli huo, maudhui ya hati ya
makubaliano na ikiwa changamoto zilizobainishwa kwenye muungano
zikitatuliwa kisheria na kikatiba, serikali mbili ndiyo mfumo unaofaa
kuendelea kuongoza Tanzania.
Wanapinga rasimu iliyoandaliwa na Tume ya
Mabadiliko ya Katiba inayopendekeza Mfumo wa Serikali tatu kwa maelezo
kuwa ni mwendelezo wa Hati ya Makubaliano, wakisema hati hiyo ilikusudia
kuanzishwa muundo wa serikali mbili.
“Waasisi walitia sahihi makubaliano ya serikali
mbili, waliunganisha nchi mbili, hivyo kisheria na kisiasa hati hii
haiwezi kurekebishwa na watu ambao hawakuasisi Muungano huu,” anaeleza
Hamad Rashid Mohammed.
Mohammed anasema msingi wa muundo wa Serikali tatu
unaopendekezwa na Rasimu, hauwezi kuwa hati hiyo ya muungano na kwamba
ikiwa kuna nia ya kuunda aina hiyo ya muungano lazima kuwe na
makubaliano mapya.
Sababu nyingine ambayo inaonekana kuwa na uzito wa
aina yake, ni inayoeleza kuwa pendekezo la Serikali tatu halitekelezeki
kwa kuwa Tanganyika haipo; mamlaka, uendeshaji na masuala yake yote
yalikwishakabidhiwa kikatiba na kisheria kwa nchi inayoitwa “Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania” tangu mwaka 1964.
source ya Habari: mwananchi
source ya Habari: mwananchi
No comments:
Post a Comment