Bila shaka wananchi wengi wa pande zote mbili za Muungano watakuwa wameshtushwa na kauli ya mnadhimu wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Salmin Awadh Salmin kwamba wawakilishi wa chama chake cha CCM wanajiandaa kuwasilisha hoja binafsi kwenye Baraza hilo ili kuwapa nafasi wananchi kuulizwa iwapo wanataka kuendelea na Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) au vinginevyo.
Akihutubia mkutano wa hadhara wa chama hicho
ulioongozwa na katibu mkuu wake, Abdulrahman Kinana mwishoni mwa wiki
mjini Zanzibar, Salmin alisema wajumbe hao wamefikia hatua hiyo kutokana
na kile alichodai kuwa wanaona kwamba lengo na matumaini ya kuundwa
kwake yamefutika. Alisema ni vyema wananchi wakaulizwa kama bado wana
hamu na mfumo huo au ule wa zamani urejeshwe.
Aliwatuhumu viongozi wa CUF kwa kile alichokiita
kitendo chao cha kupinga Muungano na Mapinduzi ya Zanzibar. Kauli ya
kiongozi huyo iliungwa mkono na katibu wa itikadi na uenezi wa CCM,Nape
Nnauye ambaye alisema ni jambo muhimu kuitishwa kura ya maoni ili
wananchi wapate nafasi ya kuulizwa kama wanataka mfumo wa Serikali
iliyopo kabla ya kufanyika Uchaguzi Mkuu baadaye mwaka ujao.
Awali, Katibu Mkuu Abdulrahman Kinana alitumia
muda mrefu kumshambulia katibu mkuu wa CUF, Maalim Seif Shariff Hamad na
kudai kwamba kiongozi huyo amekuwa akiwayumbisha Wazanzibari kwa kile
alichokiita tabia yake ya kubadilisha ajenda za kisiasa na kutikisa
misingi ya umoja wa kitaifa nchini. Alidai kwamba kiongozi huyo
haeleweki na haijulikani anatafuta kitu gani licha ya kuwa Makamu wa
Kwanza wa Rais wa SUK.
CUF imepinga madai hayo na kusema wanasiasa
wanaojadili suala la kuendelea au kutokuendelea na SUK wanapaswa
kujiuzulu. Mkurugenzi wa Haki za Binadamu na Mawasiliano ya Umma wa CUF,
Salum Abdallah Bimani anasema viongozi hao wanakwenda kinyume na uamuzi
wa vyama vyao ambao ulipitishwa na kuridhiwa na vikao vya juu, huku
akisema CUF haina ajenda ya siri ya kuvunja Muungano au kuyasambaratisha
mapinduzi, bali inapigania kile alichokiita Muungano wenye usawa, haki
na heshima kwa kila upande wa washirika.
Tumeandika kauli za viongozi hao kwa kirefu
kutokana na unyeti wa kauli zenyewe. Tumekuwa tukisema mara kwa mara
kwamba sisi ni waumini wakubwa wa Muungano ambao SUK ni sehemu yake. Kwa
maneno mengine, kuiyumbisha SUK ni kuuyumbisha Muungano na kuuyumbisha
Muungano ni kuiyumbisha SUK. Katika hali hiyo, hatuwezi kukaa kimya pale
tunapoona hatari inayoweza kusababisha nyufa katika msingi wa Muungano.
Tungependa kuwashauri viongozi wa Zanzibar
kuilinda SUK kama mboni za macho yao. Wasisahau kwamba SUK ilitokana na
maridhiano baina ya vyama hivyo baada ya kuwapo machafuko ya muda mrefu
kutokana na siasa za visasi na utengano visiwani humo. Kutokana na
ushindani mkubwa wa kisiasa uliopo kati ya vyama hivyo, amani
itatamalaki pale tu vyama hivyo vitakaposhirikiana katika masuala ya
msingi kama kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa kama ilivyo sasa.
Rai yetu kwa viongozi wa CUF na CCM ni kwamba
tofauti kati yao hazitamalizika kwa kuivunja SUK, bali kwa mazungumzo na
maridhiano. Kuivunja SUK ni kuwakwaza wananchi na kuirejesha Zanzibar
katika machafuko na zama za giza za kulia na kusaga meno.
chanzo cha habari: mwananchi
chanzo cha habari: mwananchi
No comments:
Post a Comment