Mmoja atokwa damu masikioni, puani
Mwingine alikuwa anamuuguza nduguye
Ugonjwa wa homa ya dengue unazidi kuenea nchini na sasa katika mikoa Tanga, Pwani, Arusha na Zanzibar, inaripotiwa kuwako kwa wagonjwa waliolazwa hospitalini.
Taarifa ambazo gazeti hili imezikusanya kutoka mikoa hiyo zinasema kuwa watu hao na idadi yao kwenye mabano wamelazwa katika Hospitali za Bombo (1), Tanga; Tumbi (1), Pwani; Mount Meru (1), Arusha na Mnazi Mmoja (3), Zanzibar.
Akizungumza na waandishi wa habari kisiwani Zanzibar jana, Waziri wa Afya, Juma Duni Haji, alisema hadi sasa watu watatu wanaosadikiwa kuugua ugonjwa huo wamelazwa katika hospitali kuu ya Mnazi Mmoja.
Alisema wagonjwa hao ni wanawake na wanatoka eneo la Mwera, Kama na mkazi wa Dar es Salaam ambaye alifika Zanzibar.
Alisema ni mara ya kwanza kutokea kwa ugonjwa huo Zanzibar na tayari wamekwisha kuwasiliana na mashirika mbalimbali yakiwamo Shirika la Afya Dunaini (WHO), Shirika la Taifa la Utafiti Tiba (NIMR) na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii ya Tanzania.
Alisema uchunguzi wa kidaktari kwa wagonjwa hao unaendelea ili kuthibitisha kwa uhakaki kuwa ni za ugojwa huo.
Alisema Wizara ya Afya itahakikisha inachukuwa vipimo (sample) ili kuchunguza kuwapo kwa virusi vinavyosababisha ugonjwa huo na kunyunyizia dawa katika mazalio ya mbu ikiwamo sehemu zenye kutuwama maji machafu na vichaka.
Hata hivyo aliwataka wananchi kuhakikisha wanatunza mazingira ili kuweza kutokomeza mbuu wanaosababisha ugojwa huo.
TUMBI
Ofisa Uhusiano wa Tumbi, Gerald Chami, alisema kuwa wamepokea mgonjwa anayedhaniwa kuwa ana ugonjwa wa homa ya dengue baada ya kukutwa na dalidali zote za ugonjwa huo ikiwemo kutokwa damu puani na masikioni pia homa kali na kichwa kuuma sana.
Alisema mgonjwa huyo alikuwa anatokea Mbezi jijini Dar es Salaam na kuwa aliletwa hosiptalini hapo jana majira ya saa 2 usiku na kuwa hadi sasa anaendelea vizuri, baada ya juhudi kubwa za kitabibu za madaktari.
“Siwezi kusema kuwa ana huo ugonjwa wa homa ya dengue kwani sisi hapa hatuna kitengo cha wagonjwa hao, lakini ana dalili zote zinaonyesha kuwa ana ugonjwa huo, hata hivyo hadi sasa madaktari wamejitahidi na kule kutoka damu kumeacha imebaki kichwa kuuma mfululizo tu,” alisema Ofisa uhusiano huyo.
Alisema kuwa hivi sasa mgonjwa huyo yuko kwenye chumba maalumu ambacho muda mwote kinapigwa dawa ya kuzuia mbu pia amewekewa neti kwa ajli ya kuzuaia mbu.
Hata hivyo, alisema elimu inaendelea kutolewa kwa wagonjwa wanaofika hosptalini hapo ili wajue dalili ambazo nyingi zinafanana na zile za ugonjwa wa malaria na pia jinsi ya kujikinga na ugonjwa huo.
BOMBO
Kutoka Tanga, habari zinasema kuwa Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Tanga Bombo imepokea na kumlaza mgonjwa mmoja anayedhaniwa kuwa na ugonjwa wa dengue.
Akizungumza katika mahojiano na NIPASHE Kaimu Mganga Mkuu wa mkoa wa Tanga Dk. Clemence Marcel, alisema kuwa mgonjwa huyo mwenye umri wa miaka 56 (jina linahifadhiwa) alipokewa Mei 13 mwaka huu akitokea Mbagala Jijini Dar es Salaam.
Dk. Marcel alisema mgonjwa huyo alikuwa na dalili za ugonjwa wa dengue, lakini wameshindwa kuthibitisha kutokana na kukosekana kwa vipimo sahihi vya ugonjwa huo ambavyo mpaka sasa wanasubiri kupatiwa na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii.
“Ni kweli yupo mgonjwa ambaye tunahisi anaweza kuwa na dengue, lakini haijathibitishwa mpaka sasa kwa sababu tunasubiri vipimo kutoka wizarani ingawa kwa mujibu wa maelezo ya mgonjwa ni kwamba huko alikotoka aliuguza mgonjwa wa dengue,” alisema Kaimu Mganga Mkuu huyo wa mkoa.
Hata hivyo, alisema kuwa pia wamefanya jitahada za kuwasiliana na Bohari Kuu ya Madawa (MSD) ili kupata vipimo hivyo, lakini nayo inasubiri kupatiwa na wizara.
Kwa mujibu wa Dk. Marcel mara tu watakapokea vipimo hivyo vitasambazwa kwenye halmashauri zote za mkoa wa Tanga pamoja na mipakani ili kuwapima wageni wanaoingia na kutoka nje ya nchi.
“Tumeshazitaarifu timu zote za afya kwenye halmashauri zetu wawe tayari vipimo vikifika tu tunaanza kuwapima wanaoingia na kutoka hasa katika mpaka wa Horohoro na wakipokea mgonjwa wa dalili za dengue tumewaeleza cha kufanya,” alisisitiza Dk. Marcel.
MMOJA MOUNT MERU
Hospitali ya Mkoa wa Arusha ya Mount Meru, mkoani Arusha imethibitisha kupokea mgonjwa mmoja wa dengue baada ya vipimo vyake kurejeshwa toka Dar es Salaam vilikopelekwa kwa uchunguzi.
Kaimu Mganga Mkuu wa hospitali hiyo, Dk Omar Chande, alisema jana kuwa mgonjwa huyo Frank Nnko (30) anaendelea kupata matibabu hospitalini hapo.
HATUA ZA TAHADHARI
Hospitali ya Amana imetoa dawa za kujipata kujikinga na ugonjwa huo kwa madaktari na wauguzi.
Uchunguzi uliofanywa na NIPASHE umebaini kuwa madaktari na wauguzi wameanza kupewa dawa hizo.
Daktari Kiongozi wa hospitali hiyo, Dk. Andrew Method, alisema wameshapewa dawa za kutosha za kujipaka ambazo hujipaka nyakati wanapokuwa kazini wakihudumia wagonjwa.
“Tumepewa dawa zinazotosha madaktari na wauguzi wote, tunajipaka nyakati za asuhuhi, mchana na usiku kwa wanaokuwa zamu wakitoa huduma, zoezi linaendelea vizuri bila usumbufu wowote,” alisema.
“Tunaendelea kutoa elimu kwa wagonjwa waliopo na watu wanaowaleta jinsi ya ugonjwa unavyoenezwa na njia zipi watumie katika mazingira yao wanaoishi ili kupunguza maambukizi yasiendelee kuongezeka,” aliongeza.
Aidha, alisema utawala wa hospitali hiyo tayari umechukua hatua stahiki za kuwakinga wagonjwa waliolazwa hospitalini hapo kwa kuhakikisha wanalala kwenye vyandarua vilivyowekwa dawa, kufyeka nyasi ndefu, kupulizia dawa na kufukia mashimo na madimbwi eneo linalozunguka hospitali.
Aliongeza kuwa, hadi sasa kuna wagonjwa saba wanaougua dengue wamelazwa kiwamo mtoto wa kiume mwenye umri wa miaka mitano.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadiki, amesema serikali imeandaa utaratibu wa kuwa na vituo vya kupimia wagonjwa wa dengue kila halmashauri mkoani humo.
Sadiki amliyasema ya jana alipokuwa akizungumza kwenye kipindi cha NIPASHE kinachorushwa hewani kila siku na kituo cha Redio One cha jjini Dr es Salaam.
Sadiki alisema kwa sasa vipimo vinafanyika kwenye hospitali za Temeke, Ilala pamoja na Kinondoni na kwamba vipimo vya ugonjwa huo kwenye hospitali binafsi ni vya gharama kubwa kuliko vituo vya serikali.
Sadiki alisema manispaa zote zimenunua dawa kwa ajili ya kutokomeza viluwiluwi vinavyosababisha mazalia ya mbu wanaoeneza ugonjwa huo.Sadiki aliyaomba kampuni zenye uwezo wa kusaidia serikali katika kukabiliana na ugonjwa huo zijitokeze.
Wizara ya Afya na ustawi wa Jamii wafanyakazi na wataalamu katika sekta hiyo wana ufahamu wa mbinu za kupambana pamoja na kujikinga na ugonjwa huo wanapotoa tiba.
Msemaji wa wizara hiyo, Nsachris Mwamwaja, alisema: “Mafunzo waliyopata vyuoni wauguzi na madaktari yanatosha kujilinda dhidi ya magonjwa na ikitokea ameumwa daktari au muuguzi ni sawa na anavyoumwa mwananchi mwingine yeyote.”
Hata hivyo, alisema tayari baadhi ya hospitali za mikoa ya jiji la Dar es Salaam zimeanza kuchukuwa hatua ya kuwakinga wa uguuzi na madaktari wanaotoa huduma kwa wagonjwa hao.
Imeandikwa na Kamili Mmbando, Samson Fridolin, Cristina Mwakangale, Huseni Ndubikile na Jimmy Mfuru, Dar; Rahma Suleiman, Zanzibar na John Ngunge, Arusha
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment