Peter Muthirika anayeongoza chama cha DPP ndiye rais mteule nchini Malawi
Hatimaye Malawi imepata Rais mpya baada ya mivutano ya kisheria kwa wiki nzima.
Mwandishi wa BBC Baruan Muhuza amesema kutoka mjini Blantyre kuwa Profesa Peter Mutharika
ameshinda uchaguzi huo kwa kupata asilimia 36.4 ya kura zote akifuatiwa na Dr Lazarus Chakwera mwenye asilimia 27.8 huku Rais anayemaliza muda wake Dr Joyce Banda akishika nafasi ya tatu kwa asilimia 20.2 na Atupele Muluzi amekuwa wa nne na asilimia 13.7
Mwenyekiti wa tume ya uchaguzi Jaji Mackson Mbendera amesema uchaguzi huo ulikumbwa na changamoto nyingi lakini mwishowe nchi ni lazima ipate kiongozi wake na kuwaomba wananchi kuwa na utulivu .
Kesi Mahakamani
Awali Jaji Kenyata Nyirenda wa mahakama kuu mjini humo jana usiku alitoa uamuzi kuwa hawezi kuvunja sheria kwa kuruhusu tume iongeze muda wa
kuhesabu upya kura kwenye maeneo yenye utata.
Na kwamba sheria inaitaka tume kutangaza matokeo ndani ya siku nane na si vinginevyo.
Uchaguzi wa Malawi ulifanyika Mei 20 nchini kote lakini siku moja tu baada ya kupiga kura, malalamiko yakiambatana na mapingamizi ya kisheria yakatawala kwenye mahakama kuu za Lilongwe na Blantyre.
(P.T) Chanzo:BBC