Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
AZAM FC pekee ndio klabu ya Tanzania yenye uwanja wake wa kisasa kwa ajili ya mazoezi, mechi za ligi kuu na michuano yote inayosimamiwa na shirikisho la soka barani Afrika, CAF.
Katika historia ya soka la Tanzania, Azam fc haiwezi kunusa ukongwe wa klabu mbili za Simba na Yanga.
Hizi ni klabu zenye mafanikio ndani na nje ya uwanja. Ni klabu zenye mashabiki kila kona ya nchi hii.
Lakini licha ya kukaa miaka mingi katika soka la ushindani nchini Tanzania na michuano ya Kimataifa, Yanga na Simba hazijawahi kumiliki viwanja vyake vya mazoezi na mechi za ligi kuu.
Kwa miaka mingi sasa viongozi wanaopita katika klabu hizo wanakuja na ndoto za kujenga viwanja, lakini zinayeyuka kutokana sababu mbalimbali ikiwemo kuendekeza siasa kuliko vitendo.
Kwasasa mwenyekiti wa Yanga, Yusuf Manji ana mkakati kabambe wa kujenga uwanja wa klabu hiyo maeneo ya Jangwani, wakati huo huo, naye mwenyekiti wa Simba, Alhaj Ismail Rage akipambana na mpango kama huo maeneo ya Bunju jijini Dar es salaam.
Kwa miezi miwili sasa, Uongozi wa Simba unaendelea na ujenzi wa uwanjao wake na sasa umefikia hatua nzuri ya kuanza kutumika kwenye mazoezi ya klabu hiyo ikiwa ni mara ya kwanza kumiliki uwanja katika historia yake.
Kutokana na maendeleo hayo,uongozi wa Simba umewakaribisha wapenzi na wanachama wake kesho Jumamosi katika Uwanja wao Bunju kwa ajili ya kuangalia maendeleo ya ujenzi wa uwanja wa mazoezi wa klabu.
Katibu mkuu wa Simba sc, Ezekiel Kamwaga amesema ujenzi huo ulioanza miezi miwili iliyopita, unakaribia kukamilika na utakuwa uwanja wa kwanza rasmi wa mazoezi wa klabu katika historia yake.
Vyombo vya habari navyo vinaalikwa katika tukio hilo litakaloanza saa tano kamili asubuhi.
source: matukiotz.com
No comments:
Post a Comment