Na Hudugu Ng'amilo
HATIMAYE Profesa Peter Mutharika ameapishwa rasmi jana kuwa Rais wa Malawi baada ya kumbwaga aliyekuwa Rais wa nchi hiyo, Joyce Banda.
Licha ya kucheleweshwa matokeo ya uchaguzi uliogubikwa na madai ya udanganyifu na wizi wa kura, Prof. Mutharika amekalia kiti hicho kilichowahi kushikwa na marehemu ndugu yake, Bingu wa Mutharika.
Prof. Mutharika aliibuka mshindi baada ya kupata zaidi ya asilimia 36 ya kura zote akifuatiwa na Dk. Lazarus Chakwera (asilimia 27.8) na Banda akishika nafasi ya tatu kwa asilimia (20.2).
Uchaguzi wa Malawi uligubikwa na hali ya sintofahamu baada ya Mahakama Kuu, kupinga ombi la kura kuhesabiwa upya huku Banda akidai kulikuwa na udanganyifu mkubwa.
Banda akubali matokeo
Jumamosi ya wiki iliyopita Banda alijitoa katika kinyang'anyiro hicho kwa madai ya kuvurugwa kwa mtiririko mzima wa shughuli za upigaji kura, kuhesabu na hata namna ya kusimamia utoaji wa matokeo.
Katika kuonyesha kwamba amekomaa kisiasa, Banda alikubali matokeo yaliyotangazwa juzi na Tume ya Uchaguzi (MEC) na kuwataka wafuasi wake pia kuyeheshimu.
Yaliyojiri kabla Mutharika kutangazwa rais Miongoni mwa matukio yaliyojiri kabla ya MEC kutangaza matokeo juzi pamoja na Mutharika kuapishwa kuwa rais jana, ni pamoja na kuitishwa kwa zoezi la kuhesabu kura.
Banda aliyeachia madaraka aliamuru MEC kusitisha shughuli ya kuhesabu na kutangaza matokeo ya uchaguzi mkuu uliofanyika Jumanne ya wiki iliyopita urudiwe ndani ya siku 90 kuanzia Jumamosi iliyopita.
CHANZO TANZANIA DAIMA.
No comments:
Post a Comment