Shekhe Muhammed Abdallah Mkumbalagula (27), mwenyeji wa Tanga, ameuawa kwenye mlipuko wa bomu uliotokea juzi usiku eneo la Darajani kisiwani Zanzibar.
Licha ya Mkumbalagula kupoteza maisha waumini wengine nane waliokuwa wanatoka msikitini, wamejeruhiwa baada ya kulipukiwa na bomu hilo lililokuwa limetegwa karibu na maegesho ya magari ambako nao walikuwa wameweka gari lao.
Mlipuko huo ulitokea usiku wa kuamkia jana na kujeruhi waumini wengine nane waliokuwa wanatoka msikitini, kwa mujibu wa polisi.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Mkadam Khamis Mkadam, aliiambia NIPASHE kuwa Mkumbalagula aliingia Zanzibar Jumapili iliyopita akitokea Tanga kwa nia ya kuhubiri Uislam.
Aliwataja majeruhi kuwa ni Kassim Mafuta Kassim (38) kutoka Tanga pia na waliobaki ni wenyeji wa Zanzibar ambao ni Hamad Masour Khamis (46), Suleiman Ali Juma (21) wakazi wa Bububu, wengine ni Khelef Abdallah Abdallah (21) anayeishi Magomeni.
Wengine ni Kassim Issa Mahmoud wa Fuoni, Ahmed Haidar (47) na mtoto Halid Ahmed Haidar (16) wote wanatoka Kiembesamaki.
“ Hao ndiyo waathirika wa bomu ambao walikuwa wanatoka kufanya ibada maeneo ya Darajani marufu kwa Muzamil na walipofika katika eneo la maegesho ya magari ambapo ndipo ilipokuwa gari yao bomu lilipolipuka na kuwajeruhi,”alisema Mkadam.
Alieleza kuwa Polisi Zanzibar imeanza msako maalum wa wahalifu wa mlipuko huo uliotokea juzi saa 2 usiku, kuua na kujeruhi wengine saba.
Aidha alisema Salama Iddi (20) mkazi wa Magomeni Zanzibar alipata mshtuko kutokana na mlipuko huo.
Mkadam alisema majeruhi wote walikimbizwa katika hospitali ya rufaa ya Mnazi Mmoja na watatu kati yao wamepata ruhusa na watano bado wamelazwa hospitalini.
Alisema Haidar na mtoto Halid Haidar wamelazwa kwenye hospitali ya Alrahma na Salama wakati Iddi, Hamad Masoud na Suleiman Juma wapo hospitali ya Mnazimmoja na hali zao zinaendelea vizuri.
Mukadam alisema gari lililolipuliwa ni aina ya Land Cruiser Prado lenye namba Z 675 CN ambalo limeharibiwa vioo, magurudumu na mlango.
Alisema katika eneo la tukio kulikutwa na mabaki ya vipande vya bomu yenye rangi ya kijivujivu na kusema mlipuko huo ni wa bomu la kutengenezwa kienyeji kama mabomu yaliyoharibu eneo la Mkunazini na Forodhani Februari mwaka huu.
Alisema hadi sasa hakuna aliyekamatwa kuhusiana na tukio hilo na hata ile milipuko mingine minne ya mabomu iliyotokea visiwani hapa mwaka huu.
SHEIKH AZIKWA
Mazishi ya Sheikh Mkumbalagula yalifanyika jana kwenye makaburi ya Mwanakwerekwe.
DARAJANI SHWARI
NIPASHE ilitembelea eneo la Darajani ilipotokea ajali hiyo na kuona wafanyabiashara na wananchi wakiendelea na kazi zao kama kawaida.
TAARIFA ZA MITANDAO
Kamanda Mukadamu, alipoulizwa kuhusu habari za masheikh kutoka Mombasa kuwa ndiyo walikuwa wamelengwa na shambulio hilo alipinga taarifa hizo.
Awali taarifa zilizokuwa ndani ya mtandao zilidai kuwa katika msikiti huo kulikuwa na Masheikh kutoka nchini Kenya pamoja na wenyeji wao ambao wakati wa tukio walikuwa wanakwenda kupanda gari lao lililokuwa kwenye maegesho hayo.
Akizungumzia madai hayo kuwa mashambulizi yalimlenga Sheikh kutoka Mombasa, Kamanda Mukadam alipinga na kusema wageni hao hawakuwa kwenye msikiti wa Darajani.
Alisema walikuwa kwenye Jitimai (mkusanyiko wa waumini) wa Kiislam kukumbushana mafundisho ya dini iliyopangwa kufanyika siku tatu na kumalizika leo ambapo yalihudhuriwa na wageni kutoka sehemu mbalimbali, kwenye msikiti wa mtaa wa Fuoni.
Alisema waliokuwapo wanatoka Kenya, Uganda, Burundi na wenyeji Tanzania.
Habari za mitandaoni zilizozagaa sehemu mbalimbali zilidai kuwa shambulio hilo lilimlenga Sheikh Abulfadh'li Qassim ambaye katika tukio hilo, amejeruhiwa mkono na mguuni na anaendelea vizuri.
Sheikh Qassim inadaiwa kuwa na msimamo unaopingana na baadhi ya Waislam na imetajwa kuwa mhubiri aliyeuawa ni mwanafunzi wa sheikh huyo.
MATUKIO YA MASHAMBULIO
Kwa mwaka huu mashambulio kadhaa ya mabomu yameripotiwa visiwani Zanzibar yakiwa yametengezwa kienyeji. Mabomu hayo yalilipuliwa nje ya Kanisa Anglikana mjini Mkongwe pamoja na mgahawa uliokuwa karibu na kanisa hilo.
*Rahma Suleiman, Zanzibar na Romana Mallya, Dar
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI
No comments:
Post a Comment