Kocha huyo wa zamani wa timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars aliyezaliwa Aprili 29, mwaka 1962, amesaini mkataba wa miaka miwili kwa ajili ya kuifundisha timu hiyo akirithi mikoba ya Mholanzi Hans van der Pluijm.
Yanga itatisha: Kocha Mbrazil, Marcio Maximo akizungumza na Waandishi wa Habari mchana wa leo Dar es Salaam
WASIFU WA MAXIMO:
JINA: Márcio Máximo Barcellos
KUZALIWA: 29 April 1962 (age 52)
ALIKOZALIWA: Rio de Janeiro (RJ) Brazil
TIMU ALIZOFUNDISHA:
Klabu ya sasa: Yanga SC
Timu Mwaka
1992-1993 Brazil U20
1992-1993 Brazil U17
1992 Mesquita
1994 Barra da Tijuca FC
1994 Qatar U20
1995 Al-Ahli
2002 Cayman Islands
2003 Livingston
2006-2010 Tanzania
2012 Democrata-GV
2013 Francana
Tangu Juni 27, 2014; Yanga SC
Mbrazil akizungumza na Waandishi wa Habari mchana wa leo mjini Dar es Salaam, amesema pamoja na changamoto ambazo anatarajia kuzipata kutoka timu pinzani wa Yanga, kama Azam FC, Simba na Mbeya City, lakini atahakikisha anajenga msingi bora ya soka itakayowezesha kutimiza majukumu yake vizuri.
Amesema anataka kuona timu inashinda mechi zake za ndani ya nchi na nje, kwani anaamini Yanga ni klabu kubwa barani Afrika.
“Nataka kuibadilisha soka ya Yanga ili liweze kufikia katika kiwango wa kimataifa na hili linawezekana, kwani nani alikuwa anaijua TP Mazembe ya DRC, lakini kwa kuwa iliandaliwa na kufanyika uwekezaji sasa ni klabu kubwa Afrika” amesema Maximo.
Maximo amesema, atahakikisha anajenga soka ya vijana kwa kuwa ni msingi wa soka inapoanzia ambapo atakuwa na timu zenye umri tofauti.
Amesema, kikubwa anatarajia kuona jitihadi za wachezaji wa timu hiyo ndani ya uwanja, kwani kitu muhimu kwake ni ushindi.
Maximo, pia atakuwa ni Mkurugenzi wa ufundi wa timu hiyo, akisaidiwa na Mbrazil mwenzake Leornado Neiva ambaye atafundisha timu ya vijana waliochini ya umri wa miaka 20, aliyesaini mkataba wa miaka miwili juzi.
Neiva pamoja na kuwa na kocha wa vijana atamsaidia Maximo katika majukumu yake katika kikosi cha kwanza cha timu hiyo.
Maximo akiwa kocha mkuu wa timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ aliyeifundisha kuanzia mwaka 2006-2010, aliwahi kumleta wasaidizi wake kutoka Brazili, ambao ni Markus Tinoco, ambaye alikuwa kocha wa timu ya vijana waliochini ya miaka 20.
|
Maximo na Msaidizi wake, Leonardo Neiva Martins kulia |
Lakini Yanga wanatarajia kumwajiri kocha mwingine mzawa na kuwa wanne akiwemo kocha wa makipa, Juma Pondamali kwa lengo la kuleta ufanisi zaidi.
Katika hatua nyingine, Maximo alisema anatarajia kuanza programu ya mazoezi Jumatatu ijayo kujiandaa na msimu mpya wa Ligi Kuu Bara.
Maximo aliyezaliwa mjini Rio de Janeiro, alikuwepo kwenye mabenchi ya Ufundi ya timu za taifa za vijana za Brazil chini ya umri wa miaka 17 na 20 kuanzia mwaka 1992 hadi 1993.
Vikosi hivyo ndani yake vilikuwa vina wachezaji walioibuka nyota wakubwa Brazil baadaye kama Ronaldo Lima na Ronaldinho Gaucho, ambaye wote sasa wamestaafu baada ya kuwika hadi kuwa Wanasoka Bora wa Dunia.
Kabla ya hapo, mwaka 1992 alifundisha Mesquita, 1994 Barra da Tijuca FC za kwao Brazil, 1994 akainoa U20 ya Qatar na mwaka 1995 akafundisha Al-Ahliya huko.
Alifanya kazi pia kama Mkurugenzi wa Ufundi wa viswia vya Grand Cayman kwa miaka mitatu ambako alikataa ofa ya kuongeza mkataba kwa miaka 10 ili akajiunge na Livingston FC ya Scotland Juni 5 mwaka 2003, alikosaini Mkataba wa mwaka mmoja na kuwa kocha wa kwanza Mbrazil kufundisha timu ya Uingereza.
Pamoja na hayo, mambo hayakumuendea vizuri huko, baada ya mechi tisa akiambulia ushindi wa mechi tatu, sare tatu na vipigo vitatu, akajiuzulu Oktoba 14.
Juni 29 mwaka 2006, Maximo akasaini Mkataba wa kuifundisha Taifa Stars ambayo mwaka 2009, aliiwezesha kufuzu kucheza fainali za kwanza za CHAN nchini Ivory Coast.
Maximo alijiuzulu kuifundisha Taifa Stars mwaka 2010, akiwaacha Watanzania bado wanampenda- akaenda Democrata ya nyumbani kwao, Brazil.
Alifukuzwa katika timu hiyo Februari 13 mwaka 2012 na Juni mwaka huo huo alikaribia kujiunga na Yanga SC kurithi mikoba ya Mserbia, Kosta Papic, lakini wakashindwana dau na klabu hiyo ikamchukua Mbelgiji, Tom Saintfiet.
Novemba 2012, akajiunga na Francana ya kwao Brazil ambako ndipo anatokea sasa kuja Yanga SC baada ya kumaliza Mkataba wake.
source: matukiotz.com