Na
BARAKA MBOLEMBOLE
Wakati ligi kuu ikianza, mchezaji mwenye
thamani kubwa zaidi, Mganda, Emmanuel Okwi amekuwa mmoja wa watazamaji
mwenye thamani kubwa. Je, Yanga wameingia ' mkenge' katika usajili wake?.
Hili linaweza kuwa swali ambalo majibu yake yapo wazi. Kwanza, Okwi ni
mchezaji wa Etoile du Salehe ya Tunisia ambao walimnunua kutoka timu ya
Simba.
Kwa nini yupo Yanga?. Alikuwa akiichezea timu ya SC Villa ya kwao Uganda kwa mkataba wa mkopo wa miezi sita akitokea Etoile. Narudia tena, alikuwa akiichezea Villa kwa mkopo. Fifa ilimruhusu Okwi kucheza Villa kwa muda wakati kesi tatu zinazomuhusu Mganda huyo zikitafutiwa mhuafaka. Okwi kwa upande wake anadai kuwa Watunisia hao walivunja mkataba kwa kushindwa kumlipa pesa zake kama ilivyotakiwa. Simba nao wanadai malipo yao kutoka kwa Etoile.
Okwi aliruhusiwa
kuichezea Villa ili kulinda kiwango chake, na wala hakuwa mchezaji
anayemilikiwa na timu hiyo. Alizuiwa kuichezea timu ya Taifa ya Uganda katika
michuano inayoendelea ya Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ligi za ndani,
CHAN, kwa kuwa alikuwa Villa kwa mkopo kutoka timu ya ng'ambo. Ila, ni Villa
ndiyo wanaosemekana kumuuza Okwi kwa timu ya Yanga. Kwa mamlaka gani?. Hadi
hapa Yanga watakuwa wameliwa. Kwa kuwa Okwi ni mchezaji wa Etoile si Villa.
Yanga wamemsaini Okwi
huku wakijiaminisha kuwa wapo sahihi. Wanaamini Okwi ni mchezaji huru au wa
Villa. Ila, alitakiwa kucheza Villa kwa miezi sita, lakini akaitumikia miezi
isiyozidi miwili tu na kununuliwa. Caf, Shirikisho la soka Afrika
wamemuhidhinisha Okwi kuichezea Yanga. Kamati ya sheria na hadhi ya wachezaji
imemzuia matumizi yake hadi watakapopata ufafanuzi kutoka FIFA, Shirikisho la
soka ulimwenguni.
Ndiyo, wapo sahihi kwa
kuwa FIFA, ndiyo waliosema mchezaji huyo acheze Villa kwa miezi sita wakati
kesi zake zikishughulikiwa.
FIFA, wanaweza kumruhusu
Okwi kuchezea Yanga kwa maslai ya kipaji chake. Ila, wanaweza pia kumzuia
endapo watajua kuwa mchezaji huyu amekiuka maagizo yao ya awali ambayo
walimwambia acheze Villa. Inawezekana mchezaji huyo akaonekana tapeli, kwa
kuwaadaa Yanga wakati akijua fika mkataba wake upo Etoile. Wapo wachezaji
walioshinda vita kama hii ya Okwi, ila wapo pia walioingia katika vifungo vya
FIFA.
Huenda Yanga wakamtumia
Okwi siku za mbele, ila kwa sasa ni uhalali wa mchezaji huyo. Kama, Etoile
wataendelea kushikilia msimamo wao kuwa hawajui mchezaji wao mahali alipo, Okwi
ataoneka ni mtoro. Endapo, Okwi ataonekana ni halali madai yake anaweza kulipwa
fidia na Etoile, ila kasheshe ni wapi ambapo Villa walipata kibali cha kumuuza
Okwi kwa timu ya Yanga?
Kila upande udai una
wanasheria wake. Duh!. Lakini mwanasheria wa Okwi anaweza kuwa mjanja zaidi,
mwenye akili zaidi, kwa kuweza kupata saini na mamillioni ya Yanga kwa
ufafanuzi wake wakati akimpigia debe mteja wake kuwa hana tatizo. Kama sheria
iliwekwa ili ivunjwe, na kama mikataba siku zote inaweza kutenguliwa, Yanga
watamtumia Okwi, ila tusije kushangaa FIFA, wakisema mchezaji huyo mali ya
Etoile. Yanga walimnunua wapi Emmanuel Okwi? Labda hapa ndipo kuna hoja ya
msingi.
Source: shaffih Dauda blog
No comments:
Post a Comment