Dar es Salaam. Sheria ya Mabadiliko ya
Katiba bado ina upungufu ambao utaathiri utendaji wa Bunge Maalumu,
ambalo huenda likaanza Februari 11 mwaka huu, mjini Dodoma.
Sheria hiyo Namba 8 ya 2011,
imeishafanyiwa marekebisho mara mbili yakiwamo ya Februari 2012 na
Novemba 2013, lakini mabadiliko hayo yameacha kasoro ambazo zinapaswa
zifanyiwe tena kazi, kupitia Bunge. (JM)
Kasoro zipo katika Kifungu cha 22
kinachohusu uchaguzi wa Mwenyekiti wa Muda wa Bunge Maalum, pamoja na
kifungu cha 24 kinachozungumzia Katibu na Naibu Katibu wa Bunge hilo
wanavyoanza kutekeleza wajibu wao.
Kupitia Sheria ya Marekebisho (Na:2)
ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya 2013, Bunge katika mkutano wa 12,
liliwapa mamlaka Katibu wa Bunge na Katibu wa Baraza la Wawakilishi,
'kufanya maandalizi muhimu kwa ajili ya utekelezaji bora wa shughuli za
Bunge Maalumu'.
Watendaji hao kwa mujibu wa sheria
ndio watakaoteuliwa kuwa Katibu na Naibu Katibu wa Bunge Maalumu baada
ya Rais kutangaza kuitishwa kwa Bunge hilo, lakini kiapo chao kitasubiri
hadi pale watakapochaguliwa Mwenyekiti na Makamu wa Bunge hilo.
Sheria husika inaweka sharti kwamba
ikiwa Mwenyekiti atatoka upande mmoja wa Muungano basi Katibu atoke
upande mwingine na kinyume chake. Hivyo lazima wasubiri uchaguzi huo ili
wajue ni nani Katibu na Naibu Katibu.
Kifungu cha 24 (2) kinasema: "Katibu
na Naibu Katibu wa Bunge Maalumu, watashika nyadhifa zao kwa misingi
kwamba, endapo Mwenyekiti atachaguliwa kutoka upande mmoja wa Jamhuri ya
Muungano basi Katibu wa Bunge Maalumu atatoka upande wa pili wa Jamhuri
ya Muungano".
Uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa
tayari baadhi ya wataalamu kutoka Ofisi ya Bunge na ile ya Baraza la
Wawakilishi (BLW) wameanza maandalizi ya awali katika moja ya hoteli za
jijini Dar es Salaam.
Katibu wa Bunge Dk Thomas Kashililah
mbali na kukiri kuanza kwa maandalizi hayo, hakuwa tayari kuzungumzia
kwa undani suala hilo kwa maelezo kuwa lazima ashirikiane na Katibu wa
Baraza la Wawakilishi.
Hata hivyo, kutokana na mkanganyiko
mkubwa uliopo katika Sheria hiyo, ni dhahiri watendaji hao watapata
wakati mgumu katika kuanza kutekeleza majukumu, hasa katika kuteua
wajumbe wa sekretarieti ya Bunge hilo.
Uteuzi wa wajumbe hao kwa mujibu wa
kifungu cha 24 (4) unapaswa kufanywa na Katibu kwa kushauriana na Naibu
wake, nafasi ambazo hazitakuwapo hadi pale Mwenyekiti na Makamu wake
watakapochaguliwa.
CHANZO MWANANCHI
No comments:
Post a Comment