WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Friday, January 24, 2014

FIFA: Simba ilipwe fedha za Okwi

  Yanga: Hatuna imani na TFF kumzuia Okwi

 
Emmanuel Okwi
Wakati usajili wa Emmanuel Okwi Yanga ukizuiwa na Shirikisho la Soka barani Afrika (CAF), Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) limeitaka klabu ya Etoile du Sahel (ESS) ya Tunisia kuhakikisha inalipa fedha inazodaiwa na Simba kufikia Jumanne ijayo.
Yanga nayo iliibuka jana na kusema kwamba haina imani na shirikisho la soka nchini (TFF) kwa kuzuia usajili wa Okwi siku chache kabla ya ligi kuanza huku FIFA ikiwa haijamzuia Mganda huyo kuichezea klabu hiyo ya Jangwani licha ya kuzitambua kesi tatu zilizo mbele yao kuhusu nyota huyo.

Januari mwaka jana Simba ilimuuza Mganda huyo kwa mali kauli ya dola za Marekani 300,000 (Sh. milioni 480), ambazo hadi sasa bado hazijalipwa huku mchezaji huyo akiuzwa kiutata na SC Villa ya Uganda kwa Yanga Desemba mwaka jana.

Juzi Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), lilisimamisha usajili wa mshambuliaji huyo hatari kutoka Uganda katika Klabu ya Yanga wakati likisubiri ufafanuzi kutoka Fifa, ufafanuzi ambao pia unasubiriwa na CAF kabla ya kumuidhinisha kushiriki katika mashindano ya Afrika akiwa na Yanga au ESS.

Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage alisema jijini Dar es Salaam jana kuwa amepokea barua kutoka kwa Kamati ya Hadhi za Wachezaji ya Fifa (PSC) ikieleza hatua zinazochukuliwa na shirikisho hilo la kimataifa kuhusu malipo ya fedha zao.

"Jana (juzi) nilipata barua kutoka kwa Laura Santanel ambaye ni kiongozi katika 'Fifa Players' Status' (Kamati ya Hadhi za Wachezaji ya Fifa) wakinieleza kwamba wameitaka Etoile itulipe fedha kufikia Januari 27 mwaka huu (Jumanne)," alisema Rage.

"Pasipo kufanya hivyo, itabidi mwanasheria aliyeteuliwa kushughulikia suala hilo aanze kulishughulikia kikanuni. Ikumbukwe sisi (Simba) tulishalipa dola 5,900 kwa Fifa ili wateue mwanasheria atayeshughulikia kesi hiyo.

"Tulijua suala la Okwi litawaletea matatizo hata wenzetu Yanga kwa sababu mchezaji huyo bado ana kesi kibao Fifa zinazohitaji utatuzi. Sisi (Simba) hatujalipwa fedha za uhamisho wake kwenda Etoile na ile asilimia 20 ya mauzo yake Yanga ambayo imo kwenye mkataba wetu na Watunisia, katika hali kama hii si rahisi Simba kukaa kimya," alifafanua zaidi Rage.

Kamati ya Hadhi za Wachezaji ya Fifa inayoongozwa na Mwenyekiti, Mjerumani Theo Zwanziger, ina kesi nne kuhusiana na suala la mchezaji huyo. Wakati Okwi ameishitaki klabu hiyo Fifa kwa kutomlipa mshahara, Etoile du Sahel imemshitaki kwa utoro. Nayo Simba imeishitaki Etoile du Sahel kwa kushindwa kuilipa ada ya mauzo ya mchezaji huyo ambayo ni dola za Marekani 300,000.

Aidha, siku moja baada ya usajli wa Okwi Yanga, Shirikisho la Soka Uganda (Fufa) lilihitaji kujiridhisha kwa kuiandikia barua Fifa kusaka uhalali wa uhamisho wa mshambuliaji huyo hatari kwenda Jangwani.

Desemba 15, mwaka jana Yanga ilikamilisha usajili wa miaka miwili na nusu wa mshambuliaji huyo wa zamani wa watani wao wa jadi, Simba kwa dau kubwa linalotajwa kuwa Dola za Marekani 150,000 (Sh. milioni 240 za Tanzania).

Katibu Mkuu wa Yanga, Benno Njovu alisema katika mkutano na waandishi wa habari jana kuwa klabu hiyo haina imani na TFF kwani imekuwa ikifanya mambo ya kuwachanganya kila ligi inapokaribia kuanza. Alisema TFF ilifanya hivyo walipomsajili Mbuyu Twite, Mrisho Ngasa na sasa Okwi.

Njovu alisema Yanga ilifuata taratibu zote katika kumsajili Okwi hivyo ni mchezaji halali wanayepaswa kumtumia.

Alisema pia Yanga inahofu kwamba baadhi ya wajumbe waliohusika katika kupitisha maamuzi ya kuzuia usajili wa Okwi hawana sifa zinazostahili na akawaomba wanachama watulie kwani kamati ya utendaji ya Yanga itakaa kutoa tamko zito juu ya sakata hilo.

ESS KUIHARIBIA ZAIDI YANGA
Taarifa zilizonaswa na NIPASHE jana zilieleza kuwa viongozi wa ESS wamepanga kuwasilisha kesi nyingine Fifa dhidi ya Yanga kwa kumnunua Okwi bila kuwashirikisha.

"Uongozi umepanga kukutana Jumanne ijayo ili kuzungumzia masuala yote yanayomhusu Okwi. Tumepanga kuwasilisha malalamiko yetu Fifa kuhusu usajili wa Okwi katika klabu inayommiliki kwa sasa nchini Tanzania (Yanga)," alisema mmoja wa viongozi wa ESS katika barua ambayo alikuwa anamweleza mmoja wa vigogo wa Simba.

Barua hiyo iliyotumwa kwa mtandao (email) juzi saa 2:01 usiku ambayo NIPASHE imeiona, pia inaeleza kuwa ESS bado wanamtambua Okwi kama mchezaji wao halali na wanaushangaa uongozi wa Yanga kumsajili pasipo kuwasiliana nao. 
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment