KATIKA mabadiliko ya Baraza la Mawaziri
yaliyofanyika majuzi, inaweza kabisa kusemwa, kuwa Waziri mpya wa Katiba na
Sheria, Dk. Asha -Rose Migiro ndiye Mtanzania pekee kwa sasa aliyebebeshwa
dhamana kubwa ya kuuongoza, kuusimamia na kuhakikisha unahitimishwa salama,
mchakato wa nchi yetu kupata Katiba Mpya inayotokana na utashi wa wananchi, na
si wa wanasiasa na vyama vyao. Hii ni dhamana kubwa. Ni heshima kubwa aliyopewa
Asha-Rose Migiro. Hakika, iinaweza kusemwa, kuwa mustakabali wa nchi yetu uko
mikononi mwake.
Ni dhamana yenye kumtaka aliyepewa,
kuitanguliza haki. Namna yoyote ile, ya kwa makusudi au kwa hila, kujaribu
kuipindisha haki, na hivyo kuwanyima walo wengi haki, itapelekea kwenye kupanda
mbegu za chuki na ulipaji wa visasi. Mbegu za utengano kama taifa. Ni dhambi
tutakayohukumiwa nayo kwa siku ama miaka ambayo hata sisi tutakuwa
tumeshatangulia mbele ya haki. Na siku zote, hukumu ya kutotenda haki, kwa
kudhamiria au kwa hila, hutolewa humu duniani, na huko tunakokwenda.
Na hakika, kama Mtanzania, mzaliwa na
mzalendo wa nchi hii, nimefarijika kuisikia kauli ya awali ya Asha- Rose
Migiro. Amenukuliwa akitamka; kuwa moja ya majukumu atakayoyafanya ni
kuhakikisha kuwa mchakato wa Katiba Mpya unakwenda kama ulivyopangwa, huku
akisisitiza kuwa hawezi kukipendelea CCM katika mchakato huo. Na akazidi
kuongeza;
“Nitasimamia mchakato wa Katiba katika
kipindi hiki ambacho tunaelekea kwenye Bunge la Katiba na baadaye Kura ya
Maoni. Jambo zuri ni kwamba mchakato huu unakwenda kwa mujibu wa sheria.
Nawahakikishia Watanzania nitafanya kazi kwa uaminifu na kujituma,” amenukuliwa
akisema Waziri Migiro.
Na nyongeza hapa ni kuwa, kwa Asha-Rose
Migiro, umma na umwamini, kuwa sio tu hawezi kukipendelea CCM ( Chama chake)
katika mchakato huu, bali, haitarajiwi akipendelee chama chochote, kikundi
chochote au mtu yeyote. Anatakiwa aipendelee Tanzania. Atangulize maslahi ya
nchi kwa kutazama zaidi leo, kesho, keshokutwa na mtondogoo. Kwamba vyama vya
siasa na viongozi wanakuja na kuondoka, lakini nchi itabaki.
Na ikumbukwe, katika hili la Katiba,
yanayokuja ni mabadiliko makubwa kuwahi kufanyika tangu mwaka 1977. Ni pale
ambapo Katiba ya Jamhuri ya Muungano ilifanyiwa marekebisho makubwa. Mwaka huo
wa 1977 yalifanyika mabadiliko makubwa pia kwenye uongozi wa chama tawala na
hata mfumo wa uongozi wa serikali.
Nimepata kuandika, kuwa katika dunia
hii, mabadiliko ya kijamii husababisha mabadiliko ya kisiasa. Wanasosholojia
wanasema, kuna sababu mbili zenye kufanya mabadiliko hayo; sababu za ndani ya
jamii husika (endogenous) na sababu za nje ya jamii (exogenous).
Kwa upande wetu, tunaona kuwa, sababu
za ndani na za nje, kwa pamoja, zimesukuma kwenye kufikia hatua hii ya
kufanyika mabadiliko haya makubwa ya Katiba.
Na kwa jamii yetu kwa upana wake, ina
sababu za msingi za kuyafurahia mabadiliko haya yanayokuja. Ni mabadiliko
yenye kuleta matumaini mapya.
Na Rais kikwete , hadi kufikia hatua
hii, ameonyesha ujasiri wake mkubwa wa kiuongozi. Ni katika kuyafanya
hata yale ambayo hayakufikiriwa kabla kwamba yangefanyika katika nchi hii.
Kamwe tusiruhusu jazba, chuki na
visasi vitawale siasa zetu. Hii ni nchi yetu. Ni nchi yetu sote. Hakuna
mtu, kikundi au chama cha siasa chenye haki zaidi ya kuongoza nchi hii
kuliko wengine wote.
Na kwa mwanadamu, lililo kubwa ni uwepo
wa matumaini. Na imani ya wananchi kwa taifa na viongozi wao ni shina la
matumaini yao. Katiba yetu inayokuja chachu ya kurudisha mioyo ya
uzalendo kwa taifa letu.
Mungu Ibariki Tanzania.
Chanzo:
www.raiamwema.co.tz: Maggid Mjengwa
No comments:
Post a Comment