Ndugu zangu,
KESHO Januari 12 ndugu zetu wa Zanzibar wanatimiza miaka 50 ya Mapinduzi yao.
Naam, jambo la waZanzibar ni letu
waTanganyika. Na hakika, Mapinduzi ya Zanzibar yalikuwa mapinduzi yetu
pia. Na leo hii Waunguja na Bara tumo kwenye mchakato wa Katiba Mpya
ambapo pia, kuna mapendekezo ya uwepo wa Serikali Tatu, mapendekezo
yalitokana na wananchi wa pande hizi mbili.
Naam, inahusu maridhiano ya kindugu yasiyotokana na uhasama na yenye lengo la kubaki kuwa wanandugu.
Na tunasoma, kuwa Mfalme Suleiman
aliambiwa ndotoni aombe kitu chochote kwa Mola wake, naye akajibu; " Ewe
Mola wangu, nipe mimi mtumwa wako moyo wa adili ili niwahukumu watu
wako, na kupambanua mema na mabaya, maana ni nani awezaye kuwahukumu
hawa watu wako walio wengi?" Hivyo basi, Mfalme Suleiman aliichagua
hekima. Maana, ni Mfalme Suleiman huyo anayekaririwa na vitabu vya dini
akitamka, ; " Watu wangu wanaangamia kwa kukosa hekima".
Naam, hekima ndilo jambo lililo bora
kabisa kwa mwanadamu kuwa nalo. Mwanadamu aliyepunguwa hekima ana hasara
kubwa maishani. Hekima ni tunu na kipaji ambacho Mwenyezi Mungu
amewajalia waja wake, ili nao waweze kupambanua na kuamua kati ya yalo
mema na maovu. Duniani hakuna shule ya hekima.
Ndio, furaha ya waZanzibar ni yetu, na
huzuni yao ni yetu pia, sisi waTanganyika. Binafsi nilifika Zanzibar
kwa mara ya kwanza mwaka 1988 ( pichani). Nilikuwa kijana mdogo sana.
Zanzibar ndio kisiwa cha kwanza kupata kukitembelea.
Tangu hapo niliipenda Zanzibar,
nimefika Zanzibar mara kadhaa. Ningelipenda sana niwe Zanzibar katika
siku ya kesho kushuhudia waZanzibar wakitimiza miaka 50 ya Mapinduzi.
Naam, ningependa kushiriki sherehe
hizo nikiwa na ndugu zangu waZanzibar. Maana, bado naukumbuka ukarimu wa
wenyeji wangu wa Zanzibar tangu safari yangu ya kwanza Unguja, Desemba,
1988.
Nakumbuka pia kushiriki sherehe za Mapinduzi Zanzibar, Januari 12, 1989.
Naam, Wazanzibar hata katika Serikali
Tatu, kama zitapitishwa, watabaki kuwa ndugu zetu. Na kwamba, jambo la
waZanzibar litabaki kuwa letu pia waTanganyika, iwe la furaha au huzuni.
Happy Mapinduzi Day!
Ni Neno Fupi La Usiku.
Maggid Mjengwa,
No comments:
Post a Comment