WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Saturday, January 11, 2014

Miaka 50 ya Mapinduzi Z’bar yaadhimishwa kwa fikra tofauti


Rais mstaafu wa Zanzibar Aman Abeid Karume akiteta jambo na Makamu wa Rais wa kwanza Seif Sharrif Hamad.

Zanzibar. Wananchi wa Zanzibar leo wanaadhimisha miaka 50 ya Mapinduzi ya visiwa hivyo yaliyouangusha utawala wa kisultan wakiwa na fikra tofauti.

Wakizungumza na gazeti hili kuhusu sherehe hizo walisema kuwa katika kipindi hicho wananchi wametambua hata kupevuka katika kudai haki zao na demokrasia, huku wakitaja changamoto mbalimbali ikiwamo uduni wa huduma za afya, elimu na udhaifu wa viongozi.

Mapinduzi hayo yalioongozwa Chama cha Afro Shiraz Party (ASP) yalihitimisha miaka 160 ya kutawaliwa na Waarabu iliyoanza mwaka 1804, utawala ambao ulilindwa na Waingereza.
Kufanyika kwa Mapinduzi Januari 12 mwaka 1964 kuliuweka madarakani utawala wa kizalendo wa 

Waafrika ulioongozwa na Hayati Abeid Amani Karume, aliyekuwa Rais wa Kwanza wa Zanzibar, ambaye hata hivyo aliuawa kwa kupigwa risasi na wapinga mapinduzi mwaka 1972.
Katika kuadhimisha sherehe hizo wananchi mbalimbali wametoa maoni tofauti wakidai kupevuka katika kudai haki zao na demokrasia.

Akitoa maoni yake Rashid Salum Adiy (54)mkazi wa Kikwajuni mjini Unguja alisema kuwa katika kipindi cha miaka 50 ya Wazanzibari wamepata fursa ya kuongeza ushirikiano na watu wa nje ya visiwa hivyo, huku pia wakiwa makini kudai haki zao za msingi na kidemokrasia.
“Pamoja na matatizo mengi yaliyopo, Zanzibar imeendelea kubaki nchi yenye amani, utulivu na umoja tofauti na mataifa mengine kama Somali, Sudan Kusini na DRC, lakini tuna changamoto ya kukosekana viongozi wa waaminifu na waadilifu,”alisema Adiy na kuongeza:

“Si viongozi wa kisasa wala wa kiserikali wenye kutii miiko ya uadilifu, uzalendo na uaminifu kwa wananchi wanaowaongoza, rushwa, ubinafsi na upendeleo vimechukua nafasi kuliko maendeleo na uzalendo.”
Naye Habiba Ali Mohamed (42) alisema Mapinduzi ya Zanzibar yamefungua milango na fursa mbalimbali za kiuchumi na maendeleo akitoa mfano wa wananchi wa Zanzibar walilivyoweza kujenga makazi bora ya kuishi tofauti na zamani.

Alisema: “Mapinduzi ndiyo chimbuko la Muungano na Serikali zote mbili zinapaswa kulinda mfumo uliopo. Anayesema hakuna lolote lililofanyika na kuleta  maendeleo ni mgeni hapa Unguja na Pemba, tunajijua tulivyokuwa na sasa hali za wananachi  zilivyobadilika”

Kwa upande wake Haroun Abdallah Said(40) anayeishi nje ya Mji wa Unguja anaeleza kuwa Mapinduzi yameweza kudumusha amani,udugu na maelewano baina ya Wazanzibari lakini akasema hali ya uchumi ni mbaya na kwamba wananchi wanateseka.

Alisema kwamba hadi sasa baada ya miaka 50 kupita tangu yafanyike Mapinduzi, kuna baadhi ya familia hazimudu kupata milo mitata kwa siku jambo analolitaja kama ukoloni mpya.

“Watoto wanakwenda skuli bila hata kandambili, wanasoma kwa kukaa chini, wanakosa madawati, walimu hawalipwi mishahara inayokidhi haja, hawana nyumba za kuishi, hata mazingira ya kufundishia ni mabaya,”alilalamika Said.
Akizungumzia sherehe hizo Suleiaman Ali Mohamed (68) Mkazi wa Mkunazini alisema malego ya Mapinduzi yamefanikiwa kwa asilimia 25 tangu mwaka 1964 na kwamba huduma za jamii zimezorota na ubora wake kushuka viwango.
Aliyataja maeneo hayo kuwa ni elimu, afya, majisafi na salama, matibabu na mazingira ya mji kutokuwa na usafi unaoridhisha. Akifafanua kwamba jamii imezungukwa pia na tatizo kubwa la rushwa hasa katika vyombo vya kutoa haki, huku viongozi na watendaji wa juu wakionekana kuwa na maisha bora.
“Mapinduzi yamekusudia kuondoa unyonge, matokeo yake unyonge,udhalili wa maisha ya watu na ufukura vimechukua nafasi. Hili siyo sawa na linawakera wananchi,”alisema Suleiman.
Kauli ya Suleiman iliungwa mkono na Dk Vuai Ali Vuai (69) mkazi wa Michenzani aliyesema kuwa malengo ya Mapinduzi bado hayajafikiwa kutokana na kuwepo kwa watendaji dhaifu katika utumishi wa umma.
Akitoa mfano alisema kwamba katika awamu ya kwanza ya utawala wa Mzee Karume majengo ya Michenzani yalikuwa yakipata huduma za maji na kushangaa hali ya sasa ambapo maji hayafiki hata ghrofa ya kwanza huku uchafu ukihatarisha afya za wakazi wake.
“Lengo la kutoa elimu bure halipo, sasa wazazi wanachangia na kulipia, wanafunzi hawana vitabu vya kiada na ziada na wengine husoma wakiwa wamekaa chini, darasa moja lina zaidi ya watoto 80,” alisema Dk Vuai.
Othman Salum Ali (37)mkazi wa Daraja Bovu anaeleza kuwa jambo pekee linalotakiwa kufanywa na Serikali ni kubuni sera na mkakati wa ujenzi wa viwanda vidogo na vikubwa, kuwainua kimitaji na nyenzo wakulima, wafugaji na wavuvi ambao ndiyo wengi katika jamii.
Mkazi wa Mwanakwerekwe, Bimkubwa Juma Wadi(52) alisema kuwa maendeleo yaliyofikiwa ni makubwa na kwamba ongezeko la ujenzi wa vituo vya afya limesaidia kunusuru vifo vya wanawake wajawazito na watoto kupatiwa chanjo.
Alisema kuwa pamoja na kosaro zilizopo, bado watoto wa maskini wanaendelea kupata elimu katika shule zilizojengwa na Serikali huku akiitahadharisha kwamba ujenzi wa shule za matabaka zisirejee tena visiwani humo.
Mwananchi mwingine Fatuma Haji Khamis(48), alisema kuwa katika miaka 50 ya Mapinduzi wanawake wamefanikiwa kutoka nyuma ya pazia la ukandamizaji na kunyimwa kwa haki zao, badala yake sasa wanakijua haki zao.
“Sasa wanawake Zanzibar tunaendesha baiskeli, pikipiki na kumiliki magari. Tunatoka asubuhi kwenda kazini, tunapata mishahara na kujenga nyumba zinazomilikiwa na wanawake wenyewe,” alieleza na kufurahia hali hiyo.
Wakati Zanzibar ikiadhimisha miaka 50 ya Mapinduzi hayo, visiwa hivyo vipo katika awamu ya saba ya Serikali, iliyo chini ya Rais wake Dk Ali Mohamed Shein.
Awamu nyingine zilizopita baada ya Sheikh Karume ziliongozwa na marais Abouud Jumbe Mwinyi(Rais wa pili), Ali Hassan Mwinyi; wa tatu, wa nne akiwa Idris Abul Wakil, Dk Salmin Amour Juma ni Rais wa tano, ambaye alifuatiwa na Dk Amani Karume kabla ya utawala wa sasa.

source: mwananchi

No comments:

Post a Comment