Dar es Salaam. Azam wamekalia usukani wa Ligi
Kuu Tanzania Bara baada ya Yanga kulazimishwa sare 0-0 na Coastal Union
kwenye Uwanja wa Mkwakwani.
Azam wamekalia uongozi ligi hiyo baada ya kuichapa Rhino Rangers kwa bao 1-0 kwenye uwanja wa Azam Complex, Chamazi, na kufikisha pointi 33, huku Yanga wakiwa na pointi 32 na Mbeya City (31) wakibaki nafasi ya tatu baada ya kulazimishwa sare 1-1 na Ruvu Shooting.
Mshambuliaji Kipre Tchetche ameendelea kuibeba Azam baada ya kuifungia bao pekee dakika 26, kwa shuti kali la mguu wa kushoto akiunganisha pasi ya Mohamed Kone.
Tchetche amefikisha mabao tisa hadi sasa akiwa nyuma kwa bao moja kwa kinara wa ufungaji Amisi Tambwe wa Simba mwenye magoli 10.
Tanga; Mabingwa watetezi Yanga, watajilaumu wenyewe kwa kushindwa kutumia nafasi nyingi walizozipata katika kipindi cha kwanza baada ya kupata kona sita katika dakika 30 za kwanza kabla ya wenyeji Coastal Union kuamka.
Kiungo Haruna Niyonzima alikosa bao baada ya shuti lake kudakwa na Shaabani Kado dakika 12, mashabiki wa Yanga dakika 29 walirusha chupa za maji uwanjani kupinga uamuzi wa mwamuzi wa mchezo huo, Simon Mbelwa, Pwani.
Wenyeji Coastal Union waliamka dakika ya 30, na kuanza kushambulia, lakini mashuti ya Yayo Lutimba, Haruna Moshi na Kenneth Masumbuko yaliokolewa kwa ustadi mkubwa na kipa Deo Munishi wa Yanga.
Mlandizi, Wenyeji Ruvu Shooting wameipunguza kasi Mbeya City baada ya kuilazimisha sare 1-1 kwenye Uwanja wa Mabatini
Shooting walikuwa wa kwanza kupata bao kupitia Jerome Lembele dakika 4, kabla ya City kusawazisha kupitia Deus Kaseke dakika 14.
Kagera Sugar wameendelea kusuasua baada ya kulazimisha sare 0-0 na Mtibwa Sugar kwenye uwanja wake wa nyumbani wa Kaitaba.
Mashabiki Yanga wapata ajali Tanga
Mashabiki wanaodhaniwa wa Yanga, wamepata ajali
wakiwa safarini kuelekea mkoani Tanga kuishangilia timu yao ikivaana na
Coastal Union.
Ajali hiyo ilitokea maeneo ya Tange karibu na Tanga mjini jana wakiwa kwenye gari lao aina ya Toyota Noah.
Kwa mujibu wa Kaimu Kamanda Polisi wa Mkoa wa Tanga, Juma Ndaki katika ajali hiyo alikuwepo Meneja wa Bendi wa Jahazi Modern Taarab, Ally Boha ambaye yeye ni majeruhi.
Aliwataja wengine waliopata majeraha ni dereva wa gari hilo aliyemtaja kwa jina moja la Yasini, Kondo Karume na Mbaraka Madenga ambao wote wamepata matibabu kwenye Hospitali ya Mkoa wa Tanga, Bombo.
“Haikuwa ajali ndogo, lakini kikubwa cha kushukuru kuwa waliokuwepo kwenye ajali hiyo wote wanaendelea vizuri baada ya kupatiwa matibabu kwenye hospitali ya mkoa wa Tanga.
Vikosi
Coastal: Shaaban Kado, Hamad Hamis, Abdu Banda, Mbwana Hamisi, Juma Nyoso, Jerry Santo, Daniel Lyanga, Chrispine Wadenya, Yayo Lutimba, Haruna Moshi, Kenneth Masumbuko
Yanga: Deogratius Munishi, Mbuyu Twite, Oscar Joshua, Nadir Haroub, Kelvin Yondani, Frank Domayo, Simon Msuva, Haruna Niyonzima, Didier Kavumbagu, Mrisho Ngassa na David Luhende.
Imeandaliwa na Burhan Yakubu (Tanga), Sosthenes Nyoni (Dar), Msafiri Sanjito (Pwani), na William Paul (Kagera)
SOURCE: mwananchi blog
No comments:
Post a Comment